Thursday, August 27, 2009

Tulipenda Kusoma-Mjomba


Juzi Jumanne nilimtembelea mjomba wangu Dr. Gregory P.Mluge nyumbani kwake Mbezi Beach. Ni muda mrefu hatujaonana na kuzungumza kwa kweli. Alifurahi sana kuniona na tukapata chakula cha pamoja na Binti yake Janet na wajukuu zake.

Wakati tukiwa kwenye mazungumzo tuligusia mambo mbalimbali kwa kifupi sana, kilimo chetu na maisha kwa ujumla hasa nyumbani Matombo. Kwa maneno yake mwenyewe alisikitika kuona kuwa jinsi maendeleo ya Matombo yanavyosuasua. Yeye anaona kama Matombo inarudi nyuma vile. Vijana hawachapi kazi wapo tu vijiweni.

Kwa Upande wa Elimu yeye alisema zamani wao walipenda sana kujifunza tena walitumia muda mchache lakini walikuwa wakielewa mambo na kuyazingatia wafundishwayo.

Dr. Mluge amesoma shule nyingi zikiwemo Bigwa Primary School, Kigurunyembe, Tabora Boys, Pugu High School hatimaye Makerere Uganda alikohitimu udaktari. Baadaye alikwenda Uingereza kwa masomo ya Juu ya Udaktari na kufanya kazi huko kwa miaka mingi na baadaye Saudi Arabia. Hivi sasa anapumzika nyumbani Mbezi lakini anapenda sana shughuli za Kilimo ingawa kwa maneno yake mwenyewe kilimo cha Tanzania hakilipi na kinategemea sana hali ya hewa hasa mvua. Mazao hasa ya matunda yanaharibika hovyo wakati wa msimu na mkulima hafaidiki kutokana na kazi kubwa anayoifanya kwa kuzalisha mazao hayo.

Wakati akiwa Makerere walikuwa pamoja na Rais Mstaafu wa awamu ya tatu Mhe. Benjamin William Mkapa. Pichani Dr. G.Mluge akiwa na mkewe kushoto akitambulishwa na Blogu hii kwenye moja ya sherehe za kifamilia.

No comments: