Friday, February 29, 2008

Wachezaji wanapojisahau kula "Pilau" kablaya mechi!

Juzi pale Kisemvule, kulifanyika pambano la fainali kugombea mbuzi kati ya Timu ya TanBlock (Ksemvule) na Motohaulambwi (Vikindu). Tanblock walikuwa wanauwa ndege wawili kwa jiwe moja. Kwanza walikuwa wanaifungua rasmi kampuni yao ya kufytatua matofali ya TanBlock kwahiyo ilifanyika Maulid kubwa pale. Mchele kilo 150. Pilau ililika saa 8 mchana na mechi kuanza saa 10.30. Inasemekana kuwa karibu wachezaji wote wa Tanblock walikula punga lile. Huku wakiwa na matumaini makubwa ya kumbeba mbuzi (yaani kushinda mechi). Mambo hayakuwa hivyo.

Katika kipindi cha kwanza Motohaulambwi waliandika bao la kwanza na katika kipindi cha pili wakaongeza bao la pili kabla Tanblock hawajasawazisha na hatimaye “Moto” kubeba mbuzi.

Utakulaje “Pilau” chakula chenye mafuta mengi ambayo huchukuwa muda mrefu kuyeyushwa masaa machache kabla ya kuingia uwanjani? Pilau “iliwaloga” Tanblock. Tanblock hawakuwa na mshauri kuhusu mechi ile.

Kijungu

Mkoa wa Mbeya una maajabu mengi lakini hayjatangazwa. Moja ya maajabu hayo ni sehemu inayoitwa “KIJUNGU” iliyopo ndani ya mto Kiwira, wilayani Rungwe ndani ya na Chuo cha Magereza Kiwira..Hapa maji yanapita chini ya mwamba kwa kina kirefu sana na yanazunguka. Kuna maelezo mengi yanayotolewa na wenyeji kuhusu sehemu hiyo. Lakini utafiti wa kina haujafanyika. Na kama umeandikwa basi uko kwenye makabrasha kama ilivyo kawaida yetu. Wasomi mpo? Hapa yanaweza kuandikwa mengi katika nyanja mbalimbali. Changamkieni tenda. Mnaweza kupata shahada mbalimbali kutokana na “KIJUNGU”

"Daraja la Mungu"

Tanzania ina mambo mengi ya kuvutia na ya ajabu. Ukibahitika kusafiri kwenda mkoa wa Mbeya wilaya ya Rungwe karibu na Chuo cha Magereza cha Kiwira. Mto wa Kiwira unapita chini ya mwamba mkubwa na kufanya kuwa daraja. Daraja hilo ni kubwa na linajulikana kwa jina la “Daraja la Mungu.” Nilibahatika kuliona daraja hilo mwezi wa Desemba, 2008. Sehemu hiyo ikitengenezwa vizuri ni moja ya vivutio vya watalii mkoani Mbeya na nchini. Moja ya chanzo cha mapato kupitia sekta ya Utalii. Tuchanganke!

Kilwa Road Mkeka umeanza

Ndiyo, Kampuni ya Kajima imeanza kuweka “mkeka” (lami) kwenye barabara ya Kilwa ingawa kwa vipande vipande lakini inatia moyo sana. Kajima ilianza kama mchezo lakini barabara ile wameijinga strategically walianza kujenga ‘culverts” madaraja na mifereji. Wakamwaga vifusi. Sasa hawana wasiwasi na masika tena kwani hata kushindilia wameshashindilia. Kilichobaki ni lami na nakshi nakshi. Sasa Mbagala kumekucha! Tatizo la foleni ni historia. MADCM yameanza kupungua kwa kasi ya kufurahisha. Buguruni-Mbagala tunaona “Pamba nyepesi” ya Civilian. Nasikia watakabidhi barabara (Hadi Mtoni Mtongani) mwezi Aprili, 2008. Kazi nzuri sana KAJIMA

Mwanafunzi anapokuwa mwizi

Hivi karibuni kuna matokeo mawili yaliyotokea yanayofanana lakini yamefanyika katika sehemu mbalimbali. Moja limetangazwa kwenye vyombo vya habari lakini moja bado halijatangazwa. Matokeo yote mawili ni ya wizi. Matokeo yote mawili wahusika ni wanafunzi. Moja linamuhusu mwanafunzi wa shule ya sekondari na mwingine shule ya msingi. Moja limetokea mkoani Pwani lingine Mkoani Mbeya. Mmoja ameuwawa kama jambazi aliyekutwa na silaha akitaka kuiba kwenye shule anayosoma mwenyewe. Mmoja amekutwa akiiba dawati kwenye shule ya msingi Kisemvule mkoani Pwani.

