Friday, November 14, 2008

Kanisa Katoliki Parokia ya Vikindu -Mt. Vincent wa Paulo



Hili ndilo Kanisa ninalosali mimi. Kanisa Katoliki la Parokia ya Vikindu. Kanisa hili tumelijenga kwa nguvu zetu sisi waumini pamoja na marafiki zetu wa ndani na nje ya nchi. Kanisa hili limejengwa na baadhi ya waislamu waliojitolea bila kujali tofauti ya dini.Ndiyo hatukumsubiri OBAMA.Tulijtegemea wenyewe.

Nilipohamia Vikindu-Kisemvule mwaka 2004, tulikuwa tunasali kwenye ukumbi mdogo tu. waumini tulikuwa wachache sana hata sadaka ilikuwa chache pia. Ibada Takatifu siku ya Jumapili ilikuwa ni moja sasa kuna misa ya pili ya watoto. Kanisa hili zuri lina vipaaza sauti, lina madawati mazuri ya kukalia, lina kwaya nzuri pia na kwa kweli linapendeza ndani na nje. Karibuni sana Vikindu.
Parokiani Vikindu kuna Zahanati nzuri tu, kuna shule ya watoto wadogo na shule ya msingi ambayo hufundisha kwa kiingereza zote zinamilikwa na Parokia ya Vikindu. Kanisa limeleta maendeleo ya kiroho na kimwili. Watawa wa Vikindu wanapaita mahali hapo "Jesus Town"

Hongera wanamichezo wa "KILIMO"

Timu ya michezo ya Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika mwaka huu 2008 imefanya maajabu kule Morogoro kwenye mashindano ya SHIMIWI. Wameweza kuwa washindi wa jumla wa tatu kati ya timu 54 zilizoshiriki.

Kilimo imeweza kuwa mshindi wa tatu katika mpira wa Miguu, mshindi wa nne mpira wa pete, bao mshindi wa pili na riadha wamepata medali. Hii imetokana na maandalizi mazuri, kujituma na nidhamu ya hali ya juu waliokuwa nayo wachezaji wakati wote wamaandalizi na mashindano. Hongera sana Mwenyekiti wa Kilimo Sports Klabu Bw. George Mbelwa.

Maximo unaikomoa Tanzania si Kaseja

Anayekomolewa ni Mtanzania na si Kaseja. Kama Kocha Maximo una ugomvi na Kaseja basi nendeni kortini. Usituharibie soka letu. Kaseja bado ni mlinda mlango na 1 hapa nchini. Mimi ni mpenzi wa Simba hata hivyo bado namuona Kaseja ni golikipa bora licha ya kuwa amehamia Yanga. Maximo mpange Kaseja timu ya Taifa uone vitu vyake achana na huyo Ivo Mapunda anayetematema mipira hovyo.

Machungwa yako sokoni

Watanzania sasa tunaanza kufaidi matokeo ya teknolojia bora za kilimo. Machungwa sasa yanapatikana sokoni wakati huu mwezi Novemba tena matamu sana, tena makubwa na tena kwa bei poa.

Iwapo sekta ya kilimo itaongezewa raslimali kwa asilimia 5 tu , kile kisichowezekana kitawezekana na kuwa na ziada. Mazao mengi yanayoonekana sokoni hivi sasa ni juhudi za mkulima huyu mdogomdogo, asiyekuwa na pembejeo bora za kilimo, anayetumia zana duni za kilimo na anayetegemea kilimo cha mvua!

Si mshabikii OBAMA

Nimefurahi kuwa OBAMA ameshinda kinyang'anyiro cha kiti cha Rais nchini Marekani.
  • Lakini sitegemei maajabu kutoka kwa OBAMA katika kuboresha maisha yangu
  • Kwa wale wanaotegemea misaada hiyo wasahau na haitakuwa rahisi kama wanavyofikiri wao
  • Wakumbuke kuwa OBAMA ni Mwamerika licha yakuwa ana rangi nyeusi!
  • Watanzania tuchape kazi
  • Watanzania tuongeze uzalendo na tuipende nchi yetu
  • Watanzania tuwe wabunifu
  • Watanzania tupunguze kulalamika bila sababu ya msingi
  • Tupunguze vitendo vya rushwa

Kwa hiyo simshabikii OBAMA

Viongozi wa nchi wavalia njuga kilimo na kuona kuwa inawezekana

Viongozi wetu wengi wameanza kuhamasisha na kufuatilia shughuli za uzalishaji wa kilimo kwa vitendo na sasa inaonekana kuwa kila kitu kinawezekana kwa ajili ya kuendeleza Kilimo.


Hivi majuzi tu Waziri Mkuu Mhe. Mizengo Pinda katika ziara yake mkoani Dodoma aliweka mkwara mkali kwa wakuu wa wilaya na mikoa kwamba wakati wa kuvaa suti kila siku umekwisha wanahitajika kuvalia njuga kilimo kwa nguvu zao zote.


Tayari Mkuu wa wilaya ya Kondoa Bw Seif Mpembenwe amemweleza Waziri Mkuu kuwa wilaya yake inaweza kujitosheleza kwa chakula. Sasa kama wilaya zote zitaahidi hivyo na kukipa kilimo kipaumbele katika shughuli zake, tatizo liko wapi?

Thursday, November 13, 2008

Wamisionari wametuachia urithi mkubwa lakini bado tumelala

Wiki ya jana nilisafiri kwenda Morogoro kushiriki katika mazishi ya Binti yetu Rose Aniani Mbiki (Mtoto wa mdogo wangu) aliyefariki pale Bigwa Morogoro. Mungu ailaze mahali pema peponi roho ya marehemu Rose.

Ibada takatifu ya mazishi ya kumuombea marehemu ilifanyika kwenye kanisa la Bigwa (Sekondari ya Masista-Bigwa). Sijawahi kuingia ndani ya Kanisa hilo lakini nilivutiwa sana kwa jinsi Kanisa hilo lilivyojengwa kwa matofali ya kuchoma kwa mpangilio mzuri tu. Milango ilivyotengenezwa inapendeza na utaalamu wa hali juu umetumika.

Makanisa mengi ya jimbo la Morogoro yamejengwa zamani na Wamisionari. Ukiangalia utaalamu uliotumika ni wa hali ya juu sana ukizingatia na hali halisi ya vifaa kwa wakati ule. Bado sielewi, hivi ni kwanini tunashindwa kuuendeleza utaalamu ule? Udongo ni uleule watu wapo kwanini tusiboreshe yale tuliyoyakuta na kusonga mbele? Ajira tunazozitafuta si kama hizi za ujenzi? Vijana wangapi wa Bigwa, Matombo na Morogoro kwa ujumla wamerithi taalama hii ya ujenzi au wanajenga kwa kulipua tu?

Wafanyabiashara ndogondogo waelimishwe

Idadi kubwa ya watu jijini Dar Es Salaam na miji mingine hapa nchini hufanya biashara ndogondogo. Lakini leo hii nitazungumzia biashara za vyakula, matunda na vitafunwa.

Utamkuta mtu anauza korosho, karanga, majibaridi, maembe, pilau, samaki wa kukaanga n.k. Lakini yeye mwenyewe mchafu, chombo alichowekea chakula kichafu, mazingira anayouzia chakula ni machafu. Hivi kweli kwa hali hii mteja anaweza kuvutiwa na biashara yako?

Mimi napenda sana kutafuna korosho, lakini wakati mwingine nasita kununua korosho ambazo zinauzwa na mtoto mdogo mchafu ambaye huchezea chezea korosho hizo wakati akizipanga kwenye mafungu. Au utakuta mwanamama anauza chakula huku ananyonyesha au kujikuna sehemu mbalimbali. Kwa hali hii ni vizuri wafanyabiashara ndogondogo wakaelimishwa. Si elimu ya mikopo tu bali jinsi gani wanavyoweza kuvutia biashara zao.

Sababu za foleni barabara ya Kilwa

Barabara ya Kilwa ninaitumia karibu kila siku. Kwa sasa barabara hiyo iko kwenye ukarabati mkubwa. Barabara inapanuliwa na madaraja mapya yanajengwa. Kutokana na hali hiyo huwa kunatokea usumbufu mkubwa wa usafiri wakati wa asubuhi na jioni. Safari ya dkika ishirini inaweza kuchukua zaidi ya saa moja. Sababu kubwa ya kuwa na foleni yakukatisha tamaa hata kusababisha watu wengi kutembea kwa miguu ni hizi hapa.

  • Madereva wasiozingatia sheria na taratibu za kuendesha magari
  • Wajenzi wa barabara kutoweka vizuizi kwa sehemu ambazo hazistahili kupita magari
  • Askari wa Usalama barabarani (Traffic Police) kutofanya kazi yao barabara kwa kuelekeza za kupita magari.
  • Viongozi wa Manispaa ya Temeke kutolishughulikia suala hili ili liweze kupatiwa ufumbuzi wa muda wakati barabara hiyo inajengwa.

Wafanyakazi wa Kilimo watakiwa kufanya Kazi kwa taaluma

Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi la Wizara hiyo Bw Peniel Lyimo, ametoa agizo kwa wafanyakazi wote wa wizara yake kufanya kazi kwa kuzingatia taaluma zao walizoajiriwa ili kuboresha utendaji wa kazi.
Akitoa mfano alisema kuwa si vizuri kwa Mkufunzi kufanya kazi za Mhasibu au Mhasibu kufanya kazi za ugavi. Alisisitiza kwa kusema kuwa kazi zote zinafanywa kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu kulingana na taaluma.

Mwenyekiti huyo alitoa agizo hilo wakati wa kikao cha Baraza kilichofanyika tarehe 8/11/2008 mjini Morogoro katika Ukumbi wa Morogoro Hotel na kuhudhuriwa na wajumbe mbalimbali wa Baraza hilo wakiwemo Wakurugenzi, Wakurugenzi wa Kanda, Wawakilishi kutoka Vyama Vya Wafanyakazi (TUGHE & RAAWU) na Wawakilishi wa Wafanyakazi.

Keep Left hiki cha Kituo cha Polisi Chang'ombe

Imenipasa kuandika kuhusu "Keepleft" kilichojengwa katika makutano ya barabara ya Sokota na na Chang'ombe karibu kabisa na Kituo cha Polisi Chang'ombe na Kanisa Katoliki Parokia ya Chang'ombe hapa jijini Dar Es Salaam.

Ukarabati wa barabara wa mahali hapo ambapo hapo awali palikuwa korofi sana sasa umekamilika na kipya kilichoongezwa ni kujengwa "Keepleft" asante sana. Lakini tangu kijengwe "Keepleft" hicho hakuona lolote la zaidi. Maua hayajapandwa.Kwa kifupi "Keepleft" hicho hakivutii kabisa sijui ni jukumu la nani. Manisapaa ya Temeke? TANROADS au nani ?Tuelewesheni basi.

Tuesday, November 4, 2008

Familia hii inapatikana SINZA kwa WAJANJA!



Ndiyo, familia kama hii inapatikana tu Sinza kwa wajanja. Wangalie walivyotulia. Bw na Bi Joseph Kamsopi Mdimi na wasimamizi wao pamoja na Binti yao EKA.

Hata Makaka na Madada walikuwapo na walitoa zawadi



Furaha ilioje kwa mdogo wetu, kaka yetu mpendwa wetu Kamsopi kupata jiko. Basi pokea zawadi yetu ya JIKO ili Flora akaangize!

Ninyweshe ni kunyweshe!


Ndivyo ilivyokuwa pale Africentre. Flora na Joe wakinyweshwana usiku wa tarehe 18 Oktoba 2008. Hakika raha tupu!

Flora alipata Kabati ya "Mbeho"




Inasemekana kuwa ukitaka kuchumbia mtoto wa Kichagga utaulizwa kuwa je huyo mchumba ana Kabati ya Mbeho? Na kweli Flora aliuliza swali hilo na Joseph alijibu ndiyo. Na kweli bwana, Mwenyekiti wa Kamati Bw Inno Banzi alimkabidhi Flora Yesusaa Msechu Kabati ya Mbeho siku ya harusi yao tarehe 18/10/2008.

Bwana na Bibi Mangengesa Mdimi walifurahi


Tarehe 18/10/2008 pale Afri-Centre jijini Dar- Bw na Bibi Mangengesa Mdimi walijawa na furaha kubwa kushuhudia sherehe ya watoto wao Joseph na Flora. Waangalie wanavyowakaribisha wageni waalikwa kwa kupunga mikono yao juuu juuu kabisa. Hongera sana

Monday, November 3, 2008

Joseph Kamsopi afanya kweli


Kijana mtanashati wa mchanganyiko wa Kimanda kutoka ziwa Nyasa na Kiluguru kutoka Morogoro mji kasoro bahari-Matombo, Kiswira - Joseph Kamsopi Mdimi amefanya kweli baada ya kufunga pingu za maisha na Bi Flora Yesusaa Msechu wa Kilimanjaro.



Harusi hii ilifungwa katika Kanisa Katoliki la Mwenye Heri Anuarite, Makuburi -External - Dar Es Salaam tarehe 18/10/2008 na kisha sherehe ya kufana ilifanyika katika Ukumbi wa Afri-Centre Msimbazi - jijini Dar Es Salaam. Hebu waone maharusi hapo kushoto juu wanapendeza ehee!

Friday, October 24, 2008

Watanzania wameanza kutojiamini

Inavyoonekana kuwa kwa sasa hali ya kujiamini kwa Watanzania inapungua kwa kasi ya kutisha. Hii inajionyesha kwa kuvuja mitihani, majengo kuanguka, mabarabara kujengwa kwa kiwango cha hali ya chini. Wagonjwa kupata tiba isiyowahusu. Kutofanya vizuri kwenye michezo ( olimpiki 2008).

Kama mwanafunzi amehudhuria elimu ya sekondari kwa miaka 4 kwa nini aibe mtihani? (Huko ni kutojiamini). Kama mwanamichezo amefanya mazoezi vizuri na kufuata miiko ya wanamichezo sioni sababu ya kutofanya vizuri.

Kama wahandisi wamepata elimu na uzoefu wa kutosha katika kazi yao kwanini washindwe kusimamia kazi zao za ujenzi.

Watanzania turudishe hali ya kujiamini hata kama tunakosea lakini tunajifunza kutokana na makosa tunakokwenda siko. Watakuja wageni kutufanyia kila kitu kwani hatujiamini na hatuaminiani.

Asilimia 62 ya wahitimu wa darasa la saba kupata sifuri kwenye hisabati ni hatari

Waziri Mkuu Mhe.Mizengo Pinda alipokuwa akitoa hoja ya kuahirisha mkutano wa kumi na mbili wa Bunge-Dodoma tarehe 29 Agosti 2008 moja ya mambo aliyozungumza kwa uchungu sana ni wanafunzi kushindwa vibaya mtihani wa hisabati. Alisema. Kwa mfano mwaka 2001, katika mtihani wa kumaliza Darasa la saba, asilimia 62 ya watahiniwa katika Wilaya ya Morogoro Vijijini walipata sifuri katika Mtihani wa Hisabati. Hii ina maana kuwa asilimia 62 walimaliza shule bila kujua Hisabati rahisi za kujumlisha, kutoa , kuzidisha na kugawanya.

Hali hii ni mbaya sana. Inaonekana kuwa wanafunzi hawaoni umuhimu wa somo la hesabu, walimu pia kadhalika na wazazi tuseme na taifa zima.

Enzi zetu mwanafunzi ukifahamu hesabu hizo sifa tu unazomwagiwa mwenyewe utapenda hesabu. Na kama hujui hesabu ulikuwa unadharauliwa. Hata Sekondari waliokuwa wanachukua sayansi waliheshimika na wale wa sanaa au "arts' kwa kweli walionekana kama wapo wapo tu. Hata mzazi aliona ni sifa kwa mwanae kuchukua sayansi.

Tatizo letu Watanzania ni jinsi tulivyobadilika kirahisi kimtazamo katika mambo mbalimbali hasa elimu. Tunapenda mambo rahisi. Sasa hivi kila mtu yuko kwenye menejimenti, siasa na biashara! Kwa hali hii si rahisi mtoto kupenda hesabu. Hesabu zinatakiwa kutulia. Kama alivyosema Waziri Mkuu. Hesabu inajenga dhana ya kujiamini, kujenga falsafa ya mambo kwa mpangilio wenye mantiki (Logical Thinking).

Wito wangu ni kufufua ari ya kupenda hesabu na ionekana kwa watoto wetu kuwa bila hesabu huko mbele ni giza.Ijionyeshe waziwazi katika maisha yetu ya kila siku jinsi hesabu zinavyofanya kazi. Labda nihitimishe kwa kusema kuwa mwanafunzi yeyote anayepuuzia hesabu atapata matatizo makubwa katika kuendelea na elimu yake popote pale.


Wenzangu wa Moro sijui kama tumeshaanza kuchukua hatua ya kujikwamua kutoka katika aibu hii. Na hasa ikizingatiwa kuwa ni Morogoro vijijini kwani huko hakuna shule za kulipia kwa hiyo ni watoto wa malofa hawajui hesabu toba!

Thursday, October 23, 2008

Machungwa bado yanapatikana Dar

Msimu wa maembe umeanza, lakini machungwa bado yanapatikana Dar tena kwa bei nafuu sana. Shilingi 100/= kwa chungwa moja. Machungwa ya sasa ni matamu sana. Nawapongeza sana wakulima wetu kwa jitahada zao kubwa za kuhakikisha kuwa karibu kila zao linapatikana mwaka mzima. Miaka ya nyuma ilikuwa ni nadra sana kula chungwa hapa Dar kwa wakati huu. Hii ni dalili nzuri kuwa kuna teknolojia imeongezeka katika kilimo. Hii ni dalili nzuri pia kuwa wakulima hawa wakiongezewa uwezo wanaweza kufanya makubwa.


Nchi yetu imebahatika kuwa agroekolojia mbalimbali ambazo zinaweza kustawisha mazao mbalimbali kwa nyakati tofauti. Vile vile zina aina tofauti za udongo licha ya kuwa na vyanzo vingi vya maji ambavyo bado havijatumika kikamilifu kwa uzalishaji wa kilimo.