Ukisikia kuperemba ndiyo huku. Huwa ni wataalamu wa Tume ya Mipango wakiperemba mradi wa Maji kwenye moja ya Halmashauri nchini. Ilibidi waende mpaka juu kabisa kuhakikisha hilo tank la maji linalojengwa ili kujihakikishia ubora wa tanki hilo baadaye kuandika taarifa. Sijui wameona nini, mimi sijui.
Friday, November 21, 2014
Kutoka Bukoba hadi Bungeni Dodoma
Hivi ndivyo tunavyotakiwa kuwajenga watoto wetu wawe na uelewa mpana na kujenga uzalendo wa kuipenda nchi yetu. Wanafunzi hawa wa shule ya Rweikiza kutoka Bukoba wamesafiri hadi Dodoma kutembelea Bunge letu kujifunza jinsi Bunge linavyofanya kazi. Hivi kweli hawa wakipata swali linalouliza jinsi Bunge linavyofanya kazi watashindwa kulijibu? Hapa wanakutana na Waziri Mkuu Mh. Mizengo Pinda. Ona jinsi Pinda alivyofurahi akizungumza nao. Shule zinatakiwa kuwa na programu za aina hii. Huwezi kuzungumzia Bunge la London wakati la kwenu la Dodoma hulifahamu!
Dr. Florence Turuka Matawi ya Juu
Tulipokuwa Tosamaganga High School, Dr. Florence Turuka (kulia) alikuwa Form V maana yake alikuwa mdogo wetu! Dr. Turuka sasa ni Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (kushoto ni bosi wake Waziri Mkuu Mh. Mizengo Pinda). Ninavyomfahamu Turuka tangu tukiwa Tosa ni 'kichwa' mwadilifu, social na mtu wa watu. Mpaka leo tukikutana hakosi kuniita Kaka Banzi.Je, wengine wanaweza? Dr. Turuka umetupaisha sana wana TOSA. Hata George Nyaupumbwe a.k.a. Ngi anafahamu hilo. (Picha imenyofolewa kutoka Michuzi Blog)
Wednesday, November 19, 2014
Tuesday, November 18, 2014
Vifaa ninavyotumia ofisini
Nilianza kuchukia mwandiko mbaya tangu nikiwa shule ya msingi, nilipenda kuiga mwandiko wa Mama Beatrice Mhango, shangazi Pauline Mloka, Baba yangu Mkubwa Mwl. Ephrem Ephrem Mbiki, Kaka Seraphin Chibby na marehemu uncle Longin Mizambwa hawa walinivutia kwa wakati huo na kwa kweli niliwaiga kwa kuumba herufi mojamoja niipendayo na kuchanganya na kutoka na mwandiko wangu 'unique'. Nilipofika sekondari pale Njombe niliwakuta wanafunzi wanaoandika miandiko mizuri sana akiwemo rafiki yangu marehemu John Makoroma (The Printer) wengine walionivuta kuandika mwandiko mzuri ni uncle Nestory Daulinge, uncle Balozi Daniel Mloka, rafiki na wengine wengi walioandika vizuri. Kwa hali hiyo nilipenda pia kutumia kalamu nzuri ndiyo maana mpaka sasa moja ya vitu ninavyovipenda kuwa navyo katika maisha yangu ni kuwa na kalamu nzuri. Ingawa kuna kompyuta na ni mtumiaji mzuri lakini sikosi kununua kalamu nzuri hata fountain pens ninazo na si moja ni za aina aina. Angalia vifaa ninavyotumia kikazi na kwa mawasiliano ninavipenda na vinanipa motisha ya kuandika. Napenda kuandika katika maisha yangu napenda pia kutumia zana bora.
Mbeya City Kwishneee
Kuna msemo wa Kiswahili unaosema kuwa, ngoma ikilia sana haikawia kupasuka. Hiki ndicho kilichotokea kwa timu ya soka ya Mbeya City. Msimu uliopita ilikuwa tishio kwa timu nyingine kila timu iliyotia mguu Mbeya ilifungwa au kutoka sare.Mwaka huu kinyume chake watu wanakwenda Mbeya wanajichukulia pointi kirahisi. Nasikia kisa ni ukata. Mwaka wa jana timu ikishinda kila mchezaji alipata posho ya shilingi 25,000/= na sare 15,000/= mwaka huu mpango huo haupo. Nimesoma hivi karibuni kwenye gazeti moja hapa nchini kuwa kocha wa timu hiyo Bw. Mwambusi 'amebwaga manyanga.' Sijui ni kweli.
Subscribe to:
Posts (Atom)