Thursday, December 31, 2009

KWAHERI 2009 KARIBU 2010

Pamoja na changamoto nyingi zilizojitokeza kwa mwaka 2009. Namshukuru Mungu mwaka 2009 ulikuwa wa mafanikio kwangu. Nawashukuru wote walionisadia kufikia malengo yangu. Nawashukuru wote waliopata fursa ya kupitia blog hii. Shukurani za pekee zimwendee Prosper Bello aliyekuwa wa kwanza kufuatilia blog hii na kutoa maoni yake. Namshukuru pia mfuatiliaji wa pili aliyejitokeza mwaka huu ambaye ameonekana kuwa mfuatiliaji mzuri wa Banzi wa Moro (Haja taja jina). Ingawa nimeshindwa kufikia lengo la kuning'iniza vitu 365 lakini 250 nazo si haba nimevunja rekodi ya mwaka jana. Endapo Mungu akinijalia nikaweza kumiliki camera yangu mwenyewe naahidi kuwaletea vitu vizuri mwaka 2010. HAPPY NEW YEAR.

NAMSHUKURU MUNGU NIMEWEZA KUNING'INIZA MENGI KWENYE BANZI WA MORO


Pamoja na majukumu mengi na mapya niliyokuwa nayo mwaka 2009 lakini namshukuru Mungu nimeweza kuning'iniza mengi katika blog hii. Kuna wakati nilining'iniza chache sana hasa mwezi Novemba 7 tu. Sababu ni nyingi- mtandao kugoma, na kutingwa na shughuli za ofisi pamoja na misiba haya yalionifanya nishindwe kutuma mambo mtandaoni. Namshukuru Mungu

MWAKA 2009 NILIIKOSA XMASS YA MATOMBO

Nilipanga kwenda kijijini Matombo Morogoro kwa likizo ya muda mfupi kusherekea sikukuu ya XMASS mwaka huu ilishindikana kutokana na majukumu ya hapa kazini. Pengine hiki ni moja ya kitu nilichokikosa mwaka huu

Kila kifo ni cha ghafula-Sheikh Yahya

Mapema leo asubuhi nilikuwa nikitazama kipindi cha Jambo Tanzania kinachorushwa na TBC. Mmoja wa wageni waliokaribishwa katika kipindi hicho ni Mnajimu wa siku nyingi Afrika Mashariki na Kati Sheikh Yahya ambaye hivi karibuni utabiri wake uliodai kuwa atakayegombea nafasi ya Rais katika uchaguzi wa mwakani kumpinga Rais wa sasa Mhe. Jakaya Kikwete atakufa ghafla. Akionyesha uhodari wa kujenga na kutetea utabiri wake na hoja hiyo alisema kuwa wanadamu tusiogope kifo kwani kinapotokea kina faida na hasara. Kwa mfano ni pale tu mzazi anapofariki ndipo watoto wanapopata fursa ya kurithi mali za mzazi.

Samaki mkunje angali mbichi


Ni dhahiri mtoto huyu akiendelea kushirikishwa kazi za shamba na kukipenda kilimo tangu utoto wake hatochukia kilimo na hatochukia maisha ya shamba. Samaki mkunje angali mbichi.

TUTOKE HUKU


Vijiji vingi vya kiafrika haya ndiyo maisha ya wakulima.Usafiri wa shida, nyumba duni miundo mbinu ya kubahatisha. Lakini hebu angalia kwenye picha unavutiwa na rangi ya kijani ya uoto. Maana yake rutuba ipo. Je, wakulima wetu wataendelea kuishi kwenye mazingira haya mpaka lini? Hata, tutoke huku.

Simu inapotumika na mkulima kutika kupanga bei ya mazao shambani


Mwisho huu wa mwaka nawaletea picha iliyoshinda kwenye mashindano yaliyoendeshwa na jarida la kimataifa liitwalo 'Farming Matters.' Picha hii ni ya wakulima wa Phillipines maarufu kwa zao la mpunga. Mkulima anaweza kuwasiliana na mfanyabiashara kwa kutumia simu ya kiganjani kabla ya mavuno hivyo kuepukana na walanguzi kwani kwa kupitia simu majadiliano kuhusu bei hufanyika.

KAWAWA AMETUACHA


Simba wa Vita na mkongwe wa Siasa katika Historia ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Rashidi Mfaume Kawawa amefariki leo asubuhi. MUNGU ailaze mahali pema peponi roho ya Mzee wetu, Kiongozi wetu asiye na makuu Marehemu Kawawa.

Tuesday, December 29, 2009

Mifereji ya barabara ya Kilwa isilipuliwe

Kuna zoezi linalokwenda kwa kasi la kujenga mifereji kwenye barabara ya Kilwa. Naambiwa kuwa hilo lilikuwa ni agizo la Mhe. Waziri Mkuu, Mizengo Pinda aliyeagiza mamlaka husika kushughulikia mifereji hiyo haraka iwezekanavyo kuepusha hatari ya kuharibika barabara mpya iliyojengwa. Ninachoona mimi ni kuwa mifereji hiyo inajengwa haraka lakini si kwa kiwango kinachotakiwa. Ni kweli wajenzi ni wazawa. Lakini uzawa isiwe 'issue' ya kulipua kazi. Kwa maana nimeshaona baadhi ya maeneo mifereji imeshaanza kuchimbika kutokana na mvua hizi zinazonyeesha.

Dawasco bomba linavuja kituo cha Msikiti-Kilwa Road

Leo asubuhi wakati nikija kazini karibu kabisa ya kituo cha Msikiti mara baada ya kumaliza makaburi ya Mbagala Mission tulikuta maji ya kitiririka barabarani yakiashiria kuvuja kwa bomba. Hatari ni kwamba hali hiyo isipodhibitiwa haraka maji yatachimba barabara na hivyo magari kukwepa shimo hilo hatimaye kusababisha msongamano wa magari pengine hata ajali ndiyo maana nawakumbusha DAWASCO wafanye hima kurekebisha hali hiyo.

Garage za mtaa wa Mkumba-Wailes ni uchafu

Jana jioni wakati nikitoka kazini nilibahatika kupitia mtaa wa Mkumba uliopo Wailes-Temeke na kuona magari mabovu pande zote za barabara hiyo. Nilipojaribu kuuliza ni kwanini kuwepo kwa hali hiyo? Nikajibiwa aah mzee usishangae hizo ni garage za mitaani.

Hivi kweli watendaji wa Temeke mmerizika na hali hiyo? Jiji hili bado kunakuwa na garage za mitaani? Aah ondoeni uchafu huo haipendezi hata kidogo.

Monday, December 28, 2009

Yanga Imara bado


Gazeti la Yanga Imara halivutii hata kidogo. Ubora wa gazeti hili kuanzia karatasi zake, usanifu pamoja na habari zenyewe hazivutii hata chembe ni za kitoto mno. Hebu soma ukarasa wa mbele wa gazeti hili lililotoka leo kufuatia Yanga kutwaa ubingwa wa TUSKER CUP. Mwee kichefuchefu kabisa.

RUZUKU IPIMWE KWA UZALISHAJI


Yapata miaka mitatu sasa tangu serikali ianze utaratibu wa kutoa ruzuku ya pembejeo hasa mbolea kwa wakulima hapa nchini. Ruzuku hii hutolewa kwa mfumo wa vocha. Mfumo huu wa ruzuku kwa kutumia vocha unakuwaje hasa. Hapa kichafanyika ni kwa serikali kugharamia asilimia fulani ya gharama za pembejeo kwa mfumo wa vocha hivyo kumpunguzia makali ya uzalishaji mkulima. Mfumo huu ulipoanza ulikumbana na matatizo mengi kila mwaka maboresho yamekuwa yakifanywa ili ruzuku iweze kutoa matokeo yanayokusudiwa. Mimi naamini kuwa matokeo mazuri yatapatikana kwa kuongezeka uzalishaji na kuleta tija kwa wakulima.

SIKUKUU NI YA WATOTO


Hivi ndivyo ilivyokuwa kwa watoto hawa wa kijiji cha Kisemvule wilaya ya Mkuranga, Pwani walivyosherehekea sikukuu ya X-mass 2009. Wameulamba na kwa kweli wamependeza. Watoto walipiga picha hii baada ya kupata pilau nzito. Baadaye wakatafuna korosho na embe hii ndiyo raha ya pwani usipime mwanangu!

Friday, December 18, 2009

Ni kweli mazingira ya dhiki hayatakuza elimu


Wakati nakaribia kutoka ofisini siku ya Ijumaa. Kwa haraka nilipata kusoma kichwa cha habari kisemacho "Mazingira ya dhiki hayatakuza elimu" makala iliyoandikwa kwenye gazeti la Rai 17-23 2009. Kichwa cha habari hii kimenivutia kusoma makala hii iliyoandikwa na Masumbuko Nesphory. Serikali haitaki lawama na walimu nao hawataki kulaumiwa. "Tuache siasa tuache porojo katika elimu. Tusilaumiane tuwajibike." Anamaliza mwandishi wa makala hii. Mwandishi ameandika mengi kwa pande zote mbili. Ni kweli mazingira ya sasa ya kutoa elimu kwa shule za umma hayaridhishi. Tafuta gazeti hili na soma makala hiyo. Picha kushoto kwa hisani ya gazeti la Rai

Naambiwa hiki ni kijiji cha China


Miaka takribani ishirini iliyopita China ilikuwa ikidharaulika sana. Labda ilikuwa ikiogopwa kwa wingi wa watu wake na umahiri wao kwenye vita. Lakini nchi za magharibi iliiponda sana hasa kutokana na siasa yake Ujamaa.

Lakini sasa ni tishio. Waamerika wanaigwaya China. Kitu gani ambacho China hawawezi kukifanya. China wamebakia kuwa wajamaa huku wakiboresha maisha ya wananchi wao. Hebu angalia picha kushoto kwako, hicho ni kijiji mojawapo kilichopo China. Wanapanga na kutekeleza haya ndiyo maendeleo tunayotaka. Ubepari sawa lakini kwa faida ya nani? Ubepari huku tunashindwa kuzibua mitaro ya maji machafu? Ubepari huku tukishindwa kupaka rangi hata majengo ya umma?Ubepari wakati makao makuu ya nchi umeme kwa mgao?

Ziara za mafunzo kwa wakulima


Moja ya urithi alioucha marehemu mama yangu ni doti ya Khanga iliyoandikwa "Tembea Uone" Ni kweli mimi mwenyewe nimetembea na kuona mengi na kujifunza mengi na kuacha mengi.

Tunapotaka wakulima wajifunze teknolojia mpya moja ya mbinu zinazotumika ni kuwapatia ziara za mafunzo. Bado tunaamini kuwa "Tembea uone." Kwenye ziara hizi wakulima huona na kujifunza haraka. Wanaweza kujifunza jinsi ya kufuga kuku kutoka kwa wakulima wenzao kwa mazingira yanayofanana na ya kwao, jinsi ya kulima aina fulani ya zao kama vile nyanya, vitunguu n.k. kwa ufanisi zaidi. Wanajifunza pia jinsi wakulima wanavyoweza kujenga nyumba nzuri kwa kutumia raslimali walizonazo. Wanaweza kujifunza pia kumbe hata mkulima wa embe anaweza kumiliki gari!
Ukiona huwezi kusahau kwa urahisi. Nahitimisha kwa kusema kuwa ziara za mafunzo kwa wakulima ni muhimu. Pichani wakulima wakiwa katika ziara ya mafunzo wakionyeshwa namna ya kuchota maji kwa ajili ya umwagiliaji toka kwenye kisima nyumbani kwake huko Ibumila Njombe.

Ungefuga kuku wa kienyeji


Sikukuu ya X-MASS na mwaka mpya inakaribia. Ni wazi kuwa bei ya nyama itaongezeka hata mara mbili. Familia nyingi hazitoweza kumudu kula nyama. Nyama ya kuku ndo usiombe kabisa nafikiri X-mass hii kuku atauzwa kuanzia shilingi 10,000 hadi 20,000/- Lakini mwananchi naomba nikuulize utashindwa kweli kufuga kuku wawili au watatu kwenye kibanda kidogo kwa mfumon huria? Mimi naamini ungefuga kuku wa kienyeji usingetaabika na kitoweo wakati wa sherehe hizi zinazokaribia tubadilike tuanze kufuga sasa kwa ajili ya Pasaka na Idd-Elftri ya mwakani.

Tuwasikilize wakulima kuhusu mfumo wa stakabadhi ghalani


Nimewasikia wakulima wakilalamika kuhusu mfumo wa kuuza mazao wa stakabadhi ghalani. Pengine wazo ni zuri lakini utaratibu uliopo wa kuwezesha mfumo huo kufanya kazi haujakaa sawa. Nikiwa kwenye gari dogo la abiria likitokea Mkuranga kwenda Mbagala Rangi tatu mama mmoja alikuwa akiulalamikia mfumo huo kwa zao la korosho. Fedha wanazolipwa mara tu wanapouza korosho ni kidogo aidha malipo yaliyosalia hayajulikani yatalipwa lini. Kwa maoni yake anaona heri korosho zao zingenunuliwa na wafanyabiashara wa kujitegemea kuliko vyama vya ushirika. Kwa hili tuwasikilize wakulima na penye dosari turekebishe.

TUSIDHARAU KAULI WANAZOTOA VIONGOZI WA DINI


Hivi karibuni gazeti moja litolewalo kila siku hapa nchini liliandika kuwa "KILIMO KWANZA NI WIMBO TU" kauli hii imetolewa na Mhashamu Kardinali Polycarp Pengo kiongozi wa Wakatoliki hapa nchini.

Tulio wataalamu wa Kilimo tusibeze kauli hii eti kwa kuwa sisi na watu wa kilimo au kuona kuwa Pengo hakipi umuhimu KILIMO. Viongozi nan wataalamu tujiulize kipi kifanyike ili kweli KILIMO KIONEKANE KUWA KWANZA hapa nchini. Tuone mabadiliko kwenye sekta hiyo kuanzia kwenye kupanga raslimali na utekelezaji wake vinginevyo inawezekana kabisa kuwa WIMBO TU. Kwa maoni yangu huenda viongozi wa dini wako sahihi. Hawa wako karibu sana na wananchi na wananchi huwa huru kueleza hisia zao kwa viongozi wa dini.

Wednesday, December 16, 2009

Kwanini Benki Kuu?


Leo hii kuna habari nyeti kwenye gazeti la Rai Mwema Desemba 16-Desemba 22,2009 inayosema "Ulaji wa Vigogo wa BoT wahojiwa." Ninachohoji mimi ni kwanini wafanyakazi wa Benki Kuu wanapewa kipaumbele katika maslahi? Mishahara yao ni ya Juu. Bado wanapewa motisha wa kukopa kiasi kikubwa cha fedha. Na inawezekana kabisa bila riba. Ikiwa mfanyakazi wa chini kiwango cha kukopa ni milioni 30 Mungu akupe nini. Kuna haja gani ya kusoma hesabu au fizikia nchi hii ikiwa kwa kuwa muhudumu wa ofisi tu Benki unalipwa mshahara mkubwa kuliko Mhandisi au Bwanashamba?

Hivi karibuni Rais Jakaya Mrisho Kikwete alitoa agizo kwa watafiti wa sekta ya kilimo kuongezewa mishahara yao kutokana na kazi nzuri wanayoifanya katika sekta hiyo. Hadi leo agizo halijatekelezwa. Kwa hali hii nani afanye kazi sekta ya kilimo. Watoto wetu watakimbilia sekta nyingine hasa za fedha. Tuangalie hili. Picha kushoto Prof.Beno Ndulu, Gavana wa Benki Kuu Tanzania.

Jamani eh Maximo kichwa ngumu tuachane naye


Karibu miaka mitano sasa. Sioni la kushangaza kutoka kwa Maximo kwa timu yetu ya Soka ya Taifa. Nionacho mimi ni kutuchanganya tu. Tunaishi kwa matumaini kuwa iko siku. Siku iko wapi wakati kila siku anaunda timu ya Taifa. Kocha mwenye kinyongo kwa baadhi ya wachezaji, kocha asiyejua lugha yetu ya Taifa kweli huyu ni kocha? Tuachane naye. Kiasi anacholipwa Maximo hata kama nusu yake angalipwa Mziray, Kibadeni, Mkwasa, au Kayuni timu ingefanya vizuri tu. Timu inapata misaad ya nguvu kutoka kwa NMB, Serengeti na wadau wengine lakini upangaji mbovu wa timu ndo unaoiua Taifa na Kilimanjaro Stars

TUACHE MALUMBANO YASIYO NA MSINGI TUJENGE NCHI

Kwa muda mrefu sasa kumekuwa na malumbano yasiyo kwisha kwa viongozi wa vyama vya siasa wakituhumiana kama watoto wadogo. Huyu akimwambia mwenzake hana elimu, mwingine akimweleza mwenzie hana busara. Na hawa wote ni watu wakubwa kwenye vyama vyao. Wakati wananchi wengine wakihangaika jinsi ya kupata riziki tena kwa shida kubwa. Wakubwa hawa wako kwenye malumbano tena kwa faida yao. Watoto wetu wanapata elimu duni, hospitali za umma bado ni dhaifu kwa huduma zinazotolewa, miundo mbinu bado ni duni. Wananchi wananyonywa vibaya kupitia simu za mkononi, miji yetu ni michafu hasa Dar.Tuache malumbano tujenge nchi yetu.

Sunday, December 13, 2009

Kutemewa mate ni dharau

Mtu anapokutumea mate ni dharau. Huyu Mkanada aliyemtemea mate askari wetu wa barabarani pamoja na mwandishi wetu wa habari Jerry Muro amefanya dharau kubwa kwa nchi hii. Kwa maoni yangu wazungu walio wengi wanatudharau sana sisi waafrika hata ukitembelea nchi zao utaona kabisa dharau machoni mwao. Kama kicheko basi ni cha kejeri. Pamoja na kuwa aliyefanya kitendo hicho ni mfanyakazi wa balozi hiyo, naomba serikali yetu iwe na msimamo kwa hili wasituchezee.

Do value chains help farmers out of poverty?


While reading a journal titled-KILIMO endelevu Africa Vol 1 issue 1 July 2009 I came across on a debate titled above-in summary the issue is- "does an emphasis on value chain development indeed lead to farmers becoming more entrepreneurial And is it the key to poverty reduction in rural areas?" Please kindly discuss. Karibuni.

Kipi kinachoitangaza Tanzania?

Elimu ya msingi, wanafunzi 50% hawakufaulu mtihani wa darasa la saba mwaka huu. Jiji la Dar Es Salaam ni chafu. Uzalishaji katika kilimo bado ni wa chini. Miundo mbinu ni ya ubabaishaji. Umeme si wa uhakika. Maji ni kwa mgao. Michezo- Mpira wa mguu timu ya Taifa haijafanikiwa kupata ushindi na kutwaa kikombe kwa muda mrefu. Madini ndo tunaambulia athari za kuharibika kwa mazingira pamojan na wananchi kupata vilema badala ya kuwa matajari. Hivi Tanzania ukiondoa amani na usalama tuna lipi la kujivunia. Hata usafi tu ni issue! Mwe!

