Saturday, October 10, 2009

Wanasoma wajipatie maarifa


Kuna ushahidi wa kutosha kuwa Watanzania wengi hatuna utamaduni wa kusoma. Kusoma kunakupatia maarifa, kunaburudisha na unapata taarifa mablimbali nzuri na mbaya. Tuanze sasa kusoma, tuanze kwenye familia kama inavyoonekana familia hii pichani

Kila mmoja na kuku wake


Wengi hupenda kula nyama ya kuku. Hasa vijana wanapopata 'offer' ukiwauliza utakula nini utasikia - Chips kuku. Lakini kwanini tusifuge kuku majumbani kwetu. Sisemi kuku wa kisasa la hasha hawa hawa tuliowazoea. Labda niseme kuku wa asili. Angalia familia hii pichani ilivyofanikiwa kufuga kuku wengi wa asili mpaka raha kila mmoja na kuku wake. Kila mmoja anatabasamu. Picha kwa hisani ya jarida la KILIMO endelevu Africa.

Wanashangaa maembe!


Ndiyo wanashangaa maembe. Haiwezekani mti mdogo ukazaa maembe kama yanavyoonekana pichani, tena chini chini kabisa. Usibishe. Kuna aina mbalimbali za maembe ambazo huzaa wakati ina kimo kifupi sana. Hii ni baadhi ya teknolojia za kisasa za kilimo za kuzalisha matunda. Ukitaka maelezo zaidi wasiliana na bwanashamba aliye karibu nawe, ofisi za kilimo au vituo vya utafiti.

Wakati wa Ujana wangu



UJANA mali waswahili wanasema. Wakati wa ujana wangu nilikuwa na nguvu na kufanya mambo mengi. Muda mwingi niliutumia kujipatia elimu ndani na nje ya nchi. Wakati mwingine nilikuwa najirusha kwa sana tu hasa DISCO ah nilipenda sana mziki. Nakumbuka miaka ya themanini mimi na ndugu yangu Lawrence Mkude (Sasa Afisa Utumishi Bandari) Silversands kila w-end. Namkumbuka sana DJ. John Peter Pantalakis na HOLLIDAY!

Friday, October 2, 2009

Utafiti shirikishi


Utafiti wa kitu chochote kile ni vizuri ikishirikisha wadau wengi. Pichani wakulima wanawake wakitafiti aina bora ya mpunga. Utafiti huu unajulikana kama utafiti shirikishi. Utafiti wa aina hii hutoa matokeo mazuri yanayokubaliwa na wadau.

Ninatubu Lema Baba shirikishi


Sherehe za kuwaaga wastaafu wa Idara ya Utafiti na Maendeleo ziliratibiwa na Mtafiti Mkuu Bw.Ninatubu Lema (a.k.a Baba Shirikishi). Pichani akipitia kwa makini ratiba ya sherehe.

Baada ya yote ni kulisakata rumba!


Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika Bi Sophia Kaduma akifungua dansi la kuwaaga wastaafu wa Idara ya Utafiti na Maendeleo mwaka 2008/09

Viongozi na wastaafu


Wamestaafu wakiwa wana nguvu na hekima tele. Pichani wastaafu pamoja na viongozi wa Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika katika picha ya pamoja. Watano kutoka kushoto waliosimama ni Bw. Ahmed J.Ahmed (a.k.a Kaka Ahmed) aliyekuwa mkuu wa kitengo cha mipango cha Idara (PEU).

Wawaaa Mama Beatrice Gembe!




Inapotokea shughuli na mwana mama akiwa mmojawapo kati ya wahusika wa shughuli hiyo basi ujue akina mama wenzie watamtunza tu. Ndivyo ilivyotokea kwenye hafla ya tarehe 3/7/2009 kina mama wafanyakazi wa Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika walimzawadiwa mstaafu Mama Beatrice Gembe (aliyekumbatiwa na kutabasamu) aliyekuwa PS wa Mkurugenzi wa Idara ya Utafiti na Maendeleo zawadi mbalimbali. Hebu angalia chereko chereko. Inapendeza enh!

Mwanzo 3 alisherehesha


Wafanyakazi wa Idara ya Utafiti na Maendeleo wanamfahamu Paul Masanja Ndondi (Mwanzo 3) kwa uchangamfu wake na kwa kuchapa kazi katika mazingira tofauti. Huyu amesafiri sehemu nyingi ndani na nje ya nchi na kujifunza mengi. Pichani Mwanzo 3 akisherehesha hafla ya watafiti wastaafu kwenye viwanja vya KILIMO 2.

Sisi tupo


Wakati watafiti wastaafu wakiagwa waliokuwa vijana miaka 10 iliyopita bado wapo. Pichani kutoka kulia Bi Eva Kanyeka, Smwel Undule, Deogratias Lwezaura na John Banzi wakisikiliza kwa makini wosia wa wastaafu.

Hongera Dkt. Haki


Ndivyo inavyoonekana pichani. Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika Bi. Sophia Kaduma akimpongeza na kumkabidhi Mkurugenzi mstaafu wa Idara ya Utafiti na Maendeleo Dkt. Jeremiah Haki. Katika hafla fupi ya kuwaaga wastaafu wa mwaka 2008/09 kutoka Idara ya Utafiti na Maendeleo. Dkt. Haki ameiongoza Idara hiyo kwa mafanikio makubwa takribani kwa miaka 10. Tafrija hiyo ilifanyika tarehe 3/07/2009 kwenye viwanja vya Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika - KILIMO II.

Nampigia debe mrembo wa Moro 2009


Yehu! Kinyang'anyiro cha Miss Tanzania ni leo katika Ukumbi wa Mlimani City -Dar es Salaam. Mshindi ataibuka na gari aina ya Suzuki Vitara pamoja na fedha taslimu 9m/=. Banzi wa Moro anampigia chapuo mrembo wa Moro Bi Tory Oscar. Tuvute subira macho yetu wote luningani. TBC Live mwanawane!

Huyu ndiye Dkt Alfred Moshi wa mahindi


Wadau wa Kilimo hapa nchini hasa wa kanda ya Mashariki unapozungumzia mahindi basi akilini mwao unamzungumzia Dkt. Alfred Moshi aliyekuwa Mkurugenzi wa Utafiti Kanda ya Mashariki. Moshi kwa muda mwingi amekuwa akitafiti mbegu bora ya zao la mahindi. Pichani Dkt Moshi akitoa neno kwa niaba ya watafiti waliostaafu mwaka 2008/09 kwenye viwanja vya Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika - Kilimo II kwenye tafrija ya kuwaaga waliyoandaliwa na Idara ya Utafiti na Maendeleo tarehe 3/07/2009

MORO - Neema ya vyakula


Mkoa wa Morogoro ni mmoja ya mikoa iliyobarikiwa kuwa na mazingira mazuri kwa kuzalisha mazao mbalimbali ya chakula. Hivi karibuni Makamu wa Rais Mh. Dkt.Ali Shein alitembelea kijiji cha Lupilo, Mahenge mkoani Morogoro. Angalia karanga, viazi mviringo, vitungu saumu na maji pamoja na nyanya vilivyojaa sokoni bwelele!

Makwaia wa Kuhenga


Ni mwandishi mwandamizi hapa nchini. Kalamu yake imefichua mengi na kuyaweka bayana. Ni mjuzi wa lugha pia ni mcheshi katika maisha ya kawaida. Huyu ni Makwaia wa Kuhenga. Nimemfahamu mwandishi huyu tangu miaka ya 80 na hadi leo ninapoona makala zake huwa nazikimbilia kuzisoma kwani hufanya uchambuzi wa kina.

Thursday, October 1, 2009

Dr. Shao - kama FORM VI vile!


Dr.Frank Shao ni mmoja ya Wakurugenzi waliopata kuongoza Idara ya Utafiti na Maendeleo. Miaka zaidi ya kumi sasa tangu astaafu lakini yu na afya na nguvu tele. Muulize Dr. Shao atakwambi ni nidhamu ya maisha na kuwa na kiasi. Angalia kinywaji anachokunywa- MAJI. Hapa alikuwa mwalikwa kwenye tafrija ya kuwaaga wastaafu wa Idara ya Utafiti na Maendeleo mwaka 2008/09

Komunio ya Kwanza -Matombo


Sikukuu ya kupata Komunio ya Kwanza kwa waluguru wa Matombo ni Sikukuu kubwa isiyofanyiwa mzaha hata kidogo. Maandalizi kwa watoto ya kiroho na kimwili ni makubwa na sherehe ni nzito. Banzi wa Moro alishuhudia sherehe kabambe za Ekaristi katika Kanisa la Watakatifu Petro na Paul Matombo. Ibada iliyoendeshwa tarehe 27/9/2009 katika Parokia hiyo ni ya kukumbuka. Siku hiyo pia kinanda kipya kilichonuliwa na waumini pamoja na wafadhili wazalendo kilichezwa kanisani. Pichani watoto waliopata ekaristi wakibebwa kuelekea nyumbani huku ngoma ikiwasindikiza - Nafikiri ilikuwa sh2!

Wednesday, September 30, 2009

Afadhali kuwa na pikipiki

Mwishoni mwa juma la jana nilisafiri kwenda kijijini Matombo. Kipya nilichoona ni usafiri wa pikipiki ulivyopamba moto. Nilikuta pikipiki Kiroka, Mkuyuni, Njia panda ya Kinole na Mtamba. Hii ina ashiria nini? Usafiri vijijini unaanza kuboreka. Baiskeli zinaanza kupungua kidogo kidogo. Hii ni hatua kubwa ya maendeleo. Tulitembea kwa miguu, baadaye wachache wakabahatika kuwa na baiskeli lakini tulianza kurukia magari kabla ya kuwa na pikipiki. Tumerudi mahali pake ndo maana nasema afadhali kuwa na pikipiki kuliko kutembea kwa miguu. Lakini pikipiki hizi zitumiwe kwa uangalifu la sivyo zitaleta madhara kwa jamii.

Friday, September 18, 2009

LULU anahamasisha TUGHE


Si jambo la kawaida kwa mzazi kumshirikisha mtoto wake kwenye shughuli za kitaifa tena ikiwa mtoto mwenyewe ni binti. Si hivyo kwa Bw. Omari Shomari mfanyakazi wa Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika aliyekuwa tayari kwenda kwenye maandamano ya Sherehe za Wafanyakazi mwaka huu zilizofanyika mkoa wa Dar ES Salaam kwenye uwanja wa UHURU. Pichani Bi Lulu Shomari akifurahia maandamano akiwa na baba yake Omari Shomari, Banzi wa Moro na Salehe Mkwawa (Mzee wa Yanga) tarehe 1/5/2009. Bw. Omari Shomari ni mwanachama mwanzilishi wa TUGHE-KILIMO MAKAO MAKUU. Kweli Lulu anahamasisha TUGHE.