Tuesday, July 29, 2008

Shughuli imeanza Mtongani-Mbagala

Makaravati yanazikwa ardhini, njia za mkato zinatengenezwa, nguzo mpya za umeme zinasimikwa. Kweli, awamu ya Pili ya ujenzi wa barabara ya Kilwa imeshaanza na mambo yanakwenda kwa kasi ya ajabu. Siku hizi kutoka kwa Aziz Ally hadi Mtongani ni kuteleza tu. Imebaki sehemu ndogo pale Mtoni Mtongani. Wananchi wanangojea maajabu wayaone ya kupitisha barabara pale darajani itakuwaje? Twasubiri tuwaone Kajima.

Shughuli imeanza Mtongani-Mbagala

Siku hizi

Wakulima hawazioni fursa zilizopo kubadili maisha yao


Baada ya kusafiri sehemu mbalimbali za nchi yetu nimebahatika kuona mengi mazuri na mabaya na kujifunza mengi hasa kwa sekta ya kilimo.



Wakulima wana fursa nyingi ya kujikwamua kiuchumi kupitia sekta hii iwapo fursa hizo zitatumiwa vizuri kwa mahali husika na wakati muafaka. Mazao ya aina mbalimbali yanayostawi hapa nchini yanaweza kupata soko la ndani na nje. Mifugo ya aina mbalimbali inayopatikana hapa nchini na inaweza kupata soko la ndani na la nje.



Mwezi mmoja uliopita nilikuwa nikifanya utafiti fulani na kutembelea kiwanda cha Chibuku hapa Dar Es Salaam na kuelezwa kuwa mtama na mahindi ni mali ghafi ya kutengeneza pombe ya chibuku. Muhogo unatumiwa kwa mahitaji ya chakula cha binadamu na mifugo, viwandani na kwenye maabara ya madawa. Soko la Korosho lipo ndani na nje ya nchi. Ukipita pale Kibaha, Ruvu korosho 10 za kukuaanga ni shilingi 500!



Machungwa sasa yanapatikana karibu mwaka mzima. Kwa sasa chungwa moja linauzwa kati ya shilingi 50 hadi mia moja hapa jijini Dar. Mbogamboga, matango na matunda ya aina mbalimbali soko lipo. Mchele nao hautafuti soko. Karibu kila mkoa una sifa ya kuzalisha mazao au mifugo zaidi ya aina moja.



Kinachotakiwa sasa ni kubadili mtazamo wetu kwenye kilimo. Lazima tufahamu kuwa kilimo si chakula tu ni biashara ni biashara pia na biashara ni pesa. Mkulima sasa atambulike, apatiwe fursa ya kupata mikopo kutoka taasisi za fedha zilizopo nchini ili ziweze kumsaidia katika kuzalisha. Kwani wakizalisha kwa wingi fedha hizo hurudi huko huko. Matokeo yake pande zote zinafaidika.

Monday, July 28, 2008

Wagani wa kilimo wapatiwe vitendea kazi

Huwezi kumuona mhasibu asiye na calculator, daktari na kipima mwili chake, dereva na gari lake, mchoma mahindi na jiko lake, mama/baba ntilie na sufuria zake.
Utamtambuaje afisa ugani wa kilimo asiye na kitendea kazi? Anashauri wakulima wapande mazao kwa nafasi zinazokubalika huku kipimio hana. Anashauri wapande mbegu ya mahindi ya TMV 1 yeye mwenyewe haijui. Anawashauri wakulima wampunga watumie mbolea ya kukuzia aina ya UREA yeye mwenyewe wala hajui inakopatikana. Ndiyo maana mbunge mmoja alikumbusha kwa kweli, wakatia umefika sasa wa kuhakikisha kuwa maafisa wagani wa kilimo wanapewa vitendea kazi. Ndipo hapo tutakapowaona wakichacharika kweli kweli na watu wakiwathamini kama wanavyomthamini daktari.

Mafuta si leo, lakini hili la chakula tunaweza sasa


Hatujui ni lini Tanzania tunaweza kuzalisha mafuta mengi na kuweza kujitosheleza kwa matumizi ya ndani na kuuza ziada. Lakini kwa chakula tunaweza hata mwaka huu tukijipanga sawasawa. Hili linawezekana iwapo mipango yetu itawekwa kwa kuweka kipaumbele katika uzalishaji wa chakula. Tanzania tunayo fursa kubwa zaidi katika kilimo. Tuna ardhi ya kutosha, tuna maji ya kutosha, wataalamu wa kutosha na wananchi wetu asilimia 80 wanategemea kilimo hivi kweli hili nalo hatulioni? Tunataka tuletewe programu ya kuzalisha chakula kutoka World Bank? Hakika hili la kuzalisha chakula tunaweza sasa.

Tuwe tayari kutoa - Asema Padri Ngowi

Padri Ngowi wa Parokia ya Mkuranga amewaasa waumini wa Parokia ya Vikindu jimbo Kuu la Dar Es Salaam kuwa wawe wepesi na tayari kutoa kuliko kupokea. Padri Ngowi aliyasema hayo katika mahubiri yake aliyoyatoa Jumapili ya tarehe 27 Parokiani hapo.

Alisikitika kwa kusema kuwa, waumini Wakatoliki wamezoweshwa kupewa kuliko kutoa. Wakati umefika sasa wakuendesha Kanisa wenyewe bila ya kuwategemea wazungu na wamisionari wa kigeni. Watawa wanatakiwa kupata mahitaji muhimu kama vile chakula, mavazi, malazi na usafiri ili weze kutimiza wajibu wao wa kutoa huduma ya kiroho. Kwa hiyo ni wajibu wa waamuni kutoa sadaka na kulipa zaka kama inavyotakiwa na kanisa.

Akihubiri bila kuchoka, huku akirandaranda ndani ya kanisa na kuwahamisisha waumini na hatimaye kufanya harambee ya mavuno iliyoweza kukusanya zaidi ya shilingi 1,000,000 (fedha taslimu na ahadi) kwa ajili ya tegemeza parokia. Waumini walichangia kiwango cha sh 500/= hadi 150,000/=

Kwa hili la kuiogopa Simba, Yanga hawana la kusingizia

Kitendo cha Klabu Bingwa ya Soka ya Tanzania kwa mwaka 2008 - Dar Young Africans kushindwa kufika uwanjani kupambana na watani wao wa jadi Simba Sports Club ya Dar Es laam siku ya Jumapili katika pambano la kumpata mshindi wa tatu wa kombe la Kagame limeitia doa kubwa timu hiyo, Dar Es Salaam na Tanzania nzima.

Sababu za madai ya malipo ya ziada hayana msingi. Yanga kanuni za mashindano hayo wanayafahamu, iweje leo kusisitiza walipwe fedha zaidi kuliko hata anachapata mshindi wa mashindano hayo, ni kichekesho!

Dar Young Africans wamefanya usajili mzuri na wa gharama mwaka huu, wanamakocha watatu wakigeni tena wazungu! Hata golikipa mzungu pia amesajiliwa yanga, iweje leo kukacha mechi hiyo? Mi sielewi, hata Nicholaus Musonye ameshindwa kuwaelewa Yanga na hata kuwaita "wahaini wa CECAFA." Tusubiri maamuzi ya CECAFA kwa tukio hilo.

Thursday, July 24, 2008

Tuwatambue wakulima wetu

Sawa kabisa, inavyoelekea, bado hatujawatambua wakulima wetu. Ni kina nani? wangapi? wako wapi? na wanahitaji nini?wanafanya nini kwa sasa? wanafanyaje? kwanini wanafanya hivyo? Hayo ni maswali ya msingi kabisa yanayotakiwa kufahamika kutoka kwa wakulima wetu ili tuweze kuwatambua.

Tusipowatambua, mipango ya kuwapatia pembejeo za kilimo itakuwa ni ya mashaka, mipango ya kuwatafutia masoko utakuwa ni wa kubuni tu, teknolojia za kilimo zinazobuniwa kumsaidia mkulima katika kuboresha uzalishaji zitakuwa ni za watafiti tu ni si mahitaji ya mkulima, tunaweza kununua matrekta na kuyasambaza kila mkoa kumbe si kila mkoa unahitaji matrekta idadi sawa, tunaweza kumwaga mabilioni kwa kutoa mikopo kwa wakulima kumbe wakulima hawajui jinsi ya kutumia mikopo hiyo na pengine mikopo inaweza kutolewa wakati usio mwafaka kwa kilimo.

Kwahiyo basi suala la kuwatambua wakulima wetu ni la msingi kama baadhi ya wabunge walivyochangia kwenye hotuba ya Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika mwaka 2008/09

"Mapinduzi ni Vita"

Mara nyingi neno Mapinduzi hutumiwa sana na watu wengi wanapotaka kufanya mabadiliko ya kitu fulani au jambo fulani. Watu wanapoingia kwenye mapambano ya aina yoyote hawachelei kusema kuwa tuko vitani. Maneno haya ukiyaunganisha na "ni" unapata sentensi inayosema "Mapinduzi ni Vita."

Nimeshasikia mara nyingi kutoka kwa viongozi wetu hapa nchini kuwa tunataka kufanya mapinduzi katika kilimo. Je, wanafahamu kuwa mapinduzi ni vita? Ni nilazima kujiandaa barabara, kwenye vita hakuna kurudi nyuma hadi ushindi upatikane. Makamanda je wapo? Makomandoo wa kilimo wapo? Ni kina nani hao? Tusipotambua hilo mapinduzi ya kilimo ni ndoto.

Je, wananchi wanafahamu maana hasa ya Ushirika

Binafsi huwa napenda kumsikiliza Mbunge wa Kibakwe Mh.Simbachawene anavyofafanua mambo au kujenga hoja. Na hivi karibuni katika Bunge la Bajeti linaloendelea hivi sasa mjini Dodoma, Mh.Simbachawene alieleza kuwa kimsingi "Ushirika ni kuunganisha nguvu ndogondogo ili kuweza kutekekeleza jambo kubwa." Kama tunafahamu maneno hayo ya msingi aliyosema Mh. Mbunge basi tunaweza kupiga hatua kubwa katika kujenga ushirika ambao utatuletea maendeleo. Asante sana Mh.Simbachawene.

FM ACADEMIA FUNGA KAZI

Kama u mpenzi wa muziki wa dansi, naomba kukuuliza swali moja. Je, umeshawahi kuhudhuria show moja ya bendi ya "FM ACADEMIA?" Kama hapana, basi ukiwa Dar fanya hamu siku moja uwatembelee pale "nyumbani kwao" Kijiji cha Makumbusho ili upate muziki mzito na show kamambe kutoka kwa "FM ACADEMIA."

Uongo dhambi, vijana hao wanajituma kweli wanapokuwa jukwaani. Kila mwenye kipaji kwenye bendi hiyo hutumia kipaji chake barabara kuwaburudisha wateja wao na kweli thamani ya fedhaa mbayo ni kiingilio (value for money) unaipata ukiingia kwenye show ya"FM ACADEMIA."

Chakufurahisha ni kwamba wanamuziki hawa karibu wote wanaweza kutumia vyombo vya muziki, kuimba na kucheza. Akina dada wa show ndo usiseme kwa kweli wanakonga nyoyo za washabiki.

Siandiki haya kwa ushabiki tu bali mimi mwenyewe yapata mwezi mmoja uliopita, Jumamosi moja marafiki zangu walinipa "offer" mimi na mke wangu kwenda kuwaona wanamuziki hao. Sijapata kwenda dansi karibu miaka 15 sasa lakini siku hiyo nilirudisha ari ya kupenda muziki wa dansi na sasa nina usongo wa kuwaona "AKUDO IMPACT" nasikia nao ni mwisho wa njia. Wanamuziki wetu wana la kujifunza kutoka "FM ACADEMIA."

Ni kweli "FM ACADEMIA" funga kazi na siku hiyo nilicheza nakuimba "Songo na matembele!" Na kwakweli ilikuwa siku nzuri sana kwani ni siku ambayo Taifa Stars ilitoka sare na Cameroon ndani ya uwanja wa Taifa. Ndipo Nyoshi "El Sadat" alipotuimbisha "Taifa Stars Oyee!"

Uhariri wa kursasa gazeti la Mwananchi ni wa wasiwasi

Kwa wale wasomaji wa magazeti ya kila siku, sijui kama mlipata bahati ya kusoma gazeti la Mwananchi la tarehe 13 Julai 2008. Gazeti hili lilikuwa na kasoro kadhaa katika upangaji wa kurasa za magazeti na hasa tarehe. Ukurasa wa 28 ulisomeka Juni, 22 na ukurasa wa 26 ulisomeka Juni 14, 2008. Lakini ukweli ni kwamba gazeti hilo lilikuwa ni la Jumapili tarehe 13 Julai 2008. Ndiyo maana nasema uhariri wa gazeti la mwananchi ni wa mashaka. Inaelekea ni tatizo la "cut and paste" ambao wasanifu wa kurasa hawakugundua, naomba muwe makini.

Monday, July 21, 2008

Hata Kisemvule wanafahamu Shamba Darasa


Jana Jumapili tarehe 20/06/2008 ilikuwa siku muhimu sana katika kumbukumbu ya maisha yangu. Jana, kwa mara ya kwanza niliweza kuhudhuria Mkutano Mkuu wa Kijiji ninachoishi, kijiji cha Kisemvule kilichopo wilaya ya Mkuranga Mkoa wa Pwani. Kilomita 27 kutoka mahali ninapofanyia kazi jijini Dar Es Salaam.


Agenda kuu muhimu katika kikao hicho zilikuwa ni kuwakilisha utekelezaji wa bajeti ya kijiji kwa mwaka 2007/08 na mapendekezo ya Bajeti ya Kijiji kwa mwaka 2008/09. Nilichofurahishwa ni kuona jinsi gani mawasilisho hayo yalivyowasilishwa vizuri tena kwa kitaalamu na jinsi wanakijiji walivyozijadili taarifa hizo kwa ufasaha na kupatiwa ufumbuzi.


Nilifurahi zaidi nilipoona nguvu ya wanakijiji pale walipoweka kipaumbele cha kununua madawawati ya shule ya msingi Kisemvule kwanza baada ya kupata taarifa kuwa shule ina madawati 34 tu. Walisema kuwa uendelezaji wa ujenzi wa ofisi ya kijiji usubiri kwanza.


Jingine lililojitokeza ni pale mwanakijiji mmoja alipouliza nini maana ya shamba darasa baada ya kusikia kwenye bajeti ya mwaka 2008/09 sekta ya kilimo kuwa moja ya shughuli zitakazofanywa na kijiji ni pamoja na kuwa na shamba darasa. Mwanakijiji huyu alipata maelezo ya ufasaha kutoka kwa mwanakijiji mwenzake kuhusu shamba darasa. Pamoja na kwamba mimi nafahamu vizuri kuhusu shamba darasa, maelezo yaliyotolewa na mwanakijiji yule yalikuwa sahihi ndiyo maana nasema hata Kisemvule wanafahamu Shamba Darasa. Kazi kwenu wataalamu wa Kilimo pelekeni teknolojia.

Friday, July 11, 2008

Hakika tunaweza kutumia umeme wa jua

Juzi niliona picha moja nzuri kwenye gazeti la kila siku la Kiingereza "DAILY NEWS" yenye maelezo - Wavietnam wakushughulikia kuweka Panel za Solar kwa ajili ya umeme vijijini.
Niliisoma makala ile kwa makini sana. Nilichogundua ni kwamba tayari Wavietnam wameshaona umuhimu na uwezekano wa kutumia umeme wa mionzi ya jua ili kutoa nishati huko vijijini hata kwa kuanzia kutoa mwanga tu.

Jumapili iliyopita katika pitapita yangu pale Kariakoo karibu kabisa na mzunguko wa barabara ya Uhuru na Msimbazi niliona duka moja linauza vifaa vya umeme wa jua. Nilipouliza niliambiwa vinauzwa kwa jumla ya shilingi 225,000/= na vinaweza kuwasha umeme wa taa nne ndogo. Kumbe inawezekana!

Inawezekana umeme huu ukaanza kasambazwa vijijini hata kwa njia ya mkopo. Laki 2 ni sawa na kuuza magunia 4 ya mpunga. je haiwezekani kufunga "solar" kwa wakulima wa mpunga, kahawa, chai, mahindi, maharage, ndizi, viazi. Tatizo hatuna mkakati na hatutaki kusoma wataalamu wetu wanashauri nini kuhusu nishati. Kwa kifupi watu ni wabinafsi na hatutaki kuwasaidia wenzetu walioko vijijini.

Tuanze sasa kutumia umeme wa jua. Uwezekano upo na ni rahisi. Vinginevyo tutasoma asilimia 90 ya Wavietnam sasa wanapata umeme. Wameshatupita kwenye kilimo na viwanda sasa wanaangalia mambo ya nishati. Sisi tunabaki kusema aah! Wote tulikuwa masikini miaka ya sabini. Haisaidii kitu.

Zimbabwe ni sawa na Marekani tu

Bob Mugabe amewapasha Wamarekani na Waingereza kuwa wasipende kuingilia mambo ya ndani ya nchi yake. Marekani ni kama Zimbabwe. Kinachomkera BOB ni Wamerekani na Waingereza kulishupalia suala la Zimbabwe ili wananchi wa Zimbabwe wamuone BOB hafai. Tumpe nafasi Mugabe aseme.

"Conductor Perhaps!"

Leo asubuhi wakati nakuja kazini kwenye bus nililopanda nilimkuta "conductor perhaps" mmoja. Kwanini nasema hivyo. Kondakta huyo alikuwa wa ajabu kweli lugha chafu ya matusi, amevaa hovyo hovyo tu. Nina maana hana vazi rasmi. Lakini alionekana kama mpiga debe tu huku akiwa amening'inia mlangoni kazi yake ni kutoa amri-Eeeh mwanangu rudi nyuma! Alifoka.Hiyo ndiyo ilikuwa kazi yake na maneno machafu kwa abiria.

Abiria wa bus lile nami nikiwa mmoja wapo hatukuweza kumvumilia hata kidogo. Tukaanza kumuelimisha.
  • Kwanza kijana hatukutambui
  • Huna vazi rasmi
  • Hakuna kazi unayoifanya hapo mlangoni
  • Lugha yako ya matusi inatukera

Tunachoweza kukifanya ni kukuwasilisha kwa Kamanda Kova akushughulikie.

Baada ya kupashwa nafikiri alitambua makosa yake na aliufyata. Huyo ndiye "Conductor Perhaps."

Mpiga debe huyu!

Leo asubuhi wakati nakuja kazini kwenye bus nililopanda

Wednesday, July 9, 2008

Mtongani hadi Kariakoo sasa dakika 10

Ile adha, karaha na kashkash ya usafiri barabara ya Kilwa inatarajiwa kupungua kwa kiasi kikubwa baada ya mkandarasi wa Kampuni ya Kajima kukaribia kumaliza kujenga kipande cha barabara kutoka Bandarini hadi Mtoni Mtongani.

Jumapili iliyopita nilitumia dakika 8 kutoka Mtongani hadi Kariakoo. Sehemu kubwa ya barabara imeshakamilika kilichobaki ni nakshi nakshi pamoja na kipande kidogo unapokaribia Mtongani penyewe. Mkeka umeshamwagwa kwa sehemu kubwa ya barabara.

Dalili za kuanza awamu ya pili zimeanza kuonekana. Tayari pale Mbagala Zakhem kambi ya ujenzi inajengwa na sehemu kubwa imeshaanza kusafishwa.Tusubiri na tuone adha ya usafiri Mbagala itakuwa historia, wawekezaji karibuni Mbagala na Vikindu!

Bado sijamuona mfungaji Taifa Stars

Mimi sijui kama tunaye mfungaji wa kuaminika kwenye timu yetu ya Taifa Stars. Magoli yote yanayopatikana yanapatikana kwa bahati tu. Leo kafunga Abdi Kassim, kesho Emmanuel Gabriel, kesho kutwa Danny Mrwanda. Kwa hakika hatuna mfungaji!

Miaka ya sabini hadi tisini tulikuwa na wafungaji wakuaminika kama akina Edward Chumila (Marehemu), Abdallah Kibaden, Gibson Sembuli (Marehemu), Kitwana Manara Popat, Jumanne Masumenti (Marehemu), Peter Tino, Zamoyoni Mogella, Mohamed Salim na wengineo wengi. Hata wakishika mpira unategemea goli litapatikana. Walijua kujipanga vizuri ili wapate goli. Wakati kona inapigwa ilikuwa ni lazima umchunge sana Kitwana Popat Manara au Jumanne Masumenti na walijua kufunga kwa kichwa, mpira unaweza kudunda chini kwanza kabla ya kuingia au kuupeleka pembeni kabisa mwa goli.

Siku hizi hata tukipata kona 10 ni bure. Wachezaji wetu wa mbele si watafutaji wa magoli. Hivi kweli hatuwezi kuwapata wafungaji wazuri wa magoli kama ilivyokuwa zamani? Bila ya kufanya hivyo hakuna maajabu.

Tunategemea kuvuna kutoka misitu ya asili

Sasa imebainika kuwa misitu yetu ya asili ni mali.
Hivi karibuni niliweza kuzungumza na baadhi ya watafiti wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo-Tumbi, Tabora kuhusu utafiti wa Kilimo Misitu. Nilichojifunza ni kwamba misitu yetu ya asili ikitumiwa vizuri inaweza kabisa kuwasaidia wakulima wanaoishi karibu na misitu hiyo kuboresha maisha yao kwa mazao yanayotokana na misitu hiyo.

Misitu yetu kama ilivyo kwa vijiji vyetu ni vyanzo vya kuni lakini pia hutoa malisho ya mifugo yetu, hutoa mbao kwa ajili ya ujenzi na samani, hurutubisha ardhi, hutoa dawa na matunda pori ambayo yakitayarishwa yanaweza kutumika kwa kutengeneza mvinyo, jamu na pombe aina ya amarula.

Watafiti wa kituo hicho wameshaanza kufanya utafiti wa miti aina mbalimbali na baadhi ya teknolojia zimeshapelekwa kwa wakulima na kupokelewa vizuri. Hivyo tunategemea kuvuna kutoka kwenye misitu ya asili.

Matunda ya Kutengeneza Amarula yanapatikana Tabora

Kile kinywaji maarufu cha Amarula kinachotengenezwa Afrika ya Kusini na kupendwa sana na wanawake hapa Tanzania, matunda yake yanapatikana kwa wingi kwenye misitu ya Miombo huko Tabora. Watafiti wa kituo cha Utafiti wa Kilimo Tumbi, Tabora wamegundua. Matunda hayo yapo kwa wingi ingawa yanapatikana msituni.

Iwapo utafiti wa kina utafanyika, miti hiyo inaweza kuoteshwa na kuzalishwa kwa wingi hivyo kutoa matunda ya kutosha na kuwezesha wakulima kujiongezea kipato kwa kuuza matunda hayo ya Amarula.

Fursa ipo kwenye Kilimo Misitu

Timu ya Kupelemba na Kutathmini shughuli za Utafiti Kanda ya Magharibi imebaini kuwa kuna fursa kubwa kwa wasomi asilia kuendeleza utafiti wa Kilimo Misitu hadi kufikia ngazi ya shahada za uzamili (MSc) na Uzamivu (PhD).

Fursa hii imebainika baada ya kuona kuwa kuna mazao asilia mengi kwenye mistu yetu ya asili ya miombo kanda ya Magharibi. Misitu hii ina toa matunda mengi ya asili ambayo yakifanyiwa utafiti yanaweza kutoa mazao mbalimbali ambayo yatasaidia kuchangia kipato cha familia kwa wakulima wetu.

Kinachotakiwa kwa sasa ni Serikali kuhakikisha kuwa programu hiyo inapata fedha za kutosha, usafiri wa kuaminika, na wataalamu ili iweze kuendeleza utafiti uliokwisha anzishwa na kuleta mafanikio lakini kutokana na ufinyu wa bajeti utafiti huo unaanza kurudi nyuma.

ARI -Tumbi-TABORA-Hazina ya Kilimo Misitu

Utafiti wa Kilimo nchini umegawanywa kwenye kanda saba nazo ni Kati, Mashariki, Ziwa, Kaskazini, Kusini, Nyanda za Juu Kusini na Magharibi.

Kituo cha Utafiti wa Kilimo Tumbi -Tabora (ARI-Tumbi) kanda ya Magharibi ndicho chenye jukumu la kushughulikia utafiti wa Kilimo Misitu (Agro Forestry).

Wengi wetu hatufahamu Kilimo Miti ni nini? Mtafiti wa Kilimo Misitu kutoka Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika Bw. N.Lema anaeleza kuwa watu wengi wanachanganya Kilimo Mseto (Mixed Farming ) na Kilimo Misitu (Agroforestry). Kilimo Misitu ni kilimo kinachohusu ustawishaji wa mimea kwa ajili ya kuni malisho ya wanyama, kurutubisha ardhi, ujenzi, matunda na mimea ya dawa.

Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tumbi kwa muda mrefu imekuwa ikifanya utafiti wa Kilimo Misitu kwa kushirikiana na ICRAF. Utafiti umekwenda mbali zaidi hadi kubaini miti ya matunda pori na dawa na aina mbalimbali za miti imeshakusanywa ndani na nje ya Tanzania.

Thursday, July 3, 2008

Utemi wa akina Fundikira bado unaenziwa Tabora

Kando kando ya barabara ya kwenda Sikonge kilomita chache kutoka Tabora mjini ndiko kwenye asili ya ukoo wa akina Fundikira.

Mtemi Kalunde Fundikira ndiye aliyemzaa Mtemi Saidi Fundikira baba wa Chifu Abdallah Fundikira aliyefariki hivi karibuni.

Nyumbani kwao akina Fundikira kuna historia isiyofutika. Makaburi yapo, nyumba ya kutawazia watemi ipo na kuna dalili zote za kufuata taratibu za kimila.

Nani ambaye ameachiwa uchifu kwenye ukoo wa akina Fundikira?

Soma blog hii upate jibu.

Unajua asili ya jina Tabora?

Mji wa Tabora asili yake ni mzee mmoja aliyekuwa akiuza viazi vitamu vilivyojulikna kwa jina la matoborwa. Wasafiri na watu wengine wakapaita mahali hapo ni kwa Mzee Matoborwa sijui ilikuwaje hadi kufupisha kuitwa Tabora pengine wazungu walishindwa kutamka Matoborwa!

Lakini wakati wa ukoloni wa Kijerumani Tabora ilikuwa inajulikana kwa jina la UNYANYEMBE.

Mwandishi wa Habari Henry M.Stanley

Mwishoni mwa mwezi Juni mwaka 2008 nilitembelea kanda ya Magharibi hasa mkoa wa Tabora kwa shughuli ya kukagua na kutathmini kazi za utafiti kwenye kanda hiyo. Nikiwa huko nilipata fursa ya kutembelea moja ya makumbusho ya Taifa yaliyopo Tabora barabara ya kwenda Sikonge. Pale pana mambo mengi ya ukumbusho. Kwanza kuna jumba kubwa la tembe (sasa limekarabatiwa). Jumba hilo lilikuwa la mwarabu mmoja aliyejishughulisha sana na biashara ya utumwa. Baadaye lilinuliwa na wajerumani na kufanyiwa marekebisho. Ndani kuna nakala za machapisho ya gazeti la NewYork Herald -1872 zilizoandikwa na Henry M.Stanley mwandishi wa habari mahiri aliyetumwa kumtafuta Dr.David Livingstone aliyefia Afrika lakini maiti yake ilizikwa kwao kwa kubebwa na waafirika Susi na Chuma ambao walikuwa ni wasaidizi wa Livingstone wakati wa safari zake. Ndani ya jumba hilo kuna minyororo ya utumwa, kuna msalaba wa mzungu John Shaw aliyejipiga risasi na kuzikwa hapohapo Tabora, kuna kigoda alichokalia Stanley kuna barua alizoandika Livingstone kwenda kwa rafiki yake Benjamin Pyne n.k.

Utakapofika kwenye kituo hicho kuna bango la chuma lenye maandishi haya:- " David Livingstone after he had met H.M.Stanley at Ujiji on Nov.10.1871 he left this spot on August 25.1872 to undertake what was to be his last journey in Africa."

Hebu soma filosofia hii ya Waluguru

  1. Bita ako si miyage (Kupita njia tofauti si vuzuri)
  2. Chikwili ng'awingagwa na seko ( "Chikwili" hafukuzwi kwa kicheko)
  3. Chibwarabwatzi ukaye, kumgunda hoya
  4. Chibweregeni dawalaga uye, mdawalo gumuhonza ng'uku ( "chibweregeni" ucheze ukumbuke kurudi nyumbani mchezo umemponza kuku)
  5. Chimbulumbulu kokwila mti gwagumanyile ("Chimbulumbulu" hupanda mti anaoufahamu)
  6. Chujile cho chako, chiliumoto chamuhimba kaburi (Ulichokula ndiyo riziki yako kinachopikwa ni cha mchmba kaburi)
  7. Chamunu mahvi ung'achona uchiteme mate ( Cha mtu ni mavi na ukikiona ukiteme mate)
  8. Chihvile chola (Kilichoiva kimeoza)
  9. Mguluko gwa ng'anga wosi lunga lumwe
  10. Mlonga yeka kahuma
  11. Mwana ng'weleke mkulu miyago (Mtoto usiyemzaa mkubwa mwenzio)
  12. Kala mwatzi uhone (Kaa uchi upone)
  13. Chilondola cha imchua chohonela tungwe (Kidonda cha masikini huponywa kwa umande)
  14. Msimulila mvula imtowela (Msimulia mvua imemnyeshea)
  15. Mgulu gwangile (Mguu uliotembea nao)
  16. Mbewa kengila mchikalango (Panya kaingia kwenye kikaango)
  17. Moko gwamile mahvi ng'ugukana (Mkono uliokamata mavi haukatwi)
  18. Chinyala chikoma ng'enge (Aibu imemua kenge)
  19. Msongola lwiko kalema ukulakala
  20. Mtowa malati inguhvu muda (Mpiga baragamu nguvu inatoka tumboni)
  21. Ukulu tzalala (ukubwa jalala)
  22. Tudawale hatwibone (Tucheze tunapoonana)
  23. Uchuwa we ng'anga, inguku kana mtwatza (Ukiwa wa kanga kuku ana mfadhili)
  24. Kulawile ichijo kwa nzala (kulikotoka chakula kuna njaa)
  25. Uje chikuleme (Ule kikukatae)
  26. Cha nzala chilola hasi (Chenye njaa kimeangalia chini)
  27. Isi igalamka indetsi kowinga yumbwa (Nchi imechangamka ndezi anafukuza mbwa)
  28. Legela wakohe (Legea wakufunge)
  29. Msegetsa mno katula imbugi
  30. Mbama usafi kajila hasi
  31. Chuhuwile yumbwa kaja
  32. Cheleko cheleko ne mwenye mwana (Cheleko kipigwe na mwenye mtoto pia)
  33. Udodo ng'uku
  34. Mabuku mengi ng'agohimba mshimo gugendegende (mapanya wengi hawawezi kuchimba shimo mrefu)
  35. Tzeketzeke ni jako (Hata kama mpumbavu ni wako)

Ongeza kama una zaidi ya haya