Kuzaliwa: 18 Julai, 1919
Kufariki: 19 Desemba, 2011
Bibi Annastasia Hugo Chuma alizaliwa tarehe 18 Julai, 1919 Matombo, Morogoro.
Katika uhai wake, Bibi Annastasia Chuma Hugo hakuwahi kupata malezi ya moja kwa moja ya mama yake mzazi, bali alilelewa kwa upendo na Baba yake mkubwa, Mzee Clemence Pius Boko.
Bibi Chuma alipata bahati ya kusoma elimu ya msingi hadi ngazi ya Standard IV (akiwa ni miongoni mwa waasisi wa Shule ya Msingi ya Matombo).
Bibi Annastasia Chuma Hugo alibahatika kufunga ndoa na Mwl. Paul Lugonzo na kubahatika kupata naye watoto 7 kati ya mwaka 1934 na mwaka 1954.
Watoto hao ni:
1. Sister Philomena Mluge
2. Dk. Gregory Mluge
3. Bibi Janeth Kaaya Kishongo
4. Bibi Beatrice Mhango
5. Frederick Mluge
6. Bibi Rosemary Mokiwa
7. Bibi Maria Dolores P. Mdimi
Kwa mipango ya Mungu Mume wa Marehemu, Mwl. Paul Lugonzo na watoto wanne kati ya saba (Sister Philomena Mluge, Bibi Janeth Kaaya Kishongo, Bibi Rosemary Mokiwa na Frederick Mluge) wamekwishatangulia mbele ya haki, Raha ya Milele uwape Ee Bwana, na Mwanga wa Milele uwaangazie, wapumzike kwa amani, Amina.
Kwa kuwa mumewe alikuwa ni Mwalimu, Marehemu Bibi Annastasia Chuma Hugo aliambatana na mumewe katika maeneo mbalimbali ya nchi alipowahi kufanya kazi mumewe, ikiwa ni pamoja na Bagamoyo na Singiza.
Bibi Annastasia Chuma Hugo pia alipata bahati ya kusafiri hadi nchi za ng’ambo kwa nyakati mbalimbali kwa matibabu ya macho na kutembelea watoto na wajukuu zake huko Uingereza na Saudi Arabia kati ya 1979 na 1985.
Annastasia Hugo Chuma alikuwa ni mcheshi na aliyependa kusimulia masuala mbalimbali ya historia, hasa zilizogusa maisha yake kwa karibu. Bibi Annastasia Chuma Hugo ana kumbukumbu za kutokewa “katika njozi” na mtu aliyemfananisha na mama yake, wakati huo akiwa na umri wa miaka mitatu, ambaye alimuasa kuwa na upendo na heshima kwa watu wote, na kumcha Mungu. Mambo yalikuwa nguzo kuu katika uhai wake wote wa jumla ya miaka 92 na miezi mitano, aliyojaliwa kuishi hapa duniani.
Afya ya Bibi Annastasia Chuma Hugo ilianza kudorora mwaka 2001 ambapo alianza kusumbuliwa na maradhi ya kichwa. Pamoja na kupatiwa matibabu, bado hali yake ya afya haikuweza kuimarika sana. Hali ya afya ya Bibi Annastasia Chuma Hugo iliendelea kudorora na hatimaye matatizo yake yalizidi na kumfanya ashindwe kutembea, akawa ni mtu wa kulala zaidi na aliyehitaji zaidi kusaidiwa kwa karibu kila kitu.
Hali ya Bibi Annastsia Chuma Hugo ilibadilika zaidi katika wiki ya pili ya mwezi Desemba ambapo kula kwake kulikuwa kwa tabu. Aidha, alipumua kwa tabu.
Ilipofika tarehe 19 Desemba, 2011, bibi Annastasia Chuma Hugo alifariki dunia majira ya saa kumi alfajiri. Bwana Ametoa na Bwana Ametwaa, Jina la Bwana Lihimidiwe. Raha ya Milele Umpe Ee Bwana, na Mwanga wa Milele Umwangazie, Apumzike kwa amani. Amina.
Bibi Annastasia Chuma Hugo ameacha watoto watatu (3), wajukuu kumi na saba (17) na vitukuu ishirini na mbili (22). Watoto wa Bibi Chuma(Dolores na Beatrice) pamoja na mjukuu wake (katikati) mwandishi wa wasifu huu Bw. Frank Shaniel Mdimi
1 comment:
Poleni sana,
Apumzike kwa Amani
Post a Comment