Tuesday, April 8, 2014

Tanzania 'Bingwa wa Kandanda wa Dunia' 2014

Bingwa ni Bingwa tu. Ndiyo, Tanzania tumekuwa Bingwa wa Kandanda wa Dunia  kwa Watoto wa Mitaani mwaka 2014. Ni gazeti  la Daily News pekee lililoipa umuhimu wa kwanza habari hii katika ukurasa wake wa michezo toleo la tarehe 8/4/2014. Hii ni habari kubwa katika michezo. Nashangaa kuona hata magazeti ya michezo hayakutoa kipaumbele kwa habari hii kwenye magazeti yao. Mengi yanaandaika habari za Manchester United, Barcelona, Chelsea, Liverpool!  Zinatuhusu nini Watanzania. Watoto wa Mitaani wametuletea sifa Watanzania. Waliondoka wakiwa na maandalizi hafifu. Hawakukata tamaa. Safari tu kwao ni motisha. Kutoka mtoto wa mitaani hadi kupanda ndege kuna tofauti kubwa sana. Kutoka mitaani hadi kwenda kuishi hoteli zenye hadhi ya Kimataifa ni hadhi kubwa sana. Mimi nimefurahishwa sana na matokeo haya. Kijana pichani  anayepeperusha bendera ya Taifa hata jina halijulikani anaonekana kuwa na furaha ya pekee. Iko siku atakuja kuwa maarufu. Tunasoma kuwa wachezaji wengi kutoka Amerika ya Kusini wametoka kwenye familia duni na kuwa maarufu katika Soka Duniani. Hawa huwa na bidii sana wanapopata kitu cha kushika. Hivi bado hatujafumbuka macho na kuweza kuanza kuwekeza huko mitaani. Kuwa mtoto wa mtaani si dhambi, yote ni maisha. HONGERA TANZANIA KWA KUTWAA UBINGWA WA DUNIA. (Picha kwa hisani ya gazeti la Daily News 8/4/2014)

Friday, April 4, 2014

Ndege mpya ya ATCL yaongeza ufanisi

Ndege mpya ya kukodi ya Shirka la Ndege la Taifa (ATCL) aina CRJ-200 yenye uwezo wa kubeba abiria 50  imeweza kuongeza uwezo wa Shirika wa kusafirisha abiria kwa asilimia 57 hayo yameelezwa na Kaimu Mtendaji Mkuu wa Shirika hilo Captain Milton Lazaro. Aidha Lazaro ametangaza 'offer' maalumu wakati wa Pasaka kwa abiria watakaosafiri  kwa anga kwa shirka lake  Dar-Mtwara-Dar kuwa  itakuwa ni Tshs 250,000/=. (Picha kwa hisani ya gazeti la DailyNews 4/4/2014 - Tafsiri ya Kiswahili ya habari -Banzi wa Moro)

Msongamano wa magari barabara za Mandela na Kilimo jijini Dar

Hapa ni makutano ya barabara ya Kilimo na Nelson Mandela karibu kabisa na yalipo makao makuu ya  Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika wilayani Temeke eneo la Veterinary. Kuanzia saa nane hadi 12.30 jioni kila siku kwenye makutano haya mpaka mpale TAZARA  kunakuwa na msongamano wa magari. Hivi hakuna utaratibu wa kuyafanya magari yanayotoka Bandari kutumia barabara ya Mandela kwa masaa maalumu? Je ni nani aliyempa  Mamlaka mmiliki wa Kampuni ya Magari ya Dandho kuweka malori yake kwenye barabara ya Kilimo na kuwafanya Wafanyakazi wa Kilimo kukosa amani katika kufanya kazi wakibugudhiwa na kelele za magari hayo na msongamano?

Madereva Wizara ya Kilimo wakijadili jambo



 Madereva wa Wizara ya Kilimo Chakula  wakiwa katika mazungumzo ofisini kwao.

Nguvu ya Jua yasukuma maji Kisemvule-Mkuranga




Asilimia kubwa ya nchi yetu ya Tanzania inapata mwanga wa jua kwa muda mrefu kwa siku. Mwanga huu ukitumiwa vizuri kwa kuzingatia teknolojia zilizopo zinazoendeshwa kwa nguvu ya juu utasaidia sana kuboresha maendeleo ya watu wetu vijijini. Nguvu ya jua (solar power) inaweza kusukuma pump za maji, kutoa umeme kwa matumizi ya nyumbani  na hata viwanda vidogovidogo. Miaka ya hivi karibuni Shirika lisilo la Kiserikali  la African Reflections kutoka Marekani  limekuwa likichimba visima vya maji katika mkoa wa Pwani hasa wilaya ya Mkuranga. Pichani mtaalamu akifunga panel ya solar kijijini Kisemvule itakayotumika kutoa nguvu ya kusukuma pump ya maji ya kisima. Kinachotakiwa ni utunzaji wa  miundo mbinu hiyo. Kwa kutumia solar power wananchi watapata huduma ya maji wakati wowote. Hii itapunguza kwa kiasi kikubwa gharama ya kulipia bill ya umeme wa TANESCO.

Thursday, April 3, 2014

Makaburini Matombo

God Banzi, Michael Mloka na Daniel J.Mloka wakisali - Makaburini Matombo

Jordan -Juu ya kaburi la babu Balozi Mloka



Jordan Japhet akiwa juu ya kaburi la babu yake Balozi Daniel Mloka wakati maadhimisho ya kumbukumbu ya miaka 20 tangu kufa kwake yaliyofanyika kijijini Kiswira, Matombo-Morogoro

Akina mama Kanisani Matombo

Hata vijijini waumini wengi wanaosali ni akina mama. Hapa ni Matombo. Parokia ya Mt. Paul

Mama Mloka akiwa Matombo

   Shangazi Mama Mloka, mtoto wake Cesar na wajukuu  zake wakiwa Matombo,Morogoro

Usafi wa makaburi Parokiani Matombo



Usafi wa makaburi ni muhimu. Wakristu Wakatoliki wa Parokia zote huwa na utaratabu wa kufagilia makaburi angalau mara mbili kwa mwaka kabla ya Sikukuu ya Pasaka na tunapokaribia sikukuu ya watakatifu wote. Sehemu hizi wamezikwa Babu na Bibi zetu, Baba na Mama zetu, Shangazi na wajomba zetu, Kaka na Dada zetu, Watoto wetu marafiki na ndugu wengine. Ni ajabu kuona wakristu tunategea kufanya usafi wa sehemu za makaburi ingawa utaratibu upo kwa kila Parokia. Kufagilia makaburi hakuhitaji uwezo wa kifedha, la hasha, kinachohitajika ni utashi na nia ya kujituma kwa kutumia nguvu alizotupa Mungu wetu.

Nilipotembelea kijiji changu hivi karibuni na kupata bahati ya kusali na kuhiji kwenye makaburi yetu sikufurahishwa na hali niliyoiona. Upande mmoja makaburi yamesafishwa na kunapendeza (Picha ya kati). Sehemu nyingine (Picha ya chini) kuna nyasi nyingi kiasi cha kushindwa kutambua alipozikwa ndugu yako au mzazi wako. Naipongeza Jumuiya (picha ya Juu) iliyojipanga na kufanya usafi. Ndugu zangu wa Matombo IMANI yetu na moyo wa kujitolea vimepotelea wapi? Hivi kweli tumefikia mahali kuwa hata kusafisha makaburi lazima tutoe fedha? Nawasihi kuwa wakati tunajiandaa kwa PASAKA usafi wa makaburi upewe kipaumbele.

Duka la Mzee Moris wa Kiswira -Matombo

Miaka ya sitini na sabini kijijini kwetu maduka yalikuwa yanahesabika. Hili ni duka la Mzee Moris Martin. Mtoto wa Akida Martin. Hapa tuliweza kununua sukari, chumvi,viberiti  na vinginevyo. Duka hili lilikuwa kijijini Kiswira Matombo, Morogoro karibu kabisa na Kanisa Katoliki Parokia ya Matombo. Kwa sasa duka hilo halina bidhaa tena. Kijijini Kiswira maduka sasa ni mengi  na bidhaaa mbalimbali zinapatikana kama zinavyopatikana mjini Morogoro.Kweli wakati ukuta.

Tuesday, April 1, 2014

Padri Kobelo kanisani Matombo

Paroko wa Matombo, Fr. Kobelo akibariki misalaba tayari kwa kusimikwa tarehe 22/03/2014

Banda la Serikali-Matombo

Kwenye mti huu ndipo lilipojengwa banda la serikali Kswira, Matombo enzi za wakoloni. Nimeelezwa kuwa hapa mashauri yalikuwa yakifanyika karibu kabisa na nyumba ya Akida Martin. Hapa wazee wetu walichapwa viboko kama adhabu kutokana na makosa waliyohukumiwa. Historia hii inabidi kuandikwa na kuhifadhiwa.

Mzee Mchope wa Kiswira-Matombo

Nilipokwenda kijijini kwangu  Kiswira Matombo, Morogoro, nilkutana na Mzee 'Mchope' huyu ni mwanajeshi mstaafu anayefanya shughuli zake za kilimo na biashara pia ni fundi rangi. Tukiwa kwenye mazungumzo alinieleza na kunikumbusha mambo mengi. Kama asili ya baadhi ya wazee wa zamani wa Kijiji chetu na jinsi kijiji kilivyokuwa hapo zamani. Kumbukumbu aliyonayo ni vizuri kuhifadhiwa.

Dukani Kiswira-Matombo

Hili ni moja ya maduka maarufu lilipo kijijini kwangu Kiswira Matombo. Maarufu dukani kwa Mode. Hapa unapata takribani kila kitu kuanzia vocha, kutuma na kupokea fedha mitandao yote, vinywaji, sabuni, kandambili, unga, mchele, chumvi, dagaa, mabeseni, ndoo, kanga, vitenge, maharage, kandambaili n.k. Sina sababu ya kubeba vitu hivyo ninaporudi nyumbani.

Tayari kupigwa picha

Nilipokuwa naelekea kanisani  Matombo nilimkuta kijana huyu karibu kabisa na nyumba ya marehemu Christian Mchuma wa Kiswira. Huyu alikuwa tayari kupigwa picha. Kweli ameweka kumbukumbu yake.

Huyu hakutaka kupigwa picha

Nilipotaka kumpiga picha alijificha. Hakutaka kupigwa picha hapa ni Kswira, Matombo, Morogoro kijijini kwangu.

Kiswira-Matombo 'the Pub'

Nikiwa kijijini huwa na pata moja mbili tatu kwenye kiosk hiki aua nachukua nanywea nyumbani ambapo ni hatua chache tu kutoka kwenye nyumba yetu kijijini Kiswira, Matombo, Morogoro

Scouts wa Matombo Secondary

Wote hawa ni scouts. Wengine wamevalia rasmi vazi scout wengine wakom kwenye uniform ya shule na wengine katika bukta. Wengi wamefunga skafu ya scout. Hongera sana wanafunzi wa Matombo kwa kuwa na chama chenu cha Scout huko mtajenga ukakamavu na mbinu mbalimbali.

Matombo Secondary School

Haya ndiyo mandhari ya Shule ya Sekondari  Matombo iliyoko mkoa wa Morogoro. Zamani ilikuwa Middle School chini ya Kanisa Katoliki Parokia ya Matombo. Hapa ndipo nilipopata elimu yangu ya msingi. Katika shule hii niliwahi kuwa 'Time keeper' a.k.a mgonga kengele. Katika shule hii pia  niliwahi kucharazwa  viboko kwa kosa la kumtolea machukizo msichana mmoja aliyekuwa amevaa viatu vilivyochongoka huku mimi na kundi letu tukimzonga na kumwita Badoura! Naipenda Matombo!