Monday, August 31, 2009

Madereva watanashati


Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika inazingatia umuhimu wa wafanyakazi kupatiwa sare za kazi. Moja ya kada zinazopatiwa sare hizo ni madereva. Pichani wanaonekana madereva Salehe Mkwawa na Lems Nyagawa wa Idara ya Utafiti na Maendeleo wakiwa kwenye sare za kazi wakifurahia maisha!

Friday, August 28, 2009

Sidhani kama tunamuelewa Kardinali Pengo


UFISADI unaongelewa sana katika nchi yetu. Moja ya sababu inayodunisha maendeleo yetu. Watu mbalimbali wamepiga na wanaendelea kupiga kelele kuhusu UFISADI. Imefikia wakati hata Kanisa kuingia katika ngoma nalo linapiga kelele. Kiongozi wa Kanisa Katoliki hapa nchini Kardinali Polycarp Pengo ana mashaka na wote wanaopiga kelele kuhusu UFISADI kama kweli kelele hizo ni za dhati au ni wivu. Anauliza Pengo je hao wanaopiga kelele wangekuwa kwenye nafasi hizo wasingeweza kuwa MAFISADI. Tujiulize sote ni hapa tu tutakapopata jibu ndipo tutakapomulewa Kardinali Pengo.

Kila mfanyakazi wa kilimo kuwa na Mpango Kazi -Wasira


Tarehe 9-10 Agosti 2009, Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika ilikuwa na Kikao cha Baraza la Wafanyakazi mjini Dodoma ndani ya Dodoma Hoteli. Kikao hicho kilifunguliwa rasmi na Waziri wa wizara hiyo Mhe. Stephen Wasira.

Agizo moja muhimu alilolitoa ni kuhakikisha kuwa kila mfanyakazi wa wizara anakuwa na mpango wa kazi kwa mwaka 2009/10 ili baadaye apimwe kutokana na malengo aliyojiwekea.

Thursday, August 27, 2009

Watafiti wa Africa mnaifahamu FARA?

Tulipenda Kusoma-Mjomba


Juzi Jumanne nilimtembelea mjomba wangu Dr. Gregory P.Mluge nyumbani kwake Mbezi Beach. Ni muda mrefu hatujaonana na kuzungumza kwa kweli. Alifurahi sana kuniona na tukapata chakula cha pamoja na Binti yake Janet na wajukuu zake.

Wakati tukiwa kwenye mazungumzo tuligusia mambo mbalimbali kwa kifupi sana, kilimo chetu na maisha kwa ujumla hasa nyumbani Matombo. Kwa maneno yake mwenyewe alisikitika kuona kuwa jinsi maendeleo ya Matombo yanavyosuasua. Yeye anaona kama Matombo inarudi nyuma vile. Vijana hawachapi kazi wapo tu vijiweni.

Kwa Upande wa Elimu yeye alisema zamani wao walipenda sana kujifunza tena walitumia muda mchache lakini walikuwa wakielewa mambo na kuyazingatia wafundishwayo.

Dr. Mluge amesoma shule nyingi zikiwemo Bigwa Primary School, Kigurunyembe, Tabora Boys, Pugu High School hatimaye Makerere Uganda alikohitimu udaktari. Baadaye alikwenda Uingereza kwa masomo ya Juu ya Udaktari na kufanya kazi huko kwa miaka mingi na baadaye Saudi Arabia. Hivi sasa anapumzika nyumbani Mbezi lakini anapenda sana shughuli za Kilimo ingawa kwa maneno yake mwenyewe kilimo cha Tanzania hakilipi na kinategemea sana hali ya hewa hasa mvua. Mazao hasa ya matunda yanaharibika hovyo wakati wa msimu na mkulima hafaidiki kutokana na kazi kubwa anayoifanya kwa kuzalisha mazao hayo.

Wakati akiwa Makerere walikuwa pamoja na Rais Mstaafu wa awamu ya tatu Mhe. Benjamin William Mkapa. Pichani Dr. G.Mluge akiwa na mkewe kushoto akitambulishwa na Blogu hii kwenye moja ya sherehe za kifamilia.

Hivi jinsi hupimwa kwa madawa?



Caster Semenya kutoka Afrika Kusini ambaye ndiye bingwa wa dunia wa mbio za mita 800 wanawake ni gumzo hivi sasa baada ya kushinda mbio hizo huko Berlin mwezi huu. Wazungu hawaamini kuwa ni mwanamke. Eti uwezo aliokuwa nao ni wa mwanaume zaidi.

Sasa mimi sielewi. Hivi kuthibitisha kuwa ni mwanamke au mwanaume kuna haja ya kufanya vipimo zaidi. Si kuangalia tu naniiiii yake mara moja itagundulika kama mwanamke au mwanaume. Mie sioni ugumu wowote hapa. Tatizo ni nini? Wenzangu nipatieni jibu.

2nd CHANCE MKOMBOZI WA KISEMVULE

Kama kuna wafanyabiashara wanaoona mbali na kujizatiti kutoa huduma kwa umma basi ni mmiliki wa bus linaloitwa 2nd Chance linalofanyakazi kati ya Mbagala R3 na Kisemvule-Mkuranga.
Bus hili ni zuri na la kisasa, halibagui abiria nikiwa na maana wanafunzi. Wote kwake sawa. Mwanafunzi akikalia seat habuguzwi ni jukumu la mwanafunzi mwenyewe kutambua kuwa ni vizuri kuacha nafasi hizo kwa wazee na isitoshe hulipa nauli ya mwanafunzi.

Kabla ya 2nd chance kuanza kutoa huduma kwenye njia hiyo, wakazi wa Kisemvule walikuwa wakinyanyasika sana na wasafarishaji. Magari yaendayo Mkuranga yalikuwa yakiwaacha wakidai kuwa nauli hailipi. Mengine yalikuwa yakigeuzia Vikindu. Ilikuwa ni karaha kwa wakazi wa Kisemvule.

Ikumbukwe kuwa Kisemvule ni kijiji kinachukua kwa kasi ya kutisha, isitoshe kinafikika kirahisi na kina miundo mbinu imara kama vile umeme na maji ndiyo maana wahamiaji kijijini hapo wanamiminika kwa wingi tofauti na miaka ya 90. Thank you 2ND CHANCE kwa huduma bora

Dr. Msabaha astaafu baada ya miaka 60


Kaimu Mkurugenzi wa Utafiti na Maendeleo/Mkurugenzi Msaidizi Utafiti wa Mazao katika Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika Dr. Mohamed Msabaha amestaafu kuwa mtumishi wa umma tarehe 20/8/2009 baada ya kulitumikia taifa kwa takriban miaka 34.

Katika hafla fupi aliyoandaliwa na watumishi wa Idara yake waliopo makao makuu Dar Es Salaam ilielezwa kuwa Dr. Msabaha alikuwa mtafiti na kiongozi hodari aliyechapa kazi kwa bidii na kwa ufanisi mkubwa katika mazingira mbalimbali.

Baadhi ya mambo aliyofanikisha wakati akiwa kazini ni pamoja na:-
  • Kuanzisha na kuendeleza programu ya utafiti wa mazao ya mizizi hapa nchini (muhogo, viazi vitamu, na viazi mviringo)
  • Moja ya wakurugenzi wakanda waanzilishi wa mfumo wa Utafiti wa Kanda (Zonal Research System)
  • Kiongozi mwanzilishi wa uzalishaji wa mbegu za mazao kwenye vituo vya Utafiti ambao ni endelevu hususan katika kituo cha Utafiti wa Kilimo Uyole
  • Kuongoza kituo cha Utafiti wa Kilimo cha Uyole kwa mara ya kwanza katika mfumo wa serikali
  • Kusimamia uanzishwaji wa "Regional Rice Centre of Excellency' kitakachokuwa na makao makuu KATRIN-Ifakara.
Dr. Msabaha alianza kazi mwaka 1975 katika kituo cha Utafiti Ukiriguru baadaye alihamishiwa Uyole, Mbeya mwaka 1993 akiwa Mkurugenzi wa Utafiti wa Kanda kabla ya kupelekwa Makao Makuu ya Wizara akiwa Mkurugenzi Masaidizi wa Utafiti wa Mazao mwaka 2007. Mwanzoni mwa mwaka 2009 alikaimu nafasi ya Mkurugenzi wa Idara hadi alipostaafu.

Wednesday, August 26, 2009

Shujaa wa Mpango wa Elimu Bure azikwa Kenya


Mwili wa Bw Stephen Kimani Maruge kutoka Kenya umezikwa tarehe 25/8/2009 katika makaburi ya Arashi wilaya ya Nakuru,Kenya akiwa na umri wa miaka 89. Marehemu aliingia kwenye vitabu vya kumbukumbu za maajabu ya dunia (Guiness book) baada ya kujiunga na darasa la kwanza akiwa na umri wa miaka 84.

Bw. Maruge alianza kupata umaarufu mwaka 2003 wakati alipojiunga na darasa la kwanza katika shule ya msingi Kapkenduiywo iliyopo mkoani Eldoret baada ya serikali kutangaza mpango wa kutoa elimu ya msingi bure na haraka akawa kipenzi cha vyombo vya habari.

