Friday, January 30, 2015
Batobato na Michirizi ya Njano unaangamiza muhogo
Utafiti wa Muhogo Chambezi kupitia mradi wa EAAPP
Ili kupata mbegu bora ya muhogo, utafiti hupitia hatua mbalimbali ikiwemo hii ya 'clonal evaluation trial' kama tulivyoelezwa na mtafiti Karoline Sichalwe(mwenye t-shirt ya mauamaua) kutoka kituo cha Utafiti wa Kilimo-Kibaha anayefanya utafiti wa kupata aina bora ya mbegu ya muhogo kwenye mashamba yaliyopo kituoni Chambezi-Bagamoyo. Utafiti unagharamiwa na mradi wa EAAPP.
Chambezi-Kituo kidogo cha Utafiti wa Kilimo
Hiki ni kituo kidogo cha Utafiti wa Kilimo Chambezi wilayani Bagamoyo kinachosimamiwa na Kituo cha Utafiti Mikocheni kilichopo Dar Es Salaam. Kituo hiki kilianzishwa wakazi wa Mradi wa Taifa wa Kuendeleza Zao la Mnazi kwa ufadhili wa Ujerumani. Kituo hiki kwa sasa hutumika zaidi kwa utafiti wa Muhogo ingawa tafiti za mazao mengine kama vile korosho na minazi unafanyika kwa kiasi kidogo. Kituo hiki kina eneo kubwa kwa shughuli za utafiti wa kilimo endapo kiyawezeshwa kupata raslimali za kutosha kinaweza kuvutia shughuli nyingi za utafiti wa mazao kanda ya mashariki.
Tukiwa Modiporum-India kwenye Taasisi ya Utafiti ya Mifumo ya Kilimo
Tulipokuwa kwenye ziara ya mafunzo nchini India mwaka 2014, timu yetu ilipata fursa ya kutembelea Taasisi ya Utafiti wa Mifumo ya Kilimo nchini India huko Modiporum. Hapa tulikutana na watafiti nguli wa Taasisi hiyo na kuongea nao jinsi wanavyoendesha utafiti wa aina hiyo ambapo hapa kwetu ni sehemu ndogo tu. Tulipata fursa ya kutembelea tafiti zinazoendelea hapo hapo kituoni zinazohusu mifumo ya kilimo. Baada ya hapo tulipata picha ya pamoja.Mwenye vazi la Kihindi ni Dr. Mohamed Bahari aliyekuwa Mkurugenzi wa Utafiti, Mafunzo na Ugani kutoka Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi ambaye alikuwa ndiye kiongozi wa msafara kutoka Tanzania.
Utafiti wa Nyati wa maziwa nchini India
Utafiti wa kupata aina ya nyati bora kwa utoaji wa maziwa ni endelevu nchini India. Taasisi ya Utafiti wa Ng'ombe wa Maziwa wanaendelea na tafiti mbalimbali kufikia lengo hili. Huku utafiti ikiendelea ng'ombe na nyati wanaozalishwa hupewa chakula kinachohitajiwa na kutunzwa kwenye mabanda ya kisasa.
Kutunza kumbukumbu ni muhimu
Nilipokuwa kwenye ziara ya mafunzo nchini India nilikumbushwa umuhimu wa kutunza kumbukumbu ya mifugo kama inavyoonekana pichani. Kumbukumbu hizi ni za aina ya ng'ombe . Hiki ni kituo cha Utafiti kinatafiti aina bora ya ng'ombe wa maziwa anayewaza kupatikana kwa sifa wanazozihitaji ili aweze kusambazwa kwa wafugaji.
Benny Morandi kijana anayejituma kuishi maisha bora
Thursday, January 22, 2015
Tutangaze korosho kutoka Tanzania
Miaka ya 80 mpaka 90 zao la korosho lilikuwa hoi bin
taabani. Wakulima wengi waliyaacha mashamba yao ya korosho na kuangalia
shughuli nyingine zinazolipa. Jitihada zilizofanywa na serikali kupitia wadau
mbalimbali zimenyanyua uzalishaji wa zao hilo. Korosho sasa bei yake imepanda
si chini ya shilingi 1000 kwa kilo kwa korosho ambazo hazijabanguliwa. Sasa
wajasiriamali wengi wamejitokeza na kuanza kuziandaa korosho na kuzifunga
kwenye muonekano mzuri. Katika mkoa wa Mtwara, wilaya
ya Tandahimba inaongoza kwa uzalishaji wa korosho na mabadiliko unayoona
dhahiri kupitia maisha ya wananchi wa Tandahimba. Wanavijiji wana makazi bora,
huduma za shule ni nzuri hata upatikanaji wa maji safi na salama zimeboreshwa
kupitia ruzuku kutoka Halmashauri inayopatikana kutokana zaidi na kipato kutoka
zao la korosho.Hebu angalia korosho zilizofungashwa vizuri kutoka IMANI.
Korosho hizi zilikuwa kwenye maonyesho ya NaneNane 2014 mkoani Lindi viwanja
vya Ngongo.Mimi ni mmoja ya watu wanaopenda kutafuna korosho hazinikinaishi.
Korosho ni tamu. Hivi ni kwanini unaposafiri kwa usafiri wa anga, mashirika ya
ndege hapa nchini hawatangazi korosho zetu za Tanzania kwa kuwapatia abiria
watafune kama snacks? Ukipanda Air Botswana au Swazi utatafuna nyama
zilizokaushwa mpaka meno yaume na kutambua kweli unaelekea nchi ya wafugaji!
Wednesday, January 21, 2015
Mbegu za muhogo katika kiganja cha mtafiti
Hizi ndizo mbegu za muhogo. Wasio wakulima na wataalamu wa kilimo wanaweza kubisha kuwa muhogo hauna mbegu kwa kuwa wamezoea kuona muhogo ukipandikizwa kwa kutumia pingili. Nilipokuwa kwenye kituo kidogo cha majaribio ya utafiti kilichopo Chambezi, Bagamoyo, mtafiti alituonyesha mbegu za muhogo ambazo zinatumika katika mchakato wa kupata aina mbalimbali za muhogo.
Je ulishawahi kuomba 'lift' kwa Rais na kukubaliwa?
Rais wa Uruguay Jose Mujica na mkewe Lucia Topolansky (pichani) hivi karibuni wamemshangaza kijana Gerhard Acosta baada ya kumpa 'lift' kwenye gari yao ya serikali. Baadaye Gerhald alisema hivi " Nilipoteremka, nilishukuru na kufurahi sana kwa sababau si kila mtu mwenye moyo wa kumsaidia mtu asiyemjua barabarani, achilia mbali ni Rais wa nchi." Chanzo gazeti la Raia Mwema 21/01/2015.
Thursday, January 15, 2015
Subscribe to:
Posts (Atom)