Friday, August 29, 2008

Amevishwa pete ya uchumba!

Hayawi hayawi, yamekuwa. Hivi karibuni, Bw. Joseph Kamsopi Mdimi amefanya jambo kubwa katika maisha yake baada ya kumvika pete ya uchumba Bi.Flora Msechu katika hafla ya kukata na shoka iliyofanyika Mwanzo Park - Mwandege Mkoa wa Pwani. Hafla hiyo ilihudhuriwa na madada wawili, kaka na shemeji. Kamsopi anatarajia kufunga pingu za maisha tarehe 18/10/2008 jijini na Dar na sherehe za kupokea maharusi zitafanyika Afri Centre karibu kabisa na Lamada Hotel - Msimbazi

Wednesday, August 27, 2008

Tumekula machungwa mwaka mzima wabunge tusubiri maembe

Wakulima wa nchi hii wanafanya makubwa ya kulisha watu waishio hapa nchini kwa vyakula mbalimbali na katika mazingira magumu. Licha ya gharama za juu za uzalishaji. Lakini bado hawsiti kuzalisha.

Mwaka huu nimeshuhudia machungwa yakiliwa jijini Dar kwa mwaka mzima sasa.Tembelea masoko ya Buguruni, Tandika na Mbagala machungwa matamu makubwa yapo kwa bei ya shilingi 100 kwa chungwa.

Machungwa haya yanazalishwa kwa kutegemea mvua, yanazalishwa bila mbolea, yanazalishwa bila kutumia viuatilifu. Machungwa bora kabisa. Yanaweza kupata soko zuri ndani na nje ya nchi. Wakulima wetu wanajitahidi sana. Rais wetu Mh.Jakaya Kikwete analifahamu hilo ndiyo maana kama kiongozi wa nchi aliamua kuwa fedha za EPA zinazorudishwa zipelekwe kwenye sekta ya kilimo ili ziwasadie wakulima. Hapa hakuna sababu ya wabunge kupanga. Kazi ya kupanga ni ya serikali wabunge kazi yao kupitisha tu. Asante sana Spika wa Bunge Mh. Samwel Sitta kwa kulifafanua hilo, vinginevyo nalo lingetusumbua. Wabunge tusubiri maembe.

MV ARINA Reggae tu!

Moja ya boti zinazovusha abiria na magari pale Kigamboni Kivukoni ni MV ARINA. Ukipanda boti hiyo hukosi kuburudishwa na muziki kupitia kwa vipaaza sauti vya kizamani-mono (vya kutangazia mikutano). Lakini cha kushangaza, kama alivyobaini msafiri mmoja wa boti hiyo kwamba "humu hakuna taarifa ya habari wala nini - Ni Reggae tu." Hakufahamu kuwa blog hii ilikuwa karibu naye na pia huwa inatumia MV ARINA mara kwa mara na kusikia muziki wa reggae tu. Kweli MV ARINA ni reggae tu.

WANAENDESHA NA KUYAACHA KIGAMBONI

Wakati Ujenzi wa Barabara ya Kilwa ukiendelea. Wenye magari kutoka Mbagala na vitongoji vyake huamua kupitia Kigamboni ili kukwepa foleni ya magari kwenye barabara hiyo wakati wa asubuhi. Hali inakuwa mbaya wanapotaka kuvuka kwa kutumia pantoni. Kunakuwa na msururu mrefu wa magari. Kutokana na hali hiyo wengi wao huamua kuyaacha magari yao Kigamboni na kupanda pantoni. Hii imekuwa biashara nzuri kwa walinzi waliopo maeneo ya kivukoni gari dogo hulindwa kwa kiasi kisichopungua shilingi 500. Blog hii ilishuhudia hali hii leo asubuhi.

Si YANGA

Ukiwa ndiyo mara yako ya kwanza kuingia jijini Dar Es Salaam. Na mara yako ya kwanza kutembelea maeneo ya Buguruni, karibu kabisa na Makao Makuu ya chama cha CUF kuna jengo dogo hivi lililopakwa rangi za njano na kijani na kuandikwa kwa herufi kubwa YANGA nafikiri utajiuliza je hayo ndiyo makao Makuu ya Klabu ya Dar Es Salaam Young Africans al maarufu -YANGA? Usidanganyike, hicho ni kitawi kidogo tu cha Yanga cha Buguruni. Makao Makuu ya Yanga yako Jangwani, ndo maana wanaitwa watoto wa Jangwani!

Lakini nyie Yanga wa Buguruni, kwanini msiandike Yanga Tawi la Buguruni? Mnawapotosha wananchi.

Monday, August 25, 2008

Wakulima wajipange fedha za EPA zinakuja


Mhe. Rais Jakaya Mrisho Kikwete ametamka kwenye hotuba yake ya hivi karibuNI wakati akilihutubia BUNGE kuwa, fedha zinazorudishwa na mafisadi wa EPA zitatumika katika kuendeleza sekta ya kilimo. Ndiyo ametamka. Je, wakulima na wafugaji wamejipanga sawa kuzipokea fedha za EPA?

Wakulima wajipangaje fedha za EPA zinakuja

Mhe. Rais Jakaya Mrisho Kikwete ametamka kwenye hotuba yake ya hivi karibu wakati akilihutubia BUNGE kuwa fedha zinazorudishwa na mafisadi wa EPA zitumike katika kuendeleza sekta ya kilimo. Ndiyo ametamka. Je, wakulima na wafugaji wamejipanga sawa kuzipokea fedha za EPA?

Usafiri Mtoni Mtongani-Mbagala ni kero tupu

Barabara ya Kilwa iko kwenye ujenzi mkubwa. Awamu ya pili imeanza na kazi inakwenda kwa kasi kwa kweli. Sambamba na ujenzi huu, usafiri kwenye barabara hiyo umekuwa wa shida sasa. Madaraja yanayojengwa (mto Kizinga) pamoja na uzikwaji wa makalavati yanafanya kuwe na michepuko ya barabara hapa na pale kiasi cha kupunguza mwendo wa magari na kusababisha msururu mrefu wa magari. Ubadilishaji wa nguzo za umeme nao huenda sanjari na ujenzi wa barabara. Miti hukatwa na mitaro kuchimbwa. Hapo ndipo shughuli inapokuwa kubwa. Unaweza kutumia masaa mawili hadi matatu kufika mahali ulipokusudia. Tatizo ni kubwa wakati wa jioni na asubuhi.

Hatukujiandaa Olimpiki

Hii ni aibu kubwa. Timu yetu ya Olimpiki inarejea mikono mitupu. Tulikuwa wasindikizaji. Umaarufu wetu umepotea kabisa. Umasikini wetu umejionyesha hata kwenye michezo. Hata siku ya ufunguzi wanamichezo wetu walijitambulisha pasi na kujiamini hata sare zao zilikuwa za ubabaishaji zilikosa mvuto. Kweli Olimpiki ya mwaka huu hatukujiandaa.

Friday, August 22, 2008

Habari ya bilioni 9 za wakulima kuwekwa kushoto uk 18 si sahihi

Leo nimepata fursa ya kulisoma gazeti la serikali la "Daily News" katika ukurasa wa 18 upande wa kushoto nakuta kichwa cha habari "Nanyumbu farmers Bask in rich harvest" kwa kuwa mimi ni mtu wa kilimo nashtushwa na habari hiyo. Nachimba zaidi napata habari kuwa wakulima wa karanga wa wilaya ya Nanyumbu wamepata zaidi ya shilingi bilioni 9 kwa kilimo cha karanga msimu huu wa 2007/08. Jamani bilioni 9 kwa kulima karanga kwa wilaya moja tena ya Tanzania hiyo siyo habari muhimu kweli? Kwa kweli mhariri hukuitendea haki habari hii. Mimi nilitazamia kuiona kwenye ukurasa wa kwanza tena upande wa kulia. Lakini hapa imewekwa ukurasa wa 18 kushoto!

Taasisi ya Utafiti Kilimo chanzo cha bilioni 9 Nanyumbu

Teknolojia ya mbegu bora za karanga kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo -Naliendele, Mtwara zimewawezesha wakulima wa karanga kuvuna tani 12,241 za karanga na hivyo kujipatia jumla ya shilingi bilioni 19.18 msimu wa 2007/08. Akitoa taarifa hiyo, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Nanyumbu Bw. Farid Mhina amesema kuwa zaidi ya asilimia 90 ya wakulima wa karanga wilayani humo wanatumia mbegu bora.

Karanga ni moja ya zao la biashara linalokuja kwa kasi katika wilaya ya Nanyumbu, huku Korosho ikishika nafasi ya kwanza kwa kuwa chanzo cha kipato cha wananchi wa Nanyumbu. Hii ni kwa mujibu wa gazeti la Daily News la tarehe 22/08/2008.

Anamwakilisha Papa nchini Tanzania

Cardinali Joseph Chernoty Balozi wa Vatican nchini Tanzania akimkabidhi cheti cha Komunio Bi. Catherine I.J.Banzi kanisani Vikindu.

Waluguru hawaachi kumnema mwali!

Palikuwa hapatoshi Vikindu-Kisemvule. Catherine Banzi akinemwa na shangazi zake.

Huenda hawa wakatuletea ushindi


Kutoka kushoto Sisty Innocent Banzi, Peter Linus Banzi a.k.a Mkude

Ngoma inapochezwa na msinga!


Thursday, August 21, 2008

Ngoma na msinga!

Wapi hapo?

Huree nimefikisha Post 100!

Namshukuru Mungu kwa kunijalia afya njema, akili timamu na fursa ya kutosha ya kuweza kuingiza post 100 hadi sasa. Hili lilikuwa ni lengo langu la mwaka 2008. Miaka iliyotangulia zikuweza kufikisha hata post 25 kwa mwaka. Lakini mwaka huu nimeweza, nimevunja rekodi yangu mwenyewe.
Lakini kuna sababu nyingi zilizonifanya niweze kuingiza post nyingi mwaka huu. Mwaka huu nilipata fursa ya kusafiri sehemu mbalimbali nchini kikazi. Nimehudhuria mikutano, semina na warsha nyingi ambazo zimeniwezesha kukusanya niliyoyaona yanafaa kuwepo kwenye blog hii. Safari yangu Mbeya kwenye maonyesho ya Nane Nane nimejifunza mengi na nimeandika mengi kwenye blog hii kuhusu Nane Nane Mbeya.

Safari za kwenye Kanda kwa ajili ya kutoa elimu kwa wadau kuhusu Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo (ASDP) nayo imeniwezesha kukusanya habari kutoka Tabora, Arusha, Mbeya, Morogoro na Pwani.
Usafiri wa daladala nao umeniwezesha kupitia na kuona mengi ya jiji hili la Dar Es Salaam. Niliyoyasikia na kuyaona nimeyaning'iniza kwenye blog hii ingawa si yote.

Maisha yangu kijijini Vikindu-Kisemvule, ushiriki wangu katika shughuli za Parokia ya Kanisa Katoliki Vikindu pia ni hazina kubwa kwangu katika kufurisha blog hii. Naamini kuwa nitaweza kuingiza mengi kwenye blog hii kabla ya mwisho wa mwaka 2008 na iwapo nitapata camera habari zitaambatana na picha. Wateja wa Banzi wa Moro naomba maoni yenu

Takwimu za wasichana wanaokatisha masomo kwa ujauzito zinatisha

Habari inayosema kuwa asilimia 40 ya wasichana katika shule za sekondari mkoani Shinyanga hukatisha masomo yao kwa kupata ujazito. Asilimia hii ni kubwa. Je, ni asilimia ngapi ambao hushindwa kimasomo na sababu nyingine? Kwa mwendo huu kweli wanawake wasomi watapatikana kutoka mkoa wa Shinyanga? Sidhani. Kwa kweli hali ni mbaya. Asilimia 40 ni picha mbaya sana hasa inapokuwa inasababishwa na sababu moja!

Takwimu za wasichana wanaokatisha masomo kwa ujauzito zinatisha

Habari inayosema kuwa asilimia 40 ya wasichana

Ripoti kubwa majina yamo?

Nimeona kupitia luningani Mhe.Rais Jakaya Mrisho Kikwete akikabidhiwa ripoti ya uchunguzi wa skandali ya EPA. Kitabu kikubwa kwa kweli na inataka umakini wa kutosha kuisoma ripoti hiyo ili kuweza kutoa maamuzi sahihi. Swali moja najiuliza, kweli ripoti kubwa kama ile inaweza kukosa majina ya mafisadi wa EPA?

Mchakato wa kupata mikopo ya kilimo ina vikwazo vingi

Wakulima James Kyandarora, Bi Salma Mlwilo na Bw.Godwin Manase kwa pamoja wanakiri kuwa kilimo kimeweza kuboresha maisha yao kwa kuweza kujenga nyumba bora, kununua zana za kilimo, kununua baiskeli na kusomesha watoto (baadhi hadi chuo kikuu). Hawa ni wakulima wa mpunga kutoka Mbarali kupitia SACCOS ijulikanayo kwa jina la "RWANDA MAJENJE SACCOS." Wakulima hawa walishiriki kwenye maonyesho ya Nane Nane ya mwaka huu kwenye uwanja wa John Mwakangale jijini Mbeya.

Wakulima hawa hujishughulisha zaidi na kilimo cha mpunga ambacho uzalishaji huweza kufikia kilo 2500 kwa hekta moja. Tatizo kubwa la uzalishaji wa mpunga ni upatikanaji wa maji kwa wakati pia mchakato wa kupata mikopo ya kilimo ina vikwazo vingi walilalamika wakulima hao.

K.F.HANSEN KUTOKA DENMARK HADI MBARALI

Maonyesho ya wakulima maarufu kwa jina la Nane Nane yaliyofanyika kwenye uwanja wa John Mwakangale jijini Mbeya mwaka huu (2008)uliwashirikisha wadau wengi. Mmoja wa wadau aliyepata bahati ya kuzungumza na blog hii ni mzungu K.F.Hansen wa asasi isiyo ya serikali ijulikanayo kwa jina la SOK iliyoko Mbarali. Asasi hii hujishughulisha zaidi na uuzaji wa pembejeo za kilimo hasa madawa na mbegu kwa ajili ya uzalishaji wa mbogamboga na matunda. SOK ilianza shughuli zake mwaka 2000.

Kwa mujibu wa Bw. Hansen, wakulima wa Tanzania wanakabiliwa na matatizo makubwa ya ukosefu wa pembejeo na elimu ya kilimo bora, aidha bei za mazao ya kilimo hailipi. Gharama za uzalishaji ni kubwa kuliko za kuuzia. Hansen anatambua kuwa wakulima wengi ni wadogowadogo. Zana za kilimo pia hazipatikani kwa urahisi lakini anakiri kuwa sasa kuna mabadiliko makubwa katika sekta ya kilimo kuhusu upatikanaji wa pembejeo na zana za kilimo. Hansen amekuwepo nchini Tanzania tangu mwaka 1985 anazungumza kiswahili kwa ufasaha na kwa kweli anafahamu matatizo ya wakulima.

Saturday, August 16, 2008

Kuiona Black Stars Tshs 35,000 hivi tunamkomoa nani?

TFF imetangaza viingilio vya mechi ya Black Stars ya Ghana na Taifa Stars huku kiwango cha juu kikiwa shilingi 35,000. Mchezo huo utakaochezwa kwenye uwanja mkuu wa Taifa Agosti 20. Hivi hapa tunajifunza nini? TFF haijawahamasisha wananchi kuhudhuria mchezo huo wa kirafiki. La msingi kwao ni kutangaza viingilio. Huku wakiweka wazi kuwa gharama ya kuileta Black Stars ni shilingi 175,000,000.

Kwa uelewa wangu Black Stars wanakuja kucheza na Taifa Stars ili kuweza kuipima timu yetu ya Taifa na ikiwezekana kujifunza kutoka kwa Waghana hao kwani tunaaamini kuwa kiwango chao cha soka ni kikubwa ukilinganisha na cha kwetu, pia wana wachezaji wengi wenye uzoefu wa kimataifa. Sasa tunapoweka viingilio vya kukomoa, tunamkomoa nani?

Manispaa ya Morogoro yaboresha miundombinu

Manispaa ya mji wa Morogoro inaendelea kuboresha barabara zake kuu zinazounganisha mji huo. Barabara ambazo zinakaribia kukamilika kwa kiwango cha lami ni ile ya Uhuru inayopita benki ya "National Microfinance (NMB) na ile inayotoka njia panda ya Hospitali Kuu wa Mkoa hadi Morogoro Hotel na kupandisha hadi "uzunguni" maji yatiririka! Huenda haya yakawa ni moja ya matayarisho ya kuufanya mji huu kuwa JIJI. Barabara hizi na nyingine zikikamilika zitapinguza vumbi kwenye mji huo na kuboresha usafiri pia kuufanya upendeze. Morogoro ni moja kati ya miji maarufu na inayopendwa na watanzania na wageni kwa vile ina huduma muhimu na hali ya hewa ni nzuri.Tusubiri tuone.

Thursday, August 14, 2008

PROKON kuzalisha mafuta kutoka mbono

Kampuni ya PROKON kutoka Mpanda inatarajia kuanza kuzalisha mafuta kutoka mmea wa mbono ifikapo mwaka 2010.

Hayo yalielezwa na wawakilishi wa Kampuni hiyo kwenye maonyesho ya nane nane 2008 yaliyofanyika kwenye Uwanja wa John Mwakangale jijini Mbeya.

Wakiwa na sampuli ya mafuta hayo, ambayo ni mbadala wa mafuta ya petroli kwa kuendesha mitambo na magari, wawakilishi hao walieleza kuwa kwa sasa kiwanda kimeshaaanza kujengwa mjini Mpanda. Kilo moja ya mbegu za mbono kwa sasa zinauzwa kwa bei ya shilingi 1,200/= huko Mpanda, lakini mara nyingi bei huwa ni makubaliano kati ya mkulima na mfanyabiashara.

Kalalu aina mpya ya mbegu ya Mpunga

Watafiti wa Kilimo wa Taasisi ya Utafiti Uyole wameweza kutoa aina mpya ya mbegu ya mpunga ijulikanayo kwa jina la Kalalu. Mbegu hiyo ilitolewa rasmi mwaka 2005.

Jina la mbegu hiyo limetokana na Mkuu wa wilaya ya Kyela aliyewahi kufanya kazi kwenye wilaya hiyo ambaye alikuwa mstari wa mbele katika kuhimiza na kusimamia kilimo Mh. Mama Kalalu.

Sifa ya mbegu hiyo ni uvumilivu wa ugonjwa wa "Yellow Mottle Virus", hutoa mavuno tani 5 hadi 6 kwa hekta.

Mpunga ni zao maarufu kwa chakula na biashara wilayani Kyela.

Ngano aina ya Sifa "bomba" kwa mkate

Mbegu ya ngano ijulikanayo kwa jina la Sifa iliyotolewa na watafiti wa Kilimo wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Uyole mkoani Mbeya ni moja ya aina nzuri ya ngano inayofaa kwa kuoka mkate.

Mbegu hiyo yenye sifa ya kukomaa kwa muda wa siku 105 (miezi 3). Ni tegemeo kubwa kwa wakulima wa wilaya za Njombe(Iringa), Sumbawanga Vijijini na Nkasi (Rukwa).

Aina hiyo ya ngano ilionyeshwa kwenye maonyesho ya wakulima yaliyofanyika mwaka huu jijini Mbeya kwenye uwanja wa John Mwakangale. Mtafiti Mkuu Elanga ilidai kuwa pamoja na kuwa na aina mbalimbali za mbegu bora za ngano zilizozalishwa na Taasisi hiyo bado hazijasambazwa kwa wakulima wengi.

Mafuta ya Alizeti yang'aayo

Kwa wale waliotembelea banda la Kilimo la Halmashauri ya Sumbawanga kwenye uwanja wa John Mwakangale Mbeya na kukutana na wakulima wa Laela, nadhani watakubaliana nami kuwa moja ya vivutio vikubwa kwenye banda hilo lilikuwa ni mafuta ya alizeti.

Mafuta hayo yalizutia wadau wengi. Baadhi ya wadau walipenda kufahamu, kwanini mafuta mengine ya alizeti yanayotayarishwa kienyeji huwa na harufu mbaya na hayana mvuto (kwa rangi). Mkulima wa Laela alijibu kuwa hii inatokana na jinsi yanavyotayarishwa. "Yakitayarishwa vibaya ni kweli huwa yanakuwa na harufu mbaya." Alikiri mkulima huyo. Mafuta hayo ya alizeti yaliuzwa kwa bei ya shilingi (T) 2500/= kwa lita moja.

Kilimo cha alizeti ni maarufu mkoani Rukwa, kama wakulima watapata mitaji ya kutosha inawezekana kuwaondolea umasikini kwa kuwaongezea kipato chao.

Acheni vifuto,pensili, calculators na rula

Mkufunzi Mwandamizi wa Teknolojia ya Mawasiliano na Habari (ICT) wa VETA - Morogoro amewataka wahasibu na maafisa ugavi wa Idara ya Utafiti na Mafunzo kutoka Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika kuachana na matumizi ya vifuto, kalamu za risasi, rula, na calculators kwani shughuli hizo sasa zinafanywa na kompyuta.

Aliyasema hayo wakati akitoa mafunzo ya ICT ya muda wa juma moja mjini Morogoro. Mkufunzi huyo alisema kuwa programu ya Microsoft Excel inaweza kuwatatulia matatizo ya wahasibu na maafisa ugavi katika kutayarisha taarifa mbalimbali zinazohusu fani yao kwa ufanisi zaidi iwapo wafanyakazi hao wataielewa vizuri na kuitumia katika kazi zao za kila siku.

Moja ya sifa za programu ya excel ni kurahisha katika kufanya mahesabu, kutengeneza majedwali na chart mbalimbali. Zaidi ya wataalamu 40 wanaendelea na mafunzo hayo yanayotarajiwa kumalizika tarehe 17 Agosti 2008. Mafunzo hayo yameandaliwa na Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika chini ya Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo (ASDP)

Wednesday, August 13, 2008

Manispaa ya Sumbawanga yazalisha tani 64,338 za mahindi

Mahindi ni zao maarufu linalolimwa kwenye Manispaa ya Sumbawanga. Katika msimu wa 2007/08 Manispaa hiyo imeweza kuzalisha tani 64,338 za mahindi.Kiasi hicho ni kikubwa ikilinganishwa na uzalishaji wa mazao mengine yanayolimwa katika Manispaa hiyo. Mazao hayo ni kama vile Maharage (tani 8,100) na viazi vitamu (tani 13,622). Wakizungumza na blog hii, wakulima walioshiriki kwenye maonyesho hayo kwenye banda la Halmashauri hiyo, walisema kuwa utaalamu wa kilimo bora na teknolojia za kisasa hupata kutoka kwa maafisa ugani na kituo cha Utafiti wa Kilimo Uyole. Sumbawanga huzalisha pia chakula cha asili kijulikanacho kwa jina la kikanda ambalo husaidia kwa wagonjwa wa vidonda vya tumbo pamoja kuwapa wagonjwa hamu ya chakula.

Ludewa imepiga hatua kwa shamba darasa

Wakati wa sherehe za nane nane mwaka huu, banda la Halmashauri ya Ludewa lilikuja na takwimu nzuri za kuonyesha jinsi wakulima walivyopokea "approach" ya shamba darasa katika kujifunza teknolojia bora za kilimo.

Taarifa inaonyesha kuwa shamba darasa lilianza kutekelezwa kwenye Halmashauri hiyo tangu mwaka wa fedha 2005/06. Mwaka huo kulikuwa na mashamba darasa 13 ambayo 8 yalikuwa ya mazao na 5 mifugo. Mwaka 2006/07 kumekuwa na mashamba darasa 35 . Kumi na tisa ya mazao na kumi na sita ya mifugo. Kwa msimu wa mwaka 2007/08 kumekuwa na mashamba darasa 40 ambayo 22 ni mazao na 18 ni mifugo. Kwa takwimu hizo inaonyesha kuwa Ludewa inaendelea vizuri na shamba darasa.

Akizungumza na blog hii, Bw. Luoga aliyewakilisha Halmashauri katika maonyesho hayo, yaliyofanyika kwenye kiwanja cha maonyesho ya kilimo cha John Mwakangale kilichopo Uyole Mbeya(Kanda ya Nyanda za Juu Kusini), mtaalamu huyo wa kilimo alisema kuwa, wanawake wanaongoza kwa kupokea haraka "approach" ya shamba darasa lakini sasa wanaume wengi hujiunga na mashamba darasa ili kuweza kujifunza teknolojia mbalimbali za kilimo na ufugaji bora.

Tuesday, August 12, 2008

Morogoro Internet kama kazi

Sasa ni saa tatu na dakika sita (6) usiku nipo ndani ya jiji la Moro. Siyo siri mwanangu mi niko kwenye mtandao. Ndiyo maana nimeweza kupost habari kama mbili tatu hivi. Kwa kweli siyo siri, Moro kumekucha. Nasikia kuna maoni yanaendelea kutolewa na wakazi wa jiji hili kama Moro inastahili kuwa Jiji? Pamoja na ukweli kuwa mimi ni Banzi wa Moro mambo bado kidogo. Manispaa inatakiwa kuboresha miundo mbinu ya mji wa huu hasa barabara. Hata ile barabara ya kwenda Mji Mpya bado ni ya udongo. DDC ileile aliyopiga Marehemu Mbaraka Mwinshehe na Cubano Marimba na yalipo makao Makuu ya Lugaluga Agricultural and Marketing Cooperative Society. Hata, lazima tuwe wa kweli. Mambo mengi mazuri yapo Moro, lakini hili la barabara lazima liboreshwe na usafi uboreshwe. Vingenevyo kwa mtandao tu Moro ni kama kazi.

Kwa huduma hizi hatuwezi kuendelea

Nipo mji kasoro bahari (Morogoro). Hali ya hewa si mbaya kwa kweli. Nimekuja kwa shughuli za kikazi. Kuna mafunzo ya teknolojia ya mawasiliano (ICT) inayoendelea hapa VETA Morogoro kwa wahasibu na maafisa ugavi wa Idara ya Utafiti na Mafunzo - Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika. Wakati wa mapumziko washiriki wanapata chai na chakula. Lakini watoaji huduma ni goigoi, wakielezwa wananuna. Hawana ahadi za uhakika. Wanaweza kukueleza kuwa chakula kitakuwa tayari baada ya dakika tano kumbe ndo kwanza ugali unasongwa! Hivi kwa huduma ya aina hii tunaweza kuendelea? Lakini wanaotua huduma hii sio VETA Morogoro, bali kuna mjasiriamali moja ambao watendaji wake wanamuangusha. Kwa mwenendo huu kweli tutaendelea?

Tujifunze kwa Wachina

Michezo ya Olimpiki inaendelea huko Uchina. Wengi hawakutarajia kuwa Wachina wangeweza kuandaa michezo hiyo kwa kiwango cha hali ya juu hasa wazungu wa Ulaya ya Magharibi na Wamarekani. Lakini tumeona jinsi ufunguzi wa michezo hiyo ilivyofana huko Beijing. Angalia halaiki yao, angalia ubunifu wao kwa kweli ni "excellent" hata hao tunaowaita wazungu walibaki kupiga makofi na kushangaa. Watu wa marika yote walishirikishwa, wa jinsi zote walishirikishwa. Lugha waliotumia ilikuwa ni ya Kichina na kila kiongozi wao alipoongea wao walishangilia. Walishangilia kwa kuwa walielewa, walshangilia kwa kuwa walikuwa wazalendo. Kwa kweli Wachina wanaweza,wanajitegemea na ndiyo maana wanakuwa tishio katika dunia ya leo. Kweli Watanzania inatupasa kujifunza kutoka kwa wachina.

Sunday, August 10, 2008

Licha ya lumbesa kupigwa marufuku - Wakulima bado wananyonywa


Hivi karibuni serikali ilipiga marufuku mtindo wa kufunga magunia ya mazao kwa mtindo wa"lumbesa" kwa sababu mtindo huo ulikuwa unawaibia wakulima.

Safari yangu ya Mbeya kwenye sherehe za nane nane nilibahatika kuongea na mkulima mmoja kuhusu agizo hilo je kwa wakulima lina manufaa yoyote? Mkulima huyo ambaye ni mwanamama alinijibu kwa kusema kuwa kwa sasa hali imekuwa mbaya zaidi.
Alitoa mfano kuwa yeye ni mkulima wa viazi mviringo. Kwa mtindo wa "lumbesa" alikuwa akiuza sh.42,000/= (Bei ya mwaka jana). Lakini sasa ujazo wa kawaida anauza kwa sh. 15,000/=. Kutokana na hali hiyo wanaibiwa sana na mkulima hapati chochote.

Wednesday, August 6, 2008

Usipofika Msamvu Makuti unakosa mengi

Ukipata bahati ya kutembelea mji wa Morogoro. Usipate shida, moja ya sehemu nzuri na za kupendeza na zenye kutoa huduma za uhakika za chakula na vinywaji ni Msamvu Makuti.

Msamvu Makuti ipo ndani ya kituo kikuu cha mabasi cha mji wa Morogoro. Inafikika kirahisi ukielekea Dodoma, Dar Es Salaam au Iringa. Msamvu Makuti imeweza kujijengea jina hasa kwa nyama choma, supu na mchesho!

Watoa huduma wa Msamvu Makuti ni vijana wachangamfu wake kwa waume na huwapokea wateja mara tu wanapokaribia milango ya banda hilo la Makuti lilioezekwa kiutamaduni.

Ifikapo usiku starehe ya muziki inapatokana na usafiri wa kurudi sehemu uliyofikia au nyumbani kwako ni "bwelele." Msamvu Makuti inatoa faraja kwa wasafiri wakati wote kwa huduma ya chakula na vinywaji. Ukiwa Msamvu Makuti unaweza kujinunulia matunda ya aina mbalimbali yanayopatikana mkoani Morogoro hasa ndizi ,machungwa, maembe na mananasi.

Uwapo Msamvu Makuti milima ya Uluguru inakukonyeza huku maji yakitiririka!

Gwami Internet Cafe Morogoro

Mji wa Morogoro unapanda chati kwa kasi ya ajabu. Hii pengine inatokana na taasisi nyingi kuwepo kwenye mji huu. Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA), Chuo Kikuu Mzumbe, Chuo Kikuu cha Kiislamu, Chuo cha Ardhi, VETA Morogoro, Hospitali ya Mkoa, Chuo cha Mifugo, Stesheni ya Gari Moshi (Reli) Shule za Sekondari nyingi tu, kumbi za mikutano , mahoteli na nyumba za wageni na nyingine ambazo sijazitaja. Mji huu ni wa biashara hasa yanayotokana na mazao ya kilimo na madini.

Kuwepo kwa taasisi hizi kunasababisha kuongezeka kwa idadi ya wakazi na wageni wa mji huu kila siku. Kwa kuwa wageni na wakazi wanaongezeka basi mahitaji huongezeka.

Moja ya huduma muhimu katika enzi hizi za sayansi na teknolojia ni ile ya mtandao au "Internet". Internet inasaidia sana katika kurahisisha mawasiliano. Kwa mji kama huu wenye Maprofesa, wataalamu wazamivu na wazamili pamoja na wanafunzi wa ngazi zote huduma hii ni muhimu.

Ukiwa Moro usihangaike sana ulizia ilipo ofisi ya CCM wilaya ya Morogoro karibu kabisa na mahali pa starehe panapoitwa Chipukizi utakuta Internet Cafe moja bomba sana inaitwa Gwami Internet Cafe.

Internet Cafe hii ni moja ya internet ya kisasa hapa nchini naweza kusema bila ya kuuma meno. Computer zake ni safi na mtandao una speed kubwa. Usafi ndani ya cafe ni wa hali ya juu, vijana wachangamfu na wenye utaalamu wa mtandao wanatoa huduma safi. Hata maji ya kunywa yapo ndani ya cafe yanayopatikana kupitia mashine maalum. Dakika 30 ya kutumia mtandao ni shilingi 400/= tu.

Tuesday, August 5, 2008

"B One" Mtandao bora wa nyumba za wageni Morogoro

Ukiwa ni mara yako ya kwanza kutembelea mji wa Morogoro usipate shida ulizia "B one" kwa ajili ya huduma za malazi.

Wiki iliyopita nilikuwa Morogoro. Huwa nauona mtandao wa B one wa nyumba za wageni lakini niseme ukweli nilikuwa naogopa kuulizia nikidhani kuwa ni za gharama kubwa yaani si ya kiwango changu. Kumbe nilikuwa sina taarifa sahihi za kutosha. Nilipojaribu kuulizia nafasi ya malazi nilibahatika kupta kwenye moja ya nyumba hizo. Lazima ni kiri kwa mambo yafuatayo niliyoyaona kwenye nyumba hiyo.
  • Usafi wa hali ya juu
  • Kauli nzuri ya wahudumu
  • Unapata kifungua kinywaji kamili (+juice ya matunda ya Morogoro!)
  • Ulinzi wa uhakika
  • Utulivu masaa 24
  • Kila chumba kina TV
  • Gharama ya kuridhisha

Kilichobaki "B One" ni kujitangaza kwa njia zote ikiwezekana kukamata soko la nyumba za wageni Morogoro. Kula 5 mjasiriamali wa "B one."

Kwa mtandao kama huu, Moro sasa chati yake inapanda kwa kasi ya kutisha. Tembelea Moro na usikose kuulizia "B one" halafu toa maoni yako kupitia www.innobanzi.blogspot.com

Msamvu - Morogoro "Keep left" Kikubwa Tanzania

Nimebahatika kutembelea mikoa mingi hapa Tanzania lakini sijapata kuona "keepleft" kubwa na inayotunzwa vizuri kama ile ya Msamvu, Morogoro. "Keep left" hiki kiko kwenye makutano ya barabara ya morogoro, Iringa na Dodoma kwa kweli ni kikubwa. Kinachofurahisha zaidi ni jinsi Manispaaa ya Morogoro inavyokitunza. Kina maua mazuri ya aina mbalimbali na uhudumiwa vizuri kwa kumwagiliwa maji na kuondoa magugu yasiyohitajiwa. Sasa naweza kusema kuwa " Keepleft" cha Msamvu ni nambari wani hapa Tanzania. Aliyeona kikubwa zaidi ya hicho akitaje basi!

Monday, August 4, 2008

Zongo Mwenyekiti Lugaluga Agricultural and Marketing Cooperative Society

Mkutano Mkuu wa Ushirika wa Kilimo na Masoko - Lugaluga (Lugaluga Agricultural and Marketing Cooperative Society) uliofanyika tarehe 2 Agosti 2008 kwa kauli moja umepitisha jina la Bw. Ally Rashid Zongo kuwa Mwenyekiti mpya wa chama hicho baada ya aliyekuwa Mwenyekiti wa ushirka huo Bw. Chaula kuhamia Mbeya kikazi.

Kabla ya hapo Bw. Zongo alikwa akishika nafasi ya Makamu wa Mwenyekiti katika Ushirika huo. Kwa maana hiyo, Bw. Zongo ndiye Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Ushirika huo.

Chama cha Ushirika wa Kilimo na Masoko Lugaluga kilichopo Morogoro kilisajiliwa rasmi Septemba 2005 na kupewa namba 344. Hadi sasa ushirika una wanachama 88 wanaotimiza masharti na kanuni za chama.

Ushirika wa Lugaluga una mpango kabambe wa kumiliki ekari 20,000 zitakazotumiwa na wanachama wake katika uzalishaji wa kilimo na ufugaji.

Dira ya Lugaluga ni kuinua na kustawisha hali ya uchumi na maisha ya wanachama na jamii kupitia vyama vya ushirika.

Lugaluga ni chama chenye kuona mbalimbali katika uzalishaji wa kilimo na ushirika.
Pamoja na raslimali kubwa ya ardhi iliyoko mbele yao, Lugaluga inakosa mtaji wa kujiendesha.

Kwa kuwa mkoa wa Morogoro umetajwa kuwa ni kapu la uzalishaji wa mazao ya kilimo hapa nchini kuna haja ya viongozi wa ngazi zote kutoa machango wao katika kuhakikisha kuwa Lugaluga inakuwa mfano bora wa ushirika mkoani Morogoro na kwa Taifa. Jambo la msingi ni kusimamia na kuona kuwa wanachama wake wanapata mikopo itakayowawezesha katika uzalishaji kwa kununua pembejeo za kilimo, kutayarisha mashamba na kupata teknolojia za kisasa za kilimo.

Vyombo husika vitayarishe mipango na kuitekeleza katika kuboresha miundo mbinu ya shambani na hasa barabara. Hili ni tatizo kubwa lilojitokeza wakati wa kutayarisha mashamba kwa msimu wa mwaka 2007/08.

Saturday, August 2, 2008

Nauli Mpya Utafiti wa kina haujafanywa

Jana tarehe 1 Agosti nauli za vyombo vya usafiri zimepanda nchini kote hasa kwa usafiri wa magari. Kupanda huku kwa nauli kumewafanya watanzania wengi kufikiri jinsi ya kufanya ili kuweza kukabiliana na kupanda huku kwa nauli.

Tatizo hili limejitokeza kwa kina zaidi jijini Dar Es Salaam hadi kufikia wanafunzi wa shule za msingi na sekondari kuandamana kwenda ofisi za Mkuu wa Mkoa wa Dar Es Salaam ili kuonana na Mh. Kandoro wamueleze kukerwa kwao na uwezo walio nao wanafunzi.

Wafanyakazi wengi hasa wa kipato cha chini kuongezeka kwa nauli ni kero kwao. Wafanyabiashara wadodowadogo "wamachinga, mamantilie" nao ni pigo itabidi waongeze bei ya sahani ya wali au wapige panga kwa bei hiyohiyo ili waweze kupata faida. Bidhaa feki nazo zitaoongezeka madukani.
Nasema utafiti haujafanyika kwa nauli mpya za sasa.

Asha Rose Migiro anavyoonekana kwa watu

Dkt. Asha Rose Migiro ni jina maarufu si hapa Tanzania bali hata kwa mataifa mengine.
Dkt. Migiro Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN) ni moja ya matunda bora kutoka Tanzania yanayowaka katika anga za Kimataifa.

Ninavyomfahamu mimi, Dkt. Asha Rose Migiro aliwahi kuwa mhadhiri pale Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam na ameshawahi kuwa Waziri wa Maendeleo ya Jamii na Wanawake na Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje na Uhusiano wa Kimataifa.

Hivi sasa yupo Tanzania kwa likizo fupi. Kwa muda wa wiki moja sasa amekuwa akifanya mambo mengi hapa nchini. Ameshahudhuria kikao cha Bunge na kulihutubia na kuhojiwa na vyombo vya habari hapa nchini.

Wakati wote huo nilichojifunza kutoka kwake, mwanamama huyu ni makini sana. Anajua nini cha kuongea na wakati gani na kwa akina nani. Ana kipaji kikubwa cha kutumia lugha. Anaweza kujieleza barabara kwa kiswahili fasaha na kiingereza makini.

Huyu ni mtu ambaye ameshatembelea nchi nyingi na kukutana na watu wengi maarufu na wa kawaida hapa duniani lakini haachi kujitambulisha Utanzania wake. Kwa kweli nimempenda jinsi anavyojiweka katika hali ya kawaida kabisa.

Nimesikia kuwa mpaka sasa anaishi kwenye nyumba za wahadhiri kule Chuo Kikuu Dar Es Salaam na hata alipokuwa waziri. Huyo ndiye Dkt. Asha Rose Migiro kioo cha Tanzania na mfano bora kwa wanawake.

Kamokerere-Kijiji cha Chacha Wangwe

Sijawahi kufika Musoma,Tarime husan kijiji cha Kamokerere. Sijawahi kumuona uso kwa uso marehemu Chacha Wangwe aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Tarime. Lakini kwa takriban wiki moja sasa, kijiji cha Kamokerere kimekuwa maarufu kupitia vyombo vya habari kufuatia kifo cha Chacha Wangwe.

Kwanini Kamokerere? Chacha Wangwe alikuwa mmoja wa wabunge maarufu kwa hoja zake nzito akiwa bungeni. Aliwawakilisha ipasavyo wapiga kura wake wa jimbo la Tarime ingawa alikuwa si wa chama tawala, yeye alikuwa ni wa CHADEMA.

Marehemu Chacha Wangwe alipata ajali akiwa safarini kutoka Dodoma kuelekea Dar Es Salaam. Kwa kuwa kifo chake hakikutarajiwa, wengi walidhani kuwa kifo hicho kilikuwa ni cha kupangwa yaani aliuawa ndiyo maana wapiga kura wake hasa kutoka kijiji cha Chamokerere walipandwa jazba kutaka kufahamu sababu ya kifo hicho.

Lakini kwa mujibu wa habari kupitia televesheni na magazeti ya leo asubuhi baada ya uchunguzi wa kitaalamu kufanyika mbele ya mashahidi ya pande husika imebainika kuwa marehemu Chacha Wangwe alikufa kwa ajali ya gari na kupasuka fuvu na ubongo kumwagika. Apumzike kwa amani Chacha Wangwe.

Friday, August 1, 2008

Foleni ya Mbagala inasababishwa na ubinafsi wa madereva

Licha ya kuamka mapema ili kuweza kuwahi ofisini, leo nimejikuta nikikwama Mbagala Sabasaba takribani kwa saa moja kutokana na foleni ya magari iliyosababishwa na baadhi ya madereva kutofuata utaratibu wa kuendesha gari.

Magari mengi yalikuwa yanakatiza njia wanazojua wenyewe na kusababisha magari kufungana karibu kabisa na kiwanda cha nguo- KTM.

Hali hiyo iliendelea hadi walipojitokeza askari wa usalama barabarani na kuchukua hatua kali kwa wale madereva waliokatiza njia ikiwemo kuwanyang'anya funguo za gari. Kuna askari mmoja wa kike alinifurahisha sana pale aliposimama mbele ya gari lililotaka kuingia barabara kuu kwa makosa. Bila kusema chochote alimgandisha kwa muda mrefu na hata gari letu kufanikiwa kupita. Ndiyo maana nasema foleni ya Mbagala (Barabara ya Kilwa) inasababishwa na ubinafsi wa madereva.

Viazi, mihogo hadi barabarani


Wakulima wetu wanajituma sana katika uzalishaji licha ya mazingira magumu waliyonayo lakini wameza kulisha taifa hili na kuweza kuimarisha uchumi wa nchi hii kupitia kilimo na ufugaji.


Juzi nilitembelea soko la Mbagala. Nilishangaa kuona mazao mbalimbali ya kilimo yamefurika soko hadi kuzagaa kwenye barabara.Muhogo na viazi bwerere kabisa. Ndani ya soko nyanya,bamia, mchele, maharage, vitunguu, karoti,mchicha, kabichi, mbaazi, njegere, ndimu, karanga, matango, pilipili hoho, pilipili mbuzi, tangawizi, nyanya chungu na vingine vingi vyote hivyo vimezalishwa na wakulima wadogowadogo. Licha ya kutegemea kilimo cha mvua kwa silimia kubwa lakini vyakula vipo. Kwa kweli wakulima wetu wanafanya kazi kubwa sana lakini bado mtazamo wa nchi kwenye kilimo naweza kusema ni hasi! Maneno mengi lakini wakulima tuseme ukweli hawajaendelezwa katika kilimo na hii inatokana na bajeti finyu inayotolewa kwa sekta ya kilimo

"TIGO" PEKEE WAMEWAONA WAKULIMA?


Sikukuuu ya wakulima "NANE NANE" ndiyo hiyo imeingia. Lakini kwa mujibu wa gazeti la "This Day." Kampuni ya simu "TIGO" ndiyo inayoonekana kudhamini maonyesho hayo tena kwa shilingi milioni 10 tu!

Kampuni nyingine ziko wapi? Kuna kampuni ambayo hainufaiki na Kilimo? Mbona kimya? Hata huo ufadhili wa shilingi milioni 10 kutoka TIGO ni mdogo sana. Hivi kuna wakulima wangapi wanaotumia mtandao wa TIGO? Hata kwetu Matombo, Morogoro mtandao unaotamba ni "TIGO" mnara wake umewekwa mlimani kileleni hivyo kuwafunika kabisa Celtel mtandao wa kwanza Matombo.

Huo ndio mtazamo wa watanzania wengi kwenye kilimo, hatukipi stahili yake kwenye mipango yetu licha ya mchango mkubwa unaotoa kwenye uchumi wa Taifa na maisha ya wananchi wetu.

Nashangaa " Serengeti" wamedhamini mpira wa miguu kwa mamilioni ya fedha huku wakisahau kuwa bia wanazotengeneza, malighafi kubwa ni mazao ya kilimo (ngano na shayiri).

Tunakula nyama za aina mbalimbali (kuku, ng'ombe, mbuzi, kondoo, bata) kutokana na juhudi za wafugaji lakini wanapotaka kuonyesha shughuli zao tunasita kudhamini. Mimi sipati picha kwa kweli.
Mwakani tuhamasiki kwa kudhamini maonyesho ya kilimo (NANE) iwe kampuni, vikundi au binafsi tuelekeze nguvu zetu kwenye kilimo. Kila mmoja wetu anafaidika na kilimo.