Kama u mpenzi wa muziki wa dansi, naomba kukuuliza swali moja. Je, umeshawahi kuhudhuria show moja ya bendi ya "FM ACADEMIA?" Kama hapana, basi ukiwa Dar fanya hamu siku moja uwatembelee pale "nyumbani kwao" Kijiji cha Makumbusho ili upate muziki mzito na show kamambe kutoka kwa "FM ACADEMIA."
Uongo dhambi, vijana hao wanajituma kweli wanapokuwa jukwaani. Kila mwenye kipaji kwenye bendi hiyo hutumia kipaji chake barabara kuwaburudisha wateja wao na kweli thamani ya fedhaa mbayo ni kiingilio (value for money) unaipata ukiingia kwenye show ya"FM ACADEMIA."
Chakufurahisha ni kwamba wanamuziki hawa karibu wote wanaweza kutumia vyombo vya muziki, kuimba na kucheza. Akina dada wa show ndo usiseme kwa kweli wanakonga nyoyo za washabiki.
Siandiki haya kwa ushabiki tu bali mimi mwenyewe yapata mwezi mmoja uliopita, Jumamosi moja marafiki zangu walinipa "offer" mimi na mke wangu kwenda kuwaona wanamuziki hao. Sijapata kwenda dansi karibu miaka 15 sasa lakini siku hiyo nilirudisha ari ya kupenda muziki wa dansi na sasa nina usongo wa kuwaona "AKUDO IMPACT" nasikia nao ni mwisho wa njia. Wanamuziki wetu wana la kujifunza kutoka "FM ACADEMIA."
Ni kweli "FM ACADEMIA" funga kazi na siku hiyo nilicheza nakuimba "Songo na matembele!" Na kwakweli ilikuwa siku nzuri sana kwani ni siku ambayo Taifa Stars ilitoka sare na Cameroon ndani ya uwanja wa Taifa. Ndipo Nyoshi "El Sadat" alipotuimbisha "Taifa Stars Oyee!"
No comments:
Post a Comment