Friday, February 6, 2015
Tuesday, February 3, 2015
Tulichojifunza kutoka kwa wafugaji wa Amani - Muheza
Amani-Muheza ni sehemu nzuri ya milimani. Wananchi wa Amani wanategemea kilimo na ufugaji kwa maisha yao ya kila siku. Mazao ya chai na ndizi yanalimwa kwa wingi. Miti ya mdalasini,pilipili manga na hata karafuu inaoteshwa pia. Kikubwa kilichotupeleka Amani ni kuongea na kuona shughuli za ufugaji wa ng'ombe wa maziwa. Ni kweli, ufugaji wa ng'ombe wa maziwa unaendelea na baadhi ya wafugaji wamebahatika kupata mafunzo mbalimbali ya ufugaji bora wa ng'ombe wa maziwa kupitia miradi mbalimbali ukiwemo wa EAAPP. Manung'uniko ya wafugaji hawa ni soko la maziwa si la uhakika na bei yake ni ya chini mno. Lita moja ya maziwa huuzwa kwa bei ya shilingi 600. Vituo vya kukusanya maziwa viko mbali sana hivyo kumfanya mfugaji kutembea umbali mrefu kabla ya kuuza maziwa yake. Wakati mwingine maziwa huharibika na kumwagwa.
Ili kuwaandeleza wafugaji wa ng'ombe wa maziwa wa Amani, kuna haja ya kuboresha miundo mbinu ya barabara na kuongeza vituo vya kukusanyia maziwa. Ni vyema wafugaji wakapata bei nzuri ya maziwa yao. Timu yetu ilitoa ushauri kwa wafugaji wa kuboresha malisho ili kuongeza uzalishaji wa maziwa. Miradi mingine ya ufugaji itakayoanzishwa kuwasaidia wafugaji hao iangalie mambo hayo.
Fursa ya kuongea na wafugaji
Tulipopata nafasi ya kuongea na mfugaji Longido Shambakubwa wa Dakawa, Morogoro (mwenye suti) alionekana kujiamini na kuwa na uelewa mpana kuhusu ufugaji na kuwa na mipango endelevu. Kwa maneno yake mwenyewe, ujasiri huu ameupata kupitia mafunzo ya ufugaji wa ng'ombe wa maziwa pamoja na ziara za mafunzo ndani na nje ya nchi(Nairobi, Kenya) yaliyoandaliwa na Mradi wa EAAPP. Wakulima wakipata mafunzo pamoja na kuwatembelea wakulima wenzao wanabadilika haraka katika upokeaji wa teknolojia za kisasa za kilimo na ufugaji.
Mke anaposhiriki kwenye miradi ya familia
Mama Longido Shamba kubwa wa Dakawa-Morogoro akiwa ndani ya ghala la kisasa ya kuhifadhia vyakula vya mifugo. Kabla mumewe hajafika, mama huyu alitutembeza kwenye sehemu muhimu za shamba lao la mifugo na kuonekana kuwa na uelewa na kinachoendelea kwenye shamba lao. Kwa mawasiliano waliyoyafanya na mumewe mama huyu wa jamii ya Kimasai kwa ukarimu wa kipekee alituandalia maziwa ya kuchemsha pamoja na ya mgando. Mke anaposhiriki kwenye miradi ya familia inakuwa endelevu. Moja ya nguzo za utekelezaji wa Mradi wa EAAPP ni kuhakikisha kuwa masuala ya jinsia yanaangaliwa na kupenyezwa katika kutekeleza mradi kwa kufanya hivi familia hii bila kufahamu wanatekeleza masuala ya jinsia.
Monday, February 2, 2015
Kituo cha kuuza maziwa Bumbuli
Hiki ni moja ya vituo vya kununulia maziwa vilivyopo kwenye Halmashauri ya Bumbuli. Hifadhi ya maziwa ipo, maziwa huletwa kwenye vyombo safi. Kumbukumbu za maziwa kwa kila mfugaji hutunzwa ili kutoa malipo sahihi. Mfumo huu huendeshwa na vyama vya shirika vilivyopo katika Halmashauri hiyo. Maziwa yaliyochakachuliwa hayanunuliwi mara tu yanapobainika kutokana na vipimo vinavyotumika kupata maziwa safi na salama.
Wakulima wa Skimu ya Umwagiliaji ya Mlali-Morogoro
Hii ni skimu ya umwagiliaji ya Mlali mkoani Morogoro. Si mbali sana kutoka Chuo Kikuu cha Mzumbe. Wakulima wa Skimu hii wamepata mafunzo ya kilimo bora cha mpunga kutoka mradi wa wa EAAPP kuanzia mwaka 2012. Uzalishaji katika skimu hii sasa umeongezeka kutoka uzalishaji wa magunia 18 hadi kufikia 30 kwa ekari. Mwezi Januari ni wakati wa kaanda mashamba ndiyo hali tuliyoikuta kwenye skimu hiyo.
Kwa kupitia vyanzo vingine vya fedha, wakulima wa skimu ya Mlali wamejengewa ghala ya mazao. Hii itawasaidia wakulima kuhifadhi mazao yao na pia kuyauza kwa bei yenye faida.
Mkulima anayejiamini
Mwaka jana nilibahatika kuongea na wakulima wa mpunga katika skimu ya umwagiliaji ya Kamtonga wilayani Mvomero. Kilichonifurahisha ni kuona wakulima wengi vijana waume kwa wanawake wakijieleza kwa umakini mkubwa jinsi wanavyotumia teknolojia za kisasa za kilimo walizofundishwa kupitia mradi wa EAAPP kwa lengo la kuongeza uzalishaji na tija katika zao la mpunga. Bila kubabaika walisema kuwa mbegu ya mpunga TXD 306 (SARO) ni nzuri kwa uzalishaji ukilinganisha na mbegu nyingi za asili.
Mikocheni na 'mafuta mwali'
Kutokana na utafiti wa siku nyingi wa zao la mnazi, kituo cha utafiti cha Mikocheni kimeweza kutoa mafuta ya nazi yanayotumika kwa matumizi mbalimbali. Mafuta hayo yanajulikana kwa jina la 'mafuta mwali.' Mafuta haya yana manufaa mengi. Moja yanaongeza kinga ya mwili. Mafuta haya ni mazuri kupaka kwenye nywele hasa kwa watoto wadogo, yanasaidia pia kuyeyusha chakula kwenye mfumo wa chakula. Timu ya wataalamu wa kilimo na mifugo iliyotembelea kituo kidogo cha utafiti cha Chambezi kilichopo Bagamoyo iliweza kupata maelezo ya mafuta hayo na kila mmoja alinunua chupa moja ndogo kwa bei ya shilingi 10,000.
Subscribe to:
Posts (Atom)











