Saturday, October 24, 2009

Hawakujiandikisha kwasababu mambo ni yaleyale


Uchaguzi wa viongozi wa Serikali za mtaa na vijiji unatarajiwa kufanyika kesho. Wananchi wengi inasemekana kuwa hawakujiandikisha. Ni kweli, Banzi wa Moro katika pitapita yake mjini na vijijini amegundua kuwa watu wamekata tamaa na uongozi wa vijiji na mitaa kwani kasi ya maendeleo hasa huko vijijini ni kidogo sana. Mambo ni yale yale. Viongozi wanaomba nafasi hizo kwa manufaa yao binafsi na wala si ya wananchi. Utasikia ah nikipata nafasi hii baada ya muda wangu wa uongozi kumalizika lazima ninunue 'daladala.'Hivi ndiyo lengo kweli la kugombania uongozi ? Wakati wa kampeni nimeshuhudia vibweka vingi kwa vyama vyote wakishindana kwa rusha roho! Hivi kweli kuna lolote hapa? Ndo maana wengi hawajajiandikisha! (Picha kwa hisani ya gazeti la mwananchi tarehe 24 Oktoba 2009)

Tuesday, October 13, 2009

Mchicha upo wanunuzi je?


Vijana hawa wameamua kuuza mazao ya kilimo hasa mbogamboga. Lakini, wanunuzi wako wapi? Ona mchicha umeanza kunyauka!

Mbuzi wanauzwa


Kama utatembelea 'Kiembe Mbuzi'- Vingunguti na kukuta mbuzi wa aina hii wanauzwa sidhani kama utasita kununua na sifikirii kwamba utampata kwa bei poa. Je, mbuzi wa aina hii wanaweza kupatikana hapa nchini? Fika katika Taasisi ya Utafiti wa Mifugo ya Taifa - Mpwapwa utapata jibu na utaanza kufuga na kuuza mbuzi.

Mtafiti wa Kilimo inaijua Bodi ya Utendaji ya FARA na sekretariati yake?


Kama umeshafika Accra Ghana na kama wewe ni mtafiti wa kilimo lazima utakuwa umefika kwenye makao makuu ya FARA (Forum for Agricultural Research in Africa)- Ni mkono wa kiufundi wa AU katika masuala ya uendelezaji Kilimo na Uchumi wa vijijini katika Bara la Afrika. Pichani ni Bodi ya Utendaji na Sekretariati ya FARA.

Hana uhakika wa soko


Mwangalie msichana huyu anatembeza mboga kwa wateja. Tatizo ni moja je atauza? Upatikanaji wa soko la uhakika kwa mazao ya kilimo ni tatizo linalorudisha nyuma maendeleo ya kilimo barani Afrika na kusababisha wakulima wasipokee kwa urahisi teknolojia bora za uzalishaji.

Vichwa vya Kilimo Afrika


Afrika hatujapiga hatua kubwa katika kilimo. Uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara bado ni mdogo sana. Mazao yatokanayo na mifugo nayo ni haba na duni. Matokeo yake njaa inapiga hodi kwenye bara hili. Hata viwanda vinavyohitaji mali ghafi kutokana na kilimo havitoshelezwi. Hata hivyo kuna vichwa vinavyokuna ubongo kuhakikisha kuwa Afrika inapata teknolojia bora zitakazosaidia kuinua uzalishaji katika kilimo. Angalia vichwa hivyo katika picha.

Mafuta kwenye mahindi tumekwisha!


Wakati wananchi wetu wanahangaika kupata mlo. Wenzetu wako 'busy' kupata mafuta yakuendeshea mitambo kutoka mimea kama vile mahindi. Hii maana yake nini hasa? Chakula kwao kinatosheleza ila wana wasiwasi wa nishati! Upuuzi mtupu. Hivi kweli unaweza kuendesha gari kama una njaa? Watanzania lazima tuangalie suala la nishati na chakula kwa uangalifu mkubwa na kutoa kipaumbele kinachostahili tuwe makini na sera ztu vinginevyo tumekwisha.

Saturday, October 10, 2009

Raphael Benitez wa Liverpool


Mmoja wa makocha wanaojiamini katika Ligi Kuu ya Uingereza ni Raphael Benitez wa Liverpool. Hebu angalia mbwembwe za Benitez pichani. Lakini Banzi wa Moro anaipenda sana timu ya Liverpool kwa sababu gani? Wachezaji wake wanajituma sana hasa Stephen Gerald - The Captain. Lakini zaidi ya hilo nyuzi zao kama wekundu wa Msimbazi!

