Baharini kuna mambo. Huyu naye ni samaki! Hayo mazaga zaga yote ni kwa kujilinda. Ni misumari yenye sumu kali. Ukikanyaga tu lazima udhurike. Samaki wa aina hii anapatikana Australia anaitwa 'the reef stonefish.' Pamoja ya kuwa ni samaki lakini sijui kama analiwa. Kwanza utamkamataje samaki wa aina hii?
Monday, May 18, 2015
Unaweza kusafiri na nyoka ndani ya ndege
Hebu angalia vizuri nadhani kwenye picha hii unaweza kuona nyoka. Unaposafiri na nyoka ndani ya ndege na ghafla akatokea ndani ya mkoba wako, kwa akili za kawaida utadhani kuwa umerogwa na hasa kama unakwenda majuu kusoma tena majuu yenyewe ni USA! Kwa Australia ni kitu cha kawaida kwa nyoka kuingia ndani ya ndege. Picha kwa hisani ya mtandao.
Pweza huyu ni hatari
Pweza huyu anajulikana kwa jina la 'blue ringed octopus' ana sumu kali sana. Inasemekana kuwa akikuuma basi huchukui masaa mawili umeshaisha! Pweza wa aina hii wanapatikana Australia. Sijui kama kwenye bahari yetu ya Hindi wapo. Kwa kawaida samaki aina ya Pweza hupatikana baharini tu (maji chumvi). Pamoja na kupenda kula Pweza huyu anatisha!
Wednesday, May 13, 2015
Ng'ombe wenye nundu bado lulu India
Wahindi hawajatelekeza ng'ombe wao wa asili, isipokuwa wanazidi kuendelea na utafiti ili waweze kuleta tija, kwani ng'ombe hao wapo siku nyingi wanastahimili mazingira ya sehemu hizo. Wako wapi ng'ombe wetu wenye nundu? Wako wapi Zebu wetu wenye nyama tamu. Wako wapi? Watafiti tuambieni, utafiti unaendelea? Je, tumewekeza vya kutosha katika utafiti wa mifugo? Jibu sina uhakika kwa hilo.
Teknolijia zinavyosambazwa na Taasisi zinavyojitangaza India
Mwaka jana nilibahatika kuwa katika msafara wa mafunzo nchini India. Madhumuni ya msafara huo ni kujifunza jinsi wenzetu wa India wanavyoendesha Taasisi za Utafiti. Moja ya kitu ambacho nimevutiwa nacho ni jinsi wanavyotunza kumbukumbu na jinsi wanavyosambaza teknolojia za kilimo na jinsi taasisi zinavyojitangaza. Kikubwa wenzetu ni wazalendo. Hata katika lugha, mabango yote yanatanguliwa na lugha yao na kufuata Kiingereza hii haidhoofishi sayansi, badala yake inakuza sayansi kwani mtu anafanya kitu anachokielewa na pia wadau wanafaida nacho.
Unapopokelewa katika taasisi kabla ya kupata maelezo ya shughuli za kituo hicho, unawekewa clip yenye nyimbo ya Taasisi na wote wanajivunia. Nyimbo inapoimbwa unajionea na kusoma historia ya taasisi, shughuli wanazofanya na mafanikio waliyoyapata. Na hiki ndicho tumekishauri kwa Taasisi zetu za Utafiti kuiga, kwani gharama yake si kubwa kama inavyodhaniwa. Angalia mabango hayo hapo juu yanajitosheleza. Kwa njia hii teknolojia inasambazwa kwa haraka na Taasisi inajitangaza.
Ninapomkumbuka Uncle Dr. G.Mluge
Dr. Gregory Paul Mluge (R.I.P.) na mkewe Restituta Mluge wakiwa na mjukuu wao katika picha ya pamoja mwaka 2011. Baada ya kuipata picha hii nimeamua kuining'iniza kwenye blog hii ya Banzi wa Moro kwa kumbukumbu. Nitakukumbuka daima unlce Dr. Mluge ulikuwa nguzo ya familia na utaendelea kuwa nguzo ya familia kwa msingi uliouweka katika maisha yako. Dr. Mluge alifariki mwaka 2013 na kuzikwa nyumbani Matombo (Kiswira), Morogoro. Amina.
St. Francis Secondary School ya Mbeya yakabidhiwa Tuzo
Wengi tunaisikia St. Francis Secondary School ya Mbeya. Ni shule inayofanya vizuri kitaaluma. Imekuwa ikishikilia nafasi 10 za juu za ufaulu hapa nchini karibu kila mwaka. Shule hii iko makini sana katika kudahiri wanafunzi wanaojiunga na shule hiyo. Si rahisi kupata nafasi kama kijana hana uwezo. Na anapojiunga na shule hiyo pamoja na ukweli kuwa iko vizuri kitaaluma lakini wanaangalia sana nidhamu ya mwanafunzi.Wanafunzi wanatakiwa kuchapa kazi wakiwa shuleni, kutambua kuwa MUNGU yupo na kumwabudu. Nimeambiwa kuwa hakuna kujidai ukiwa shuleni hapo kama baba au mama yako ni Waziri, Mbunge,Mkurugenzi, Profesa au Meneja hiyo ni kwenu. Hakuna kuleta majidai ukiwa shuleni hapo. Pichani Waziri Mkuu Mhe. Mizengo Pinda akikabidhi Tuzo kwa mwakilishi wa shule hiyo mjini Dodoma hivi karibuni.
Thursday, May 7, 2015
Friday, May 1, 2015
Subscribe to:
Posts (Atom)