Matukio yote mawili si ya ajabu lakini ni ya kushangaza. Wezi wanafunzi. Wezi wanaibia shule zao wenyewe. Hawa bado ni vijana wadogo je watakapoanza kazi itakuwaje. Tutafakari.

Tuesday, February 12, 2008

NAMIBIA WANAPIGIA DEBE KISWAHILI

Nimekamata gazeti la "Daily News" la Februari 2/2008. Namsoma Kiangiosekazi wa Nyoka kutoka Windhoek.

Barua hii kutoka Namibia pamoja na mambo mengine, Rais wa Namibia Hifikepunye Pohamba anakifagilia sana Kiswahili na anasema hana neno kwa kukiona Kiswahili kuwa lugha ya Afrika. Anasema, jitahada za kutosha hazijafanywa kukifanya Kiswahili kuwa lugha ya Taifa. Anaongeza kuwa, utashi wa kisiasa ya Namibia unakipa nafasi kubwa Kiswahili kuwa lugha ya Afrika.

Kwa hili nani wenye nafasi kubwa? Wanamibia au Watanzania? Tuchangamke.

UZALENDO USIISHIE KWA MAWAZIRI TU

Ni saa 8.30 sasa. Dakika 30 kabla ya kutangaza Baraza jipya la Mawaziri. Radio Tanzania inaendesha mjadala kuhusu matarajio ya Baraza jipya la Mawaziri. Mmoja anasema Mawaziri wawe wazalendo.



Mimi nasema uzalendo usiishie kwa mawaziri tu. Watanzania sasa turudishe ile hali ya uzalendo. Watu wanafanya haya kwa sababu hakuna uzalendo. Ufisadi huu mkubwa umetokea siyo kwamba umepitia gizani, si kwamba mashetani wamehusika kufanya wizi huu. Watu wengi wamehusika, walifahamu, wameona, wamebeba. Wamenyamaza. Hii ina maana hakukuwa na uzalendo.



Mikutano inafanyika, mambo yanaharibika watu wananyamaza. Hadi leo watu wamenyamaza. Kuna wengine wana heshima kubwa nchini, hawajasema lolote kwenye sakata hili.



Nchi hii haiwezi kuendelea, kama wananchi wake hawatakuwa wazalendo. Uzalendo usiishie kwa mawaziri tu. Makatibu wakuu wawe wazalendo, wakurugenzi wawe wazalendo, wakuu wa mkoa wawe wazalendo, wakuu wa wilaya wawe wazalendo, wenyekiti wa vijiji wawe wazalendo lakini kikubwa, wananchi tuwe wazalendo.

MABUS YA VICTORY NI MFANO MBAGALA

Nimekuwa nikisafiri kuelekea Mbagala mara kwa mara kwa kutumia daladala.

Mbagala kuna wakazi wengi sana. Mbagala kuna daladala nyingi sana. Kwa kweli njia ya Mbagala haikauki abiria. Kwa muda wote huo nimekuwa nikuchunguza jinsi daladala zinavyotoa huduma kwa abiria wa Mbagala.



Mabus ya VICTORY yamekuwa yakitoa huduma bora na ni mfano wa kuigwa. Kwanza mabus yake yako katika hali nzuri, pili ndani kuna burudani safi inayomfanya abiria asichoke na safari, tatu huiwabugudhi wanafunzi, nne haikai hazipotezi muda bila sababu kwenye vituo, tano hayana tabia ya kujaza mafuta kwenye vituo vya mafuta wakiwa na abiria, sita nadra kukatisha njia, saba dereva na kondakta daima ni wasafi na wako katika sare zao, nane hazikamatwi hovyo hovyo na traffic, tisa hawalazi damu katika kurudisha chenji, kumi wahudumu wana lugha nzuri kwa abiria.

TUANZE KUWAAMINI WAANDISHI WAHABARI

Katika toleo lake 81 la tarehe 23-29, 2008 Gazeti la Mwanahalisi liliandika Vigogo watatu kuumbuka. Hatukuamini. Toleo la 83 likaandika Sakata la Richmond: Lowassa kitanzini - Mawaziri watatu kujiuzulu, mmoja adai kutolewa kafara- Hatukuamini. Sasa yametokea. Tuanze kuwaamini waandishi wahabari.

SIKU MOJA TUTALIA SANA!

Siku moja Taifa litaomboleza msiba mkubwa tusipokuwa waangalifu.

Wanafunzi wanaosoma katika shule zilizopo kwenye barabara ya Kongowe - Kigamboni wana matatizo makubwa ya usafiri.

Magari ya daladala yaliyopo mengi huwapiga chenga. Matokeo yake wengi husafiri kwa magari ya kubeba mchanga. Iwe mvulana au msichana ni kudandia tu malori. Wengi hufika shuleni wamechafuka na wengine kuumia. Si vibaya sana, lakini ninachoogopa mimi ni kutokea kwa ajali. Magari haya huenda kwa mwendo wa kasi huku wanafunzi wakiwa juu kabisa ya malori.

Sawa wanasaidiwa usafiri lakini iko siku moja tutalia Taifa zima. Naomba hatua za haraka zichukuliwe kunusuru hilo lisije kutokea

Friday, February 1, 2008

Mkuranga:-Mtajikomboa kwa kilimo cha mboga na matunda

Wilaya ya Mkuranga ni moja ya wilaya za mkoa wa Pwani.

Kiuchumi wilaya hii hutegemea sana zao la korosho na nazi kwa kiasi kidogo.

Lakini miaka ya hivi karibuni baada ya kukamilika kwa barabara ya Kilwa ipitayo katika wilaya ya Mkuranga. Maisha ya jamii yamebadilika sana. Watu wa Pwani si wavivu tena. Wapwani wameanza kujishughulisha na kilimo cha mboga mboga na matunda. Wilaya ya Mkuranga kwa sasa inazalisha matikiti maji mengi na mazuri karibu kwa wakati wote. Mkuranga sasa inazalisha mbogamboga nyingi hasa mchicha, Mkuranga matunda ya "passion". Ikizingatiwa kuwa upatikanaji wa maji ya visima ni mkubwa katika vitongoji vya Mkuranga umwagiliaji hutumika ingawa kwa vifaa duni. Wakulima wanafahamu sasa kuwa kilimo kinalipa. Hebu tembelea Kisemvule stendi uone jinsi biashara ya smadi ya kuku ilivyoshamiri, wakulima hutoka sehemu mbalimbali kununua samadi ya kuku. Nayo biashara hii ya mbolea inalipa!

Wakulima wameanza kubadili maisha yao. Wengi wameanza kujenga nyumba za kisasa, wengi wamenunua baiskeli na sasa watoto wao wanapata elimu ya Sekondari kwenye shule ya Sekondari Vikindu. Hayo ni maendeleo. Vitu kama hivi havikuonekana miaka mitano iliyopita. Leo mtu anaona fahari kuitwa mkulima kwa kuwa kilimo kinalipa.

MADEREVA AKINA MAMA WAKO MAKINI

Kwa muda mrefu nimekuwa nikichunguza uendeshaji wa magari kwa akina mama. Nimegundua kuwa akina mama wengi madereva wako makini sana kwenye uendeshaji kuliko akina baba.

Hebu chunguza ajali nyingi za barabarani zinazotokea hapa Dar. Zilizo nyingi wahusika ni akina baba.

Mwanamke akifahamu kuendesha gari kwanza anazingatia sheria za uendeshaji halafu anajijali yeye mwenyewe pamoja na abiria wake. Lakini wanaume wengi wanajifanya wao wanajua sana kuendesha. Watayapita magari kwenye mlima, kwenye kona na pengine kusiko ruhusiwa. Matokeo yake ni ajali zisizo na msingi. Halafu tunasema bahati mbaya! Ajali zinaua na kutesa pengine kuliko ukimwi. Tuwe waangalifu wanaume madereva.

Hongera akina mama na dada zetu kwa uendeshaji makini!

DALADALA HILI MBAGALA R3/BUGURUNI

Daladala T848 ASY-S.1887G. Lenye njia ya Mbagala R3 - Buguruni kwenye kioo cha mbele cha gari yameandikwa maneno " No Discation." kwenye tikiti za bus hilo pia imeandikwa "No Discation." Nimeshindwa kupata ujumbe wa maneno hayo. Nimeangalia kwenye kamusi ya Kiingereza nimeshindwa kupata maana ya neno "discation."

Huenda alitaka kuandika " No Discussion" kwa kiswahili chepesi yaani hakuna mazungumzo, majadiliano au "POA" lakini jinsi lilivyoandikwa kwenye bus lile halina maana kabisa.

Kweli tunapenda kutumia maneno ya kiingereza ili "kuweka msisitizo" wanasema watoto wa mjini, lakini basi tuandike kiingereza sahihi vinginevyo hutueleweki kama nilivyoshindwa kupata ujumbe ulioandikwa kwenye bus hilo.

Si kwenye magari tu. Lakini tumekuwa tukikosea maandishi ya kiingereza kwenye sehemu nyingi tu k.m. "Gerege!" badala ya Garage.

Tuwe makini katika kutumia lugha mbalimbali. Na kama hatuzifahamu vizuri basi tuache kuzitumia au tuwaulize wenzetu wanaozifahamu.
Hivi kwanini tusiandike kwa kiswahili au hata kwa lugha zetu za asili/kabila?