Tuesday, November 25, 2008

Utekelezaji mbovu Afrika ndo unaotufanya tusifikie malengo

Jana katika hotel ya Intercontinental hapa Nairobi, Kenya tulikuwa tunajadili masuala ya "kupelemba na kutathmini" (Monitoring and Evaluation) kwenye utafiti wa Kilimo.

Imedhihirika kuwa tuna mipango mizuri yenye malengo mazuri. Na malengo yetu makuu kwnye nchi hizi za Afrika Mashariki na ya Kati kwa bahati nzuri ni ya muda mrefu sana kama vile kuondoa umaskini, ujinga, maradhi lakini hadi hii leo tunazungumzia hayo hayo tokea tupate UHURU. Korea ya Kusini walikuwa kwenye hali kama yetu miaka 40 iliyopita sasa wameshatoka. India sasa wanajitosheleza kwa chakula! Sisi misaada, misaada misaada!

Eti sisi Waafrika ni wabaguzi zaidi kuliko wazungu?

Kuna baadhi ya watu wanasema kuwa Obama kuwa Rais Amerika ni rahisi zaidi kuliko Clinton kuwa Rais wa Kenya! Wanasema kuwa sisi Waafrika ni wabaguzi zaidi kuliko wazungu je ni kweli?

Monday, November 24, 2008

Huduma za Hotelini Kenya ni zaidi

Ukiwa Hotelini Nairobi Kenya, huduma nyingi zinapatikana ikiwamo hii ya Internet. Hapa nilipo nimeweza kuwasiliana nanyi kwa kutumia "Wireless internet connection" huna haja ya kuonana na mtu anayekupa hiyo huduma. Upo chumbani kwako unapiga simu na unapata huduma kwa maelekezo.Malipo baadaye na ni malipo nafuu.

Hee, hata kama mimi ni mtalii ningeweza kupendelea kwenda Kenya. Hivi vitu vinawezekana kwetu pia. Nafahamu huduma hizi zipo kwetu lakini hazijaenea kwa kiasi cha kutosha lakini inawezekana. Tunapoteza hela nyingi kwenye sekta ya mawasiliano tumeng'ang'ania simu za mkononi tu. Wenzetu wanahama taratibu!

Nikiwa Kenya niko Nyumbani

Nairobi, watu wake, miti yake na udongo wake ni kama Arusha tu. Isitoshe Wakenya wanaongea na kukipenda Kiswahili tofauti na jinsi Watanzania wengi wanavyohisi kuhusu Wakenya. Kwa kweli ukiwa Kenya unajisikia nyumbani. Utasikia watu wanakusalimia habari mzee. Wanasema yule "demu" ameondoka. Wanakuambia bia baridi ndiyo yenyewe. Wageni wengi wangependa kufahamu na kuzungumza Kiswahili wakiwa Kenya. Watanzania mpo?

Nairobi nayo inatatizo ya “traffic jam”

Mara baada ya kutua Jomo Kenyata International Airport na kuelekea Intercontinental Hotel, katikati ya jiji la Nairobi, tunapambana na Traffic jam kubwa. Pamoja na kuwa na barabara nyingi na zile zinazokatisha juu, lakini bado jiji la Nairobi lina tatizo la Traffic jams!

Kumbe si Dar tu. Kama hakuna utaratibu mzuri, kuwa na barabara nyingi na pana hakuwezi kumaliza tatizo la "traffic jam" katika miji yetu.

Kweli inawezekana watoto wasiwe wa kwako

Nipo hapa Intercontinental Hotel Nairobi, Kenya. Nimekutana na wasomi kutoka Kenya, Uganda, Eriteria, Burundi na Rwanda. Siku ya leo tumezungumzia sana kuhusu kilichotuleta hapa Kenya hasa kuhusu masuala ya "Kupelemba na Kutathmini "( Monitoring and Evaluation)shughuli za Utafiti, Ugani na Mafunzo katika eneo hili la Afrika ya Mashariki na ya Kati.

Mazungumzo nje ya hilo yanagusa masuala mbalimbali.Lakini kwa kuwa ni watu wazima na tupo jinsi mbili tunazungumza yanayotuhusu katika maisha yetu ya kila siku. Katika hilo lililochukua muda mwingi ni mahusiano ya ndoa. Imebainika kuwa mwanamke anaweza kubeba siri kubwa kuhusu baba halisi wa watoto. Je hili mnalionaje wana mtandao?

Taxi za njano

Ukitua uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta jijini Nairobi utakutana na magari mengi sana ya aina mbalimbali na mazuri kwa kusema ukweli. Hata hivyo magari madogo ya abiria yaliyopakwa rangi ya njano yanavutia zaidi hapo uwanjani (Lakini si magari ya Dar Young Africans). Magari hayo ni utambulisho kuwa ni zile Taxi zinazo park uwanjani hapo na ubavuni kuandikwa JKIA. Magari hayo ni masafi yanavutia na yana utaratibu mzuri kwa abiria. Ni vizuri kwa Taxi za zinazo park Dar- Mwl. Julius Nyerere International Airport zikaiga utaratibu huu na kuwa na nauli zakuridhisha kwa wateja na si kuwatega watejawaingizwe king! Kipato hakipatikani kwa ujanja ujanja! Tuwe wastaarabu na tuvute wateja kwa mambo mazuri.

Watanzania tulishapita hatua ya Waamerika

Niko hapa Nairobi Kenya, nimetoka kwenye "reception dinner" iliyoandaliwa na wenyeji wetu ASARECA kwenye warsha hii ya "Kupelemba na Kutathmini" miradi ya ASARECA.



Kwa faida ya wale ambao hawaifahamu ASARECA. Huu ni chombo cha Afrika mashariki na Kati kinachoangalia masuala ya Utafiti, Ugani na Mafunzo Katika Kilimo.



Ndugu zangu wa Kenya wamekiri kuwa hakuna cha kushangaza kuhusu Obama kuwa Rais wa Amerika. Watanzania wameshapita hatua hiyo siku nyingi. Wanaeleza wenyewe kuwa kwa Tanzania hawakuwa na sababu ya kufahamu kuwa Mkapa alikuwa anatoka wapi. Walichotaka ni kuwa na Rais atakayeweza kuisimamia nchi ya Tanzania. Watanzania tupige makofi basi kuwa tunawazidi hata Waamerika kwa hilo. Lakini kwa nini hatupigi hatu kwenye Maendeleo?

Friday, November 14, 2008

Habari na Mawasiliano ni nyenzo muhimu katika Kilimo

Mwezi Septemba mwaka 2008 nilibahatika kuhudhuria warsha ya wadau wa habari na mawasiliano katika sekta ya Kilimo kutoka nchi za SADC iliyofanyika nchini Botswana, jijini Gaborone.

Nchi 14 ukiondoa Afrika ya Kusini zilishiriki warsha hiyo iliyokuwa na dhumuni la kuona jinsi gani nchi za SADC zinavyoweza kuwasiliana na kutumia tekenoljia ya habari, katika masuala mbalimbali ya kilimo kwa kutumia vyombo mbalimbali kwa kuzingatia wadau.

Wakati umefika sasa wa kukitangaza kilimo kama vile inavyotangazwa " cocacola" lakini mawasiliano hayo ni vyema yakawaongezea maarifa wadau wetu wa kilimo. Tunataka kilimo chenye kumnufaisha mkulima.

Kuna mambo mazuri yanayofanyika katika nchi hizi ambazo yanawezwa kuigwa na nchi nyingine lakini hayafahamiki. Kuna matukio muhimu yanayotokea katika sekta ya kilimo lakini yanabakia palepale. Basi ilionekana kuwa kuna umuhimu wa kila nchi kuangalia jinsi ya kutumia taarifa, mawasiliano na teknolojia ya habari katika kuboresha sekta hii.

Wakati viongozi wetu wanapiga kelele na kuhamasisha uzalishaji katika kilimo, habari na mawasiliano ni nyenzo muhimu itakayosaidia kuboresha kilimo chetu. Pichani wanaonekana washiriki wa warasha hiyo.

Kanisa Katoliki Parokia ya Vikindu -Mt. Vincent wa Paulo



Hili ndilo Kanisa ninalosali mimi. Kanisa Katoliki la Parokia ya Vikindu. Kanisa hili tumelijenga kwa nguvu zetu sisi waumini pamoja na marafiki zetu wa ndani na nje ya nchi. Kanisa hili limejengwa na baadhi ya waislamu waliojitolea bila kujali tofauti ya dini.Ndiyo hatukumsubiri OBAMA.Tulijtegemea wenyewe.

Nilipohamia Vikindu-Kisemvule mwaka 2004, tulikuwa tunasali kwenye ukumbi mdogo tu. waumini tulikuwa wachache sana hata sadaka ilikuwa chache pia. Ibada Takatifu siku ya Jumapili ilikuwa ni moja sasa kuna misa ya pili ya watoto. Kanisa hili zuri lina vipaaza sauti, lina madawati mazuri ya kukalia, lina kwaya nzuri pia na kwa kweli linapendeza ndani na nje. Karibuni sana Vikindu.
Parokiani Vikindu kuna Zahanati nzuri tu, kuna shule ya watoto wadogo na shule ya msingi ambayo hufundisha kwa kiingereza zote zinamilikwa na Parokia ya Vikindu. Kanisa limeleta maendeleo ya kiroho na kimwili. Watawa wa Vikindu wanapaita mahali hapo "Jesus Town"

Hongera wanamichezo wa "KILIMO"

Timu ya michezo ya Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika mwaka huu 2008 imefanya maajabu kule Morogoro kwenye mashindano ya SHIMIWI. Wameweza kuwa washindi wa jumla wa tatu kati ya timu 54 zilizoshiriki.

Kilimo imeweza kuwa mshindi wa tatu katika mpira wa Miguu, mshindi wa nne mpira wa pete, bao mshindi wa pili na riadha wamepata medali. Hii imetokana na maandalizi mazuri, kujituma na nidhamu ya hali ya juu waliokuwa nayo wachezaji wakati wote wamaandalizi na mashindano. Hongera sana Mwenyekiti wa Kilimo Sports Klabu Bw. George Mbelwa.

Maximo unaikomoa Tanzania si Kaseja

Anayekomolewa ni Mtanzania na si Kaseja. Kama Kocha Maximo una ugomvi na Kaseja basi nendeni kortini. Usituharibie soka letu. Kaseja bado ni mlinda mlango na 1 hapa nchini. Mimi ni mpenzi wa Simba hata hivyo bado namuona Kaseja ni golikipa bora licha ya kuwa amehamia Yanga. Maximo mpange Kaseja timu ya Taifa uone vitu vyake achana na huyo Ivo Mapunda anayetematema mipira hovyo.

Machungwa yako sokoni

Watanzania sasa tunaanza kufaidi matokeo ya teknolojia bora za kilimo. Machungwa sasa yanapatikana sokoni wakati huu mwezi Novemba tena matamu sana, tena makubwa na tena kwa bei poa.

Iwapo sekta ya kilimo itaongezewa raslimali kwa asilimia 5 tu , kile kisichowezekana kitawezekana na kuwa na ziada. Mazao mengi yanayoonekana sokoni hivi sasa ni juhudi za mkulima huyu mdogomdogo, asiyekuwa na pembejeo bora za kilimo, anayetumia zana duni za kilimo na anayetegemea kilimo cha mvua!

Si mshabikii OBAMA

Nimefurahi kuwa OBAMA ameshinda kinyang'anyiro cha kiti cha Rais nchini Marekani.
  • Lakini sitegemei maajabu kutoka kwa OBAMA katika kuboresha maisha yangu
  • Kwa wale wanaotegemea misaada hiyo wasahau na haitakuwa rahisi kama wanavyofikiri wao
  • Wakumbuke kuwa OBAMA ni Mwamerika licha yakuwa ana rangi nyeusi!
  • Watanzania tuchape kazi
  • Watanzania tuongeze uzalendo na tuipende nchi yetu
  • Watanzania tuwe wabunifu
  • Watanzania tupunguze kulalamika bila sababu ya msingi
  • Tupunguze vitendo vya rushwa

Kwa hiyo simshabikii OBAMA

Viongozi wa nchi wavalia njuga kilimo na kuona kuwa inawezekana

Viongozi wetu wengi wameanza kuhamasisha na kufuatilia shughuli za uzalishaji wa kilimo kwa vitendo na sasa inaonekana kuwa kila kitu kinawezekana kwa ajili ya kuendeleza Kilimo.


Hivi majuzi tu Waziri Mkuu Mhe. Mizengo Pinda katika ziara yake mkoani Dodoma aliweka mkwara mkali kwa wakuu wa wilaya na mikoa kwamba wakati wa kuvaa suti kila siku umekwisha wanahitajika kuvalia njuga kilimo kwa nguvu zao zote.


Tayari Mkuu wa wilaya ya Kondoa Bw Seif Mpembenwe amemweleza Waziri Mkuu kuwa wilaya yake inaweza kujitosheleza kwa chakula. Sasa kama wilaya zote zitaahidi hivyo na kukipa kilimo kipaumbele katika shughuli zake, tatizo liko wapi?

Thursday, November 13, 2008

Wamisionari wametuachia urithi mkubwa lakini bado tumelala

Wiki ya jana nilisafiri kwenda Morogoro kushiriki katika mazishi ya Binti yetu Rose Aniani Mbiki (Mtoto wa mdogo wangu) aliyefariki pale Bigwa Morogoro. Mungu ailaze mahali pema peponi roho ya marehemu Rose.

Ibada takatifu ya mazishi ya kumuombea marehemu ilifanyika kwenye kanisa la Bigwa (Sekondari ya Masista-Bigwa). Sijawahi kuingia ndani ya Kanisa hilo lakini nilivutiwa sana kwa jinsi Kanisa hilo lilivyojengwa kwa matofali ya kuchoma kwa mpangilio mzuri tu. Milango ilivyotengenezwa inapendeza na utaalamu wa hali juu umetumika.

Makanisa mengi ya jimbo la Morogoro yamejengwa zamani na Wamisionari. Ukiangalia utaalamu uliotumika ni wa hali ya juu sana ukizingatia na hali halisi ya vifaa kwa wakati ule. Bado sielewi, hivi ni kwanini tunashindwa kuuendeleza utaalamu ule? Udongo ni uleule watu wapo kwanini tusiboreshe yale tuliyoyakuta na kusonga mbele? Ajira tunazozitafuta si kama hizi za ujenzi? Vijana wangapi wa Bigwa, Matombo na Morogoro kwa ujumla wamerithi taalama hii ya ujenzi au wanajenga kwa kulipua tu?

Wafanyabiashara ndogondogo waelimishwe

Idadi kubwa ya watu jijini Dar Es Salaam na miji mingine hapa nchini hufanya biashara ndogondogo. Lakini leo hii nitazungumzia biashara za vyakula, matunda na vitafunwa.

Utamkuta mtu anauza korosho, karanga, majibaridi, maembe, pilau, samaki wa kukaanga n.k. Lakini yeye mwenyewe mchafu, chombo alichowekea chakula kichafu, mazingira anayouzia chakula ni machafu. Hivi kweli kwa hali hii mteja anaweza kuvutiwa na biashara yako?

Mimi napenda sana kutafuna korosho, lakini wakati mwingine nasita kununua korosho ambazo zinauzwa na mtoto mdogo mchafu ambaye huchezea chezea korosho hizo wakati akizipanga kwenye mafungu. Au utakuta mwanamama anauza chakula huku ananyonyesha au kujikuna sehemu mbalimbali. Kwa hali hii ni vizuri wafanyabiashara ndogondogo wakaelimishwa. Si elimu ya mikopo tu bali jinsi gani wanavyoweza kuvutia biashara zao.

Sababu za foleni barabara ya Kilwa

Barabara ya Kilwa ninaitumia karibu kila siku. Kwa sasa barabara hiyo iko kwenye ukarabati mkubwa. Barabara inapanuliwa na madaraja mapya yanajengwa. Kutokana na hali hiyo huwa kunatokea usumbufu mkubwa wa usafiri wakati wa asubuhi na jioni. Safari ya dkika ishirini inaweza kuchukua zaidi ya saa moja. Sababu kubwa ya kuwa na foleni yakukatisha tamaa hata kusababisha watu wengi kutembea kwa miguu ni hizi hapa.

  • Madereva wasiozingatia sheria na taratibu za kuendesha magari
  • Wajenzi wa barabara kutoweka vizuizi kwa sehemu ambazo hazistahili kupita magari
  • Askari wa Usalama barabarani (Traffic Police) kutofanya kazi yao barabara kwa kuelekeza za kupita magari.
  • Viongozi wa Manispaa ya Temeke kutolishughulikia suala hili ili liweze kupatiwa ufumbuzi wa muda wakati barabara hiyo inajengwa.

Wafanyakazi wa Kilimo watakiwa kufanya Kazi kwa taaluma

Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi la Wizara hiyo Bw Peniel Lyimo, ametoa agizo kwa wafanyakazi wote wa wizara yake kufanya kazi kwa kuzingatia taaluma zao walizoajiriwa ili kuboresha utendaji wa kazi.
Akitoa mfano alisema kuwa si vizuri kwa Mkufunzi kufanya kazi za Mhasibu au Mhasibu kufanya kazi za ugavi. Alisisitiza kwa kusema kuwa kazi zote zinafanywa kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu kulingana na taaluma.

Mwenyekiti huyo alitoa agizo hilo wakati wa kikao cha Baraza kilichofanyika tarehe 8/11/2008 mjini Morogoro katika Ukumbi wa Morogoro Hotel na kuhudhuriwa na wajumbe mbalimbali wa Baraza hilo wakiwemo Wakurugenzi, Wakurugenzi wa Kanda, Wawakilishi kutoka Vyama Vya Wafanyakazi (TUGHE & RAAWU) na Wawakilishi wa Wafanyakazi.

Keep Left hiki cha Kituo cha Polisi Chang'ombe

Imenipasa kuandika kuhusu "Keepleft" kilichojengwa katika makutano ya barabara ya Sokota na na Chang'ombe karibu kabisa na Kituo cha Polisi Chang'ombe na Kanisa Katoliki Parokia ya Chang'ombe hapa jijini Dar Es Salaam.

Ukarabati wa barabara wa mahali hapo ambapo hapo awali palikuwa korofi sana sasa umekamilika na kipya kilichoongezwa ni kujengwa "Keepleft" asante sana. Lakini tangu kijengwe "Keepleft" hicho hakuona lolote la zaidi. Maua hayajapandwa.Kwa kifupi "Keepleft" hicho hakivutii kabisa sijui ni jukumu la nani. Manisapaa ya Temeke? TANROADS au nani ?Tuelewesheni basi.

Tuesday, November 4, 2008

Familia hii inapatikana SINZA kwa WAJANJA!



Ndiyo, familia kama hii inapatikana tu Sinza kwa wajanja. Wangalie walivyotulia. Bw na Bi Joseph Kamsopi Mdimi na wasimamizi wao pamoja na Binti yao EKA.

Hata Makaka na Madada walikuwapo na walitoa zawadi



Furaha ilioje kwa mdogo wetu, kaka yetu mpendwa wetu Kamsopi kupata jiko. Basi pokea zawadi yetu ya JIKO ili Flora akaangize!

Ninyweshe ni kunyweshe!


Ndivyo ilivyokuwa pale Africentre. Flora na Joe wakinyweshwana usiku wa tarehe 18 Oktoba 2008. Hakika raha tupu!

Flora alipata Kabati ya "Mbeho"




Inasemekana kuwa ukitaka kuchumbia mtoto wa Kichagga utaulizwa kuwa je huyo mchumba ana Kabati ya Mbeho? Na kweli Flora aliuliza swali hilo na Joseph alijibu ndiyo. Na kweli bwana, Mwenyekiti wa Kamati Bw Inno Banzi alimkabidhi Flora Yesusaa Msechu Kabati ya Mbeho siku ya harusi yao tarehe 18/10/2008.

Bwana na Bibi Mangengesa Mdimi walifurahi


Tarehe 18/10/2008 pale Afri-Centre jijini Dar- Bw na Bibi Mangengesa Mdimi walijawa na furaha kubwa kushuhudia sherehe ya watoto wao Joseph na Flora. Waangalie wanavyowakaribisha wageni waalikwa kwa kupunga mikono yao juuu juuu kabisa. Hongera sana

Monday, November 3, 2008

Joseph Kamsopi afanya kweli


Kijana mtanashati wa mchanganyiko wa Kimanda kutoka ziwa Nyasa na Kiluguru kutoka Morogoro mji kasoro bahari-Matombo, Kiswira - Joseph Kamsopi Mdimi amefanya kweli baada ya kufunga pingu za maisha na Bi Flora Yesusaa Msechu wa Kilimanjaro.



Harusi hii ilifungwa katika Kanisa Katoliki la Mwenye Heri Anuarite, Makuburi -External - Dar Es Salaam tarehe 18/10/2008 na kisha sherehe ya kufana ilifanyika katika Ukumbi wa Afri-Centre Msimbazi - jijini Dar Es Salaam. Hebu waone maharusi hapo kushoto juu wanapendeza ehee!