Friday, February 4, 2011
Picha Ya JK Na Freeman Mbowe: Tafsiri Yangu
Ndugu Zangu,
JANA tumeona picha ya pamoja; JK akiwa na Freeman Mbowe.
Katika sanaa ya picha inasemwa, kuwa picha moja yaweza kuwa sawa na maneno elfu moja. Picha moja yaweza kutoa tafsiri nyingi.
Nimeitafakari picha ile. Ni moja ya picha nzuri iliyobeba ujumbe muhimu kwa Watanzania hususan tukikumbuka Uchaguzi uliopita na matukio baada ya uchaguzi.
Ni picha inayobeba matumaini badala ya kukatisha tamaa.
Inaonyesha, kuwa hata baada ya uchaguzi, maisha ya kisiasa hayana budi kuendelea. Na siasa si ugomvi. Siasa ni jambo jema. Ni wakati sasa kwa akina Freeman Mbowe na wenzake wa CHADEMA kuvua magwanda yale ya khaki na kushiriki maisha ya kawaida ya kisiasa.
Kama ningewashauri CHADEMA, basi, ningewaambia, kuwa , kwa kiongozi, vazi pia hutuma ujumbe kwa unaowaongoza. Magwanda yale ya CHADEMA yamekaa kijeshi zaidi. Labda yalitosha kuyatumia katika ’ mapambano’ ya kampeni za uchaguzi, lakini si sasa. Uchaguzi umeshapita.
Huu ni wakati wa kurekebisha tofauti zilizojitokeza na kwenda mbele. Na tuna cha kujifunza kutoka Unguja. Itakumbukwa, kuwa baada ya matokeo ya uchaguzi wa mwaka 2005, Maalim Seif alikaririwa akitamka kuwa; ”Hakuna tena mufaka wa tatu". Rais Karume naye akakaririwa akitamka; "Sitaki kusikia habari ya Serikali ya mseto". Haya , leo Maalim Seif yumo ndani ya Serikali ya Mseto!
Na hapa kwetu CHADEMA walianza na kauli za kutoitambua Serikali. Nitakuwa mtu wa mwisho kushangaa siku ile Dr Slaa na JK watakapokaa meza moja na kongea kirafiki. Na tunaamini katika mazungumzo kama njia ya kutatua migogoro yetu ya kisiasa.
Kupitia picha ile ya jana tumeona busara za Rais Jakaya Kikwete, kusimama na kuongea na Freeman Mbowe katika hali ya kirafiki. JK ameonyesha kujiamini na kuendelea na kazi ya kuifatuta suluhu ya migogoro ya ndani ya nchi.
Kwa kiongozi wa kisiasa kuitafuta suluhu si udhaifu, ni ujasiri. Na huo ndio ukomavu wa kisiasa pia. Naamini, ndani ya CCM kuna wanaoogopa kupiga picha wakiwa pamoja na viongozi wa CHADEMA. Ni kwa kuhofia kuandamwa na wenzao ndani ya chama.
Tumefika mahali tukubali, kuwa siasa si uadui. Profesa wa Sayansi ya Siasa , Robert Dahl alipata kuandika;" Ni wajibu wa dola kuendesha juhudi za kutafuta suluhu za migogoro ya kijamii. Siasa ni hatua za majadiliano endelevu yenye kuhakikisha migogoro inapatiwa ufumbuzi kwa njia za amani". ( Theory and Methods of Political Science Uk. 211)
Tofauti za kifikra na kimitazamo ni mambo ya kawaida katika siasa. Kunahitajika majadiliano endelevu katika kupata ufumbuzi wa migogoro. Si lazima papatikane mshindi katika kila mgogoro, wakati mwingine hutengenezwa mazingira ya pande zote mbili kushinda, kila mmoja kujisikia ameshinda, a win- win situation.
Kwa sasa CHADEMA iukubali ukweli, kuwa Uchaguzi uliopita umeshapita. Kwamba Serikali iliyo madarakani kwa sasa ndio hiyo inayoongozwa na JK kama Rais. Hatuna Rais mwingine. Hatuna Serikali nyingine.
Na CCM nayo iukubali ukweli, kuwa wakati umebadilika na kuwa wananchi wanaukubali upinzani. Na kwamba kwa sasa, CHADEMA ndio chama kikuu cha upinzani kikifuatiwa na CUF.
Vyama hivi na vingine vyenye uwakilishi bungeni, vina lazima ya kushirikiana katika mambo ya msingi na yenye maslahi kwa taifa letu.
Tuache kujichimbia kwenye mahandaki. Tuanze sasa kuijenga nchi yetu kwa pamoja. Hatuwezi kuijenga nchi yetu katika hali ya vurugu , uhasama na chuki. Hii ni nchi yetu. Ni nyumba yetu tunayoijenga. Kwanini tugombanie fito?
Maggid
Dar es Salaam
Februari 3, 2011
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment