Saturday, April 14, 2007

"ZOGOWALE" WANAUME WANAFANYA KAZI MASAA 4

Hivi tumeshawahi kujipima katika jamii zetu katika utendaji kazi kati ya wanawake na wanaume?

Ili kuweza kufahamu ni akina nani hasa wanaotumia muda mwingi wa kufanya kazi?Hivi karibuni kikundi cha watafiti 10 kutoka Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika kilisafiri hadi kijiji/mtaa wa Zogowale, Wilaya ya Kibaha, Mkoa wa Pwani ili kuweza kujifunza masuala ya Jinsia katika kijiji hicho.

Watafiti hao walifanya majadiliano na wakazi wa mtaa huu wapatao 47. Baada ya kudodosana kwa takribani masaa mawili. Iligundulika kuwa, wanaume hutumia masaa manne kwa siku kwa kufanya kazi, wakati wanawake wao hutumia masaa 12! Eeh jamani tutafika kweli? Maendeleo yatapatikanaje kwa kufanya kazi kwa muda mchache namna hiyo na huku mwanamke akiachiwa shughuli nyingi za kufanya.Hata hivyo katika utafiti huo, ilibainika kuwa, jamii ya

Zogowale imeshaanza kubadilika, kwani kwa sasa zile ndoa changa zimeanza kusaidiana katika kufanya kazi. Wanaume huchota maji, hufua nguo na hata kupika chakula! Safi sana.Je, akina baba wanawapeleka watoto wao hospitali mara wanapougua ?(yaani kuwabeba kama wanavyofanya akina mama?). Akina baba wa Zogowale bado ni wazito kwa hilo. Wao hutoa amri tu na kutoa fedha za tiba, lakini si rahisi kumkuta baba kutoka Zogowale amebeba mtoto na kumpeleka hospitali!Kumenya mihogo je? Kazi hii nayo hufanywa na akina mama. Ni mara chache sana kukuta baba akimenya mihogo.

Zogowale, maisha huanza mapema, katika umri wa miaka 20 ni rahisi sana kumkuta kijana akiishi na mwanamke na pengine kuwa na mtoto hata mmoja!
Labels: John Banzi

No comments: