Miaka 47 tangu tupate uhuru lakini napenda nikiri kama mtaalamu wa kilimo kuwa wakulima wengi wa Matombo hawafuata kanuni za kilimo bora. Licha ya kutotumia mbolea lakini kanuni za msingikama vile kupanda kwa nafasi hawajui, mbegu bora kwao ni ajabu tu, wadudu na magonjwa ya mimea yanashambulia yapendavyo. Kwa hali hiyo si ajabu kuona uzalishaji wa mazao Matombo ni mdogo sana.
Nilijaribu kuongea na baadhi ya ndugu zangu ambao ni wakulima wanasema kwa wastani huvuna gunia moja hadi mbili za mahindi kwa eka! Kiasi hiki cha mavuno hakiwezi kumlisha hata mtu mmoja kwa mwaka!
Sijui kama bwanashamba yupo katika kijiji chetu, sijui kama uongozi wa kijiji, kata na wilaya unatambua umuhimu wa kilimo kwa uchumi wa mwananchi wa Matombo.
Matombo imebahatika kuwa na hali nzuri ya hewa na udongo mzuri. Inafikika kirahisi kutoka Morogoro, Dodoma, Iringa na Dar kwa hiyo uhakika wa soko upo. Matunda ya tropiki kama vile machungwa, maembe, mananasi na ndizi yanapatikana kwa wingi. Siku hizi wakulima wameanza kujishughulisha na kilimo cha mazao ya viungo kama vile hiliki, pilipili manga na mdarasini sehemu za Konde, Nyangala, Tawa, Kinole na Mkuyuni.
Mazao haya yakijengewa mikakati mizuri na Halmashauri ya Wilaya kupitia DADPs yanaweza kuboresha hali ya uchumi ya watu wa Matombo.
No comments:
Post a Comment