Thursday, December 21, 2006

NI KWELI HALMASHAURI ZA WILAYA ZINAPOTEZA MAPATO

LEO asubuhi nikiwa kwenye bus litokalo Mkuranga kwenda Mbagala, tulipofika Vikindu (Kwenye kizuizi cha kukagua mazao, madini, na raslimali nyingine). Kuna abiria aliyekuwa na mzigo wa kulipia ushuru sifahamu ni mzigo gani. Basi watoza ushuru hao wa Vikindu walimwambia alipe Tshs 900/= abiria huyo alitoa chapchap wala bila kudai stakabadhi ya malipo na gari hilo likaondoka!

Kwa hakika nilimuona mtoza ushuru yule akiweka noti ya Tshs 500/= kwenye shati lake. Nikajiuliza ni kiasi gani cha mapato kinapotea kwa njia hii? Ni mamilioni. Hatuwezi kuendelea kwa njia hii. Ni hatari, hakuna usimamizi mzuri pale. Na hii ni kwa Vikindu tu. Je kuna vituo vingapi vya aina hii vinavyopoteza mapato kirahisi rahisi tu nchi nzima?

Lakini tatizo liko kwa walipaji, wao wanafikiri aa shs 900 tu mbona kidogo! Je, kwa mwezi wakitokea watu 20,000 ambao hawakupewa stakabadhi ya malipo. Halmshauri ya Mkuranga kwa kizuizi cha Vikindu kitakuwa limepoteza milioni 18! Si haba. Ni madarasa mangapi hayo ya shule ya msingi yangejengwa kwa mwezi, kwa fedha za Vikindu tu? Tuwe makini.

Tuna uwezo wa kuendelea, tatizo ni sisi wenyewe.

Chrsitmass njema.

Nitakuwa Matombo, Morogoro kwa muda wa majuma mawili. Naenda kula "mwidu" na "komola."

Wednesday, December 20, 2006

SOKONI KARIAKOO NI TOPE TUPU

Leo mchana nimetokea maeneo ya Kariakoo. Nilipita kabisa karibu na Soko la Kariakoo. Huwezi kuamini, soko hilo tunalojivunia kuwa ni la Kimataifa, hakuna kitu ni tope tupu. Mvua inayoendelea kunyesha hapa Dar es Salaam kwa kweli ni hatari tupu kwa afya zetu. Hebu fikiria mwenyewe karibu mboga na matunda hushushwa sokoni kariakoo na kwenyewe ni kuchafu sasa kweli tutapona?

Miundo mbinu inayolizunguka soko hilo pia ni mibovu, barabara zimechimbika, mitaro imeziba. Lakini waswahili wako pembeni wanajichana chips tu! Umeme nao hakuna, majenereta yanaunguruma, nyumba zinaendelea kujengwa, mikokoteni nayo inakusukuma. Daladala zilizochanika viti basi shida tu. Hili ndilo jiji la DAR ES SALAAM.

Jiji? Rekebisheni mambo hapo kariakoo, ni aibu.

KWAHERI NATHANIEL KATINILA

Msiba mkubwa umetupata Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika, Ofisi ya Waziri Mkuu na Programu ya Kuendeleza Masoko ya Kilimo (AMSDP) kwa kuondokewa na mmoja kati ya vijana waliobobea katika fani ya kilimo naye si mwingine bali ni Marehemu Nathaniel Katinila (45) juma lililopita. Marehemu alifariki kwa ajali ya Ndege Cessna 5HTZ mali ya Tanzair iliyotokea Mbeya tarehe 16/12/2006.

Mimi namfahamu sana Katinila. Mwaka 1981 tulikutana pale MATI- Ukiriguru mimi nikiwa mwaka wa pili (DIP - CROP PRODUCTION) naye akiwa amekuja kuanza kozi hiyo hiyo. Baada ya kuhitimu masomo yake akafanya kazi miaka michache (sifahamu ni sehemu gani) baadaye akajiunga na Chuo Kikuu cha Sokoine ambako alipata shahada yake ya kwanza yenye mchepuo wa Uchumi Kilimo. Tulikutana tena mwaka 1993 katika Wizara ya Kilimo na Mifugo, Idara ya Utafiti na Mafunzo, yeye akiwa ARI-Naliendele Mtwara nami nikiwa Makao Makuu Dar Es Salaam wote tukiwa wachumi kilimo mwenzangu "Kati" (Nilizoea kumwita hivyo) akiwa kwenye programu ya "Farming Systems Research and Socio-Economics" nami nikiwa kwenye Kitengo cha Mipango, Kupelemba na Kutathmini (Planning, Monitoring and Evaluation).

