Thursday, June 26, 2008

HIVI KWELI KUNA MBUNGE WA KUKWAMISHA BAJETI YA SERIKALI?

Bunge linaloendelea hivi sasa ni la Bajeti. Imeshasomwa Bajeti ya Wizara ya Fedha na Uchumi na Ofisi ya Waziri Mkuu. Majadiliano yamefanyika na yanaendelea kufanyika. Wabunge wanasimama na kutoa michango yao ile ile wanatoa kasoro zile zile za kila mwaka lakini hatimaye wanasema wanaunga mkono bajeti kwa asilimia mia moja. Mi mbona sielewi? Unaikosoa halafu unaiunga mkono kwa asilimia 100?

Leo asubuhi nikiwa uwanja wa ndege wa kimataifa pale Dar nilikutana na rafiki yangu wa siku nyingi mtaalamu wa Kodi Bw.Viani Komba ambaye tulisoma pamoja kule Tosamaganga Sekondari . Alisema, banzi hatuko serious na bajeti. Nchi nyingine wakati bajeti ya Wizara ya Fedha inasomwa siku hiyo ni ya mapumziko ya kitaifa kila mwananchi anafuatilia hatua hatua jinsi bajeti hiyo inavyowasilishwa na mwasilishaji baada ya kuwasilisha anapata glass ya maji hata kama nchi hiyo ni ya baridi! Hii ina maana bajeti ni kitu muhimu sana ni siyo cha mchezo kama inavyoonekana hapa kwetu. Lakini ninajiuliza kuna mbunge ambaye anaweza kukwamisha bajeti kama anaona ina kasoro?

Mabasi yaendayo kasi yanakuja kweli si uongo

Watanzania tunaogopa sana mabadiliko. Nikiwa ndani ya daladala nimenasa maongezi kati ya abiria na dereva. Dereva anasema tuone kama hayo mabasi yaendeayo kasi yatakuja, imeshindwa UDA! Abiria anasisitiza mabasi yatakuja na wajitayarishe kwa ushindani mkali katika sekta ya usafirishaji hasa jijini Dar. Nami nasema naam, hakuna kinachoshindikana, tujitayarishe kwa mabasi yaendayo kasi Dar. Sisi tunayasubiri kwa hamu. Wasiotaka mabadiliko kwa kulinda maslahi yao watambue hilo. Karibu sana mabasi yaendayo kasi hata kama mwaka 2o1o lakini yatakuja tu.

Precision Air kaza buti mwanangu

Nimewasili Tabora leo asubuhi kutoka Dar es Salaam kwa usafiri wa ndege wa Shirika la Precision Air. Nakwambia wamerudi kwenye chart mwanangu. Wako fit ile mbaya. Huduma zinazidi kuboreka si mchezo. Ukichelewa umeachwa. Wahudumu kauli safi. Viburudisho ndani ya ndege wawaa. Wameanza hata kutoa glass zao za Precision inapendeza eti jamani! Kaza buti Precision mwanangu mi nakupa shavu ile mbaya.

Utakumbukwa kwa lipi?

Je, umeshawahi kujiuliza kuwa ukimaliza safari yako ya hapa duniani ungependa ukumbukwe kwa lipi? Tuanze kujiuliza.

Muhogo unaweza kukutoa katika umasikini

Dkt. Nicholaus Mlingi wa TFNC anauona muhogo kama mkombozi wa mkulima na si zao la njaa kama lilinavyoonekana na wengi. Muhogo si zao la wakulima masikini. Muhogo unaweza kumtoa mkulima kutoka hali ya umasikini na kumpeleka kwenye hali ya neema kama atapata soko la uhakika, atatumia mbegu bora, ataongeza eneo la uzalishaji. Muhogo ni zao la biashara na chakula kwani lina matumizi mengi. Muhogo unaweza kutumika katika viwanda vya nguo (wanga), maabara ya kutengeneza madawa(asprin, syrup n.k.) viwanda vya kuokea biskuti na vyakula vya aina mbalimbali, viwanda vya uchapaji pia majani yake yanatumiwa kwa mboga (kisamvu).

