Friday, January 29, 2010

CAN2010 - Uzalendo?


Licha ya kuwa na vidonda kwenye paja lake lakini usiku wa Jana Andre Ayew alicheza kufa na kupona na kuisaidia timu yake ya Taifa ya Ghana (Black Stars) kuishinda Nigeria (Super Eagles) 1-0. Najiuliza uzalendo?

Ulaya wameanza kurudisha kwa umma huduma zilizobinafsishwa


Miaka ya 1980-90 wimbi la kubinafsisha huduma liliikumba karibu Ulaya yote. Kukiwa na dhana kuwa huduma ikitolewa na kampuni binfasi hutolewa kwa kiwango cha kuridhisha. Huduma kama vile za umeme, maji sasa zinaendeshwa na vyombo vya umma kama vile Halmashauri za miji au taasisi za kiserikali. Wakati Ulaya inabadilika hivyo sisi tunaendelea kubinafsisha karibu kila aina ya huduma. Tusimame na tuchunguze kwanza.

350 km kwa saa ndiyo garimoshi la china litakavyosafiri ifikapo mwaka 2011

Ah. Wakati mwendo wa gari moshi la kwetu ni km 35 kwa saa. China wataingiza garimoshi litakalosafiri kwa kasi ya kilometa 350 kwa saa. Hiyo ndiyo jeuri ya teknolojia. Huku sisi tukidharau Mchina bwana vitu vyake feki kabisa. Umeisoma hii?

Nyonya mwanangu


Mtoto wa kimasai akinyonyeshwa maziwa kutoka kwenye kibuyu. Wamasai ni kabila linaloenzi mila na tamaduni za kwao. Moja ya tamaduni hizo ni utumiaji wa maziwa. Tangu wakiwa wadogo wamasai hutumia maziwa kwa lishe kwas hali hiyo ni nadra sana kuwakuta watoto wa kimasai wenye utupiamlo. (Picha kwa hisani ya gazeti la DailyNews)

Kwa kandanda ya jana Misri wana nafasi kubwa yakuwa mabingwa ' AFCON'


Nimekuwa nikifuatilia mechi karibu zote walizocheza timu ya Misri 'Pharaos.' Kusema kweli ni wazuri. Kila idara imekamilika na wanacheza kitimu na mkakati wenye lengo. Wachezaji wanauwezo wa kumiliki mpira, kupiga chenga, kutoa pasi, mbio, stamina na mikikimiki ya mpira si haba wanaijua.

Kitendo cha kuidungua Algeria mabao 4-0 katika mchezo wa nusu fainali uliofanyika jana usiku nchini Angola katika kumtafuta bingwa wa 'AFCON' sio mchezo. Yameingia bila ubishi wowote. Pharao hawa wameshinda mechi zote tena wamezishinda timu ngumu. Timu tunazotegemea kutuwakilisha vizuri kwenye kombe la dunia ( wao hawamo). Kuna nini tena!
Kwa uwezo walionao shilingi yangu naiweka kwao. (Picha kwa hisani ya Website ya CAF)

HIVI NDIVYO GYAN ALIVYOSHANGILIA GOLI LAKE DHIDI YA NIGERIA


Wakicheza mpira wa kufundishwa na wenye mkakati wa ushindi, Ghana licha ya kuwa na wachezaji wengi majeruhi na vijana wameweza kuwaondosha wakongwe na jirani zao timu ya Super Eagels ya Nigeria kwa goli moja kwa nunge. Goli lililofungwa kwa kichwa katika dakika ya 20 na mshambuliaji hatari wa kimataifa Asomoah Gyan lilikuwa ni goli zuri.

Nigeria walijaribu kila njia kuweza kusawazisha matokeo na hatimaye kupata ushindi lakini pilika hizo zilitibuliwa na ngome imara ya Black Stars. Pengine wa kumlaumu zaidi ni Obafeni Martins wa Nigeria aliyekosa mabao mengi huku akitegemea zaidi guu lake la kushoto. Pichani Gyan akishangilia bao lake.(Picha kwa hisani ya Website ya CAF)

Thursday, January 28, 2010

KISE KIDS yaiparua Mpera 3-0


Magoli matatu yaliyofungwa katika kipindi cha pili yameiwezesha timu ya KISE KIDS inayoundwa na vijana wadogo wa kijiji cha Kisemvule kilichoko wilaya ya Mkuranga mkoa wa Pwani kuiliza timu ya Mpera. Mchezo huo ni moja ya mapambano ya ligi inayoendelea kijijini Kisemvule kwa sasa yenye lengo ya kumpata bingwa atakayezawadiwa zawadi kemkem na kutoa burudani kwa wakazi wa Kisemvule kijiji kinachokua kwa kasi katika kata ya Vikindu.

Akiongea na blog hii mwalimu wa soka wa timu hiyo Bw Abdallah Pembe amesema kuwa siri kubwa ya ushindi wa timu yake ni mazoezi pamoja na nidhamu. Mwenyekiti wa kijiji cha Kisemvule Bw. Shaaban Makuka ameahidi kuiwezesha timu hiyo ya vijana ili iweze kutoa wachezaji watakaounda timu ya kijiji cha KISEMVULE ambayo kwa siku za hivi karibuni imekuwa haisikiki sana.

Jumamosi iliyopita KISE KIDS a.k.a 'Watoto Wetu' iliwatoa kamasi baba zao -timu ya VETERANS kwa kuwafunga mabao 4-2 katika uwanja wa Kisemvule Magengeni.

Timu ya KISE KIDS imeanzishwa mapema mwaka huu na tayari imeshaanza kutoa upinzani mkali kijijini hapo na kuwa gumzo kwa wazee na vijana.

Hatuna mpango endelevu wa kudhibiti ombomba jijini


Hii ndiyo hali halisi. Ombaomba wanazidi kuongezeka jijini. Na si kweli kuwa wote wanaoomba ni walemavu hata kidogo. Wengi wamejenga tabia ya kuomba. Omba omba wamezagaa sehemu mbalimbali jijini hasa wilaya ya Ilala. Wanapatikana kwa winngi pale 'fire' na kisutu. Kibaya zaidi watoto wadogo hutumika katika shughuli hiyo ya kuomba huku wazazi (hasa kinamama) wakiweka makazi yao kandokando ya barabara. Hivi tumeshindwa kuandaa mpango endelevu wa kuwadhibiti ombaomba? (Picha kwa hisani ya gazeti la Mwananchi 28/1/2010)

Morogoro mkungu shilingi elfu 3 Dar ndizi 5 miatano


Licha ya kusafirisha mikungu yake ya ndizi hadi sokoni Morogoro. Mkulima huyu anauza mkungu mmoja kati ya shilingi 2,500 hadi 3,000/- Kwa bei hii lini ataweza kujenga nyumba bora ya kisasa na kuona kuwa kweli kilimo kinalipa? Bei ya bati moja ni shilingi 16,000/- (gauge 30) atahitaji kwa wastani mikungu saba aweze kununua bati hivyo kwa nyumba ndogo inayohitaji mabati 30 itabidi auze mikungu 180. Kutoka shamba la ukubwa upi na kwa muda gani? Kwa bei hii kweli kilimo kinalipa?

Mfanyabiashara jijini Dar huuza ndizi tano kwa shilingo 500 kwahiyo akiwa na ndizi 1000 tayari amekuwa ameshaingiza shilingi 100,000/- Tafakari.

Mizengo Pinda a.k.a Mtoto wa mkulima


Waziri Mkuu wa Serikali ya Muungano wa Tanzania Mhe. Mizengo Pinda tangu ashike madaraka hayo amekuwa mstari wa mbele kuinua uzalishaji wa kilimo. Ameshatembelea wakulima wengi shambani na taasisi nyingi zinazojishughulisha na kilimo. Nafikiri anaendelea kujifunza mengi kuhusu kinachosibu uzalishaji wa kilimo hapa nchini. Pinda sema kinachotakiwa kufanyika na kilimo kipewe kipaumbele katika kutengewa raslimali power tillers pekee haitoshi. (Picha kwa hisani ya gazeti la Mwananchi tarehe 28/1/2010)

Tuesday, January 26, 2010

Ukishindwa umejitakia mwenyewe


Mazingira mazuri kama haya si rahisi kushindwa mtihani. Vitabu vipo vya kutosha. Viti ni vizuri, meza kubwa na safi na watoto wenyewe ni wasafi. Kuinua kiwango cha elimu ni lazima serikali kuboresha shule zetu za msingi na sekondari zile tunazoita za kata ili wanaosoma shule binafsi watamani kusoma shule za kata. Hii inawezekana.

Uchaguzi una mambo eti Abood anasonga ugali!


Leo asubuhi nimeinyaka picha moja ya kejeli kwa waathirika wa mafuriko wilayani Kilosa. Picha hiyo yenye maelezo kuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, kutoka Mkoa wa Morogoro, Aziz Abood, akimsaidia kusonga ugali mmoja wa waathirika wa mafuriko... Hivi kweli kusonga ugali kunasaidia wahanga wa mafuriko au dhihaka tu. Hii ni mikikimikiki kuelekea uchaguzi 2010 tuwe macho na watu hawa. Morogoro fungueni macho mnawajua wa kuwachagua!

Huyu Mtikilla vipi?


Kila tunapokaribia uchguzi mkuu, Mchungaji Mtikilla haachi vituko na kashfa ambazo mara nyingi humfikisha mahakamani na kutumia muda mwingi mahubusu. Mimi simwelewi vizuri Mtikilla ana nini au ana lengo lipi?

Misri na Algeria wako mbali kisoka


Mimi ni mmoja wa mashabiki wa soka la kiarabu iwe Misri, Algeria, Tunisia na Morocco. Hawa jamaa wanajua mpira, wanacheza kwa malengo,uzalendo na wametulia. Wanajua sana kuusoma mchezo wa wapinzani wao.

Jana niliangalia kwa makini mchezo wa robo fainali kati ya Misri na Cameroon. Wamisri walishambuliwa sana, walianza kufungwa wao na kuelemewa na mipira mingi ya kona lakini walitulia na hatimaye kuweza kuifungisha virago Cameroon mabao 3-1.

Misri wanaye mwalimu wa siku nyingi mzalendo Hassan Shihata. Anawajua wachezaji wake anaongea kwa lugha moja isitoshe anaangaliwa vizuri! Watanzania tujifunze kutoka kwa waafrika hawa. Tusishabikie rangi ya ngozi wote tunacheza CAN na tupo barani Afrika! (Pichani-Zidan wa Misri akimtoka Alexander Song wa Cameroon - kwa hisani ya gazeti la mwananchi 26/1/2010)

Tatizo huzaa tatizo


Jumapili iliyopita niliweza kuhudhuria ibada takatifu katika Kanisa Katoliki Parokia ya Vikindu. Katika mahubiri yake Paroko Tom alitoa hadithi fupi kama ifuatavyo.

Siku mmoja mwanaume fulani aliyekuwa akiendesha gari lake alimkuta binti mrembo aliyemuomba msaada wa usafiri au 'lift' kama tulivyozoea. Bila kusita alimpa msaada huo binti huyo. Lakini mara alipoingia ndani bwana huyu alianza kujawa na wasiwasi, baada ya muda alipoangalia kiti alichokaa yule binti akaona kuwa amezirai! Bwana yule alijitahidi kumpeleka binti huyo hospitali iliyo karibu. Baada ya muda mrefu akapata habari kutoka kwa wauguzi inayompa hongera kwa kuwa baba!

Bwana yule alihamaki. Itakuwaje, yeye hamjui binti huyo. Alipoulizwa yule binti akasema haswa bwana yule ndiye baba wa mtoto. Haikuishia hapo polisi waliitwa na hatimaye bwana yule aliwekwa mahabusu kwa kosa la kufanya vurugu wakati alipokuwa akikataa kuwa si baba wa mtoto.

Shauri lilifikishwa mahakamani na ikaamuriwa kuwa bwana yule apimwe. Majibu yalipotoka iligundulika hana uwezo hata wa kuweza kuwa na mtoto. Bwana alifurahi kwani alishinda. Lakini akajiuliza sasa itakuwaje? Mbona nina watoto wawili niliyezaa na mke wangu wa ndoa. Alijiuliza? Alichanganyikiwa. Tatizo limezaa tatizo. Ni kweli kama binadamu hatuwezi kukwepa matatizo. Ubinadamu ni pamoja na kukabiliana na matatizo katika maisha yetu.(Picha kwa hisani ya gazeti la Mwananchi 26/1/2010)

Friday, January 15, 2010

Mafisadi endelezeni nchi basi

Tatizo si ufisadi, tatizo ni jinsi mafisadi wanavyotumia fedha hizo walizozipata kwa namna ambayo haisaidii nchi hii. "Hebu fikiria Banzi fisadi pamoja na kuchota fedha nyingi za nchi hii anaziweka kwenye benki ya nchi za nje, sasa hii inasaidia nini hata mwenyewe sidhani kama zinamsaidia sana.' Anahoji msomi kutoka moja ya vyuo vikuu hapa nchini ambaye amewahi kusoma darasa moja na Banzi wa Moro. Kuna mantiki hapo eh! Mwenzangu unayesoma blog hii unasemaje?