Tukiwa pale Ukiriguru, wote tulishiriki kwenye kikundi cha maigizo kilichojulikana kama "MAJOSA" chini ya mwalimu wetu Benito Mwenda ambaye alikuwa mwanachuo mwenzetu ingawa kwa sasa ni Mkufunzi hapo hapo MATIU. Tukiwa chuoni Katinila alikuwa pia "Boxer."

Akiwa Naliendele amefanya kazi nyingi za utafiti katika masuala ya farming systems. Baadaye alijiunga na mradi wa " RIPS" uliokuwa ukiendeshwa mikoa ya kusini kabla ya kurudi tena Kilimo pale Naliendele.

Mara tu ilipoanzishwa Programu ya Kuendeleza Masoko ya Kilimo. Nathaniel alibahatika kuwa Mratibu wake wa Kwanza.

Namfahamu sana Katinila kwa mema yake kuliko mabaya. Alikuwa mshauri mzuri, mpole na asiye na pupa. MUNGU AIWEKE MAHALI PEMA PEPONI ROHO YA NATHANIEL KATINILA. AMINA.

Thursday, December 14, 2006

"UCHAWI WA SYRIA"

Mhandisi Phillip Mbuligwe amerudi leo leo kutoka Syria. Eeeh Mbuligwe, habari za Waarabu? Namuuliza tena kwa utani. "Acha wee Banzi, wale si Waarabu, wamepiga hatua kubwa kimaendeleo, siyo kama unavyofikiria wewe. Mimi nafikiri umezoea waarabu wa hapa "Bongo".

Ndiyo, Mbuligwe ni mhandisi. Mwezi Novemba, 2006 alikuwa kule Syria kwa mafunzo ya muda mfupi kuhusu umwagiliaji. Kwa maelezo yake, Phillip anasema kuwa, Syria hupata mvua mm 100 kwa mwaka, lakini wanajitosheleza kwa chakula. "Uchawi" mkubwa unaotumika kule ni umwagiliaji ndugu yangu anasema Phillip.

Umwagiliaji ni asilimia 100% katika kilimo. Siamini, naendelea kumdadisi. Sasa, mbona nasikia kule ardhi ni mchanga mtupu? Ni kweli, anaendelea kueleza Mbuligwe, Wasyria hufanya kila linalowezekana kupata maji. Huchimba visima virefu na pia hutumia maji ya mito inayokatiza katika ardhi yao. Serikali ilichofanya ni kutengeneza miundo mbinu ya umwagiliaji na kuendesha utafiti wa hali ya juu katika umwagiliaji.

Syria hutumia sana "Drip Irrigation" na "Sprinklers." Kwa njia hii wanatumia maji kufuatana na mahitaji ya mmea na maji hayapotei bure na kwakweli wakulima wanasema inalipa. Bila umwagiliaji, Syria isingeweza kuendesha kilimo.

Ndiyo, sasa wanalima mazao gani? Naendelea kumhoji. Aah Banzi kule kunastawi mazao mengi tu. Mbogamboga, ngano, matunda na hata mahindi. Lakini zao la chakula Syria ni ngano. Banzi, tikitimaji la Syria ni tamu utafikiri limewekwa asali anamalizia Mbuligwe.

Ndiyo, mtaalamu ndiyo huyo, amerudi toka Syria, amenieleza kuwa amejifunza mengi tena si kwa kuona tu au masomo ya nadharia, mafunzo yaliendeshwa kwa vitendo pia. Mbuligwe amerudi tumtumie kwenye utaalamu wa umwagiliaji.

Nilishawahi kusoma moja ya makala za Padri Privatus Karugendo (Kwa kweli huwa nasoma sana makala zake) anayeandikia gazeti la Rai. Katika makala hiyo, Karugendo anahoji, hivi kweli tumeshindwa kutumia vyanjo vyetu vya maji kwa umwagiliaji? Nafikiri vipaumbele vyetu vina walakini. Tujifunze basi kutoka Syria- 100 mm za mvua kwa mwaka, wanajitosheleza kwa chakula na "Tikitimaji ni tamu sana."

Wednesday, December 13, 2006

BANGO LA PAROKIA YA MAKUBURI CHA MDORI!

Jumapili iliyopita nilitembelea eneo la "External" kule Mabibo sehemu inayojulikana kwa jina la Makuburi hapa jijini Dar Es Salaam. Kwa bahati nilipita karibu kabisa na Kanisa Katoliki la Makuburi(Enuerete Mwenye Heri- Mtanisahihisha wasomaji).

Kilichonishangaza, kwanza si rahisi kufahamu kuwa hilo ndilo Kanisa Katoliki la Makuburi kama nilivyoandika hapo juu. Kuna maandishi madogo sana ambayo ukipita kwa mbali hayawezi kusomeka halafu yameandikwa hovyo hovyo tu. Hayapendezi! Lakini karibu na maandishi hayo kuna maandishi makubwa kwenye ukuta yanayosomeka kuwa Computer Training Centre. Sasa nikajiuliza hapa shughuli kubwa ni training au kuabudu?

Waumini wa Makuburi, Katekesta, Paroko nawaulizeni hivi kweli mmeshindwa kuandika bango linaloonyesha Parokia yenu? Nafahamu Makuburi ni moja ya Parokia ambazo mnatoa sadaka kwa wingi siku za dominika, mavuno na michango mingine. Hivi Bango kwenu si muhimu? Aaa jamani andikeni bango jingine zuri lenye herufi za kusomeka. Tena msimike sehemu zile muhimu kama vile kwenye vituo vya "External" na "Garage" barabara ya Mandela na pale kanisani penyewe. Nafikiri mtafanya hivyo kabla ya Christmass. Nitapita tena, na kama bado nitaandika mbado!

EL SAEDY BUS MNABOA KINOMA!

Kwa wale waliopata bahati ya kusafiri kwenda Kilosa mkoani Morogoro si rahisi kulikwepa bus la EL-SAEDY.

Mwezi uliopita nilisafiri kwenda Ilonga Kilosa kuhudhuria harusi ya rafiki yangu Alphonce Kadeng'uka (Hongera sana KADE!). Baada ya kuanganisha mabus mawili hadi kufika Ilonga, bus la mwisho nilililopanda lilikuwa ni la El- SAEDY kubwa.

Nasema mnaboa kinoma, kwanza kondakta alinipa ticket ambayo haikuonyesha mmiliki wa Bus na namba ya gari. Lakini nilimezea tu mradi kufika.Hata nauli natumaini walinilangua, sawa tu. Lakini nilipoangalia karibu namlango nikakuta maandishi "SitAfu Kiti"(Ikiwa na maana ya Staff Seat) halafu amechanganya herufi kubwa na ndogo. Lakini mmiliki anaona ni sawa na abiria nao hivyo hivyo, traffic hivyo hivyo! Kweli mnaboa. Si ingeandikwa tu kwa kiswahili kuwa ni kiti cha mfanyakazi. Hata namba za viti zimeandikwa hovyo hovyo (kichefu chefu). Kumbukeni gari hilo limenunuliwa kwa mamilioni ya shilingi kwanini mnalichezea chezea hovyo. Rekebisheni haraka. Noma wazee

TICKETS ZA DALADALA TUNALIWA

Nafikiri wengi wetu tuishio hapa Dar usafiri wetu unategemea zaidi magari ya abiria yajulikanayo kama Daladala. Unaposafiri kwenye gari hilo unatakiwa upewe ticket inayoonyesha kiasi cha nauli kwa safari yako namba ya gari, mmiliki wa gari na tarehe ya kusafiri.

Wamiliki wa magari hayo wengi hutoa ticket hizo lakini cha kushangaza ticket hizo ni vipande vya karatasi vilivyokwishatumika kwa shughuli nyingine. Utakuta umepata ticket lakini nyuma inaonyesha mshahara wa mtu au mambo mengine kabisa ambayo hayana uhusiano na usafiri.

Hivi kweli wanaomiliki magari hayo wanafahamu maana ya ticket? Je, SUMTRA wanakagua ticket hizo? Ushauri wangu ni kwamba ticket zote za Daladala ziwe na "format" moja na kuwe na rangi tofauti kwa njia tofauti. Ikiwezekana ziwe na alama ya kuingia au kutoka kwenye kituo kilichopangiwa. Huu ndiyo ustaarabu au mpangilio mzuri. Ninakerwa sana nipolipa nauli yangu nakupewa karatasi isiyo namaana lakini naambiwa eti ni ticket!

Tuesday, December 12, 2006

HIVI NI KWELI MIAKA 45 YA UHURU SEKTA YA KILIMO HAIJAFANYA LOLOTE?

Siamini kuwa miaka 45 tangu tupate UHURU wetu hakuna mafanikio kwenye sekta ya kilimo. Mafanikio yametajwa tu kwenye Elimu, Ujenzi wa Barabara kwa sababu ni rahisi kupima! Tusiwe wavivu jamani. Kweli hakuna viashiria kwenye sekta ya kilimo vinavyoonyesha mafanikio?

Imekuwa ni desturi sasa kuwa kila inapotayarishwa taarifa ya nchi hasa inapohusu mambo chanya, sekta ya Kilimo (mazao na mifugo) haimo. Ikumbukwe kuwa sekta hii inaajiri asilimia 80 ya watanzania na kulisha asilimia 100 ya watanzania sasa inawezekana vipi kutokuwa na mafanikio.

Kuna tatizo. Tatizo lipo kwa wale wanaokusanya taarifa na kuzitayarisha. Huenda hawajishughulishi kuweza kufahamu Kilimo imefanya nini. Mimi nina uhakika kuwa Kilimo imefanya mambo mengi kwenye masuala ya utafiti, umwagiliaji na mafunzo ukilinganisha kabla ya kupata uhuru. Hata uzalishaji umeongezeka pia kwa baadhi ya mazao na kuna mazao ambayo sasa yana umuhimu mkubwa katika taifa kuliko ilivyokuwa hapo awali(Kabla ya UHURU) uzalishaji wa maua ambao umeliingizia taifa fedha nyingi za kigeni. Lakini waliomwandikia Rais wetu mafanikio ya nchi miaka 45 baada ya UHURU wamepuuza hayo. Nchi imewekeza fedha nyingi sana kwenye sekta hiyo haiwezekanai kutokuwa na mafanikio. Unapozungumzia vyuo vikuu. Kwanini usiseme kuwa kuna Chuo Kikuu cha Sokoine ambacho kinatoa taaluma za sayansi ya kilimo ambapo kabla ya UHURU hatukuwa nacho. Huko unaweza kupata wataalamu wa Kilimo waliozalishwa na chuo hicho ambao wanafanya kazi ndani na nje ya nchi. Je, hayo siyo mafanikio ya nchi katika sekta ya Kilimo? Kuna mengi. Tusiwe wavivu katika kutayarisha taarifa.

MTOTO AMEZALIWA - nolema.blogspot.com

Mtoto amezaliwa leo tarehe 12/12/2006. Mtoto huyu anaitwa "BABA WA SHIRIKISHI"
Mzazi wa mtoto huyu ni Orgenness Lema. Karibu sana mtoto kwenye ulimwengu wa Blog. Kuna kaka yako "Banzi wa Moro" aliyekutangulia mwezi mmoja uliopita. Kuna kaka zako wakubwa kama vile, Ndesanjo Macha, Michuzi, Mjengwa, Jeff, Mongi na wengine wengi waone watakutunza.

Karibu sana

Thursday, December 7, 2006

HATUJAMFIKIA MKULIMA -WASSIRA

Waziri wa Kilimo Chakula na Ushirika Mh. Stephen Wassira amesema bayana kuwa wafanyakazi wa kilimo bado hawajamfikia mkulima. Mh.Wassira aliyasema hayo alipokutana kwa mara ya kwanza na wafanyakazi wa Wizara hiyo walioko Makao Makuu - Temeke Veterinary, tarehe 1/12/2006, Ijumaa.

Akiongea na wafanyakazi hao kwa muda usiozidi dakika 15. Waziri Wassira alisema kuwa, Wizara ina majukumu makuu mawili (1). Inatoa ajira kwa asilimia 80 ya Watanzania (2). Inawajibika kuhakikisha kuwa asilimia 100 ya watanzania wanapata chakula cha kutosha wakati wote.

Waziri alitoa changamoto kwa wafanyakazi hao kwa
- kumfikia mkulima kijijini ili aweze kupata mapato halisi kutokana na kilimo
- kufanya kila linalowezekana ili kuhakikisha kuwa watanzania wanapata chakula.

Aliwashauri wafanyakazi wote kuchapa kazi na kusema kuwa hakuna kazi isiyokuwa na maana na mshahara anaolipwa kwa kila mfanyakazi ni gharama kwa hiyo ni lazima kufanya kazi kwa pamoja ili Wizara iweze kutimiza malengo yake.

Kabla ya kuanza mazungumzo na wafanyakazi hao, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Mh. Peniel Lyimo alitoa taarifa kwa Waziri kuwa, Wizara ina jumla ya wafanyakazi 2,600. Kati ya hao wafanyakazi 1,165 wako kwenye Idara ya Utafiti na Mafunzo. Ni wafanyakazi 400 tu ndiyo wanaofanya kazi Makao Makuu ya Wizara.

Kikao hicho cha muda Mfupi kilihudhuriwa pia na Naibu Waziri wa Kilimo na Chakula Mh. Dr. David Matayo David na Naibu Katibu Mkuu Mh. Mohamed Muya.

Hii ni mara ya tatu kwa Waziri Wassira kuiongoza wizara hiyo. Mwaka 1973 aliteuliwa kuwa Naibu Waziri , Wizara ya Kilimo akiwa na umri wa miaka 27. Mwaka 1989 alirudi tena kwenye Wizara hiyo akiwa Waziri na mwaka huu mwezi Oktoba Rais Jakaya Mrisho Kikwete amempa jukumu la kuiongoza wizara hiyo.

KUPASISHA MBEGU MPYA (SEED RELEASE)

Ndiyo, kuna mdau mmoja amekuja na hoja kuwa kwanini wataalamu wa kilimo huwa wanasema kuwa wametoa mbegu mpya lakini wakulima wanalalamika kuwa mbegu hizo hazipatikani. Mdau huyu alikuwa na maana ya "seed release" akitafsiri kwa kiswahili kuwa ni kutoa mbegu. Ukweli ni kwamba hapa mbegu inapasishwa tayari kwa matumizi kisheria.

Mchakato wa uzalishaji mbegu za mazao kwa kweli unatumia muda mwingi, utaalamu mbalimbali na nyenzo mbalimbali ambazo waliobobea huchukua miaka mingi kufuzu utaalamu huo na wakisha fuzu wanajulikana kuwa wataalamu wazalishaji vipando (plant breeders). Kabla mbegu haijatolewa kutumika, hufanyiwa tathmini na wataalamu, wakulima, wafanya biashara na walaji. Ikionekana inafaa ndiyo inapasishwa.

Ni tofauti kidogo na bidhaa kama vile vinywaji baridi- Kampuni ya Cocacola inapotoa aina mpya ya kinywaji wakati huo inakuwa tayari katika soko. Kwa mbegu za mazao si hivyo. Wanapopasisha mbegu ina maana kuwa mkulima anaweza kuitumia mbegu hiyo kiuzalishaji. Kabla haijapasishwa kama itatumika basi mtaalamu atakuwa hana makosa kama itagundulika kuwa ina hitilafu fulani. Hivyo ndivyo nilivyoelezwa na wataalamu wazalishaji vipando.

TUANGALIE UPYA MAZAO YA BIASHARA


Huku tukiwa tunapata chakula cha mchana hapa Temeke Veterinary (Kwenye makao makuu ya wizara kuu mbili zinazowahudumia wakulima kwa pamoja). Mjadala ulizuka kati yetu wataalamu. Mmoja wetu aliyetembelea wilaya ya Mombo hivi karibuni, alishtushwa na maelezo ya moja ya viongozi wa wilaya hiyo kuwa hawana zao la biashara. Eeh, hamna zao la biashara kabisa? Aliuliza mtaalamu- Ndiyo, alijibiwa. Zamani tulikuwa na zao la mkonge lakini sasa mkonge hauna thamani tena. Tunategemea sana kuuza mpunga huko Moshi, Arusha, Tanga, Morogoro na hata Mombasa, Kenya.
Mtaalamu akahoji tena, mbona mlisema kuwa hamna zao la biashara? Kimya, wakabaki kuchekacheka tu. Na kweli, mtaalamu huyu alitueleza kuwa alipotembelea kwa wanakijiji karibu kila nyumba alikuta nje kumuanikwa mpunga!

Hivi ndivyo tulivyofundishwa na tunavyoendelea kukariri kuwa mazao ya baishara ni pamba, mkonge, kahawa, chai, tumbaku, miwa n.k. hata kama kwenu hamlimi na hujawahi kulitia macho.
Mmoja kati ya wataalamu waliokuwa pale alikiri kwa kusema kuwa hakuwahi kuuona mmea wa kahawa (mbuni) hadi alipoanza kusafiri nje ya kijiji chao.

Baada ya kusema hayo. Labda turudi kwenye mada. Hivi zao la biashara ni lipi? Ukiuza muhogo ukapata fedha siyo zao la biashara kwako? Ukiuza nyanya na ukapata fedha zao hilo siyo la biashara jamani?

Mtazamo wa wale waliotutawala (wakoloni), nadhani ulikuwa ni kwa mazao yale ambayo yaliweza kuuzwa nje kwa faida yao ndiyo waliyoyakubali kuwa mazao ya biashara lakini ndizi hata! Wakati Wachagga, Wahaya, Wanyakyusa wamesomesha watoto kwa biashara ya ndizi sasa haingii akilini mwao kusema kuwa ndizi siyo zao la biashara.
Hata kwenye mfumo wetu wa elimu, kama itatokea swali kwenye mtihani kuwa, chagua zao la biashara kati ya hayo yafuatayo basi kama ndizi lipo na mtoto wa Tukuyu akachagua hilo badala ya pamba atapata bonge la kosa! na pengine kumkosesha kuingia kidato cha kwanza.


Kuna haja ya kuangalia kwa makini mazao ya biashara. Au pengine tusiite ya biashara bali tuyaite mazao yanaoyoingizia taifa fedha za kigeni je seara zetu zinasemaje? Wataalamu wameliona hili.

Tuesday, December 5, 2006

KILIMO NI SAYANSI !

Kazi ya utafiti inafanyika katika vituo vya utafiti na kwenye mashamba ya wakulima. Pichani jopo la wataalamu wa kilimo kutoka Makao Makuu ya Utafiti Dar Es Salaam na kutoka Kanda ya Nyanda za Juu Kusini wakipelemba na kutathmini utafiti zao la mahindi katika kituo cha Utafiti wa Kilimo, Kifyulilo, Mufindi, Iringa (Picha kwa hisani ya ARI-Uyole, Mbeya -Juni, 2006)

TUWE MAKINI KATIKA KUTOA HUDUMA

Jana mchana nikiwa pale TAZARA-Station nikipata chakula cha mchana. Labda niseme wazi chips na mishkaki, nilibahatika kukaa meza moja na kijana mmoja mtanashati naye akisubiri kupata mlo. Kwa bahati mbaya huduma ilikuwa si nzuri. Ilichukua karibu dakika 30 kupatiwa nilichooagiza. Naye yule kijana aliagiza soda lakini sprite, jinsi alivyojibiwa na muhudumu inasikitisha. Basi hapo ndipo tulipoanza kujadili kama kweli wahudumu wale wanajua wanachokifanya. Lakini tulikuja kugundua kuwa wenzetu walioagiza ugali na wali huduma waliipata chapchap. Kumbe kwenye kibanda kimoja watoa huduma ni tofauti. Kuna anayemiliki kibanda cha chips na kuna anayemiliki "ubwabwa" Kwa kweli inasikitisha sana. Itakuwaje mtu usubiri chakula muda wa nusu saa wakati pale si hotelini?

