Tuesday, July 29, 2008

Wakulima hawazioni fursa zilizopo kubadili maisha yao


Baada ya kusafiri sehemu mbalimbali za nchi yetu nimebahatika kuona mengi mazuri na mabaya na kujifunza mengi hasa kwa sekta ya kilimo.



Wakulima wana fursa nyingi ya kujikwamua kiuchumi kupitia sekta hii iwapo fursa hizo zitatumiwa vizuri kwa mahali husika na wakati muafaka. Mazao ya aina mbalimbali yanayostawi hapa nchini yanaweza kupata soko la ndani na nje. Mifugo ya aina mbalimbali inayopatikana hapa nchini na inaweza kupata soko la ndani na la nje.



Mwezi mmoja uliopita nilikuwa nikifanya utafiti fulani na kutembelea kiwanda cha Chibuku hapa Dar Es Salaam na kuelezwa kuwa mtama na mahindi ni mali ghafi ya kutengeneza pombe ya chibuku. Muhogo unatumiwa kwa mahitaji ya chakula cha binadamu na mifugo, viwandani na kwenye maabara ya madawa. Soko la Korosho lipo ndani na nje ya nchi. Ukipita pale Kibaha, Ruvu korosho 10 za kukuaanga ni shilingi 500!



Machungwa sasa yanapatikana karibu mwaka mzima. Kwa sasa chungwa moja linauzwa kati ya shilingi 50 hadi mia moja hapa jijini Dar. Mbogamboga, matango na matunda ya aina mbalimbali soko lipo. Mchele nao hautafuti soko. Karibu kila mkoa una sifa ya kuzalisha mazao au mifugo zaidi ya aina moja.



Kinachotakiwa sasa ni kubadili mtazamo wetu kwenye kilimo. Lazima tufahamu kuwa kilimo si chakula tu ni biashara ni biashara pia na biashara ni pesa. Mkulima sasa atambulike, apatiwe fursa ya kupata mikopo kutoka taasisi za fedha zilizopo nchini ili ziweze kumsaidia katika kuzalisha. Kwani wakizalisha kwa wingi fedha hizo hurudi huko huko. Matokeo yake pande zote zinafaidika.

No comments: