Wednesday, August 6, 2008

Usipofika Msamvu Makuti unakosa mengi

Ukipata bahati ya kutembelea mji wa Morogoro. Usipate shida, moja ya sehemu nzuri na za kupendeza na zenye kutoa huduma za uhakika za chakula na vinywaji ni Msamvu Makuti.

Msamvu Makuti ipo ndani ya kituo kikuu cha mabasi cha mji wa Morogoro. Inafikika kirahisi ukielekea Dodoma, Dar Es Salaam au Iringa. Msamvu Makuti imeweza kujijengea jina hasa kwa nyama choma, supu na mchesho!

Watoa huduma wa Msamvu Makuti ni vijana wachangamfu wake kwa waume na huwapokea wateja mara tu wanapokaribia milango ya banda hilo la Makuti lilioezekwa kiutamaduni.

Ifikapo usiku starehe ya muziki inapatokana na usafiri wa kurudi sehemu uliyofikia au nyumbani kwako ni "bwelele." Msamvu Makuti inatoa faraja kwa wasafiri wakati wote kwa huduma ya chakula na vinywaji. Ukiwa Msamvu Makuti unaweza kujinunulia matunda ya aina mbalimbali yanayopatikana mkoani Morogoro hasa ndizi ,machungwa, maembe na mananasi.

Uwapo Msamvu Makuti milima ya Uluguru inakukonyeza huku maji yakitiririka!

Gwami Internet Cafe Morogoro

Mji wa Morogoro unapanda chati kwa kasi ya ajabu. Hii pengine inatokana na taasisi nyingi kuwepo kwenye mji huu. Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA), Chuo Kikuu Mzumbe, Chuo Kikuu cha Kiislamu, Chuo cha Ardhi, VETA Morogoro, Hospitali ya Mkoa, Chuo cha Mifugo, Stesheni ya Gari Moshi (Reli) Shule za Sekondari nyingi tu, kumbi za mikutano , mahoteli na nyumba za wageni na nyingine ambazo sijazitaja. Mji huu ni wa biashara hasa yanayotokana na mazao ya kilimo na madini.

Kuwepo kwa taasisi hizi kunasababisha kuongezeka kwa idadi ya wakazi na wageni wa mji huu kila siku. Kwa kuwa wageni na wakazi wanaongezeka basi mahitaji huongezeka.

Moja ya huduma muhimu katika enzi hizi za sayansi na teknolojia ni ile ya mtandao au "Internet". Internet inasaidia sana katika kurahisisha mawasiliano. Kwa mji kama huu wenye Maprofesa, wataalamu wazamivu na wazamili pamoja na wanafunzi wa ngazi zote huduma hii ni muhimu.

Ukiwa Moro usihangaike sana ulizia ilipo ofisi ya CCM wilaya ya Morogoro karibu kabisa na mahali pa starehe panapoitwa Chipukizi utakuta Internet Cafe moja bomba sana inaitwa Gwami Internet Cafe.

Internet Cafe hii ni moja ya internet ya kisasa hapa nchini naweza kusema bila ya kuuma meno. Computer zake ni safi na mtandao una speed kubwa. Usafi ndani ya cafe ni wa hali ya juu, vijana wachangamfu na wenye utaalamu wa mtandao wanatoa huduma safi. Hata maji ya kunywa yapo ndani ya cafe yanayopatikana kupitia mashine maalum. Dakika 30 ya kutumia mtandao ni shilingi 400/= tu.

Tuesday, August 5, 2008

"B One" Mtandao bora wa nyumba za wageni Morogoro

Ukiwa ni mara yako ya kwanza kutembelea mji wa Morogoro usipate shida ulizia "B one" kwa ajili ya huduma za malazi.

Wiki iliyopita nilikuwa Morogoro. Huwa nauona mtandao wa B one wa nyumba za wageni lakini niseme ukweli nilikuwa naogopa kuulizia nikidhani kuwa ni za gharama kubwa yaani si ya kiwango changu. Kumbe nilikuwa sina taarifa sahihi za kutosha. Nilipojaribu kuulizia nafasi ya malazi nilibahatika kupta kwenye moja ya nyumba hizo. Lazima ni kiri kwa mambo yafuatayo niliyoyaona kwenye nyumba hiyo.
  • Usafi wa hali ya juu
  • Kauli nzuri ya wahudumu
  • Unapata kifungua kinywaji kamili (+juice ya matunda ya Morogoro!)
  • Ulinzi wa uhakika
  • Utulivu masaa 24
  • Kila chumba kina TV
  • Gharama ya kuridhisha

Kilichobaki "B One" ni kujitangaza kwa njia zote ikiwezekana kukamata soko la nyumba za wageni Morogoro. Kula 5 mjasiriamali wa "B one."

Kwa mtandao kama huu, Moro sasa chati yake inapanda kwa kasi ya kutisha. Tembelea Moro na usikose kuulizia "B one" halafu toa maoni yako kupitia www.innobanzi.blogspot.com

Msamvu - Morogoro "Keep left" Kikubwa Tanzania

Nimebahatika kutembelea mikoa mingi hapa Tanzania lakini sijapata kuona "keepleft" kubwa na inayotunzwa vizuri kama ile ya Msamvu, Morogoro. "Keep left" hiki kiko kwenye makutano ya barabara ya morogoro, Iringa na Dodoma kwa kweli ni kikubwa. Kinachofurahisha zaidi ni jinsi Manispaaa ya Morogoro inavyokitunza. Kina maua mazuri ya aina mbalimbali na uhudumiwa vizuri kwa kumwagiliwa maji na kuondoa magugu yasiyohitajiwa. Sasa naweza kusema kuwa " Keepleft" cha Msamvu ni nambari wani hapa Tanzania. Aliyeona kikubwa zaidi ya hicho akitaje basi!

Monday, August 4, 2008

Zongo Mwenyekiti Lugaluga Agricultural and Marketing Cooperative Society

Mkutano Mkuu wa Ushirika wa Kilimo na Masoko - Lugaluga (Lugaluga Agricultural and Marketing Cooperative Society) uliofanyika tarehe 2 Agosti 2008 kwa kauli moja umepitisha jina la Bw. Ally Rashid Zongo kuwa Mwenyekiti mpya wa chama hicho baada ya aliyekuwa Mwenyekiti wa ushirka huo Bw. Chaula kuhamia Mbeya kikazi.

Kabla ya hapo Bw. Zongo alikwa akishika nafasi ya Makamu wa Mwenyekiti katika Ushirika huo. Kwa maana hiyo, Bw. Zongo ndiye Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Ushirika huo.

Chama cha Ushirika wa Kilimo na Masoko Lugaluga kilichopo Morogoro kilisajiliwa rasmi Septemba 2005 na kupewa namba 344. Hadi sasa ushirika una wanachama 88 wanaotimiza masharti na kanuni za chama.

Ushirika wa Lugaluga una mpango kabambe wa kumiliki ekari 20,000 zitakazotumiwa na wanachama wake katika uzalishaji wa kilimo na ufugaji.

Dira ya Lugaluga ni kuinua na kustawisha hali ya uchumi na maisha ya wanachama na jamii kupitia vyama vya ushirika.

Lugaluga ni chama chenye kuona mbalimbali katika uzalishaji wa kilimo na ushirika.
Pamoja na raslimali kubwa ya ardhi iliyoko mbele yao, Lugaluga inakosa mtaji wa kujiendesha.

Kwa kuwa mkoa wa Morogoro umetajwa kuwa ni kapu la uzalishaji wa mazao ya kilimo hapa nchini kuna haja ya viongozi wa ngazi zote kutoa machango wao katika kuhakikisha kuwa Lugaluga inakuwa mfano bora wa ushirika mkoani Morogoro na kwa Taifa. Jambo la msingi ni kusimamia na kuona kuwa wanachama wake wanapata mikopo itakayowawezesha katika uzalishaji kwa kununua pembejeo za kilimo, kutayarisha mashamba na kupata teknolojia za kisasa za kilimo.

Vyombo husika vitayarishe mipango na kuitekeleza katika kuboresha miundo mbinu ya shambani na hasa barabara. Hili ni tatizo kubwa lilojitokeza wakati wa kutayarisha mashamba kwa msimu wa mwaka 2007/08.

Saturday, August 2, 2008

Nauli Mpya Utafiti wa kina haujafanywa

Jana tarehe 1 Agosti nauli za vyombo vya usafiri zimepanda nchini kote hasa kwa usafiri wa magari. Kupanda huku kwa nauli kumewafanya watanzania wengi kufikiri jinsi ya kufanya ili kuweza kukabiliana na kupanda huku kwa nauli.

Tatizo hili limejitokeza kwa kina zaidi jijini Dar Es Salaam hadi kufikia wanafunzi wa shule za msingi na sekondari kuandamana kwenda ofisi za Mkuu wa Mkoa wa Dar Es Salaam ili kuonana na Mh. Kandoro wamueleze kukerwa kwao na uwezo walio nao wanafunzi.

Wafanyakazi wengi hasa wa kipato cha chini kuongezeka kwa nauli ni kero kwao. Wafanyabiashara wadodowadogo "wamachinga, mamantilie" nao ni pigo itabidi waongeze bei ya sahani ya wali au wapige panga kwa bei hiyohiyo ili waweze kupata faida. Bidhaa feki nazo zitaoongezeka madukani.
Nasema utafiti haujafanyika kwa nauli mpya za sasa.

Asha Rose Migiro anavyoonekana kwa watu

Dkt. Asha Rose Migiro ni jina maarufu si hapa Tanzania bali hata kwa mataifa mengine.
Dkt. Migiro Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN) ni moja ya matunda bora kutoka Tanzania yanayowaka katika anga za Kimataifa.

Ninavyomfahamu mimi, Dkt. Asha Rose Migiro aliwahi kuwa mhadhiri pale Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam na ameshawahi kuwa Waziri wa Maendeleo ya Jamii na Wanawake na Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje na Uhusiano wa Kimataifa.

Hivi sasa yupo Tanzania kwa likizo fupi. Kwa muda wa wiki moja sasa amekuwa akifanya mambo mengi hapa nchini. Ameshahudhuria kikao cha Bunge na kulihutubia na kuhojiwa na vyombo vya habari hapa nchini.

Wakati wote huo nilichojifunza kutoka kwake, mwanamama huyu ni makini sana. Anajua nini cha kuongea na wakati gani na kwa akina nani. Ana kipaji kikubwa cha kutumia lugha. Anaweza kujieleza barabara kwa kiswahili fasaha na kiingereza makini.

Huyu ni mtu ambaye ameshatembelea nchi nyingi na kukutana na watu wengi maarufu na wa kawaida hapa duniani lakini haachi kujitambulisha Utanzania wake. Kwa kweli nimempenda jinsi anavyojiweka katika hali ya kawaida kabisa.

Nimesikia kuwa mpaka sasa anaishi kwenye nyumba za wahadhiri kule Chuo Kikuu Dar Es Salaam na hata alipokuwa waziri. Huyo ndiye Dkt. Asha Rose Migiro kioo cha Tanzania na mfano bora kwa wanawake.

Kamokerere-Kijiji cha Chacha Wangwe

Sijawahi kufika Musoma,Tarime husan kijiji cha Kamokerere. Sijawahi kumuona uso kwa uso marehemu Chacha Wangwe aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Tarime. Lakini kwa takriban wiki moja sasa, kijiji cha Kamokerere kimekuwa maarufu kupitia vyombo vya habari kufuatia kifo cha Chacha Wangwe.

Kwanini Kamokerere? Chacha Wangwe alikuwa mmoja wa wabunge maarufu kwa hoja zake nzito akiwa bungeni. Aliwawakilisha ipasavyo wapiga kura wake wa jimbo la Tarime ingawa alikuwa si wa chama tawala, yeye alikuwa ni wa CHADEMA.

Marehemu Chacha Wangwe alipata ajali akiwa safarini kutoka Dodoma kuelekea Dar Es Salaam. Kwa kuwa kifo chake hakikutarajiwa, wengi walidhani kuwa kifo hicho kilikuwa ni cha kupangwa yaani aliuawa ndiyo maana wapiga kura wake hasa kutoka kijiji cha Chamokerere walipandwa jazba kutaka kufahamu sababu ya kifo hicho.

Lakini kwa mujibu wa habari kupitia televesheni na magazeti ya leo asubuhi baada ya uchunguzi wa kitaalamu kufanyika mbele ya mashahidi ya pande husika imebainika kuwa marehemu Chacha Wangwe alikufa kwa ajali ya gari na kupasuka fuvu na ubongo kumwagika. Apumzike kwa amani Chacha Wangwe.

Friday, August 1, 2008

Foleni ya Mbagala inasababishwa na ubinafsi wa madereva

Licha ya kuamka mapema ili kuweza kuwahi ofisini, leo nimejikuta nikikwama Mbagala Sabasaba takribani kwa saa moja kutokana na foleni ya magari iliyosababishwa na baadhi ya madereva kutofuata utaratibu wa kuendesha gari.

Magari mengi yalikuwa yanakatiza njia wanazojua wenyewe na kusababisha magari kufungana karibu kabisa na kiwanda cha nguo- KTM.

Hali hiyo iliendelea hadi walipojitokeza askari wa usalama barabarani na kuchukua hatua kali kwa wale madereva waliokatiza njia ikiwemo kuwanyang'anya funguo za gari. Kuna askari mmoja wa kike alinifurahisha sana pale aliposimama mbele ya gari lililotaka kuingia barabara kuu kwa makosa. Bila kusema chochote alimgandisha kwa muda mrefu na hata gari letu kufanikiwa kupita. Ndiyo maana nasema foleni ya Mbagala (Barabara ya Kilwa) inasababishwa na ubinafsi wa madereva.

Viazi, mihogo hadi barabarani


Wakulima wetu wanajituma sana katika uzalishaji licha ya mazingira magumu waliyonayo lakini wameza kulisha taifa hili na kuweza kuimarisha uchumi wa nchi hii kupitia kilimo na ufugaji.


Juzi nilitembelea soko la Mbagala. Nilishangaa kuona mazao mbalimbali ya kilimo yamefurika soko hadi kuzagaa kwenye barabara.Muhogo na viazi bwerere kabisa. Ndani ya soko nyanya,bamia, mchele, maharage, vitunguu, karoti,mchicha, kabichi, mbaazi, njegere, ndimu, karanga, matango, pilipili hoho, pilipili mbuzi, tangawizi, nyanya chungu na vingine vingi vyote hivyo vimezalishwa na wakulima wadogowadogo. Licha ya kutegemea kilimo cha mvua kwa silimia kubwa lakini vyakula vipo. Kwa kweli wakulima wetu wanafanya kazi kubwa sana lakini bado mtazamo wa nchi kwenye kilimo naweza kusema ni hasi! Maneno mengi lakini wakulima tuseme ukweli hawajaendelezwa katika kilimo na hii inatokana na bajeti finyu inayotolewa kwa sekta ya kilimo

"TIGO" PEKEE WAMEWAONA WAKULIMA?


Sikukuuu ya wakulima "NANE NANE" ndiyo hiyo imeingia. Lakini kwa mujibu wa gazeti la "This Day." Kampuni ya simu "TIGO" ndiyo inayoonekana kudhamini maonyesho hayo tena kwa shilingi milioni 10 tu!

Kampuni nyingine ziko wapi? Kuna kampuni ambayo hainufaiki na Kilimo? Mbona kimya? Hata huo ufadhili wa shilingi milioni 10 kutoka TIGO ni mdogo sana. Hivi kuna wakulima wangapi wanaotumia mtandao wa TIGO? Hata kwetu Matombo, Morogoro mtandao unaotamba ni "TIGO" mnara wake umewekwa mlimani kileleni hivyo kuwafunika kabisa Celtel mtandao wa kwanza Matombo.

Huo ndio mtazamo wa watanzania wengi kwenye kilimo, hatukipi stahili yake kwenye mipango yetu licha ya mchango mkubwa unaotoa kwenye uchumi wa Taifa na maisha ya wananchi wetu.

Nashangaa " Serengeti" wamedhamini mpira wa miguu kwa mamilioni ya fedha huku wakisahau kuwa bia wanazotengeneza, malighafi kubwa ni mazao ya kilimo (ngano na shayiri).

Tunakula nyama za aina mbalimbali (kuku, ng'ombe, mbuzi, kondoo, bata) kutokana na juhudi za wafugaji lakini wanapotaka kuonyesha shughuli zao tunasita kudhamini. Mimi sipati picha kwa kweli.
Mwakani tuhamasiki kwa kudhamini maonyesho ya kilimo (NANE) iwe kampuni, vikundi au binafsi tuelekeze nguvu zetu kwenye kilimo. Kila mmoja wetu anafaidika na kilimo.

Tuesday, July 29, 2008

Shughuli imeanza Mtongani-Mbagala

Makaravati yanazikwa ardhini, njia za mkato zinatengenezwa, nguzo mpya za umeme zinasimikwa. Kweli, awamu ya Pili ya ujenzi wa barabara ya Kilwa imeshaanza na mambo yanakwenda kwa kasi ya ajabu. Siku hizi kutoka kwa Aziz Ally hadi Mtongani ni kuteleza tu. Imebaki sehemu ndogo pale Mtoni Mtongani. Wananchi wanangojea maajabu wayaone ya kupitisha barabara pale darajani itakuwaje? Twasubiri tuwaone Kajima.

Shughuli imeanza Mtongani-Mbagala

Siku hizi

Wakulima hawazioni fursa zilizopo kubadili maisha yao


Baada ya kusafiri sehemu mbalimbali za nchi yetu nimebahatika kuona mengi mazuri na mabaya na kujifunza mengi hasa kwa sekta ya kilimo.



Wakulima wana fursa nyingi ya kujikwamua kiuchumi kupitia sekta hii iwapo fursa hizo zitatumiwa vizuri kwa mahali husika na wakati muafaka. Mazao ya aina mbalimbali yanayostawi hapa nchini yanaweza kupata soko la ndani na nje. Mifugo ya aina mbalimbali inayopatikana hapa nchini na inaweza kupata soko la ndani na la nje.



Mwezi mmoja uliopita nilikuwa nikifanya utafiti fulani na kutembelea kiwanda cha Chibuku hapa Dar Es Salaam na kuelezwa kuwa mtama na mahindi ni mali ghafi ya kutengeneza pombe ya chibuku. Muhogo unatumiwa kwa mahitaji ya chakula cha binadamu na mifugo, viwandani na kwenye maabara ya madawa. Soko la Korosho lipo ndani na nje ya nchi. Ukipita pale Kibaha, Ruvu korosho 10 za kukuaanga ni shilingi 500!



Machungwa sasa yanapatikana karibu mwaka mzima. Kwa sasa chungwa moja linauzwa kati ya shilingi 50 hadi mia moja hapa jijini Dar. Mbogamboga, matango na matunda ya aina mbalimbali soko lipo. Mchele nao hautafuti soko. Karibu kila mkoa una sifa ya kuzalisha mazao au mifugo zaidi ya aina moja.



Kinachotakiwa sasa ni kubadili mtazamo wetu kwenye kilimo. Lazima tufahamu kuwa kilimo si chakula tu ni biashara ni biashara pia na biashara ni pesa. Mkulima sasa atambulike, apatiwe fursa ya kupata mikopo kutoka taasisi za fedha zilizopo nchini ili ziweze kumsaidia katika kuzalisha. Kwani wakizalisha kwa wingi fedha hizo hurudi huko huko. Matokeo yake pande zote zinafaidika.

Monday, July 28, 2008

Wagani wa kilimo wapatiwe vitendea kazi

Huwezi kumuona mhasibu asiye na calculator, daktari na kipima mwili chake, dereva na gari lake, mchoma mahindi na jiko lake, mama/baba ntilie na sufuria zake.
Utamtambuaje afisa ugani wa kilimo asiye na kitendea kazi? Anashauri wakulima wapande mazao kwa nafasi zinazokubalika huku kipimio hana. Anashauri wapande mbegu ya mahindi ya TMV 1 yeye mwenyewe haijui. Anawashauri wakulima wampunga watumie mbolea ya kukuzia aina ya UREA yeye mwenyewe wala hajui inakopatikana. Ndiyo maana mbunge mmoja alikumbusha kwa kweli, wakatia umefika sasa wa kuhakikisha kuwa maafisa wagani wa kilimo wanapewa vitendea kazi. Ndipo hapo tutakapowaona wakichacharika kweli kweli na watu wakiwathamini kama wanavyomthamini daktari.

Mafuta si leo, lakini hili la chakula tunaweza sasa


Hatujui ni lini Tanzania tunaweza kuzalisha mafuta mengi na kuweza kujitosheleza kwa matumizi ya ndani na kuuza ziada. Lakini kwa chakula tunaweza hata mwaka huu tukijipanga sawasawa. Hili linawezekana iwapo mipango yetu itawekwa kwa kuweka kipaumbele katika uzalishaji wa chakula. Tanzania tunayo fursa kubwa zaidi katika kilimo. Tuna ardhi ya kutosha, tuna maji ya kutosha, wataalamu wa kutosha na wananchi wetu asilimia 80 wanategemea kilimo hivi kweli hili nalo hatulioni? Tunataka tuletewe programu ya kuzalisha chakula kutoka World Bank? Hakika hili la kuzalisha chakula tunaweza sasa.

Tuwe tayari kutoa - Asema Padri Ngowi

Padri Ngowi wa Parokia ya Mkuranga amewaasa waumini wa Parokia ya Vikindu jimbo Kuu la Dar Es Salaam kuwa wawe wepesi na tayari kutoa kuliko kupokea. Padri Ngowi aliyasema hayo katika mahubiri yake aliyoyatoa Jumapili ya tarehe 27 Parokiani hapo.

Alisikitika kwa kusema kuwa, waumini Wakatoliki wamezoweshwa kupewa kuliko kutoa. Wakati umefika sasa wakuendesha Kanisa wenyewe bila ya kuwategemea wazungu na wamisionari wa kigeni. Watawa wanatakiwa kupata mahitaji muhimu kama vile chakula, mavazi, malazi na usafiri ili weze kutimiza wajibu wao wa kutoa huduma ya kiroho. Kwa hiyo ni wajibu wa waamuni kutoa sadaka na kulipa zaka kama inavyotakiwa na kanisa.

Akihubiri bila kuchoka, huku akirandaranda ndani ya kanisa na kuwahamisisha waumini na hatimaye kufanya harambee ya mavuno iliyoweza kukusanya zaidi ya shilingi 1,000,000 (fedha taslimu na ahadi) kwa ajili ya tegemeza parokia. Waumini walichangia kiwango cha sh 500/= hadi 150,000/=

Kwa hili la kuiogopa Simba, Yanga hawana la kusingizia

Kitendo cha Klabu Bingwa ya Soka ya Tanzania kwa mwaka 2008 - Dar Young Africans kushindwa kufika uwanjani kupambana na watani wao wa jadi Simba Sports Club ya Dar Es laam siku ya Jumapili katika pambano la kumpata mshindi wa tatu wa kombe la Kagame limeitia doa kubwa timu hiyo, Dar Es Salaam na Tanzania nzima.

Sababu za madai ya malipo ya ziada hayana msingi. Yanga kanuni za mashindano hayo wanayafahamu, iweje leo kusisitiza walipwe fedha zaidi kuliko hata anachapata mshindi wa mashindano hayo, ni kichekesho!

Dar Young Africans wamefanya usajili mzuri na wa gharama mwaka huu, wanamakocha watatu wakigeni tena wazungu! Hata golikipa mzungu pia amesajiliwa yanga, iweje leo kukacha mechi hiyo? Mi sielewi, hata Nicholaus Musonye ameshindwa kuwaelewa Yanga na hata kuwaita "wahaini wa CECAFA." Tusubiri maamuzi ya CECAFA kwa tukio hilo.

Thursday, July 24, 2008

Tuwatambue wakulima wetu

Sawa kabisa, inavyoelekea, bado hatujawatambua wakulima wetu. Ni kina nani? wangapi? wako wapi? na wanahitaji nini?wanafanya nini kwa sasa? wanafanyaje? kwanini wanafanya hivyo? Hayo ni maswali ya msingi kabisa yanayotakiwa kufahamika kutoka kwa wakulima wetu ili tuweze kuwatambua.

Tusipowatambua, mipango ya kuwapatia pembejeo za kilimo itakuwa ni ya mashaka, mipango ya kuwatafutia masoko utakuwa ni wa kubuni tu, teknolojia za kilimo zinazobuniwa kumsaidia mkulima katika kuboresha uzalishaji zitakuwa ni za watafiti tu ni si mahitaji ya mkulima, tunaweza kununua matrekta na kuyasambaza kila mkoa kumbe si kila mkoa unahitaji matrekta idadi sawa, tunaweza kumwaga mabilioni kwa kutoa mikopo kwa wakulima kumbe wakulima hawajui jinsi ya kutumia mikopo hiyo na pengine mikopo inaweza kutolewa wakati usio mwafaka kwa kilimo.

Kwahiyo basi suala la kuwatambua wakulima wetu ni la msingi kama baadhi ya wabunge walivyochangia kwenye hotuba ya Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika mwaka 2008/09

"Mapinduzi ni Vita"

Mara nyingi neno Mapinduzi hutumiwa sana na watu wengi wanapotaka kufanya mabadiliko ya kitu fulani au jambo fulani. Watu wanapoingia kwenye mapambano ya aina yoyote hawachelei kusema kuwa tuko vitani. Maneno haya ukiyaunganisha na "ni" unapata sentensi inayosema "Mapinduzi ni Vita."

Nimeshasikia mara nyingi kutoka kwa viongozi wetu hapa nchini kuwa tunataka kufanya mapinduzi katika kilimo. Je, wanafahamu kuwa mapinduzi ni vita? Ni nilazima kujiandaa barabara, kwenye vita hakuna kurudi nyuma hadi ushindi upatikane. Makamanda je wapo? Makomandoo wa kilimo wapo? Ni kina nani hao? Tusipotambua hilo mapinduzi ya kilimo ni ndoto.