Tatizo hili la utoaji huduma hapa Tanzania kwa kweli limeshakuwa kero. Unakwenda Benki kuweka fedha au kuchukua fedha huduma ni goigoi. Ukiuliza, majibu unayopata kwa kweli yanakatisha tamaa. Unakwenda kulipa bill ya umeme unakuta dirisha la kupokelea fedha limefungwa. Unaenda kununua nyanya sokoni, muuzaji anakufokea. Umeamua kupunzika na familia yako kwa kupata kinywaji, wahudumu baada ya kuona una familia hasa mke wako basi ndiyo kabisa umewafukuza wako kuleee. Jamani kwa mtindo huu kweli tutajiajiri? Inalipa kweli kwa biashara hii. Mtu anakuletea fedha, wewe unamkatisha tamaa. Eti unasubiri mteja aanze kuuliza badala ya wewe mtoa huduma kumkaribisha vizuri na kumwelekeza. Labda niwe muwazi kidogo, hapa Tanzania kama biashara inaendeshwa na wenzetu Wachagga utaona tofauti kubwa sana. Huduma nzuri. Kma ni mahali pa chakula patakuwa pasafi, wahudumu watatoa huduma nzuri na uzimamizi mzuri. (Nimekuja kutafuta pesa msee! Atakwambia Mchagga). Lakini waswahili ndiyo hivyo tena. Yule kijana alinieleza, kule Tanga ni balaa maana huduma zinatolewa taratiiibu hawana haraka (Wajaleo.......). Kama tunataka kujiajiri lazima tubadilike katika utoaji huduma lasivyo tutabadilishwa na fedha tutazikosana na tutabaki tulivyo . Kwa mwendo huu wa kusubiri chips dakika 30 mimi nimeshindwa!

Monday, December 4, 2006

ELIMU NI KIOO?

Leo asubuhi nilikwenda Mkuranga (Makao Makuu ya Wilaya). Katika pita pita zangu nilisoma kibao kinachoonyesha kuwa mahali hapo ni Shule ya Msingi Mkuranga. Lakini kama ilivyo ada ya vibao vyote vya aina hiyo hapa nchini havikosi kauli mbiu. Kauli mbiu ya Shule ya Msingi Mkuranga ni " ELIMU NI KIOO." Nashindwa kupata tafsiri nzuri ya kauli mbiu hii. Je, Elimu ni kama kioo ambacho hutumika kukupa muono wa kitu fulani? Au Elimu ni kitu cha kutunza kwa uangalifu kwani kikikuponyoka ni vigumu kurudi katika hali yake (kioo kikivunjika). Je ni kweli? Wasomaji nisaidieni.Nimeshasoma kauli mbiu nyingi ambazo kwa kweli hazijitoshelezi. Nyingine zinakuwa ndefu mno na kukosa maana nyingine hazina uhusiano wowote na hali halisi. Tuwe makini katika kuandika kauli mbiu!

Friday, December 1, 2006

NAJARIBU KUWA MWANA BLOG


Watanzania wenzangu na wote wanaofahamu lugha ya Kiswahili.

Nabisha hodi.

Ni hivi karibuni tu ndipo nimepata kuelewa blog ni nini. Nilikuwa nasikia blog blog! Lakini baada ya kusoma na kuona mambo mbalimbali kupitia blog mbalimbali. Nimeaona kwanini nisiingine kwenye mtandao wa wanablog? Bado mchanga katika teknolojia hii, lakini nimeipenda. Kwanza kabisa mimi napenda kutoa habari hasa kwa njia ya maandishi. Napenda watu wafahamu ninayoyafahamu mimi, niliyoona mimi na kuyajua mimi. Naomba mnielekeze. Asante Ndesanjo, asante Mjengwa, asante Michuzi, Jeff, Makene, Msaki, Mongi, Dada wa Ugogoni, Dada Chemi na wengine wengi. Tupashane habari na tuwapashe wengine.