Monday, March 12, 2007

USAFIRI DAR - JUMATATU

Leo nimeamua kuandika taabu ya usafiri wa daladala hapa DAR hasa siku ya Jumatatu.

Leo nimeamka saa 10.30 asubuhi ili niwahi usafiri wa kunifikisha Mbagala. Nilipata bus la kwenda Ubungo. Kabla ya kufika Mbagala Kizuiani tayari foleni ilishaanza. Na tulipofika Mbagala Mission gari moja dogo lilijichomeka kati ya bus letu na gari jingine kutoka mjini, ajali! Hapo ndipo shughuli ilipoaanza. Safari ikafa, tukarudishiwa fedha zetu. Mimi na abiria wengine tulianza kutembea kwa miguu.

Nilitembea hadi Mtoni kwa Aziz Ally kwani nilipofika Mtoni Mtongani kulikuwa na umati mkubwa wa watu ukisubiri usafiri. Nilipata usafiri wa kwenda Tandika. Nilipofika Tandika kwenye vituo vya mabus abiria walikuwa wamefurika usafiri bado ulikuwa shida. Nilipata usafiri wa kugombea na kupata kiti cha wanafunzi, kile kiti kinachounguza hadi niliposhuka pale Tazara-Kilimo. Nilikuwa nimeshachoka sana, nimelowa jasho sana na tayari ilishafika saa 1.45. Hiyo ndiyo adha ya usafiri DAR.