Friday, February 25, 2011

Hii ndiyo FARASI FC


Timu ya wanawake ya Alex Kajumulo huko majuu inaitwa FARASI FC. Hongera Kaju kwa kukipa shavu Kiswahili huko majuu!

Radio ya Nyerere


Hii ndiyo radio iliyokuwa iikimpatia 'news' Baba wa Taifa Mwl. J.K.Nyerere.

Wanafunzi mbuyuni


Wanafunzi mbuyuni? Jibu tunalo wenyewe.

Kinyume chake

Barabara Bora Kichocheo cha Uchumi


Barabara bora na imara ni kichocheo cha uchumi. Hurahisisha mawasiliano na kuboresha hali ya maisha ya watu wake.

Hospitali duni


Hospitali ya aina hii ni vigumu sana kwa mgonjwa kuwa na imani ya kupona. Ni vigumu pia kwa waganga na wahudumu kufanya kazi katika mazingira haya. Tujirekebishe haraka

Kikao cha Baraza la Mawaziri


JK anapkuwa Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri. Lazima maamuzi ya kikao hiki yaheshimike.

Shimboni Mangi!



Hii ndiyo Mweka College iliyopo mkoani Kilamanjaro, Tanzania.

Ni bora kuliko mkokoteni


Hii ni pikipiki ya Toyo na trailer lake.Jijini Dar Es Salaam zinaanza kupata umaarufu mkubwa kwa kusomba mizigo hasa wafanyabiashara ya mazaoe, kusomba vinywaji na hata kwa wale wanaohama kutoka nyumba moja hadi nyingine. Ni bora kuliko mkokoteni na ni nafuu kuliko pickups!

Liverpool ilivyoiua Chelsea


Nawapenda Liverpool kwa uzalendo wao. Timu hii haitabiriki. Angalia jinsi walivyoiua Chelsea hivi karibuni licha ya kuondokewa na Torres. Kweli "You will never walk alone."

Changu na ugali


Napenda sana samaki wa kukaanga hasa samaki aina ya changu. Aina hii ya samaki hupatikana maji chumvi.

Monday, February 21, 2011

Gongolamboto ni zaidi ya Mbagala



Ndiyo ilivyokuwa usikuwa wa jumatano ya tarehe 16/2/2011. Ilianza kama nguromo za radi huku wengi tukitegemea mvua kubwa kunyesha hivyo kuondokana na mgao wa umeme! Haikuwa hivyo, kumbe ni mlipuko wa mabomu ulioacha simanzi kubwa kwa wakazi wa jiji la Dar Es Salaam. Kila mmoja aliokoa uhai wake. Wachache walikumbuka wake zao, watoto wao, mama zao, waume zao dada zao, kaka zao, shangazi zao, wajumbe zao na marafiki zao. Kuna walioacha magari, tv,dvd players, nyumba bila kufungwa na kuanza kukimbia hovyo. Kweli mabomu ya Gongo la Mboto ni zaidi ya Mbagala!

Friday, February 4, 2011

Picha Ya JK Na Freeman Mbowe: Tafsiri Yangu


Ndugu Zangu,


JANA tumeona picha ya pamoja; JK akiwa na Freeman Mbowe.

Katika sanaa ya picha inasemwa, kuwa picha moja yaweza kuwa sawa na maneno elfu moja. Picha moja yaweza kutoa tafsiri nyingi.


Nimeitafakari picha ile. Ni moja ya picha nzuri iliyobeba ujumbe muhimu kwa Watanzania hususan tukikumbuka Uchaguzi uliopita na matukio baada ya uchaguzi.


Ni picha inayobeba matumaini badala ya kukatisha tamaa.

Inaonyesha, kuwa hata baada ya uchaguzi, maisha ya kisiasa hayana budi kuendelea. Na siasa si ugomvi. Siasa ni jambo jema. Ni wakati sasa kwa akina Freeman Mbowe na wenzake wa CHADEMA kuvua magwanda yale ya khaki na kushiriki maisha ya kawaida ya kisiasa.


Kama ningewashauri CHADEMA, basi, ningewaambia, kuwa , kwa kiongozi, vazi pia hutuma ujumbe kwa unaowaongoza. Magwanda yale ya CHADEMA yamekaa kijeshi zaidi. Labda yalitosha kuyatumia katika ’ mapambano’ ya kampeni za uchaguzi, lakini si sasa. Uchaguzi umeshapita.


Huu ni wakati wa kurekebisha tofauti zilizojitokeza na kwenda mbele. Na tuna cha kujifunza kutoka Unguja. Itakumbukwa, kuwa baada ya matokeo ya uchaguzi wa mwaka 2005, Maalim Seif alikaririwa akitamka kuwa; ”Hakuna tena mufaka wa tatu". Rais Karume naye akakaririwa akitamka; "Sitaki kusikia habari ya Serikali ya mseto". Haya , leo Maalim Seif yumo ndani ya Serikali ya Mseto!


Na hapa kwetu CHADEMA walianza na kauli za kutoitambua Serikali. Nitakuwa mtu wa mwisho kushangaa siku ile Dr Slaa na JK watakapokaa meza moja na kongea kirafiki. Na tunaamini katika mazungumzo kama njia ya kutatua migogoro yetu ya kisiasa.


Kupitia picha ile ya jana tumeona busara za Rais Jakaya Kikwete, kusimama na kuongea na Freeman Mbowe katika hali ya kirafiki. JK ameonyesha kujiamini na kuendelea na kazi ya kuifatuta suluhu ya migogoro ya ndani ya nchi.


Kwa kiongozi wa kisiasa kuitafuta suluhu si udhaifu, ni ujasiri. Na huo ndio ukomavu wa kisiasa pia. Naamini, ndani ya CCM kuna wanaoogopa kupiga picha wakiwa pamoja na viongozi wa CHADEMA. Ni kwa kuhofia kuandamwa na wenzao ndani ya chama.



Tumefika mahali tukubali, kuwa siasa si uadui. Profesa wa Sayansi ya Siasa , Robert Dahl alipata kuandika;" Ni wajibu wa dola kuendesha juhudi za kutafuta suluhu za migogoro ya kijamii. Siasa ni hatua za majadiliano endelevu yenye kuhakikisha migogoro inapatiwa ufumbuzi kwa njia za amani". ( Theory and Methods of Political Science Uk. 211)



Tofauti za kifikra na kimitazamo ni mambo ya kawaida katika siasa. Kunahitajika majadiliano endelevu katika kupata ufumbuzi wa migogoro. Si lazima papatikane mshindi katika kila mgogoro, wakati mwingine hutengenezwa mazingira ya pande zote mbili kushinda, kila mmoja kujisikia ameshinda, a win- win situation.



Kwa sasa CHADEMA iukubali ukweli, kuwa Uchaguzi uliopita umeshapita. Kwamba Serikali iliyo madarakani kwa sasa ndio hiyo inayoongozwa na JK kama Rais. Hatuna Rais mwingine. Hatuna Serikali nyingine.


Na CCM nayo iukubali ukweli, kuwa wakati umebadilika na kuwa wananchi wanaukubali upinzani. Na kwamba kwa sasa, CHADEMA ndio chama kikuu cha upinzani kikifuatiwa na CUF.

Vyama hivi na vingine vyenye uwakilishi bungeni, vina lazima ya kushirikiana katika mambo ya msingi na yenye maslahi kwa taifa letu.


Tuache kujichimbia kwenye mahandaki. Tuanze sasa kuijenga nchi yetu kwa pamoja. Hatuwezi kuijenga nchi yetu katika hali ya vurugu , uhasama na chuki. Hii ni nchi yetu. Ni nyumba yetu tunayoijenga. Kwanini tugombanie fito?


Maggid

Dar es Salaam

Februari 3, 2011

Thursday, February 3, 2011

Ugemaji je?


Wataalamu ugemaji wa pombe ya mnazi una madhara kwa uzalishaji wa nazi?

Mahindi sh ngapi?


Msela anajibu dala! Du. Hii ndo bongo mtasha hapa kila kitu. Siyo bisi ni mahindi orijino ya kuchoma!

Pikipiki inavyorahisisha uchukuzi


Si kwa abiria tu.Kuingia kwa pikipiki nyingi za Kichina hapa nchini zimesaidia sana kurahisisha usafiri wa abiria pamoja na mizigo. Pichani mikungu ya ndizi ikisafirishwa kwenye tela la pikipiki. Haya ni maendeleo.

Vichanga vya Mwananyamala


Tukio la hivi karibuni la kukuta vichanga 10 wakiwa katika shimo moja kwenye maeneo ya Hospitali ya Mwananyamala linajieleza lenyewe jinsi Taifa linavyoangamia. Hapa nani wa kumlaumu? Tujiulize sote. Hili ni janga.

Mboga matopeni


Tunajiua wenyewe. Akina mama hawa wanachotaka ni fedha. Walaji wanataka chakula. Bwana afya hayuko. Tunakula vyakula vichafu. Picha hii impegwa Dodoma (Hisani ya Gazeti la Mwananchi 14 Jan 20110

Siyo nyanya ni matunda damu


Tanzania imebahatika kuwa na mazingira mabalimbali yanayoweza kustawisha mazao ya aina mbalimbali. Kwa mfano matunda damu yanayopatikana ulaya hapa kwetu yanlimwa kwa wingi sehemu za baridi kama vile Lushoto, Mbeya, na Mgeta (Morogoro). Pichani mfanyabiashara akiyahifadhi matunda damu kwenye vifuko tayari kwa kuyauza.

Watafiti wajengewa uwezo


Moja ya majukumu makuu ya Idara ya Utafiti na Maendeleo ya Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika ni kujenga uwezo wa watafiti wake. Mwezi Desemba 2010, Idara iliandaa mafunzo ya wiki moja ili kuwanoa watafiti katika kufanya Impact na Adoption Studies ili kuweza kupima mafao ya teknolojia katika kukuza kilimo chetu na kupima jinsi wakulima walivyoweza kupokea teknolojia zilizozalishwa. Mafunzo hayo yalifanyika mjini Dodoma kwa kutumia wataalamu wa ndani wakiwemo Dr. January Mafuru (ARI-Ukiriguru), Dr Jackson Nkuba (ARI-Maruku) na Bw Deogratias Lwezaura (DRD-HQ-DSM). Mratibu wa Mafunzo Bw. Ninatubu Lema - Mkurugenzi Msaidizi - FSR/SE. Watafiti wapatao 30 walishiriki mafunzo hayo wengi wao wakiwa ni Wachumi Kilimo.

Tuesday, February 1, 2011

Alivyozikwa Chief George Patrick Kunambi


Nianzie mchana wa tarehe 28/1/2010 Ijumaa, pale Msewe-nyumbani kwa marehemu Chief George Patrick Kunambi. Naingia maeneo ya msiba nakutana na rangi za kijani nyingi zilizovaliwa na vijana(napata picha kuwepo kwa CCM), hatimaye nakutana na umati mkubwa wa watu uliofurika sehemu ya msiba, wengine wakijipanga kwenye mistari mirefu.Wakati bado nashangaa, sauti kutoka kipaaza sauti 'ukishatoka kumuaga marehemu unaunga mstari wa kupata chakula kabla ya kuanza taratibu za mazishi.'
Hili la kumuaga nalipa kipaumbele (najisemea kimoyomoyo kumbe nimewahi!).

Naingia ndani ya nyumba kubwa,nyumba ya Chifu nakuta jeneza lililopambwa vizuri na la kupendeza likiwa na mwili wa marehemu Chief George Patrick Kunambi. Napiga ishara ya msalaba. Ni kweli 'Babu Kunambi' amefariki.

Taratibu za mazishi zinatangazwa kwa kupata salamu kutoka kwa wakilishi wa taasisi mbalimbali, na vyama vya siasa. Alikuwepo Mhe. Mbowe Mwenyekiti wa Chadema aliyemuelezea Chifu Kunambi kuwa alikuwa ni mwenye mapendo makubwa, mzalendo, na mchapa kazi. Kisha wasifu wa marehemu ulisomwa.

Chifu kunambi alizaliwa kijini Matombo tarehe 16, Agosti 1916.Chief Kunambi alipata elimu yake ya msingi katika shule ya msingi Matombo, Sekondari Tabora, Elimu ya Juu Makerere Uganda na hatimaye shahada ya Uzamili (MA) huko Marekani. Amefanya kazi katika Taasisi mbalimbali hapa nchini ikiwemo Chuo Kikuuu Dar Es Salaam akiwa kama Msajili. Aidha amefanyakazi katika Taasisi za Usafirishaji na hadi umauti unamkuta alikuwa Mwenyekiti wa Baraza la Majadiliano la Mamlaka ya Bandari kwa takribani miaka 25.Ni mmoja wa waanzilishi wa chama cha TANU kilicholeta UHURU wa Tanganyika.

Katika uhai wake Chifu Kunambi alijaliwa kufunga pingu za maisha na Bi.Bernadetha Namphombe Kunambi (Marehemu) na kubahatika watoto wanne (wanaume 2 na wanawake 2) walio hai ni wawili, Lucas Kunambi na Dr.Patricia Kunambi. Ameacha wajukuu wapatao saba.

Baada ya wasifu wake kusomwa watani wa waluguru (wasukuma, wanyamwezi, wangoni, wahehe,wadigo, wasambaa, Wapogoro...)walipata 'nguto' zao na hatimaye Jeneza la marehemu liliingizwa kwenye gari maalumu na kuelekea kanisani kwa misa takatifu huku ngoma maarufu ya waluguru ijulikanayo kwa jina la Keyamba ikisindikiza taratibu!

Ibada ya Misa Takatifu iliongozwa na Mhashamu Askofu Athony Banzi wa jimbo la Tanga akisaidiwa na Askofu Telesphor Mkude wa jimbo la Morogoro na mapadri wengine kama Mogella, Prof.Mkude,Padre Jakka kutoka Parokia ya Kidatu, Padri Kwembe kutoka St.Peters-DSM pamoja na Mapadre wenyeji wa Msewe.

Watu waliokuja kumsindikiza Chifu Kunambi katika safari yake ya mwisho ni wengi.Waluguru walio wengi walionekana siku ya mazishi ya Chifu wao. Wageni wengine waliohudhuria ni Mh.Pius Msekwa (Katibu Msaidizi wa CCM), Mzee Kingunge Ngombale Mwiru, Mhe. Betty Mkwasa, Mhe. Sophia Simba, IGP mstaafu Omari Mahita, Kamishna Mkuu wa Magereza Mstaafu Nicas Banzi,Bw. Nibuka Mnzeru (Mbunge wa zamani wa Morogoro mjini)na Dkt.Gregory P.Mluge.

Utani kwenye mazishi hayo haukukosa kwani kwa muda mrefu kuna watani wawili waliojifanya wanandoa waliojipamba vizuri huku wakiburudika kwa KONYAGI walionyesha utani wao kwa wafiwa ambao kwa mila za waluguru ni ruhusa!

Hatimaye muda wa saa 11.30 jioni jeneza la Marehemu Chifu Kunambi lilishushwa taratibu kaburini nyumbani kwake Msewe kuhitimisha mazishi yake.