Tuesday, January 27, 2009

Tulitembea na kutembea

Mvua ya jana imeleta kizazaa kwa wakazi wa Mbagala na vitongoji vyake. Kutokana na msongamano wa magari na magari mengine kukwama kwenye barabara mpya inayojengwa usafiri ulikuwa wa shida sana siku ya jana jioni hadi leo asubhi.

Blog hii ilichapa mguu kutoka Mtoni Mtongani hadi KTM. Leo asubuhi Mbagala Rangi 3 kulikuwa hakuna mabus. Blog hii iliweza kulipa shilingi elfu 1000 kutoka Rangi 3 hadi Kizinga na kuanza kutembea tena hadi Mtoni Mtongani.

Lakini matatizo haya si kutokana na ujenzi wa barabara bali ni ubinafsi wa madereva kutaka kuwahi bila kujali wengine. Pia askari wa usalama wa barabarani nao wanazembea. Matokeo yake gari zinafungana.

Monday, January 26, 2009

Wavivu wa kuweka kumbukumbu

Nimegundua tatizo la watu wengi hasa sisi Watanzania hatupendi kuweka kumbukumbu ya shughuli zetu. Awe msomi, mkulima, mfanya biashara, mwalimu, fundi....................
Hatuweki kumbukumbu na hii ni hatari. Hatuwezi kujua gharama tulizotumia. Vitu tulivyokuwa navyo, wadeni wetu...........

Kwa hali hiyo basi hatuwezi kuwa na mipango sahihi kwa sababu hatuna data! Blog hii imekuwa ikijishughulisha na kilimo cha mpunga huko Kisemvule tangu mwezi Desemba. Imelipa vibarua wa kufyeka, kukatua, na kununua mbegu. Tayari sehemu fulani mpunga umeshapandwa lakini tarehe ya kupanda mpunga huo haifahamiki. Kweli ni wavivu wa kutunza kumbukumbu na hii ni hatari kwa maendeleo yetu.

Hapa ni pabaya

Watanzania wenzangu, hapa tulipofikia sasa ni pabaya. Iwapo tunaamini kuwa tunaweza kupata maendeleo kwa njia ya ushirikina basi tumekwisha. Watoto hawatasoma, wafanyakazi hawatofanyakazi kwa bidii. Wakulima watalaza majembe yao chini.

Kisa? Mbona unaweza kutajirika kwa kuwa na mkono wa zelu zelu(Albino)! Unaweza kufaulu mtihani wa darasa la saba kwa kidole cha zelu zelu. Unaweza ukapata madini ya Tanzanite hivi hivi tena bila kuyaona wala kuchimba ikiwa utakuwa na kiganja cha zelu zelu na unaweza kwenda Marekani ikiwa utakuwa na korodani ya zelu zelu - STUPID!

Hivi Manji ana ubavu wa kumzuia Ngassa?

Mchezaji wa kutumaini wa Taifa Stars na Dar Young Africans -watoto wa Jangwani Mrisho Ngassa amefanikiwa kupata timu ya kucheza mpira wa kulipwa huko Norway.Lakini inasemekana kuwa Bw.Manji amemzuia kwa sababu anazozifahamu yeye mwenyewe. Ndo maana nauliza hivi Manji ana ubavu wa kumzuia Ngasa asiondoke? Tusubiri matokeo.

KILWA ROAD UPDATE 3!

Ingekuwaje kama madaraja ya mto Kizinga yasingekamilika kabla ya mvua hizi. Nafikiri hali ingekuwa ngumu zaidi kwa wakazi wanaotumia barabara ya Kilwa hasa wakazi wa Mbagala na vitongoji vyake.

Lakini hali ni shwari kabisa, leo hii blog ilipita asubhi sana pale Kizinga bila utata wowote. Ujenzi wa barabara ya Kilwa unaendelea vizuri hata nakshi nakshi zimeanza kuwekwa kwenye vituo vya mabasi. Keepleft cha njia panda ya Mtoni Kijichi ndo kinachongwa. Mambo saaafi Mbagala!

Nimefurahishwa wakulima kugawa vyandarua

Gazeti la Majira la tarehe 19/01/2009 lilikuwa na habari nzuri inayohusu wakulima wadogo wa chai wilayani Rungwe (RSTGA) kugawa vyandarua 120 kwa akina mama wanaojifungua watoto kwa lengo la kupunguza kasi ya ugonjwa wa malaria.

Akina mama hawa wameonyesha njia. Kwanza wametambua tatizo na wamelifanyia kazi kwa sababu linawahusu zaidi wao na watoto. Kumbe hata sisi tunaweza kununua vyandarua hata kama ni vichache.

Viko wapi vyandarua vya Rais mstaafu wa Marekani Bw. George Bush? Au ndo tuseme ahadi hiyo haitekelezeki?

Saturday, January 24, 2009

Kweli tununue matrekta na siyo mashangingi

Rais Jakaya Mrisho Kikwete ameahidi kuwa serikali itabana matumizi ya ununuzi wa magari ili fedha hizo zipelekwe kununulia matrekta kwa ajili ya wakulima. Nafikiri sasa kinaeleweka kwa wakulima - twendeni tukalime.

Waziri Mkuu ameahidi kuongeza bajeti. Rais naye ameahidi matrekta yanunuliwe badala ya magari. Ndiyo, sasa tumepata viongozi watetezi wa wakulima. Tuchape kazi uzalishaji katika sekta ya kilimo uongezeke na uchumi wa nchi ukue na wananchi waishi maisha bora.

Asante Pinda kwa ufahamu wako wa kilio cha Sekta ya Kilimo

Jana katika gazeti la 'The Guardian" nimefurahishwa kusoma kuwa Waziri Mkuu Mizengo Pinda amesema kuwa serikali itaongeza bajeti kwa sekta ya kilimo (mazao,mifugo na samaki) kwani sekta hizo ni muhimili wa uchumi wa nchi na ni kichocheo cha maendeleo. Nasubiri kuona ahadi hiyo ikitekelezwa kwani mambo hayaendi sawa kibajeti kwenye sekta hizo.

Wakulima wanapouza vocha za pembejeo

Ukiwauliza wakulima wa Tanzania kwanini wanashindwa kulima kwa tija. Moja ya sababu wanazozitoa ni pembejeo za kilimo kuwa aghali mno hasa mbolea.

Kwa kuona hilo serikali imeweka mpango wa kuwapatia ruzuku ya mbolea wakulima kwa kupitia vocha za pembejeo. Sasa tunapopata habari kuwa, kuna wakulima wanauza vocha tena kwa bei rahisi ili waweze kupata fedha za kununulia mahitaji mengi basi hao si wakulima. Kuna haja ya kuwatambua wakulima wetu pengine si asilimia 80 kama tunavyodhani.

Tuwaelimishe wauzaji wa vyakula kwa afya ya mlaji

Siku hizi watu wengi wanafanya biashara ndogondogo ili kuweza kupata kipato cha kukabili maisha ya kila siku. Biashara nyingi zinazofanywa zinahusu vyakula vya aina mbalimbali iwe vilivyotayarishwa au kutoka shambani kama vile matunda.Tatizo ninaloshuhudia kila ninapotamani kununua vyakula hivyo ni mazingira yanamouzwa biashara hizo.

Sawa, utamkuta mwanamama/dada anauza samaki wa kukaanga lakini chombo alichowekea samaki hao na ukimwangalia yeye mwenyewe hali ya usafi inakatisha tamaa. Mtu anauza maembe, ndizi, machungwa. Lakini usafi hakuna. Bibi anachuuza korosho za kukaanga kando ya barabara vumbi kibao, nzi kibao, karatasi za kufungia chafu! Kweli inatukatisha tamaa sisi walaji ingawa tunatamani kula au kutafuna vyakula hivyo. Tunapoingia kwenye soko huria ni vizuri wauzaji wa vyakula na matunda wakaelimishwa kwa faida yao na faida ya walaji wajali afya zetu.

Tupunguze kuomba misaada isiyo ya lazima

Ukipanda daladala utasikia konda msaada hapo kwenye kona! Unapokuwa ofisini mnahimizwa kuandika maandiko ya miradi ya maendeleo ili muweze kupata msaada kutoka kwa wafadhili.
Unarudi nyumbani jirani yako anakuomba msaada wa chumvi!
Mtoto wa ndugu yako anataka kuoa msaada!

Kuna misaada tunayoomba ambayo ni muhimu kama vile ya elimu, afya au msiba. Lakini mingine si muhimu sana.Ikiwezekana tusimame wenyewe kama mtu binfasi au kama nchi. Na tabia hii ya abiria kuomba msaada hata kwenye mlima au kona ili ateremshwe ikome inasababisha ajali na si ustaarabu. Tuheshimu vituo vilivyowekwa.

Tujaribu usikate tamaa

Tatizo kubwa ninaloliona mimi kwa Watanzania wengi ni kukata tamaa katika maisha yetu. Wanafunzi wanakata tamaa kuwa hawawezi kufaulu hesabu na kiingereza. Wakulima wanakata tamaa kuwa mazao wanayolima hayana bei kwahiyo wanalima kidogo tu. Dereva wa daladala haondoi gari mapema kituoni kwani anakata tamaa kuwa hakuna abiria wengine kituo kinachofuata. Mchezaji mpira wa timu ya Taifa anakata tamaa kuwa hawawezi kuishinda Ivory Coast!

Tunjaribu tena na tena tusikate tamaa iko siku tutafanikiwa tukijatihidi na kuweka malengo.

Thursday, January 22, 2009

Halmashauri ya Wilaya imedhamiria kuleta mapinduzi ya Kilimo

Gazeti la Kulikoni la tarehe 8 Januari 2009 lilikuwa na habari ya Halmashauri ya wilaya ya Rorya mkoani Mara ilivyotoa baiskeli 80 zenye thamani ya milioni 7 kwa wakulima wawezeshaji wapatao 80 kwa juhudi za kuhamasisha sekta ya kilimo wilayani humo. Huu ni mfano mzuri wa kuigwa kwa Halmashauri nyingine.

Ikumbukwe kuwa asilimia zaidi ya 80 ya wananchi wetu wanategemea kilimo. Kilimo kikiboreshwa ni dhahiri kuwa maendeleo yatapatikana na hapo ndipo maisha bora kwa wananachi walio wengi yatakapoonekana. Halmashauri zisiwe na mtazamo wa kukukusanya kodi tu. Waweke mikakati ya kuongeza uzalishaji hasa katika kilimo ili waweze kupata mapato zaidi yatakayowezesha kusaidia miradi mingine ya maendeleo kama vile ya elimu, afya na miundo mbinu.

Hata mimi sikutegemea kama Obama angekuwa Rais wa Marekani

Kwa watu walio wengi si rahisi kusema ukweli wao walivyofikiri kabla ya tukio kutokea na kuwa kinyume chake. Lakini Bi.Mwakitwange waliokuwa pamoja na Tido Mhando katika TBC1 (TV) wakirusha matangazo ya mojakwamoja wakati wakuapishwa Rais mpya wa Marekani -Rais Barack Hussein Obama alisema kuwa kwa jinsi anavyoifahamu Marekani na hasa watu weupe hakutegemea kuwa Obama angepata kura za kutosha kumfikisha "White House." Tuseme ukweli si rahisi sana kwa mzungu kumwamini mweusi kuwa naye anaweza tena katika ngazi kubwa kama ile. Hata mimi sikutegemea kama Obama angeweza kuingia White House kwa sababu weupe nawafahamu sana wengi wanatuona hatuwezi! Hongera sana Obama na Familia yako. Hongera waamerika kwa kufanya kile ambacho hapo awali wengi wetu tulifikiri hakiwezekani.

Kilimanjaro Stars ilikuwa na nafasi nzuri ya kutwaa kombe la "Challenge"

Nachukua fursa hii ya kuipongeza Timu yetu ya Mpira wa miguu ya Tanzania Bara - Kilimanjaro Stars kwa kushika nafasi ya tatu ya mashindano ya Challenge cup yalifanyika nchini Uganda jijini Kampala mwaka huu.

Hata hivyo, kwa mtazamo wangu Kilimanjaro Stars ilikuwa na nafasi nzuri ya kushinda kombe hilo kutokana na jinsi walivyojitayarisha na kujengewa uwezo wa kila hali.

Stars ilikuwa na wachezaji wengi wazuri ambao juzi juzi tu wameweza kuifanikisha Taifa Stars (wachezaji wa ndani) kupata fursa kuingia kwenye fainali za mashindano ya ubingwa wa Afrika kwa wachezaji wasio wa kulipwa.

Tatizo kubwa kwa watanzania ni kutojiamini na kujituma kwa kila hali. Hii si kwa mchezo wa mpira peke yake hata katika shughuli nyingine. Hivyo basi ili tuweze kushinda siku zijazo timu itayarishwe vizuri kisaikolojia. Mpira tunaujua ila tunakosa mbinu basi tuwe na jopo litakalosaidia kutoa mbinu au mikakati ya ushindi.

KILWA ROAD UPDATE 2!

Ukarabati wa barabara ya Kilwa, kipande cha Mtoni Mtongani hadi Mbagala Rangi 3 unaendelea vizuri. Tangu Jumapili 18 Januari madaraja ya mto Kizinga yameanza kutumika (siyo rasmi) hivyo kuondoa wasiwasi kwa watumiaji wa barabara hiyo -Masika itakuwaje? Uwekaji wa lami nao unaandelea kwa kasi nzuri tu. Tatizo lipo kidogo pale KTM - kwenye makutano ya barabara ya Kijichi na Kilwa kiasi cha kusababisha kafoleni kadogo hivi lakini si kama zamani. Umeshanunua kiwanja Mbagala? Karibu - unachelewa!

MTANDAO ULIKUWA NA MATATIZO

Takribani siku 7 mtandao wetu hapa ofisini ulikuwa na matatizo, aidha nilitingwa na majukumu ya kiofisi hivyo kushishindwa kabisa kuning'iniza angalau post 1. Leo naona mambo ni shwari tuanze.

Wednesday, January 14, 2009

Ukaguzi wa mabasi asubuhi si suluhisho la ajali

Watu wanazidi kufa kwa ajali za kutisha barabarani. Ajali ya hivi karibuni iliyohusisha basi la Tashrif na kupoteza uhai wa watu karibuni 28 si kitu cha mchezo ni tatizo.

Kinachonishangaza ni kwamba tatizo hilo ni la muda mrefu na ufumbuzi wa tatizo hili bado sijaliona. Sababu kubwa inafahamika ni uendeshaji usio na tahadhari. Blog hii imeshasafiri sehemu mablimbali kwa kutumia mabus ya kampuni mbalimbali. Ilichoshuhudia ni uendeshaji usio wa tahadhari. Lakini cha ajabu abiria hushabikia mwendo wa kasi bila sababu ya msingi. Alama za barabarani zipo lakini hakuna dereva anayejali.Wao wanapeana taarifa kwa traffic walioko barabarani basi. Nafikiri adhabu zinazotolewa bado ni ndogo na hazitoi fundisho lolote. Labda niwe mkweli tu hata dereva anapovunja sheria anawahonga matrafiki mambo yanakwisha. Blog hii ilishakutwa na tukio hilo nikiwa kwenye safari ya kikazi kuelekea Arusha tena na gari la serikali tulikuwa tukisafiri km 60 kwa saa wakati sehemu hiyo tulitakiwa kuendesha 50 km kwa saa. Trafki alituzungusha akitaka tumpe kitu kidogo. Sisi tulisema hatuna!

Magari makubwa nayo ni moja ya chanzo cha ajali nyingi barabarani. Yakiwa njiani hufanya lolote. Hupaki hovyo wanapoona wao. Tena pengine kwa sababu ya kipuuzi kabisa (kwa nyumba ndogo!) haaweki alama yoyote. Usiku mzima gari limeegeshwa vibaya! Madereva wanaendekeza ulevi wakati wanajua kuwa wako barabarani.

Blog hii inasema kuchek magari asubuhi ni kero kwa abiria na wamiliki wa magari. Magari yakaguliwe wakati yanaingia kituoni kabla ya safari ya kesho. Kwa yale yanayofanya usafiri wa umbali mfupi kama vile Dar-Moro utaratibu mwingine utumike. Ajali hutokea huko barabarabi si vituoni.

Maji machafu kutoka KTM

Unaposafiri kwenda Mbagala pale Mtoni Kizinga mkono wa kushoto utaona kuna maji maji pamoja na majani yaliyoungua. Unapopandisha kidogo Mbagala Mission upande wa kushoto kuna kiwanda cha nguo maarufu -KTM. Kiwanda hiki humwaga maji yake machafu yanayotoka kiwandani kwenye mto Kizinga.

Hutakiwi kwenda maabara kubaini kuwa maji hayo yana sumu kwani kwa macho ya kawaida kabisa unaweza kuona kote ambako maji hayo yamepita mimea imenyauka kwa eneo kubwa. Hii ni uthibitisho kuwa maji haya yanasumu kali. Hata hivyo ni ajabu kuona kuwa baadhi ya watoto wanaoga kwenye maji hayo machafu. Hivi karibuni blog hii imeshuhudia watoto wengi wakipiga mbizi kwenye maji hayo hasa wakati mvua nyingi inaponyesha kiasi cha kuchanganyika na maji hayo na kufanya bwawa kubwa hapo Kizinga.

KILWA ROAD UPDATE!

Ha! barabara ya Kilwa kipande cha Mtoni Mtongani hadi Mbagala Rangi 3 ndo kinakaribia kumalizika. Blog hii imeamua kuwapatia maendeleo ya ukamilishaji wa kipande hiki kila inapobidi. Hii inatokana na ukweli kuwa kwa miaka mingi Mbagala imeonekana kuwa na tatizo sugu la usafiri kutokana uchakavu wa barabara yake na ufinyu wa barabara hiyo ukilinganisha na magari mengi yanayotumia barabara hiyo. Hata kusababisha watu kuwakejeli watu wanaoishi Mbagala!

Kampuni ya Ujenzi ya Kajima inandelea vizuri sana. Madaraja mawili pale mtoni Kizinga yameshakamilika. Kilichobaki ni kushindilia udongo pamoja na mambo mengine madogo madogo-nakshi nakishi.

Huwezi kuamini barabara hiyo kwa sasa ni kama vile uwanja wa Taifa mpya kwani una nyavu kando ya barabara sehemu ambazo zimenyanyuliwa sana ili kuepusha magari na waendeo kwa miguu wasitumbukie korongoni.

Ukitoka Mbagala Rangi 3 upande wa kushoto tayari lami imeshawekwa hadi KTM. Baadhi ya sehemu magari yameshaanza kutumia kipande hicho kilichowekwa lami.

Wenye magari msiogope kwenda Mbagala mambo yameanza kubadilika. Nafikiri barabara hii inaweza kuwa moja ya barabara za kisasa nchini. Karibuni Mbagala!

Monday, January 5, 2009

Kuingia choo cha wanawake!

Wasomaji wapenzi wa blog hii leo nawaleteeni msemo mpya wa kiswahili ulioingia hapa jijini Dar kwa siku za karibuni hasa kwa vijana. Utasikia ah fulani ameingia choo cha wanawake!

Maana yake nini hasa? udadisi wa blog hii umegundua kuwa kuingia choo cha wanawake ni kuingia mkenge, au kushika pasipo kusudiwa. Hii haijali anayeambiwa ni mwanamke au mwanaume.

Friday, January 2, 2009

Lengo ni kuning'iniza posts 365!

Mwaka wa jana niliweka lengo la kuning'iniza post 100 kwenye blog yangu baada ya baadhi ya wasomaji wangu kunibeza kwa kuning'iniza posts 16 tu kwa mwaka 2006 nilipofungua blog yangu na hali ikawa hivyo kwa mwaka uliofuata(2007). Wapenzi wa Banzi wa Moro walikatishwa tamaa na mwenendo huo.

Kunibeza kwao kulinifanya niweke lengo mwaka wa jana (posts 100). Namshukuru Mungu kuwa nilivuka lengo kwa kupost 195! Mwaka huu naweka lengo jipya la post 365! Tuombe Mungu. Wapenzi wa Banzi wa Moro msichoke kufuatilia blog hii. Nawaomba sana mwaka huu mtume maoni yenu.

Karibuni

Beckham lazima afahamu kuwa sasa mpira basi

David Beckham ni mchezaji Mwingereza aliyewahi kutamba sana mwishoni mwa miaka ya 90 na mwanzoni mwa 2000.

Hivi karibuni vyombo vya habari vimekuwa vikimzungumza sana lakini nionanvyo mimi kama ni mpira tu Beckham hana chake. Umri unamtupa mkono na lazima akumbuke kuwa kila kitu kina mwanzo na mwisho. Hata Pele alivuma sana lakini sasa ni historia. Beckham lazima afahamu hilo.

Mwaka mpya Tulikuwa kwa Luanda

Kwangu mimi mwaka 2009 uliingia bila papara. Sikuweza kungojea hadi saa sita usiku eti nipige madebe au vibweka au kugongeana glass za vinywaji. Natumaini wakati ndo unasogea, makeke yamepungua. Ilipofika mwaka 2009 tayari nilishachoka na kujitupa kitandani.

Namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunilinda kuwa hai hadi kufikia tarehe ya leo. Mengi yametokea mwaka 2008 ambayo yangeweza kupoteza uhai wangu. Magonjwa ajali na mengineyo.

Hata hivyo lazima niseme kuwa ubinadamu ni pamoja na kuwa na watu. Mimi na familia yangu tulikaribishwa kule Kigogo darajani nyumbani kwa ndugu yangu na rafiki wa siku nyingi ambaye tumesoma wote shule ya msingi na hatimaye sekondari ya Njombe Bw. Michael Luanda.

Kwa miaka kadhaa sasa Michael hakuwa hapa jijini ila familia yake ilikuwa hapa. Sasa Michael amerudi tena Dar. Tarehe 1/1/2009 tuliitumia kwa kula, kunywa kidogo, gumzo pamoja na kujadili mambo mengi yaliyopita na si ya mwaka 2008 tu bali yote ambayo tuliweza kuyakumbuka.

Tunaishukuru sana Familia ya Michael Luanda kwa kutukaribisha kusherehekea pamoja Mwaka mpya 2009.