Hakika Makamu wa Rais ni mfano wa kuigwa


Hivi karibuni nimekuwa nikifuatilia habari za Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt Ali Mohamed Shein kwa karibu sana. Katika safari zake karibu zote iwe za kikazi au binafsi ndani na nje ya nchi yeye huambatana na mkewe Mama Mwanamwema Shein. Tarehe 8/10/2009 alifika katika kituo cha Shule ya Msingi Oysterbay, Dar Es Salaam kwa kusudi la kujiandikisha katika Daftari la wapiga kura, hebu check kushoto kwake ameambatana na nani? (Pichani kwa hisani ya gazeti la Majira).

Wanasoma wajipatie maarifa


Kuna ushahidi wa kutosha kuwa Watanzania wengi hatuna utamaduni wa kusoma. Kusoma kunakupatia maarifa, kunaburudisha na unapata taarifa mablimbali nzuri na mbaya. Tuanze sasa kusoma, tuanze kwenye familia kama inavyoonekana familia hii pichani

Kila mmoja na kuku wake


Wengi hupenda kula nyama ya kuku. Hasa vijana wanapopata 'offer' ukiwauliza utakula nini utasikia - Chips kuku. Lakini kwanini tusifuge kuku majumbani kwetu. Sisemi kuku wa kisasa la hasha hawa hawa tuliowazoea. Labda niseme kuku wa asili. Angalia familia hii pichani ilivyofanikiwa kufuga kuku wengi wa asili mpaka raha kila mmoja na kuku wake. Kila mmoja anatabasamu. Picha kwa hisani ya jarida la KILIMO endelevu Africa.

Wanashangaa maembe!


Ndiyo wanashangaa maembe. Haiwezekani mti mdogo ukazaa maembe kama yanavyoonekana pichani, tena chini chini kabisa. Usibishe. Kuna aina mbalimbali za maembe ambazo huzaa wakati ina kimo kifupi sana. Hii ni baadhi ya teknolojia za kisasa za kilimo za kuzalisha matunda. Ukitaka maelezo zaidi wasiliana na bwanashamba aliye karibu nawe, ofisi za kilimo au vituo vya utafiti.

Wakati wa Ujana wangu



UJANA mali waswahili wanasema. Wakati wa ujana wangu nilikuwa na nguvu na kufanya mambo mengi. Muda mwingi niliutumia kujipatia elimu ndani na nje ya nchi. Wakati mwingine nilikuwa najirusha kwa sana tu hasa DISCO ah nilipenda sana mziki. Nakumbuka miaka ya themanini mimi na ndugu yangu Lawrence Mkude (Sasa Afisa Utumishi Bandari) Silversands kila w-end. Namkumbuka sana DJ. John Peter Pantalakis na HOLLIDAY!

Friday, October 2, 2009

Utafiti shirikishi


Utafiti wa kitu chochote kile ni vizuri ikishirikisha wadau wengi. Pichani wakulima wanawake wakitafiti aina bora ya mpunga. Utafiti huu unajulikana kama utafiti shirikishi. Utafiti wa aina hii hutoa matokeo mazuri yanayokubaliwa na wadau.

Ninatubu Lema Baba shirikishi


Sherehe za kuwaaga wastaafu wa Idara ya Utafiti na Maendeleo ziliratibiwa na Mtafiti Mkuu Bw.Ninatubu Lema (a.k.a Baba Shirikishi). Pichani akipitia kwa makini ratiba ya sherehe.

Baada ya yote ni kulisakata rumba!


Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika Bi Sophia Kaduma akifungua dansi la kuwaaga wastaafu wa Idara ya Utafiti na Maendeleo mwaka 2008/09

Viongozi na wastaafu


Wamestaafu wakiwa wana nguvu na hekima tele. Pichani wastaafu pamoja na viongozi wa Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika katika picha ya pamoja. Watano kutoka kushoto waliosimama ni Bw. Ahmed J.Ahmed (a.k.a Kaka Ahmed) aliyekuwa mkuu wa kitengo cha mipango cha Idara (PEU).

Wawaaa Mama Beatrice Gembe!




Inapotokea shughuli na mwana mama akiwa mmojawapo kati ya wahusika wa shughuli hiyo basi ujue akina mama wenzie watamtunza tu. Ndivyo ilivyotokea kwenye hafla ya tarehe 3/7/2009 kina mama wafanyakazi wa Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika walimzawadiwa mstaafu Mama Beatrice Gembe (aliyekumbatiwa na kutabasamu) aliyekuwa PS wa Mkurugenzi wa Idara ya Utafiti na Maendeleo zawadi mbalimbali. Hebu angalia chereko chereko. Inapendeza enh!

Mwanzo 3 alisherehesha


Wafanyakazi wa Idara ya Utafiti na Maendeleo wanamfahamu Paul Masanja Ndondi (Mwanzo 3) kwa uchangamfu wake na kwa kuchapa kazi katika mazingira tofauti. Huyu amesafiri sehemu nyingi ndani na nje ya nchi na kujifunza mengi. Pichani Mwanzo 3 akisherehesha hafla ya watafiti wastaafu kwenye viwanja vya KILIMO 2.

Sisi tupo


Wakati watafiti wastaafu wakiagwa waliokuwa vijana miaka 10 iliyopita bado wapo. Pichani kutoka kulia Bi Eva Kanyeka, Smwel Undule, Deogratias Lwezaura na John Banzi wakisikiliza kwa makini wosia wa wastaafu.

Hongera Dkt. Haki


Ndivyo inavyoonekana pichani. Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika Bi. Sophia Kaduma akimpongeza na kumkabidhi Mkurugenzi mstaafu wa Idara ya Utafiti na Maendeleo Dkt. Jeremiah Haki. Katika hafla fupi ya kuwaaga wastaafu wa mwaka 2008/09 kutoka Idara ya Utafiti na Maendeleo. Dkt. Haki ameiongoza Idara hiyo kwa mafanikio makubwa takribani kwa miaka 10. Tafrija hiyo ilifanyika tarehe 3/07/2009 kwenye viwanja vya Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika - KILIMO II.

Nampigia debe mrembo wa Moro 2009


Yehu! Kinyang'anyiro cha Miss Tanzania ni leo katika Ukumbi wa Mlimani City -Dar es Salaam. Mshindi ataibuka na gari aina ya Suzuki Vitara pamoja na fedha taslimu 9m/=. Banzi wa Moro anampigia chapuo mrembo wa Moro Bi Tory Oscar. Tuvute subira macho yetu wote luningani. TBC Live mwanawane!

Huyu ndiye Dkt Alfred Moshi wa mahindi


Wadau wa Kilimo hapa nchini hasa wa kanda ya Mashariki unapozungumzia mahindi basi akilini mwao unamzungumzia Dkt. Alfred Moshi aliyekuwa Mkurugenzi wa Utafiti Kanda ya Mashariki. Moshi kwa muda mwingi amekuwa akitafiti mbegu bora ya zao la mahindi. Pichani Dkt Moshi akitoa neno kwa niaba ya watafiti waliostaafu mwaka 2008/09 kwenye viwanja vya Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika - Kilimo II kwenye tafrija ya kuwaaga waliyoandaliwa na Idara ya Utafiti na Maendeleo tarehe 3/07/2009

MORO - Neema ya vyakula


Mkoa wa Morogoro ni mmoja ya mikoa iliyobarikiwa kuwa na mazingira mazuri kwa kuzalisha mazao mbalimbali ya chakula. Hivi karibuni Makamu wa Rais Mh. Dkt.Ali Shein alitembelea kijiji cha Lupilo, Mahenge mkoani Morogoro. Angalia karanga, viazi mviringo, vitungu saumu na maji pamoja na nyanya vilivyojaa sokoni bwelele!

Makwaia wa Kuhenga


Ni mwandishi mwandamizi hapa nchini. Kalamu yake imefichua mengi na kuyaweka bayana. Ni mjuzi wa lugha pia ni mcheshi katika maisha ya kawaida. Huyu ni Makwaia wa Kuhenga. Nimemfahamu mwandishi huyu tangu miaka ya 80 na hadi leo ninapoona makala zake huwa nazikimbilia kuzisoma kwani hufanya uchambuzi wa kina.

Thursday, October 1, 2009

Dr. Shao - kama FORM VI vile!


Dr.Frank Shao ni mmoja ya Wakurugenzi waliopata kuongoza Idara ya Utafiti na Maendeleo. Miaka zaidi ya kumi sasa tangu astaafu lakini yu na afya na nguvu tele. Muulize Dr. Shao atakwambi ni nidhamu ya maisha na kuwa na kiasi. Angalia kinywaji anachokunywa- MAJI. Hapa alikuwa mwalikwa kwenye tafrija ya kuwaaga wastaafu wa Idara ya Utafiti na Maendeleo mwaka 2008/09

Komunio ya Kwanza -Matombo


Sikukuu ya kupata Komunio ya Kwanza kwa waluguru wa Matombo ni Sikukuu kubwa isiyofanyiwa mzaha hata kidogo. Maandalizi kwa watoto ya kiroho na kimwili ni makubwa na sherehe ni nzito. Banzi wa Moro alishuhudia sherehe kabambe za Ekaristi katika Kanisa la Watakatifu Petro na Paul Matombo. Ibada iliyoendeshwa tarehe 27/9/2009 katika Parokia hiyo ni ya kukumbuka. Siku hiyo pia kinanda kipya kilichonuliwa na waumini pamoja na wafadhili wazalendo kilichezwa kanisani. Pichani watoto waliopata ekaristi wakibebwa kuelekea nyumbani huku ngoma ikiwasindikiza - Nafikiri ilikuwa sh2!