Monday, July 13, 2015
Hii ni familia yangu
Ndiyo. Hii yote ni familia yangu. Ni siku mtoto wetu Frt. Linto alipokuja kutuaga pale nyumbani Kisemvule. Frt. Linto anatoka India, lakini kwa takribani mwaka mmoja alikuwa parokiani kwetu Vikindu kwa uchungaji. Alipopewa vazi la kuwa Frateri yeye alituomba mimi na mke wangu (Nancy) kuwakilisha wazazi wake ambao wasingeweza kuwepo siku hiyo. Kwa hiyo Linto ni mmoja wa familia yangu. Kwa sasa Ftr. Linto yuko Uganda kwa muda baadaye ataelekea Nairobi kwa masomo ya Teolojia.Pichani pia wanaonekana waseminari ambao walikuwepo kwa mwaka mmoja parokiani kwetu wakianza mafunzo ya useminari kwa sasa wako Uganda.
Ilibidi kuweka kumbukumbu na watoto hawa
Junior na Herieth wa Buguruni ni watoto marafiki. Nilipowatembelea nyumbani kwao nilifurahishwa jinsi walivyokuwa wakishirikiana. Wanacheza pamoja na kula pamoja. Junior ni Mluguru na Herieth ni Mchagga. Ushirikiano waliounyesha ni dalili nzuri kuwa hata wazazi wao wanashirikiana. Hii ndiyo Tanzania umoja unajengwa toka tukiwa wadogo. Nami niliona ni heri nikapiga picha ya kumbukumbu pamoja nao.
Junior na Herieth wa Buguruni-Maghorofani
Junior na Herieth wanaishi kwenye jengo moja lililopo Buguruni -Maghorofani. Hawa wanatoka familia tofauti. Junior ni mpwa wangu anatoka Morogoro-Matombo na rafikiye Herieth ni Mchagga wa kutoka Rombo-Kilimanjaro. Nilipomtania uncle Junior kama tutapeleka "mahali Uchaggani" alikuwa na aibu na kubaki kucheka tu.
Africana Group kwa Christian Mkoba
Africana Group ni kundi la familia linaloundwa na ukoo wa Wambiki na watoto wao kwa asilimia kubwa. Kundi hili lipo jijini Dar Es Salaam. Lengo Kuu la kundi hili ni kudumisha uhusiano wa kifamilia uliokuwepo tangu zamani kwa bibi na babu zetu ambao makazi yao ni Morogoro, Matombo, Nige-Kariakoo. Kila mwezi hukutana mara moja nyumbani kwa mwanakikundi. Mwezi Juni Africana Group ilikutana nyumbani kwa ndugu yao Bw. Christian Paul Mkoba huko Kisemvule,wilayani Mkuranga, Pwani. Wakati mkutano unaendelea wajumbe wanaendelea na chakula pamoja na vinywaji walivyoandaliwa na mwenyeji wao.
Tunapokea zawadi kutoka kwa watoto wetu
Mwezi Juni 15,2015. Bw na Bibi Victor Shayo walifunga pingu za maisha ndani ya Kanisa la Mt. Vinsenti wa Paulo, Vikindu. Familia hiyo ilituchagua mimi na mke wangu kuwa wazazi wao wa kiroho katika maandalizi yote ya ndoa hiyo hadi walipofunga ndoa. Hapa wanatukabidhi zawadi yao baada ya kutukaribisha kwao wanakoishi (Vikindu). Asanteni sana. Tunawatakia ndoa yenye furaha.
Watafiti kutoka Mikocheni
Baadhi ya watafiti nguli wa kituo cha utafiti wa kilimo Mikocheni wakifuatilia kwa makini hotuba ya Naibu Waziri wa Kilimo Chakula na Ushirika wakati wa uzinduzi wa taarifa ya kimataifa ya mwaka 2014 kuhusu baiteknolojia uliyozinduliwa kwenye viwanja vya makao makuu ya Wizara hiyo jijini Dar E s Salaam mwezi Juni 2015. Kituo cha Mikocheni ndiko kuliko maabara ya kisasa ya utafiti wa baiteknolojia katika kilimo.
Monday, June 8, 2015
Hebu tuone familia ya Shirika la Masista wa Carmel
Shirika la Masista wa Kikatoliki la Mlima wa Carmel limetapakaa duniani kote kama mti huo unavyoonesha. Wako katika bara la Afrika, Asia, Ulaya na Amerika. Hawa ndiyo wamiliki wa Carmel Pre & Primary School Vikindu iliyopo wilaya ya Mkuranga mkoa wa Pwani. Shule hii ni moja kati ya shule zinazoongoza wilayani na mkoani Pwani.
Ilibidi waeleze jinsi figo inavyofanya kazi
Wanafunzi hawa wenye vipaji wa shule ya Msingi ya Carmel iliyopo Vikindu wilaya ya Mkuranga, walikuwa na mada ya kueleza jinsi figo inavyofanya kazi. Nilipofika kwenye meza yao tarehe 6/6/2015 nilishangaa uwezo wa vijana hao katika kuelezea figo. Wanafunzi hawa wanajengwa kuipenda sayansi kivitendo wakiwa wangali wadogo kabisa.
Inawezekana wakawa madaktari
Pluto ni sayari iliyo mbali sana na jua kuliko zote
Nilikwisha sahau kuwa sayari ya Pluto ndiyo iliyo mbali zaidi na jua takribani kilometa 5900 milioni. Sayari yetu ya Dunia ni ya tatu kutoka sayari ya jua ambayo ni umbali wa kilometa 150 milioni. Haya nilikumbushwa kwenye maonyesho ya sayansi ya 'Carmel Convent Pre & Primary School - Vikindu-Mkuranga, Pwani. Wanafunzi huyu mwenye kipaji alinielezea kwa ufasahau mkubwa sayari zinazozunguka jua. Maonesho hayo yalifanyika tarehe 6/6/2015 shuleni kwao.
Subscribe to:
Posts (Atom)








































