Friday, October 24, 2008

Watanzania wameanza kutojiamini

Inavyoonekana kuwa kwa sasa hali ya kujiamini kwa Watanzania inapungua kwa kasi ya kutisha. Hii inajionyesha kwa kuvuja mitihani, majengo kuanguka, mabarabara kujengwa kwa kiwango cha hali ya chini. Wagonjwa kupata tiba isiyowahusu. Kutofanya vizuri kwenye michezo ( olimpiki 2008).

Kama mwanafunzi amehudhuria elimu ya sekondari kwa miaka 4 kwa nini aibe mtihani? (Huko ni kutojiamini). Kama mwanamichezo amefanya mazoezi vizuri na kufuata miiko ya wanamichezo sioni sababu ya kutofanya vizuri.

Kama wahandisi wamepata elimu na uzoefu wa kutosha katika kazi yao kwanini washindwe kusimamia kazi zao za ujenzi.

Watanzania turudishe hali ya kujiamini hata kama tunakosea lakini tunajifunza kutokana na makosa tunakokwenda siko. Watakuja wageni kutufanyia kila kitu kwani hatujiamini na hatuaminiani.

Asilimia 62 ya wahitimu wa darasa la saba kupata sifuri kwenye hisabati ni hatari

Waziri Mkuu Mhe.Mizengo Pinda alipokuwa akitoa hoja ya kuahirisha mkutano wa kumi na mbili wa Bunge-Dodoma tarehe 29 Agosti 2008 moja ya mambo aliyozungumza kwa uchungu sana ni wanafunzi kushindwa vibaya mtihani wa hisabati. Alisema. Kwa mfano mwaka 2001, katika mtihani wa kumaliza Darasa la saba, asilimia 62 ya watahiniwa katika Wilaya ya Morogoro Vijijini walipata sifuri katika Mtihani wa Hisabati. Hii ina maana kuwa asilimia 62 walimaliza shule bila kujua Hisabati rahisi za kujumlisha, kutoa , kuzidisha na kugawanya.

Hali hii ni mbaya sana. Inaonekana kuwa wanafunzi hawaoni umuhimu wa somo la hesabu, walimu pia kadhalika na wazazi tuseme na taifa zima.

Enzi zetu mwanafunzi ukifahamu hesabu hizo sifa tu unazomwagiwa mwenyewe utapenda hesabu. Na kama hujui hesabu ulikuwa unadharauliwa. Hata Sekondari waliokuwa wanachukua sayansi waliheshimika na wale wa sanaa au "arts' kwa kweli walionekana kama wapo wapo tu. Hata mzazi aliona ni sifa kwa mwanae kuchukua sayansi.

Tatizo letu Watanzania ni jinsi tulivyobadilika kirahisi kimtazamo katika mambo mbalimbali hasa elimu. Tunapenda mambo rahisi. Sasa hivi kila mtu yuko kwenye menejimenti, siasa na biashara! Kwa hali hii si rahisi mtoto kupenda hesabu. Hesabu zinatakiwa kutulia. Kama alivyosema Waziri Mkuu. Hesabu inajenga dhana ya kujiamini, kujenga falsafa ya mambo kwa mpangilio wenye mantiki (Logical Thinking).

Wito wangu ni kufufua ari ya kupenda hesabu na ionekana kwa watoto wetu kuwa bila hesabu huko mbele ni giza.Ijionyeshe waziwazi katika maisha yetu ya kila siku jinsi hesabu zinavyofanya kazi. Labda nihitimishe kwa kusema kuwa mwanafunzi yeyote anayepuuzia hesabu atapata matatizo makubwa katika kuendelea na elimu yake popote pale.


Wenzangu wa Moro sijui kama tumeshaanza kuchukua hatua ya kujikwamua kutoka katika aibu hii. Na hasa ikizingatiwa kuwa ni Morogoro vijijini kwani huko hakuna shule za kulipia kwa hiyo ni watoto wa malofa hawajui hesabu toba!

Thursday, October 23, 2008

Machungwa bado yanapatikana Dar

Msimu wa maembe umeanza, lakini machungwa bado yanapatikana Dar tena kwa bei nafuu sana. Shilingi 100/= kwa chungwa moja. Machungwa ya sasa ni matamu sana. Nawapongeza sana wakulima wetu kwa jitahada zao kubwa za kuhakikisha kuwa karibu kila zao linapatikana mwaka mzima. Miaka ya nyuma ilikuwa ni nadra sana kula chungwa hapa Dar kwa wakati huu. Hii ni dalili nzuri kuwa kuna teknolojia imeongezeka katika kilimo. Hii ni dalili nzuri pia kuwa wakulima hawa wakiongezewa uwezo wanaweza kufanya makubwa.


Nchi yetu imebahatika kuwa agroekolojia mbalimbali ambazo zinaweza kustawisha mazao mbalimbali kwa nyakati tofauti. Vile vile zina aina tofauti za udongo licha ya kuwa na vyanzo vingi vya maji ambavyo bado havijatumika kikamilifu kwa uzalishaji wa kilimo.

Wednesday, October 15, 2008

Kushindwa kwa CCM Tarime ni funzo

Licha ya kuwa jimbo la Tarime hapo awali lilikuwa chini ya umiliki wa CHADEMA na sasa baada ya kufanyika uchaguzi mdogo CHADEMA imelirudisha tena jimbo hilo kwenye himaya yake huku ikikiacha Chama Cha Mapinduzi KULIKONI Tarime?

Msimu wa maembe umeanza

Msimu wa maembe umeanza. Dalili nzuri zinaonyesha ukipanda boti pale Kivukoni. Embe ndogondogo zilizoiva vizuri zikiwa zimepakiwa kwenye matenga zinavushwa kwenda mjini kwa kuuzwa. Embe hizi ni nzuri.

Tanzania tumebahatika sana kwa kuwa na hali ya hewa inayoweza kustawisha mazao mbalimbali na kwa misimu tofauti kwa gharama nafuu. Kilimo hiki ni kizuri lakini si endelevu. Kwa mfano hakuna mikakati ya kuweza kumuinua mkulima katika uzalishaji wa matunda, mboga, korosho na nafaka. Mabenki yetu haioni kuwa wakulima wanakopeshaka na kwa vile tu wanataka fedha zao zilirudi kwa msimu mmoja. Hii haiwezekani kwenye kilimo. Mkulima lazima apewe muda mrefu ili aweze kuzalisha kwa faida na kuweza kurejesha mikopo hiyo. Hali ni ile ile kila mwaka na mkulima ni yule yule, mfanyabiashara naye habadiliki kila mwaka kusukuma tenga la maembe machache kuyachuuza mitaani!

Bei ya nyama ni juu Dar


Kwa wakazi wengi wa jiji la Dar Es Salaam hasa wa kipato cha chini kula nyama ni anasa. Bei ya nyama ya kawaida kwa sasa ni zaidi ya Tshs 3800/= kwa kilo. Hivi kweli kuna vigezo sahihi vinavyofanya nyama ipande kwa kiasi hicho?


Inasemekana hali si mbaya sana kwenye soko la jumla. Lakini wauzaji wa rejareja ndiyo wanaopandisha bei kiholela. Kibaya zaidi vipimo vinavyotumiwa si sahihi. Walaji wanadhulumiwa sana. Sijui kama Uongozi wa Jiji unafahamu hili. Hali ni mbaya lishe ya wananchi inakosekana hasa proteini inayopatikana kwa kula nyama.

Thursday, October 9, 2008

Kubonyeza kengele ovyo ndani ya bus si ustaarabu

Kutokana na tatizo la usafiri hapa jijini Dar Es Salaam.Mjasiriamali mmoja, tena Mtanzania ameleta mabus mazuri licha ya kuwa ni mitumba ili kuweza kuboresha usafiri hapa jijini. Mabus haya ni ya kisasa na ni makubwa. Kila dirisha lina kengele inayotumiwa na abiria kumtaarifu dereva asimamishe bus iwapo anataka kuteremaka kituoni au kama kuna dharura.

Jambo la kushangaza, abiria wasio wastaarabu wanazitumia kengele hizo vibaya kwa kubonyeza kila wakati na hivyo kumfanya dereva kusimama wakati hakuna anayeshuka wala hakuna dharura yoyote. Ndiyo maana nasema kubonyeza kengele ovyo ndani ya bus si ustaarabu. Kutonana na hali hiyo sasa kengele hizo hazifanyi kazi (disconnected).

WIKI YA NYERERE SIJUI MNAONAJE

Vyombo vya habari vimeanza kuandika sana kuhusu wiki ya Nyerere 13-18 Oktoba.

Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere ndiye Rais wa Kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Nyerere ameongoza Taifa hili kwa muda mrefu sana yapata miaka 21 (Tanzania). Kipindi hicho si kidogo ni umri wa mtu mzima +3. Katika kipindi hicho mambo mengi yamepangwa na mengi ambayo yametekelezwa na ambayo hayakutekelezwa.

Wakati yanaandikwa mengi kuhusu Nyerere. Kuna baadhi ya Wataznania wanadai kuwa Nyerere alitupeleka pabaya! Hivi ni kweli? Kama kweli kumbukumbu hii ni ya kinafiki. Mimi namuheshimu sana Mwl. Nyerere na sera zake nazikubali. Watanzania wengi wamefikishwa hapa walipo kutoka na sera zilizokuwepo za elimu, afya na uzalishaji. Sijui wenzangu mnaonaje.

Wednesday, October 8, 2008

Dar ikitekeleza mipango yake itaipita Gaborone

Jiji la Gaborone ni dogo ukilinganisha na jiji la Dar Es Salaam. Wakazi wake pia ni wachache sana. Hakuna pilikapilika nyingi mchana na usiku. Maduka yake si mengi na wala si ya kutisha, lakini mipango ya kuendeleza jiji hilo ipo, inaonekana na inatekelezwa. Mji ni msafi, nyumba zimejengwa kwa mpangilio mzuri. Utaratibu wa usafiri umepangwa vizuri. Si rahisi kuona malori makubwa kwenye njia za magari ya abiria.


Dar Es Salaam tuna mambo mazuri mengi tu. Jiji kubwa, watu wengi, wajanja, wakarimu . Maduka mengi, bidhaaa mbalimbali na mazao mablimbali yanayopatikana wakati wote. Bahari tunayo, mvua inapatikana misimu miwili. Wasomi wapo, mipango mizuri ipo. Tatizo ni nini?


Hatutekelezi kikamilifu tuliyojipangia- Hilo ndilo tatizo kubwa! Blaa blaa nyingi tu. Mtu anakojoa mchana kweupe, hakuna anayejali! Malori yenye shenena za mafuta yanaachiwa bandarini saa 9.00 wakati wafanyakazi wanarudi kutoka kazini - matokeo take foleni yakujitakia kabisa! Hakuna anayejali. Hilo ndilo tatizo la Dar.Vinginevyo, naipenda Dar yangu na iwapo tutarekebisha mambo yetu, ukiondoa J'BURG, na Capetown miji mingine iliyobakia kusini mwa Afrika itaburuzwa na Dar.

MASAKI SASA INAPENDEZA

Ni muda mrefu sijawahi kutembelea maeneo ya Masaki (Oysterbay). Ukiondoa Baharini na beach zake sikuwa na sababu ya kwenda huko. Lakini Jumapili iliyopita nilipata mwaliko wa ndugu yangu anayeishi huko kuhudhuria sherehe za watoto wake waliopata komunio. Kwa kweli Masaki imebadilika sana. Nyumba nzuri zimejengwa na zinaendelea kujengwa. Barabara zimekarabatiwa, mitaro ya maji machafu inajengwa.Maduka mazuri yamefunguliwa. Wale mbuzi waliokuwa wakila michongoma sasa hawapo tena! Kweli Masaki sasa inapendeza hakuna tofauti na Majuu au South!

Traffic chunguza mabus ya Mkuranga-Kigamboni

Jumamosi iliyopita wakati narudi nyumbani kwangu nilipitia Kigamboni nikidhani kuwa nitapata usafiri mzuri nikiogopa foleni ya barabara ya Kilwa wakati wa jioni.

Waswahili husema nimeruka mkojo nimekanyaga mavi! Pale Kigamboni stendi ya mabus ya kwenda Kongowe, Mjimwema na Kibada mabus yenye maandishi ya Mkuranga -Kigamboni yalikuwepo lakini yalikuwa yanakatisha mwisho Kibada au Mjimwema. Usafiri ulikuwa ni wa shida sanaTulipoteza karibu saa moja kabla hatujakubaliana na kulipa shilingi 1,000/= kwenda Kongowe!

Mabus haya ya Kigamboni-Mkuranga kwa kweli hayasafiri kwenye njia iliyopangiwa ni ujanja tu wakupata njia, Traffic angalieni hilo wananchi wanaumizwa hali ni mbaya.

Mitihani kuvuja-Lawama kwa wazazi,wamiliki shule

Kuanzia Jumatatu juma hili, mitihani ya kumaliza kidato cha nne inaendelea nchini kote. Mtihani ni utaratibu uliowekwa kwa ajili ya kuwapima wanafunzi uelewa wa masomo waliyojifunza kwa kipindi fulani.

Jambo la kusikitisha kusikitisha ni kwamba mwanzo si mzuri mwaka huu. Mara kipyenga kilipopulizwa cha kuashiria kuanza kwa mitihani hiyo, tayari mtihani wa hesabu umeshavuja!
Shule za "English Medium" na za kulipia ndiyo hasa zilizobambwa katika mkasa huu-k.m. Happy Skillful! Ni aibu kwa kweli. Ni aibu kwasababu wazazi wamewasomesha watoto wao kwa gharama kubwa lakini hatimaye wanaiba mtihani.

Lakini kwa upande mwingine wazazi nao wanahusika kwa kiasi kikubwakatika kashfa hii. Wanafunzi watapata wapi fedha za kununua mtihani? Pengine tuseme wamiliki wa shule, hasa hizi za kulipia maana wanataka sifa, wanataka kujitangaza kuwa wee-HappySkillful - Mathematics A- 20! Kati ya hao wasichana ni 12! Acha mchezo. Kwanini wazazi wasishawishike kuwapeleka watoto huko na kwa kufanya hivyo - definetily mwenye shule ataongeza karo. Mikakati iwekwe kukomesha mtindo huu vinginevyo watoto wa wanyonge hawataona Kidato cha Tano na huko Chuo Kikuu itakuwa ni ndoto. Hivi kweli tunalipeleka wapi Taifa hili. Ama kweli sitakosea kwa kuliita kuwa ni Taifa la "Vodacom"