Tuesday, January 26, 2010

Tatizo huzaa tatizo


Jumapili iliyopita niliweza kuhudhuria ibada takatifu katika Kanisa Katoliki Parokia ya Vikindu. Katika mahubiri yake Paroko Tom alitoa hadithi fupi kama ifuatavyo.

Siku mmoja mwanaume fulani aliyekuwa akiendesha gari lake alimkuta binti mrembo aliyemuomba msaada wa usafiri au 'lift' kama tulivyozoea. Bila kusita alimpa msaada huo binti huyo. Lakini mara alipoingia ndani bwana huyu alianza kujawa na wasiwasi, baada ya muda alipoangalia kiti alichokaa yule binti akaona kuwa amezirai! Bwana yule alijitahidi kumpeleka binti huyo hospitali iliyo karibu. Baada ya muda mrefu akapata habari kutoka kwa wauguzi inayompa hongera kwa kuwa baba!

Bwana yule alihamaki. Itakuwaje, yeye hamjui binti huyo. Alipoulizwa yule binti akasema haswa bwana yule ndiye baba wa mtoto. Haikuishia hapo polisi waliitwa na hatimaye bwana yule aliwekwa mahabusu kwa kosa la kufanya vurugu wakati alipokuwa akikataa kuwa si baba wa mtoto.

Shauri lilifikishwa mahakamani na ikaamuriwa kuwa bwana yule apimwe. Majibu yalipotoka iligundulika hana uwezo hata wa kuweza kuwa na mtoto. Bwana alifurahi kwani alishinda. Lakini akajiuliza sasa itakuwaje? Mbona nina watoto wawili niliyezaa na mke wangu wa ndoa. Alijiuliza? Alichanganyikiwa. Tatizo limezaa tatizo. Ni kweli kama binadamu hatuwezi kukwepa matatizo. Ubinadamu ni pamoja na kukabiliana na matatizo katika maisha yetu.(Picha kwa hisani ya gazeti la Mwananchi 26/1/2010)

No comments: