Wednesday, September 30, 2009
Afadhali kuwa na pikipiki
Mwishoni mwa juma la jana nilisafiri kwenda kijijini Matombo. Kipya nilichoona ni usafiri wa pikipiki ulivyopamba moto. Nilikuta pikipiki Kiroka, Mkuyuni, Njia panda ya Kinole na Mtamba. Hii ina ashiria nini? Usafiri vijijini unaanza kuboreka. Baiskeli zinaanza kupungua kidogo kidogo. Hii ni hatua kubwa ya maendeleo. Tulitembea kwa miguu, baadaye wachache wakabahatika kuwa na baiskeli lakini tulianza kurukia magari kabla ya kuwa na pikipiki. Tumerudi mahali pake ndo maana nasema afadhali kuwa na pikipiki kuliko kutembea kwa miguu. Lakini pikipiki hizi zitumiwe kwa uangalifu la sivyo zitaleta madhara kwa jamii.
Friday, September 18, 2009
LULU anahamasisha TUGHE
Si jambo la kawaida kwa mzazi kumshirikisha mtoto wake kwenye shughuli za kitaifa tena ikiwa mtoto mwenyewe ni binti. Si hivyo kwa Bw. Omari Shomari mfanyakazi wa Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika aliyekuwa tayari kwenda kwenye maandamano ya Sherehe za Wafanyakazi mwaka huu zilizofanyika mkoa wa Dar ES Salaam kwenye uwanja wa UHURU. Pichani Bi Lulu Shomari akifurahia maandamano akiwa na baba yake Omari Shomari, Banzi wa Moro na Salehe Mkwawa (Mzee wa Yanga) tarehe 1/5/2009. Bw. Omari Shomari ni mwanachama mwanzilishi wa TUGHE-KILIMO MAKAO MAKUU. Kweli Lulu anahamasisha TUGHE.
My Friend Dr. Sabuni
Enzi zangu Njombe Sekondari
Mwaka 1974 niliitwa 'Bazooka' 'Mugia' pale Njombe Secondary School (NJOSS). Nilikuwa mmoja kati ya wanafunzi wadogo pale shuleni si kwa ufupi tu hata kwa umri. Namkumbuka mtoto mwingine alikuwa ni Morris Calist (Mchaga) na mwingine tena Mchagga (jina nimesahau). Wenyeji wa Njombe mjini walikuwa wakitushangaa sana kuona watoto wadogo tukisoma sekondari - wenyewe wakituita 'wasekondari.'
Wakati ule shule hii ilikuwa maarufu sana wilaya nzima sekondari moja tu. Tukigoma mkuu wa wilaya anatusikia! Tulikuwa tunapata miche ya sabuni, Tanbond na karanga, chai kwa mikate (virungu), magodoro hapohapo shuleni, madaftari bure! Isitoshe tukifunga shule mabasi ya 'Railways' yalikuwa yakitusafirisha hadi nyumbani kwetu serikali inalipa. Mimi yalinifikisha hadi Magomeni Qtrs. Nakumbuka yalikuwa yanapitia barabara ya Kondoa pale Magomeni tulikuwa na akina Michael Luanda, Lawrence Mkude. Wote tulikuwa sawa hakuna tajiri wala maskini! Shuleni hapo darasa moja tulikuwa na Henry Aikael Mbowe (Kaka yake Philemon Mbowe-Mwenyekiti wa Chadema).Nyumbani tuliitwa 'WASEKO.' Sasa mambo yamebadilika kabisa wanaosoma shule za sekondari za serikali wanadharauliwa eti wanasema shule za kata ni shule za walala hoi.Mtoto akichaguliwa kwenda shule ya serikali wazazi wanamuhamisha wanampeleka 'Private.' Pichani Banzi wa Moro akiwa NJOSS nje ya Maktba ya shule mwaka 1974.
Siku ya wazazi Kisemvule
Kwa mara ya kwanza tangu Shule ya Msingi Kisemvule iliyoko wilaya ya Mkuranga mkoa wa Pwani ianzishwe, mwaka huu iliandaa siku ya wazazi na kuwaalika wazazi na wageni wengine kuona shughuli za watoto wao wakiwa shuleni. Pichani wanafunzi wakitoa burudani ya ngoma kwa wazazi wao pamoja na wageni waalikwa waliofurika shuleni hapo.
Wanafunzi wanapocheza ngoma wanaamsha morari
Pamoja na kujifunza na masomo mengine darasani ni vizuri wanafunzi wakajifunza ngoma za asili ili kujenga uzalendo na morari. Wakati mwingine mwili unachoka ati. Pichani wanafunzi wa shule ya msingi Kisemvule wilayani Mkuranga mkoa wa Pwani wakicheza ngoma kuwaaga wanafunzi waliomaliza darasa la saba mwaka huu. Sherehe hizo za wazazi 'parents day' zilifanyika kwa mara ya kwanza shuleni hapo mwezi Agosti 2009
Wednesday, September 16, 2009
Friday, September 11, 2009
Wakulima watafiti aina bora za ufuta
Hii ndiyo Kauli mbiu ya Siku ya Chakula Duniani
Safi sana Marini Hassan Marini
Marini Hassan Marini ni mmoya ya watangazaji mahiri wa TBC (Tanzania Broadcasting Company) kwa sasa.
Kwa nini ni mahiri. Hii ni jinsi anavyotayarisha vipindi vyake na jinsi anavyoripoti taarifa mbalimbali.
Kwa nini ni mahiri. Hii ni jinsi anavyotayarisha vipindi vyake na jinsi anavyoripoti taarifa mbalimbali.
- Vipindi vyake vinavutia kama vile -Jambo Tanzania
- Anahoji bila woga
- Maswali yake ni ya msingi
- Mada zinazozungumziwa ni za aina mbalimbali
- Wanaohojiwa si watu maarufu tu hata watu wa kawaida
Safi sana Marini Hassan Marini na Hongera TBC. Lakini haya ni maoni yangu.
Friday, September 4, 2009
Tunapozika 'mgomba'
Mara nyingi nimewahi kusoma au kusikia kuwa ah "wale wamezika tofauti zao" ikiwa na maana wamekubaliana kitu fulani ambacho hapo awali walikuwa na mawazo tofauti. Hapa nchini mambo haya yametokea mara nyingi kwenye vyama vya siasa. Hivi karibuni chama cha CHADEMA kiliingiwa na mtafuruku fulani kwa viongozi wenye mvuto ZITTO KABWE na FREEMAN MBOWE wote kuwania nafasi ya UENYEKITI kwenye chama hicho. Lakini baada ya ushauri wa ndani na nje ya chama hicho inasemekana kuwa wote wawili wamezika tofauti zao na sasa wote lengo lao ni kukijenga CHADEMA hasa wakati huu wanapoelekea kwenye uchaguzi wa Kitaifa wa mwaka 2010. Ndiyo maana Mchora kikatuni Nathan anataka kujua kweli wamemaliza tofauti zao au wamezika "mgomba?" Picha kwa hisani ya gazeti la Majira 4 Septemba 2009.
Ikiwa hatutambui umuhimu wa choo kwa wanafunzi wetu kazi kwelikweli
Shule ya Msingi Mnyamasi (Sijui iko wilaya na mkoa gani). Wanafunzi wa shule hiyo wanaonekana pichani wakipishana kwenda chooni. Angalia choo chenyewe. Hivi tunangojea akina nani watujengee vyoo. Wazazi, walimu hata viongozi wa kijiji hicho, kata na wilaya kweli hatutambui umuhimu wa kuwa na choo bora katika shule zetu? Tunangojea JICA watujengee choo kweli katika karne hii? Picha hii inaonekana katika Majira ya leo tarehe 4 Septemba 2009 uk.1
Jamani Mwakyembe!
Gazeti la Majira la leo tarehe 4 Septemba 2009 uk. 4 limeandika habari ya Mwakyembe kunususrika kuchomwa kisu tena nyumbani kwao Kyela wakati akihutubia mkutano wa hadhara. Kwa mujibu wa gazeti hilo, Dkt. Mwakyembe amekiri kutokea tukio hilo alipohojiwa kwa njia ya simu.Inasemekana kuwa walinzi wake Dkt. Mwakyembe waligundua mapema njama hizo na walipojaribu kumkaribia mmoja wa vijana waliohisiwa alikimbia na kudondosha kisu na mwingine wa pili alipokamawatwa alikutwa na simu aina ya Sonny Erricson na vinasa sauti.
Mei 21 mwaka huu Dkt. Mwakyembe alipata ajali ya gari huku kukiwa na taarifa tata zinazopingana, moja ikiweka wazi kwamba gari lake liligongwa na lori ambalo halikukamatwa mara moja na nyingine ikidai kwamba dereva wake aligonga shimo na kukosa uelekeo linaandika gazeti hilo la kila siku hapa nchini.
Thursday, September 3, 2009
KWA HAKIKA TUNACHANGANYA WARAKA NA ILANI
Inavyoelekea wengi hatufahamu maana ya maneno haya mawili WARAKA na ILANI ndiyo maana yanatuchanganya ni tusipompata mwalimu mzuri wa kutufafanulia hili kwa kweli tutachanganyikiwa. Mnasemaje wadau?
BABA WATAIFA ALISEMA NINI KUHUSU KILIMO?
Kwa sababu ya umhimu wa kilimo katika maendeleo yetu ingetegemewa kuwa kilimo na mahitaji ya wakulima yangekuwa ndio chanzo cha kupewa kipaumbele katika utayarishaji wa mipango yote ya uchumi wetu. Badala yeke tumechukulia kilimo kama sekta ya pembezoni au kama shughuli nyingine yoyote ya kawaida ambayo inatumiwa na sekta nyingine bila yenyewe kupewa umuhimu wowote ule.... Tunakipuuza kilimo; kama tungekuwa hatukipuuzi, basi Wizara zote, mashirika ya umma yote na mikutano yote ya chama ingekuwa inafanya kazi kushughulikia mahitaji ya wakulima. Ni lazima sasa tuache kukipuuza kilimo. Ni lazima tukifanye kilimo ndio shina na mwanzo wa mipango yetu yote ya maendeleo. Kwani kwa hakika, kilimo ndio msingi wa maendeleo yetu.
Baba wa Taifa, Mwalimu Julius K.Nyerere-1982
HIZI NDIZO NGUZO 10 ZA KILIMO KWANZA
1. UTASHI WA KISIASA KUTOA MSUKUMO WA MAPINDUZI YA KILIMO
2.KUGHARAMIA MAPINDUZI YA KILIMO
3.UBORESHAJI WA MFUMO WA UTAWALA WA KILIMO
4.MABADILIKO YA MFUMO MKAKATI KATIKA KILIMO
5.UPATIKANAJI WA ARDHI KWA AJILI YA KILIMO
6.VIVUTIO VYA KUCHOCHEA UWEKEZAJI KATIKA KILIMO
7.UENDELEZAJI WA VIWANDA KATIKA KULETA MAPINDUZI YA KILIMO
8.SAYANSI, TEKNOLOJIA NA RASLIMALI WATU KATIKA KUWEZESHA MAPINDUZI YA KILIMO
9.UENDELEZAJI WA MIUNDOMBINU ILI KUWEZESHA MAPINDUZI YA KILIMO
10.UHAMASISHAJI NA USHIRIKISHWAJI WA WATANZANIA KUUNGA MKONO NA KUTEKELEZA KILIMO KWANZA
Subscribe to:
Posts (Atom)