Tatizo teknolojia nyingi hazijatumika kumsaidia mkulima kuweza kuzalisha muhogo kwa wingi na kuweza kumuingiza kipato na kuongeza pato la taifa. Mhandisi Mkuu wa Sayansi ya Chakula kwenye Taasisi ya Taifa ya Chakula na Lishe Bw. Felix Kimenya anabainisha. Anasisitiza kwa kusema kuwa sera ya kilimo iliyopo sasa inaipa muhogo kama nafasi ya zao la njaa.Tubadilike kisera na tuwezeshe wakulima wetu kwa teknolojia mbalimbali, kuwasaidia kuwapatia mikopo pamoja na kuwaunganisha wakulima katika vikundi vya uzalishaji wa zao la muhogo. Wenzetu wanatajirika kwa muhogo sisi bado tuko usingizini. mtazamo

Kibuku si pombe ya walalahoi

Jana mchana nilikutana na Bw Sicilima Kazonda - Meneja wa uzalishaji pombe aina ya Kibuku/Chibuku inayozalishwa na Kampuni ya DARBREW iliyopo Ubungo, Dar Es Salaam karibu kabisa na Kituo Kikuu cha Mabasi yaendayo Mikoani. Ilikuwa ni safari ya kikazi kutaka kufahamu ni mali ghafi gani wanazotumia kutengeneza Kibuku na jinsi mkulima anavyoweza kufaidika kuwepo kwa DARBREW?

Kwanza nilifurahishwa na usafi wa hali ya juu niliouna kiwandani hapo. Meneja wa uzalishaji ofisi yake iko humohumo ndani ya sehemu za mitambo lakini kwa juu. Matanki pamoja na sakafu zilikuwa safi sana huwezi kuamini kama hapa ndipo panapotengenezwa kibuku ambayo wengi hufikiri kuwa ni pombe ya mlala hoi.

Kibuku hutengenezwa kwa mahindi meupe, mtama mweupe na mwekundu. Wataalamu kwa kutumia mali ghafi hizo huzalisha chibuku. Kwa sasa pombe hiyo hupatikana kwenye chupa ya plastiki (kibuku)pamoja na paketi za karatasi ngumu (chibuku) zote kwenye ujazo wa lita moja.

Nauliza swali. Je, hamchanganyi na maharage? Kwani nimepata kusikia watu wakisema kuwa moja ya mali ghafi ya chibuku ni maharage.

Si kweli, anakanusha Sicilima. Kwanza maharage ina protein nyingi kwahiyo haifai kutengeneza pombe kwani ikianza kuchachuka inatoa harufu mbaya. Watu wengi hudhani ni maharage kutokana na makapi ya mtama mwekundu.
Mtama mwekundu hutumika zaidi ili kupata rangi nyekundu.Anafafanua zaidi Sicilima.

Pombe hii ni bora kuliko pombe zinazotayarishwa kienyeji katika mazingira machafu na bila viwango ingawa hutumia malighafi zinazofanana. Bei yake ni poa (Tshs 400/= kwa lita). Labda ndiyo maana watu wanaiona ni ya walalahoi. Hata hivyo mtu yeyote anaweza kunywa chibuku. Hasa ukitilia maanani viwango (inapimwa kwenye maabara) na usafi katika utayarishaji wa chibuku.

Hiyo ndiyo chibuku. Sikuweza kuonja chibuku pale kiwandani lakini nadhani tatizo pombe hii haijatangazwa vya kutosha na walio wengi huifananisha na pombe nyingine za kienyeji.

Nchini Zambia Chibuku ni pombe maarufu sana na hutumiwa na watu wa aina mbalimbali wenye vipato na wasio na vipato vikubwa.

Wakati bia nyeupe inaendelea kupanda bei kwa kasi ya kutisha, wanywaji sasa wageukie Chibuku, si pombe ya walalahoi. Itumike hata kwenye sherehe za harusi bila kujificha!

Sicilima anamaliza kwa kusema kuwa mwaka huu wanampango wa kuongeza matumizi ya mtama kwa kutengeneza Chibuku kwani mahindi bei imeongezeka sana na ni adimu kupatikana kutokana na hali ya sasa ya upatikanaji wa mazao ya nafaka. Changamoto ipo kwenu wakulima na wadau wengine wa mtama. Lakini serikali pia iangalie swala la kodi ndiyo maana inauzwa aghali na kusababisha kupungua kwa mahitaji. Kama mahaitaji yanapungua makusanyo ya kodi nayo hupungua.

Ingekuwa si Bajaj?

Nilipokwenda Tegeta kumtembelea rafiki yangu Phillip na kuhudhuria sherehe za kommunio ya mwanae Kenny nilitumia Bajaj, juzi nilipotembelea Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Mikocheni nilitumia Bajaj kutoka Mwenge hadi hapo kituoni. Jana nilikuwa na shughuli za kikazi huko Mikocheni - Maabara ya TFNC (Chakula na Lishe) nilifika huko kwa kutumia Bajaj.

Bajaj ni aina ya chombo cha usafiri mfano wa pikipiki yenye magurudumu matatu. Usafiri huu umeanza kuenea kwa kasi kubwa hapa jijini Dar Es Salaam hasa kwa zile sehemu ambazo usafiri wa daladala haupo na barabara ni mbaya au ni nyembamba sana. Licha ya kupata upinzani mkali kutoka kwa madereva wanaondesha taxi, lakini wenye maamuzi ya kutumia au kutotumia bajaj ni wateja.

Kwanini wateja wanapenda Bajaj?
  • Bei poa ukilinganisha na taxi
  • Abiria hawazidi watatu na wote wanakaa kwenye kiti
  • Hupita kwenye barabara zilizoshindikana
  • Hazina mwendo wa kasi
  • Zinakufikisha mahali unapotaka
  • Haipotezi muda ikiwa na wateja

Nilipojaribu kumdadisi dereva mmoja wa bajaj kuona kama inalipa. Alisema " Bajaj inalipa sana Mzee." Kwa Siku yeye hupeleka Tshs 15,000/= kwa mwenye mali. Kama mambo yakienda vizuri baada ya miezi 7 inaweza kurudisha gharama za manunuzi (Kwa sasa Bajaj 1 ni Tshs 4,000,000/= sina uhakika).

Hiyo ndiyo Bajaj iliyoanza kwa shida na sasa kutapakaa Tegeta, njia panda ya White Sands, Mwenge, Kawe na kwingineko jijini Dar. Na kwakweli zinatoa huduma ya kuridhisha kwa wasafiri wa sehemu hizo. Hata hivyo nadhani bado kuna uwanja wa kuboresha huduma hii ya usafiri. Unasemaje kuhusu Bajaj?

Sunday, June 15, 2008

Remote control inapofichwa na meneja

Jumamosi iliyopita nilitembelea Hotel moja iliyopo maeneo ya Magomeni jijini Dar Es Salaam. Ni hotel mpya ya hadhi ya kati.

Hotel hii inatoa huduma muhimu karibu zote kwa wageni wanaofikia kwenye hotel hiyo kwani hata huduma ya Internet inapatikana. Lakini cha kushangaza, watoa huduma kwenye hotel hiyo wanatoa huduma bila ya kujiamini.

Nilishangaa nilipokuta chumba kina TV lakini hakuna remote control. Nilipouliza nikapata jibu kuwa wateja huiba remote. Haya, remote inapopatikana, baadaya ya muda mrefu wa kuhangaika kupata stesheni nagundua kuwa hata waya wa Antena umenyofolewa! Ninapouliza inakuwaje? Jibu ni kwamba si kosa lao. Mwenye mamlaka hayupo! Ina maana mteja anapotoka antena na antena cable hukusanywa kuogopwa kuibiwa.

Hata baadhi ya maelezo muhimu ya jinsi huduma zinavyotolewa hotelini hapo ni shida kupatikana. Kwa kweli sielewi, remote inapofichwa na meneja!

Ni hatari kama Bunge sasa limeanza kuamini "JUJU"

Leo jumapili 15/06/2008 katika ukurasa wa kwanza wa gazeti la "Sunday News" kuna habari zilizoandikwa kuwa timu iliyoundwa na Spika wa bunge la Jamuhuri kuchunguza imani za kishirikina Bungeni.

Eti inasemekana kuwa kuna mbunge mmojan anayehisiwa kujihusisha na imani za kishirikina bungeni. Kwa hali hii naona kuna hatari ikiwa tumefikia hatua ya bunge letu kuanza kuamini "JUJU." Wananchi wa kawaida wasemeje?

Maximo jifunze Kiswahili

Kocha mkuu wa mpira wa miguu hapa nchini Bw. Maxio Maximo ananishangaza sana eti hadi sasa hajui kuzungumza Kiswahili hata kile cha kubabaisha.

Maximo, ninavyofahamu mimi aliingia hapa nchini akiwa na kiingereza kibovu sana. Lakini amejiwekea mikakati ya kuhakikisha kuwa anakifahamu kiingereza vizuri. Kila anapofanyiwa mahojiano yeye hupenda kutumia kiingereza ambacho hakifahamu vizuri na hata hao wanaomuhoji hawakifahamu vizuri. Isitoshe TV au Radio zinazoendesha mahojiano naye zinatumia Kiswahili wateja wake wakubwa wanafahamu kiswahili. Ujumbe wa Maximo unamlenga nani?

Kama anataka kufanikiwa katika medani ya soka hapa Tanzania, inambidi aanze kujifunza Kiswahili kwa bidii zaidi ili aweze kuelewana na wachezaji, mashabiki na watanzania kwa ujumla. Vinginevyo muda wa kukaa Tanzania sikuzote utakuwa wa moto kwake!

Kutoka sare na Cameroun si mwujiza

Cameroon ni nchi iliyopo Afrika kama ilivyo Tanzania. Ni nchi ya dunia ya tatu. Nina maana uchumi wetu haupitani sana. Maendeleo yetu karibu ni sawa, tamaduni zetu ni sawa.

Tarehe 14/06/2008. Taifa stars ilitoka sare na Timu ya Taifa ya Cameroon " Indomitable Lions" katika kinyang'anyiro ya kupata tiketi ya kuwakilisha Afrika katika Kombe la dunia 2010 pamoja na lile la Mataifa huru ya Afrika.

Watanzania wengi hawakuamini kuwa Taifa Stars wanaweza kuibana Cameroon wasifurukute. Na wengi wanaamini kuwa Taifa Stars haiwezi kuifunga Camaroon. Huko ni kutojiamini, yote yawezekana iwapo tutajipanga sawa. Hata hivyo tusibweteke ni sare kwani hali yetu bado si nzuri point 2 tulizoweka kibindoni hadi sasa hazitoshi.

Bajeti-Mazoea?

Wiki moja baada ya kusomwa bajeti ya Taifa kwa mwaka wa fedha 2008/09 mambo ni yale yale, bia, soda bei juu. Vipaumbele ni vile vile- Elimu, Miundombinu, Afya, Kilimo......................

Watu wanazungumza sekta ya kilimo imesahaulika, kiasi kilichotengwa ni kidogo sana ukilinganisha na mchango wa sekta hiyo katika pato la Taifa na umuhimu wa Kilimo kwa wananchi wa Tanzania. Je, wanavuta kamba kwao? Sekta nyinngine wanasemaje. Tujenge viwanja vya Taifa kila mkoa!

Mimi ninajiuliza je, tunajifunza nini kutoka bajeti mbalimbali zilizopita? Kina nani wanaopanga bajeti? Nani wanaotoa maamuzi ya kupitisha bajeti? Je, kwa sasa ni akina nani wanaoichambua bajeti? Uelewa wetu kuhusu bajeti ni upi. Je, bajeti ni mazoea tuliyoyajenga au ni urithi kutoka kwa watawala wetu waliopita? (Wakoloni) bila kujiuliza maswali haya rahisi na kupata majibu, bajeti ni utamaduni wa kukaa bungeni kwa muda mrefu bila kutoka na maamuzi sahihi ya mipango ya nchi. Je wewe unasemaje?

Thursday, June 5, 2008

Inawezekana kuwapenda adui zetu ingawa ni vigumu

Tarehe 25 Mei mwaka huu, watoto watatu wa familia moja (ya Banzi) walipokea Ekaristi Takatifu kwa mara ya kwanza iliyotolewa na Balozi wa Baba Mtakatifu hapa nchini Kardinali Joseph huko Parokiani Vikindu, jimbo Kuu la Dar Es Salaam.

Watoto hao Peter L.J.Banzi, Catherine I.J.Banzi, na Sisty I.J.Banzi kutoka kijijini Kisemvule walikula mwili na damu ya Yesu Kristu baada ya kupata mafunzo ya muda wa miezi tisa kuhusu imani ya Kanisa Katoliki.

Katika mahubiri yake, Cardinali Joseph alisisitiza mapendo. Alisema kuwa inatupasa kupendana na kuwapenda hata maadui zetu ingawa ni vigumu lakini inawezekana

Mara baada ya kupata komunio, watoto hao walipokelewa kwa shangwe na ndugu na jamaa waliokuwa wakiwasubiri nyumbani kwao Kisemvule. Pamoja na mabo mengine waalikwa walisherehekea kwa chakula, vinywaji na burudani.

Katika wosia mfupi uliotolewa na baba yao mdogo Bw. Frederick Mloka, aliwaasa kufuata kwa ukamilifu mafundisho ya kanisa kwa sasa wamefungua njia ya kutambua kanisa na kulinda imani ya kanisa Katoliki.

Akitoa shukrani kwa ndugu na jamaa. Bw. Innocent J.Banzi ambaye ni Baba wa vijana hao aliwashukuru ndugu, marafiki, jamaa na majirani kwa ushirikiano wao walioutoa kwa hali na mali katika kufanikisha sherehe hiyo. Alisisitiza kupendana na kusaidiana wakati wote.