Friday, July 30, 2010

Hii ndiyo timu ya wapelembaji


Idara ya utafiti na Maendeleo iliyoko Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika imeweka utaratibu mzuri wa kupelemba na kutathmini shughuli za utafiti katika kanda zake saba za utafiti ili kuweza kufahamu utekelezaji wa mipango ya utafiti ufanisi, changamoto na kuweka mikakati ya kupambana na changamoto zinazojitokeza. Pichani wanaonekana wapelembaji waliotumwa kanda ya kaskazini mwezi Juni 2010.

Mwanamke Power Tiller


HATA wanawake wanastahili kuwa na mashine zitakazo rahisisha kazi za shambani kwa ufanisi zaidi. Power tiller inaweza kufanya shughuli nyingi za shambani. Pichani mwanamke akifurahia power tiller.

Yapo maharage yaliyotafitiwa


KAMA ilivyo kwa mahindi.Kaya nyingi hapa nchini hutumia maharage kwa mboga. Ni ukweli usiofichika kuwa kama unampata mpishi mzuri akakupikia maharage kwa nazi na akaunga wali kwa nazi hakika hutaacha kula chakula hicho. Watafiti wetu wameshafanya utafiti na wanaendelea kufanya utafiti wa aina mbalimbali za maharage. Kuna maharage ya rojorojo kuna maharage yanayopendwa kwa rangi yake na hata yale yanayostawishwa kwa ajili ya kusindika au kula yakiwa machanga. Waulize watafiti wa kutoka Selian Arusha na Uyole Mbeya utapata jibu na kuanza kustawisha maharage au kula maharage au kufanya biashara ya maharage.

Watafiti wanapojikita na utafiti wa Mahindi


HAKUNA ubishi watanzania wengi wanakula ugali.Sehemu nyingi za nchi hii zinastawisha mahindi. Utafiti wa mahindi katika nchi hii umeanza muda mrefu na umepata mafanikio makubwa pia umekutana na changamoto nyingi. Utafiti wa mahindi hasa hufanywa na kituo cha utafiti Uyole Mbeya,Selian Arusha na Ilonga Kilosa. Hebu angalia picha ya mahindi yanayofanyiwa utafiti na watafiti kutoka Selian. Hapa lazima uvune tu.

Si mpunga ni ngano


Watu wengi wa pwani hawaufahamu mmea wa ngano ingawa ni hodari sana wa kula chapati mikate na maandazi. Nchi yetu imebahatika kuwa na sehemu zinazozalisha ngano hasa kanda ya kaskazni na Nyanda za Juu Kusini. Kituo cha Utafiti wa Kilimo cha Selian kina jukumu la kutafiti uzalishaji wa ngano. Pichani ngano aina ya JUHUDI kwenye mashamba ya majaribio.

Hata viazi vitamu vinafanyiwa utafiti pia


Si viazi vyote unaweza kutumia majani yake kama mboga ya matembele! Aidha si viazi vyote vinaweza kuwa na unga mwingi. Vile vile viazi vinaweza kuwa na rangi aina tofauti njano, nyeupe hata zambarau. Kazi ya utafiti ni kuzalisha viazi kutokana na matakwa ya wadau na soko

Kilimo mseto wa mahindi na mbaazi


WATAFITI wa kilimo kanda ya Kaskazini wanaendelea na utafiti wa kilimo mseto cha mahindi na mbaazi katika mashamba ya wakulima ili wakulima wenyewe waweze kujionea faida ya kilimo hicho. Moja ya faida ni kurutubisha ardhi. Lakini pia mkulima kwa eneo hilo hilo mkulima anapata mboga na nafaka. Hapa ana uhakika wa chakula na pia kuongeza kipato kwenye familia.

Mkurugenzi anapojishughulisha na utafiti


Ndivyo afanyavyo Kaimu Mkurugenzi wa Utafiti wa Kilimo kanda ya Kaskazini Dkt. Mbuyi Mugendi aliponaswa na blog hii bila kufahamu akiielezea timu ya kitaifa iliyotumwa kupelemba na kutathmini shughuli za utafiti katika kanda yake. Ni wangapi wanaendelea kufanya kazi za taalama zao ingawa wanajukumu pia ya kusaini hundi?

Kijana katika utafiti


Mvulana huyu kutoka kanda ya kaskazini anashirikiana na watafiti katika kutafiti uzalishaji wan nyanya. Angalia nyanya zilivyostawi vizuri. Kwa kupitia utafiti atafahamu ni aina gani za nyanya astawishe katika mazingira yake. Ni kwa vipi atapambana na changamoto za magonjwa na wadudu washambuliao mimea ili aweze kuzalisha kwa faida.

Thursday, July 29, 2010

Kilimo cha Miti na Mazao-Agroforestry


AGROFORESTRY-Kilimo cha Miti na Mazao (Tafsiri yangu). Wengi hutafasiri kuwa ni Kilimo Mseto ambapo mimi sikubaliani nao. Kwani mseto ni mchanganyiko. Tuachane na habari ya tafsiri tuangalie faida ya Kilimo cha Miti na Mazao. Pamoja na kutunza mazingira, kilimo hicho kinatusaidia katika kuwa na kipato mbadala kwa vipindi tofauti mwaka mzima. Unaweza kuvuna mbao,matunda,asali,nafaka,mboga na mazao jamii ya mikunde. Kilimo hiki kinapaswa kuendelezwa hapa nchini kutokana na hali halisi ya mazingira tuliyo nayo.

Kikwete Vs Slaa


UCHAGUZI ujao unaanza kuwa na mvuto hasa pale CHADEMA walipotumbukiza kete yao SLAA kuwa mgombea wa kiti cha Urais. Pamoja na ukweli kuwa si rahisi kwa Kikwete kuangushwa na Slaa lakini nionavyo mpambano utakuwa wa kukata nashoka hasa mikoa ya Kaskazini mwa Tanzania na Nyanda za Juu Kusini. TUSUBIRI MATOKEO.

Bakhresa na kiwanda cha matunda Mwandege

Kiwanda kipya cha kusindika matunda cha Bakhresa kimeanza kufanya kazi katika eneo la Mwandege wilaya ya Mkuranga kilometa chache kutoka Kongowe mkoa wa Dar Es Salaam.Kiwanda hiki kwa hakika ni mkombozi kwa wakulima wa matunda hapa nchini hasa wa mikoa ya Pwani, Dar Es Salaam, Morogoro na Tanga ambako kunazalishwa aina mbalimbali za matunda. Huu ni fursa ya pekee kwa wakulima kuongeza uzalishaji wa matunda kwani soko lipo. Kwa habari ambazo si rasmi zinasema kuwa kiwanda hicho hutayarisha juisi nzito na kuyahifadhi katika magudulia makubwa kabla ya kupeleka Vingunguti kwa ajili ya kutengeneza juisi laini tayari kwa matumizi.Kiwanda hiki kimeanza kutoa ajira kwa watanzania.

Chuma-Banzi-Luanda wanapokutana

Siku ya tarehe 25/07/2010 marafiki wa siku nyingi yaani Banzi, Chuma na Luanda tulikutana pale Msimbazi Centre. Ni kipi kilichotukutanisha? - 'Lukemo lwa Lusona' (mwito wa ngoma). Aliyetoa mwito ni nani? Ni Bwana Michael Luanda.

Sisi watatu ni marafiki wa siku nyingi. Sote tumesoma Shule ya Msingi Matombo miaka ya mwanzo wa sabini.Sote kwa kipindi fulani tumeishi Kigogo! Isitoshe mimi na Luanda tumeenda Sekondari ya Njombe mwaka 1974. Sasa Luanda anaozesha shemeji yake. Ametuita tushirikiane kwa hilo.Tulipokutana tulikumbuka mambo mengi. Msalabani, solono za mtoni mfizigo,Kiswira Sports Club na hatukukosa kugusia mbunge mtarajiwa wa Morogoro kusini!

Thursday, July 22, 2010

Padri Antipas Abdon Nzegesela


Tulipata Neno la Bwana kutoka kwa Padri Antipas Abdon Nzegesela (mdogo wangu). Huyu ndiye aliyetuozesha. Hebu fikiria mtu anazaliwa unamuona anakua hadi kuwa Padri baadaye anakufungisha NDOA ni wangapi waliojariwa kupata bahati hii?

Namimi nilikula chakula cha bwana


Ndiyo na mimi Banzi wa Moro nilikula chakula cha Bwana huku Bestman wangu Mr.Nestor Kobelo(nyuma yangu) akitafakari. Hiyo ilikuwa tarehe 2/8/1997. Bado naendelea kupata chakula cha kiroho au kwa kiluguru 'tonge ja mitondo'

Damu ya Kristu Nancy


Mwaka 1997 tarehe 2/8/1997 nilifunga pingu za maisha na mke wangu mpenzi Nancy Ireneus Mbawala katika Kanisa Katoliki Mashahidi wa Uganda-Magomeni jijini Dar Es Salaam kwa hiyo ifikapo tarehe 2/8/2010 tutatimiza miaka 13 ya ndoa. Tumejitahidi siyo. Pichani Nancy akinywa damu ya Kristu siku ya harusi yetu.

Kama mambo yenyewe hivi STAR MEDIA mtafulia


MWEZI wa tano mwaka huu nilinunua king'amuzi kutoka kampuni ya STAR MEDIA(Tanzania) kwenye kituo chao cha Buguruni kwa lengo la kupata chaneli nyingi kupitia luninga yangu. Kilichonivutia zaidi ni bei nafuu pamoja na antena ambayo siyo lazima uwe na dish.

Tatizo linakuja pale unapoongeza muda wa matumizi kwa kutumia vocha zao. Maelezo yanayotolewa kwa kweli ni magumu.Binafsi napata shida kuweza kupata huduma za chaneli kupitia king'amuzi hicho.

Wale akina dada waliopo vituoni Buguruni na Ukonga hawajui kumuhudumia mteja. Tahadhari nawapa msiporekebisha hali hii wateja tutawakimbia sasa hivi oh!

Wednesday, July 21, 2010

BEN 1977


Mwaka 1977 Benjamin Mkapa (kulia) alipokuwa Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje. Alikuwa kijana na machachari kwelikweli!

Kwa vituo vya LUKU-TANESCO nakupa shavu

Vituo vya kununua vocha za LUKU kwa matumizi ya umeme vimezidi kuongezeka jijini Dar Es Salaam na kuanza kupunguza misururu ya watu katika vituo hivyo. Vituo vimesambazwa sehemu nyingi jijini na hivyo kupunguza kero kwa watumiaji wa huduma hiyo ya umeme. Kwa utaratibu huu kwanini nisiwape shavu TANESCO?

Zifahamu njia za mabus ya wanafunzi ya CRDB


Hizi ndizo njia za mabasi ya wanafunzi ya CRDB katika jiji la Dar Es Salaam.

Posta- Mbagala: Posta, Mnazi Mmoja, Shule ya Uhuru, Mvinjeni, Mgulani,Mtoni na Mbagala Mwisho.

Mwenge-Buguruni: Mwenge,Ubungo Darajani, External, Tabata Relini na Buguruni

Mwenge-Bunju:Mwenge, Makongo, Bondeni, Tangibovu,Makonde, Afrikana, Mbuyuni,Tegeta,Boko na Bunju

Posta-Gongolamboto:Posta,Mnazi Mmoja, Buguruni, Tazara,Vingunguti, Ukonga na Gongolamboto

Posta-Kimara-Mbezi Luis: Posta, Mnazi Mmoja, Baridi, Fire, Magomeni, Mwembechai, Manzese,Shekilango-Mkoani Ubungo, Kimara-Baruti,Kimara-Suka na Mbezi Luisi

Utaratibu mzuri lakini mabus ni machache sana. Leo asubuhi nimeshuhudia pale Mbagala jinsi wanafunzi walivyojazana kwenye bus moja kuna haja ya kuongeza mabus zaidi na kuyatunza yaliyopo.

Huyu ndiye Mwenyekiti wa Dar Young Africans


Huyu ndiye Mwenyekiti wa watoto wa Jangwani - DAR YOUNG AFRICANS SPORTS CLUB. Anaitwa LLYOD NCHUNGA. Je, ni mtu wa mpira? Maana Soka ni fitina!

Tuesday, July 20, 2010

Ajabu Yanga hawamjui mwenyekiti wao


Amini usiamini watani zetu YANGA hawamfahamu vizuri mwenyekiti wao aliyechaguliwa siku ya Jumapili. Uchunguzi nilioufanya hapa ofisini kwa washabiki wakuu wa wana Jangwani akiwemo Bw.Salehe Mkwawa umedhihirisha wazi kuwa mtu huyo hafahamiki na wengi. Hii ni dhahiri kuwa aliyechaguliwa si mtu wa mpira! Kwa kukumegea tu msomaji wa blog hii kuwa mwenyekiti huyo anajulikana kwa jina la LLYOD NCHUNGA na makamu wake ni Davis Mosha!

Sekta ya Kilimo


Unapozungumzia sekta ya kilimo ni pamoja na mifugo,nyuki,samaki,mazao ya mimea. Kwa hakika hii ndiyo sekta inayoweza kumkwamua mtanzania kutoka kwenye uvungu wa umaskini. Hali ya wakulima ikiwa nzuri ule usemi wa maisha bora kwa kila Mtanzania utakuwa kweli. TUJIKITE HUKO.

Tujipange vizuri tuongeze uzalishaji katika kilimo


Hebu angalia pichani baadhi ya mazao yanayostawi hapa Tanzania kuna ndizi,muhogo,mtama,zabibu.kabichi,viazi vitamu,maharage,ngano,mpunga,alizeti,mahindi na mbaazi. Hivi kweli nchi hii ni ya kulia njaa? Ni kwanini wananchi wake bado ni masikini? Ni vizuri wote tukajipanga na kupeana muda wa utekelezaji wa uzalishaji wa mazao mbalimbali kwa kiasi kinachohitajiwa na ubora unaotakiwa. Kilimo Kwanza isiwe maneno tu tushiriki sote.

Mnada wa Pugu unavujisha mapato


Leo hii nimesomam habari muhimu sana kwenye gazeti la serikali linalotolewa kila siku la DailyNews. Habari hiyo inatufahamisha kuwa Serikali hakosa mapato mengi kwenye soko la mnada wa mifugo wa Pugu. Utafiti ufanywe ili tuweze kufahamu mnada unaweza kuiingizia kipato cha kiasi gani serikali?

Jamani Pweza huyu

Yule Pweza aliyekuwa akitabiri matokeo mbalimbali ya mechi za kombe la dunia amefanya kweli. HISPANIA ni bingwa wa Soka 2010! Jamani Pweza huyu kazua jambo. Akija Tanzania atatutabiria mambo mengi!

Saturday, July 10, 2010

Dr. Shein kidedea!


Kama ilivyotegemewa na wengi, Dk. Ali Mohamed Shein ameibuka kidedea baada ya kupitishwa kuwa mgombea urais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika uchaguzi utakaofanyika mwezi Oktoba mwaka huu 2010.

Pweza huyu vipi? Eti anatabiri Hispania bingwa 2010


Pweza mwenye umri wa miaka miwili anatabiri Hispania itashinda dhidi ya Uholanzi kwenye fainali za kombe la dunia 2010 zitakazochezwa Afrika ya Kusini hapo kesho tusubiri tuone. Pweza huyu alishatabiri kushindwa kwa England, Argentina na Ujerumani pia.

Mwana FA bado upoupo kwanza?


Siyo siri mtu wangu Mwana FA tangu utoe kibao chako "Bado nipo nipo kwanza" umetulia kabisa sijakusikia au ndo unataka kuja na moja kuliko? Achia vitu mwanangu tuna kumis sana na filosofia zako.

Thursday, July 1, 2010

HUREE MWAKA MPYA!


Leo tarehe 1/7/2010. Serikali inaanza mwaka mpya wa 2010/11. Mwaka huu tutegemea mambo mapya mengi tu. Uchaguzi wa kuingoza serikali ya Jamhuri ya Tanzania unafanyika mwaka huu kwa hiyo matarajio ya wengi ni makubwa.Hata hivyo dalili za bajeti zinaonyesha kuwa tutajifunga mikanda zaidi kwa bidhaa kupanda bei. Hali ya maisha ya wananchi wa kawaida kwa kweli itakuwa si nzuri. Lakini kama tutatekeleza vizuri mipango tuliyoipanga katika kila sekta mambo yatakuwa shwari.