Tufanye kazi kama wanajeshi

Leo asubuhi wakati blog hii ikisafiri kuelekea Morogoro mjini ikitokea Kilosa. Ilikutana na msafara mkubwa wa magari ya Jeshi la Wananchi Tanzania. Nadhani yalikuwa yakielekea Kilosa kulikotokea maafa. Naambiwa kuwa wanaenda kujenga daraja lililoendolewa kwenye mto Mkondoa.

Jeshi limepokea agizo na tayari wameanza kutekeleza wana vifaa, wana watu na nina imani kuwa wataitekeleza kazi hiyo kwa muda mfupi sana. Blog hii inajiuliza hivi kwanini tusiwe kama wanajeshi katika kufanya kazi zetu?

Tuache kujenga nyumba za biskuti!

Nyumba nyingi zilizoanguka baada ya kukumbwa na mafuriko mjini Kilosa ni zile zilizojengwa mabondeni kwa matofali mabichi au zile zisizojengwa kwa msingi imara. Nyumba hizi wenyewe wanaziita biskuti. Kwani biskuti ikiwekwa maji tu huyeyuka. Ndivyo ilivyotokea Kilosa. Wengi wameachwa bila makazi. Hili ni fundisho kwa wote kuwa tunapojenga nyumba tujitahidi kujenga msingi imara ikiwezekana tujenge kwa mawe au matofali ya saruji.

Mafuriko yaliyoikumba Kilosa Kusini yanatisha

Ukitokea Mikumi na kuingia Kilosa mjini hutaamini macho yako, sehemu kubwa imetota maji, tope. Unapoingia mjini na kupita barabara ya kwenda Ilonga kwenye shule ya msingi Mazinyungu na hospitali ya wilaya ya Kilosa unaona makundi ya watu, vitanda viko nje, madirisha , milango, mabati huku makundi ya watoto wadogo wanacheza na mahema yamejengwa kuhifadhi waathirika na mafuriko. Ni simanzi kubwa sana. Mafuriko yamewafikisha hapo walipo kwa kipindi kifupi bila kutarajia.

Mji wa Kilosa umefurika watu wa aina mbalimbali ili kuweza kurekebisha mambo. Nyumba za wageni hazitoshi na hata huduma za chakula nazo hazikidhi haja. Haya ndiyo matokeo ya maafa. Kweli maafa ya Kilosa yanasikitisha. Yameathiri watoto, wakubwa wazee, wake kwa wakulima yamerudisha nyuma maendeleo yao.

Wengi hawakifahamu Chuo cha Taifa cha Sukari (NSTI)

Kwa kuwa kinajulikana kwa jina la Chuo cha Taifa cha Sukari wengi hufikiri kuwa chuo hicho hutoa mafunzo ya kutengeneza sukari tu. Hii si kweli. Blog hii ilipotembelea chuoni hapo hivi karibuni ilijionea mengi na kujifunza mengi.

Chuo cha Taifa cha Sukari (NSTI) kiko Ruaha karibu kabisa na kiwanda cha Sukari cha Kilombero (KI). Licha ya kutoa mafunzo ya aina mbalimbali na kuwa na miundo mbinu na mazingira ya kuvutia chuo hakifahamiki na wengi.

Baadhi ya mafunzo ya muda mfupi na muda mrefu yanayotolewa chuoni hapo ni pamoja na ufundi wa umeme wa majumbani na viwandani, utengenezaji wa kompyuta, ukarabati wa magari na utengenezaji wa vipuri vya aina mbalimbali pamoja na udereva. Mafunzo ya utengenezaji wa sukari unalenga mahitaji ya nyumbani au familia pamoja na viwandani. Chuo pia hutoa mafunzo ya kujifunza.

Tofauti na vyuo vingine chuo hicho hupokea hata wanafunzi waliomaliza darasa la saba kwani wanaamini na wanayo mifano ya wanafunzi waliopitia chuo hicho wakiwa na elimu ya darasa la saba na kufanya vizuri kuliko wale wa kidato cha nne au cha sita. Tukitafute na tuwapeleke vijana wetu NSTI-Kidatu.