Kupumzika ni afya


Banzi wa Moro hupenda kujipumzisha baada ya kazi nzito za siku. Hujilaza kwenye kiti cha kienyeji kilichosokotwa nyumbani kwake Kisemvule Mkuranga.

Nyumbani Kisemvule!


Wakati Mwingine tunapenda kupumzika. Hahaaa nyumbani Kisemvule!

Poleni wa Idodi-Hatuna budi kujifunza


Napata picha isiyo furahisha, picha ya majonzi. Vifo. Kwa ajali ya moto. Tena wanafunzi, zaidi ya hapo ni wasichana. Wamefariki wakitafuta elimu ndo kwanza wameanza safari. Tegemeo la taifa. Tumepoteza vijana 12. Msiba mkubwa. Poleni wa Idodi.

Labda ni vizuri nikasema kuwa inatubidi kuwa makini zaidi katika masuala haya ya Jumuiya. Wanapokuwa watu wengi kuna la ziada. Kwa wanafunzi kuna zaidi ya ziada. Wanafunzi wanaweza kufanya lolote katika mazingira yoyote pengine bila kutambua madhara yake. Wanaweza kugoma wakaharibu vifaa, wakawapiga walimu na wanafunzi wenzao kwa lengo la kutekelezewa wanachotaka sasa hivi.

Huyu aliyewasha mshumaa ili ajisomee hakuwa na lengo baya. Yeye alifikiri kufaulu mitihani. Suala la mshumaa kuweza kusababisha moto huenda halikuwepo. Ni wajibu kwa viongozi kutambua hayo na ndipo kazi ya ulinzi inapokuwa ni umuhimu.

Ulinzi ni usalama wa watu na mali zao. Wangekuwepo walinzi makini wangeweza kupita kwenye bweni hilo mapema na kubaini kuwa kuna mshumaa uliowashwa bila kuzimwa baada ya muda kupita na kama doria ingefanywa kila kipindi kifupi hili huenda lingegundulika mapema. Kweli ni bahati mbaya lakini hatuna bundi kujifunza lisitokee tena. Ni uchungu mkubwa kwa kweli kupoteza vijana 12 kwa muda mfupi.

Siyo Nzuguni-Hapa ni Dodoma Hotel


Kama kuna mwekezaji basi huyu wa Dodoma Hotel ni kiboko. Dodoma Hotel imebadilika kabisa kumbi za mikutano za kisasa zimeongezwa pamoja na kuboreshwa huduma. Hebu cheki chumba cha kupumzikia mgeni rasmi kabla hajafungua kikao. Pembezoni mwa Dodoma Hotel TRL-Dodoma Station choka mbaya. Habari ndiyo hiyo.

Themi-mboga kwenye mifuko ya saruji!


Hata ukiwa ghorofani, bado unaweza kustawisha mboga. Ndivyo yalivyokuwa maonyesho ya Nane Nane kwenye viwanja vya Themi mjini Arusha mwaka huu. Mboga kwenye mfuko wa saruji. Usiseme sina eneo. Pengine hujachagua teknolojia!

Wajasiriamali waliuza mazao ya mifugo


Hakika, Nzuguni Dodoma wajasiriamali walionyesha jinsi mifugo ilivyokuwa mali wakati walipouza mazao mbalimbali yanayotokana na mfigo kuanzia nyama, kuku, maziwa, samaki, jibini, siagi, viatu, mikanda, mikoba na mtindi! Pichani - Blogu hii ikipata mtindi baridi!

Nane Nane imeanza kuwa ya wakulima


Ndiyo, maonyesho ya Nane Nane sasa yameanza kuwa ya wakulima za idi kuliko iliv yokuwa hapo awali ya wataalamu! Mwaka huu nilibahatika kuwepo kwenye viwanja vya Themi Arusha na Nzuguni Dodoma. Nilikuwa na shauku ya kutembelea mabanda ya Halmashauri ili niweze kubaini kama kweli teknolojia zimeshaanza kupenyeza kwa wakulima. Kweli teknolojia sasa zipo. Wakulima wanaelewa na matokeo ni mazuri. Niliweza kuona mikungu ya ndizi mikubwa kwenye banda la Monduli na pia wakulima walionyesha baadhi tekenolojia ambazo kwa kweli zainavutia. Tatizo soko.

Poa-Nimerudi jukwaani


Kwa kipindi cha mwezi mmoja wasomaji wangu mlikosa uhondo kutoka kwa Banzi wa Moro hii imetokana na kubanwa na shughuli nyingi za kikazi, misafara, bajeti, NaneNane na kadha wa kadha . Lakini kwa muda huo wote nimefanya mengi, nimeona mengi na kujifunza mengi. Pindi itakapowezekana nitawamegea humu bloguni. Poa, nimerudi jukwaani.