Dkt. Asha Rose Migiro ni jina maarufu si hapa Tanzania bali hata kwa mataifa mengine.
Dkt. Migiro Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN) ni moja ya matunda bora kutoka Tanzania yanayowaka katika anga za Kimataifa.
Ninavyomfahamu mimi, Dkt. Asha Rose Migiro aliwahi kuwa mhadhiri pale Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam na ameshawahi kuwa Waziri wa Maendeleo ya Jamii na Wanawake na Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje na Uhusiano wa Kimataifa.
Hivi sasa yupo Tanzania kwa likizo fupi. Kwa muda wa wiki moja sasa amekuwa akifanya mambo mengi hapa nchini. Ameshahudhuria kikao cha Bunge na kulihutubia na kuhojiwa na vyombo vya habari hapa nchini.
Wakati wote huo nilichojifunza kutoka kwake, mwanamama huyu ni makini sana. Anajua nini cha kuongea na wakati gani na kwa akina nani. Ana kipaji kikubwa cha kutumia lugha. Anaweza kujieleza barabara kwa kiswahili fasaha na kiingereza makini.
Huyu ni mtu ambaye ameshatembelea nchi nyingi na kukutana na watu wengi maarufu na wa kawaida hapa duniani lakini haachi kujitambulisha Utanzania wake. Kwa kweli nimempenda jinsi anavyojiweka katika hali ya kawaida kabisa.
Nimesikia kuwa mpaka sasa anaishi kwenye nyumba za wahadhiri kule Chuo Kikuu Dar Es Salaam na hata alipokuwa waziri. Huyo ndiye Dkt. Asha Rose Migiro kioo cha Tanzania na mfano bora kwa wanawake.
No comments:
Post a Comment