Ni saa 8.30 sasa. Dakika 30 kabla ya kutangaza Baraza jipya la Mawaziri. Radio Tanzania inaendesha mjadala kuhusu matarajio ya Baraza jipya la Mawaziri. Mmoja anasema Mawaziri wawe wazalendo.
Mimi nasema uzalendo usiishie kwa mawaziri tu. Watanzania sasa turudishe ile hali ya uzalendo. Watu wanafanya haya kwa sababu hakuna uzalendo. Ufisadi huu mkubwa umetokea siyo kwamba umepitia gizani, si kwamba mashetani wamehusika kufanya wizi huu. Watu wengi wamehusika, walifahamu, wameona, wamebeba. Wamenyamaza. Hii ina maana hakukuwa na uzalendo.
Mikutano inafanyika, mambo yanaharibika watu wananyamaza. Hadi leo watu wamenyamaza. Kuna wengine wana heshima kubwa nchini, hawajasema lolote kwenye sakata hili.
Nchi hii haiwezi kuendelea, kama wananchi wake hawatakuwa wazalendo. Uzalendo usiishie kwa mawaziri tu. Makatibu wakuu wawe wazalendo, wakurugenzi wawe wazalendo, wakuu wa mkoa wawe wazalendo, wakuu wa wilaya wawe wazalendo, wenyekiti wa vijiji wawe wazalendo lakini kikubwa, wananchi tuwe wazalendo.
No comments:
Post a Comment