Kuwasimamisha MAJEMBE ni kupunguza kasi ya mabadiliko

Kwa kawaida binadamu hapendi mabadiliko. Hasa mabadiliko HASI. Hivi karibuni uongozi wa JIJI la Dar Es Salaam waliamua kuwatumia MAJEMBE Auction Mart kudhibiti hali mbaya ya usafiri hapa jijini wakisaidina na Traffic Police. Zoezi hilo halikudumu kwa muda mrefu baada ya wamiliki wa mabus kutishia kugoma (hasa kwa njia ya TABATA waligoma). Hatimaye kuufanya uongozi wa mkoa wa Dar Es Salaam kusitisha zoezi hilo. Jamani tusiogope mabadiliko tuyafanyie kazi na tutazoea tu. Kwa kawaida binadamu hapendelei mabadiliko HASI.

HONGERA JKT

Kama kuna jeshi lililoonyesha ukakamavu wa hali ya juu na kushangiliwa na maelfu ya wananchi waliokuwepo uwanja wa UHURU tarehe 9 Desemba wakati wa kusherehekea miaka 48 ya UHURU ni JKT. Walipendeza kwa sare, ukakamavu na kuwajibika pamoja na kufurahisha. HONGERA SANA JKT

Mawaziri kupanda waingia uwanjani kwa mabus miaka 48 ya UHURU

Nilikuwepo uwanja wa UHURU kwenye sherehe za miaka 48 ya Uhuru. Kwanza nikiri kuwa hii ni mara yangu ya kwanza kuhudhuria sherehe za uhuru katika uwanja wa UHURU. Pamoja na viburudisho vya ngoma za kitamaduni kutoka hapa nyumbani na nchini Uganda (Kikundi cha NDERE) na gwaride la vikosi vya majeshi ya polisi,jwtz, magereza,jkt + Halaiki ya wanafunzi. Kipya ni Mawaziri, Mabalozi, Wakurugenzi kuingia uwanjani na mabus ya kukodi. Naambiwa magari yao waliyaacha KARIMJEE! Hivi hili waandishi hawakuliona?

Tuesday, November 24, 2009

Maalim Seif na Karume kukubaliana kuachana na uhasama ni uamuzi wa kihistoria

Jambo la msingi katika maisha ni kuondoa tofauti inayoleta misuguano katika jamii inayosababisha kudumaa kwa maendeleo. Msuguano uliokuwepo kati ya vyama vikuu vya siasa visiwani Zanzibar (CCM na CUF) umeleta athari kubwa katika jamii. Baya zaidi watu wamepoteza uhai kwa msuguano huu tena raia wa kawaida kabisa huku wakiwaacha viongozi wakuu wa vyama wakidunda!

Kitendo cha viongozi wa vyama hivyo huko Zanzibar kukubaliana kuachana na uhasama na kuijenga Zanzibar ni kitendo cha AFYA. Nawapongeza sana.

Falsafa ya 'Zee la Nyeti'

Kama anaandika lugha ya kihuni, kama vile mtoto wa mijini. Lakini ndivyo mwandishi Henry Mdimu (Zee la Nyeti) anavyofikisha ujumbe wake kwa jamii kupitia gazeti la Mwananchi kila Jumamosi katika kurasa za starehe.

Blog hii imevutiwa sana na makala hizo na leo imebidi kuwafahamisha wasomaji wake ni vizuri ukalipata gazeti la Mwananchi la kila Jumamosi uweze kusoma falsafa ya Zee la Nyeti. Makala za Mdimu zina ujumbe mzito hasa kwa vijana. Lugha anayoitumia kufikisha ujumbe ni ile wanayoitumia vijana kwa hiyo haichoshi. Kwa mfano Jumamosi iliyopita kulikwa na kichwa cha habari kinachosmea 'Ngoma haipigwi kwa nyundo'.....hivi watu mkisikia mdundo wa ngoma mnafikiri ngoma huwa inapigwa kwa nyundo? Vijifimbo viwili tu, au samtaimz mkono wako tu...

Tarehe 31/10/2009. Mdimu alishuka na makala inayosema 'Ukiona manyoya...ujue keshaliwa' simulizi iliendelea hivi.....alipoingia tu anakutana na viata vya jmaa, saa iko mezani na kama nguo anazozijua hivi?.....ukiona unyayo si unajua kabisa kama kuna mtu kapita? .......Maana afadhali uone unyayo kuna siku utakuta manyoya, na itabidi ukubali...kwamba kuku keshaliwa.

Big Up Henry Blog hii imezikubali makala zako.

Tuesday, November 3, 2009

Vijana wanapaswa kutekeleza kauli mbiu ya KILIMO KWANZA


Ukitembelea katika vijiji vingi hapa nchini hutoshangaa kukuta washiriki wakuu wa kilimo ni wazee. Vijana walio wengi hawajihusishi kabisa na kilimo. Ukiwauliza wanazo sababu nyingi za kutojihusisha na kilimo zilizo nyingi si za msingi. Wakati Taifa linajipanga katika kuitikia kauli mbiu ya KILIMO KWANZA vyema vijana wakaandaliwa ili waifahamu vizuri kauli mbiu hiyo kwa kuwa tayari kwa utekelezaji wake. Kwa hiyo mafunzo mafupi ya uzalishaji wa kilimo yakiandaliwa kwa vijana wetu yatasaidia sana kuboresha uzalishaji wa kilimo. Kilimo kikiachiwa wazee kitakufa.

Tunapoteza shilingi milioni 28 za wakulima kama mchezo


Nimesikitishwa kusoma habari iliyoandikwa kwenye gazeti la Mtanzania la tarehe 2/11/2009 kuwa kiwanda cha sukari cha Ilovo kilichopo Kilombero kimetelekeza miwa ya wanachama 27 wa Chama cha Wakulima wa Miwa katika bonde la Kiliombero yenye thamanin ya shilingi ya Tanzania milioni 28. Habari hii imenistua kwa kweli, kwa umaskini walionao wakulima wetu kupoteza kiasi hicho cha fedha si jambo dogo hata kidogo. Si fahamu ni sababu zipi zilizopelekea uongozi wa kiwanda hicho kukataa miwa hiyo.

Usichelewe kusajili sim card yako


Makampuni ya simu yanayotoa huduma hapa nchini yanaendelea na zoezi la kusajili simu card kwa wateja wake. Blog hii imeshasajili simu card zake za Zain na Vodacom siku ya Jumapili. Zain hawana mlolongo mrefu wa mambo katika kusajili.Tatizo liko kwa Tigo inabidi usote katika foleni. Vipi Tigo ndo tuseme mnawateja wengi? Mimi siamini hata kidogo, hebu boresheni huduma zenu. Banzi wa Moro bado hajasajili simu card yake ya Tigo.

JK amepania kuinua utafiti nchini


Gazeti la Habari leo la tarehe 2 Novemba 2009 limeandika kuwa Rais wa Jamhuri ya Tanzania Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete ameahidi kutoa Tzs milioni 40 kwa ajili ya utafiti wa tufaa (apples) katika kituo cha Utafiti Uyole, Mbeya.

Ni hivi karibuni nimekuwa nikijiuliza kuwa kwanini biashara ya tufaa inaongezeka katika miji yetu wakati sioni wakulima wanaozalisha matunda haya hapa nchini. Jibu ni kwamba tofaa huagizwa kutoka Afrika ya Kusini.

Tanzania zipo sehemu ambazo tofaa zinaweza kuzalishwa kutokana na hali ya hewa ya maeneo hayo sehemu kama vile Lushoto (Tanga), Mgeta (Morogoro) na Mbeya. Iwapo utafiti wa kina utafanyika na kuweza kupata mbegu zinazoweza kustawishwa katika sehemu hizo kutakuwa hakuna sababu tena ya kuagiza tufaa kutoka nje ya nchi, kwahiyo auamuzi wa Mhe. Rais kutoa fedha hizo za utafiti ni chanzo cha kuanza kuzalisha tufaa bora hapa nchini.

HONGERA SIMBA SPORTS CLUB


Mimi ni shabiki wa Club ya Simba au Wekundu wa Msimbazi. Nawapa hongera nyingi wachezaji, coach na viongozi wa klabu kwa ushirikiano mliouonyesha hadi kufanikiwa kuwashinda wapinzani wetu wa jadi Dar Young Africans kwa goli 1-0 uwanja wa Taifa Dar Es Salaam. Mgosi nakupa shavu mdogo wangu!

Saturday, October 24, 2009

Hawakujiandikisha kwasababu mambo ni yaleyale


Uchaguzi wa viongozi wa Serikali za mtaa na vijiji unatarajiwa kufanyika kesho. Wananchi wengi inasemekana kuwa hawakujiandikisha. Ni kweli, Banzi wa Moro katika pitapita yake mjini na vijijini amegundua kuwa watu wamekata tamaa na uongozi wa vijiji na mitaa kwani kasi ya maendeleo hasa huko vijijini ni kidogo sana. Mambo ni yale yale. Viongozi wanaomba nafasi hizo kwa manufaa yao binafsi na wala si ya wananchi. Utasikia ah nikipata nafasi hii baada ya muda wangu wa uongozi kumalizika lazima ninunue 'daladala.'Hivi ndiyo lengo kweli la kugombania uongozi ? Wakati wa kampeni nimeshuhudia vibweka vingi kwa vyama vyote wakishindana kwa rusha roho! Hivi kweli kuna lolote hapa? Ndo maana wengi hawajajiandikisha! (Picha kwa hisani ya gazeti la mwananchi tarehe 24 Oktoba 2009)

Tuesday, October 13, 2009

Mchicha upo wanunuzi je?


Vijana hawa wameamua kuuza mazao ya kilimo hasa mbogamboga. Lakini, wanunuzi wako wapi? Ona mchicha umeanza kunyauka!

Mbuzi wanauzwa


Kama utatembelea 'Kiembe Mbuzi'- Vingunguti na kukuta mbuzi wa aina hii wanauzwa sidhani kama utasita kununua na sifikirii kwamba utampata kwa bei poa. Je, mbuzi wa aina hii wanaweza kupatikana hapa nchini? Fika katika Taasisi ya Utafiti wa Mifugo ya Taifa - Mpwapwa utapata jibu na utaanza kufuga na kuuza mbuzi.

Mtafiti wa Kilimo inaijua Bodi ya Utendaji ya FARA na sekretariati yake?


Kama umeshafika Accra Ghana na kama wewe ni mtafiti wa kilimo lazima utakuwa umefika kwenye makao makuu ya FARA (Forum for Agricultural Research in Africa)- Ni mkono wa kiufundi wa AU katika masuala ya uendelezaji Kilimo na Uchumi wa vijijini katika Bara la Afrika. Pichani ni Bodi ya Utendaji na Sekretariati ya FARA.

Hana uhakika wa soko


Mwangalie msichana huyu anatembeza mboga kwa wateja. Tatizo ni moja je atauza? Upatikanaji wa soko la uhakika kwa mazao ya kilimo ni tatizo linalorudisha nyuma maendeleo ya kilimo barani Afrika na kusababisha wakulima wasipokee kwa urahisi teknolojia bora za uzalishaji.

Vichwa vya Kilimo Afrika


Afrika hatujapiga hatua kubwa katika kilimo. Uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara bado ni mdogo sana. Mazao yatokanayo na mifugo nayo ni haba na duni. Matokeo yake njaa inapiga hodi kwenye bara hili. Hata viwanda vinavyohitaji mali ghafi kutokana na kilimo havitoshelezwi. Hata hivyo kuna vichwa vinavyokuna ubongo kuhakikisha kuwa Afrika inapata teknolojia bora zitakazosaidia kuinua uzalishaji katika kilimo. Angalia vichwa hivyo katika picha.

Mafuta kwenye mahindi tumekwisha!


Wakati wananchi wetu wanahangaika kupata mlo. Wenzetu wako 'busy' kupata mafuta yakuendeshea mitambo kutoka mimea kama vile mahindi. Hii maana yake nini hasa? Chakula kwao kinatosheleza ila wana wasiwasi wa nishati! Upuuzi mtupu. Hivi kweli unaweza kuendesha gari kama una njaa? Watanzania lazima tuangalie suala la nishati na chakula kwa uangalifu mkubwa na kutoa kipaumbele kinachostahili tuwe makini na sera ztu vinginevyo tumekwisha.

Saturday, October 10, 2009

Raphael Benitez wa Liverpool


Mmoja wa makocha wanaojiamini katika Ligi Kuu ya Uingereza ni Raphael Benitez wa Liverpool. Hebu angalia mbwembwe za Benitez pichani. Lakini Banzi wa Moro anaipenda sana timu ya Liverpool kwa sababu gani? Wachezaji wake wanajituma sana hasa Stephen Gerald - The Captain. Lakini zaidi ya hilo nyuzi zao kama wekundu wa Msimbazi!

Hakika Makamu wa Rais ni mfano wa kuigwa


Hivi karibuni nimekuwa nikifuatilia habari za Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt Ali Mohamed Shein kwa karibu sana. Katika safari zake karibu zote iwe za kikazi au binafsi ndani na nje ya nchi yeye huambatana na mkewe Mama Mwanamwema Shein. Tarehe 8/10/2009 alifika katika kituo cha Shule ya Msingi Oysterbay, Dar Es Salaam kwa kusudi la kujiandikisha katika Daftari la wapiga kura, hebu check kushoto kwake ameambatana na nani? (Pichani kwa hisani ya gazeti la Majira).

Wanasoma wajipatie maarifa


Kuna ushahidi wa kutosha kuwa Watanzania wengi hatuna utamaduni wa kusoma. Kusoma kunakupatia maarifa, kunaburudisha na unapata taarifa mablimbali nzuri na mbaya. Tuanze sasa kusoma, tuanze kwenye familia kama inavyoonekana familia hii pichani

Kila mmoja na kuku wake


Wengi hupenda kula nyama ya kuku. Hasa vijana wanapopata 'offer' ukiwauliza utakula nini utasikia - Chips kuku. Lakini kwanini tusifuge kuku majumbani kwetu. Sisemi kuku wa kisasa la hasha hawa hawa tuliowazoea. Labda niseme kuku wa asili. Angalia familia hii pichani ilivyofanikiwa kufuga kuku wengi wa asili mpaka raha kila mmoja na kuku wake. Kila mmoja anatabasamu. Picha kwa hisani ya jarida la KILIMO endelevu Africa.

Wanashangaa maembe!


Ndiyo wanashangaa maembe. Haiwezekani mti mdogo ukazaa maembe kama yanavyoonekana pichani, tena chini chini kabisa. Usibishe. Kuna aina mbalimbali za maembe ambazo huzaa wakati ina kimo kifupi sana. Hii ni baadhi ya teknolojia za kisasa za kilimo za kuzalisha matunda. Ukitaka maelezo zaidi wasiliana na bwanashamba aliye karibu nawe, ofisi za kilimo au vituo vya utafiti.

Wakati wa Ujana wangu



UJANA mali waswahili wanasema. Wakati wa ujana wangu nilikuwa na nguvu na kufanya mambo mengi. Muda mwingi niliutumia kujipatia elimu ndani na nje ya nchi. Wakati mwingine nilikuwa najirusha kwa sana tu hasa DISCO ah nilipenda sana mziki. Nakumbuka miaka ya themanini mimi na ndugu yangu Lawrence Mkude (Sasa Afisa Utumishi Bandari) Silversands kila w-end. Namkumbuka sana DJ. John Peter Pantalakis na HOLLIDAY!

Friday, October 2, 2009

Utafiti shirikishi


Utafiti wa kitu chochote kile ni vizuri ikishirikisha wadau wengi. Pichani wakulima wanawake wakitafiti aina bora ya mpunga. Utafiti huu unajulikana kama utafiti shirikishi. Utafiti wa aina hii hutoa matokeo mazuri yanayokubaliwa na wadau.

Ninatubu Lema Baba shirikishi


Sherehe za kuwaaga wastaafu wa Idara ya Utafiti na Maendeleo ziliratibiwa na Mtafiti Mkuu Bw.Ninatubu Lema (a.k.a Baba Shirikishi). Pichani akipitia kwa makini ratiba ya sherehe.

Baada ya yote ni kulisakata rumba!


Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika Bi Sophia Kaduma akifungua dansi la kuwaaga wastaafu wa Idara ya Utafiti na Maendeleo mwaka 2008/09

Viongozi na wastaafu


Wamestaafu wakiwa wana nguvu na hekima tele. Pichani wastaafu pamoja na viongozi wa Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika katika picha ya pamoja. Watano kutoka kushoto waliosimama ni Bw. Ahmed J.Ahmed (a.k.a Kaka Ahmed) aliyekuwa mkuu wa kitengo cha mipango cha Idara (PEU).

Wawaaa Mama Beatrice Gembe!




Inapotokea shughuli na mwana mama akiwa mmojawapo kati ya wahusika wa shughuli hiyo basi ujue akina mama wenzie watamtunza tu. Ndivyo ilivyotokea kwenye hafla ya tarehe 3/7/2009 kina mama wafanyakazi wa Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika walimzawadiwa mstaafu Mama Beatrice Gembe (aliyekumbatiwa na kutabasamu) aliyekuwa PS wa Mkurugenzi wa Idara ya Utafiti na Maendeleo zawadi mbalimbali. Hebu angalia chereko chereko. Inapendeza enh!

Mwanzo 3 alisherehesha


Wafanyakazi wa Idara ya Utafiti na Maendeleo wanamfahamu Paul Masanja Ndondi (Mwanzo 3) kwa uchangamfu wake na kwa kuchapa kazi katika mazingira tofauti. Huyu amesafiri sehemu nyingi ndani na nje ya nchi na kujifunza mengi. Pichani Mwanzo 3 akisherehesha hafla ya watafiti wastaafu kwenye viwanja vya KILIMO 2.

Sisi tupo


Wakati watafiti wastaafu wakiagwa waliokuwa vijana miaka 10 iliyopita bado wapo. Pichani kutoka kulia Bi Eva Kanyeka, Smwel Undule, Deogratias Lwezaura na John Banzi wakisikiliza kwa makini wosia wa wastaafu.

Hongera Dkt. Haki


Ndivyo inavyoonekana pichani. Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika Bi. Sophia Kaduma akimpongeza na kumkabidhi Mkurugenzi mstaafu wa Idara ya Utafiti na Maendeleo Dkt. Jeremiah Haki. Katika hafla fupi ya kuwaaga wastaafu wa mwaka 2008/09 kutoka Idara ya Utafiti na Maendeleo. Dkt. Haki ameiongoza Idara hiyo kwa mafanikio makubwa takribani kwa miaka 10. Tafrija hiyo ilifanyika tarehe 3/07/2009 kwenye viwanja vya Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika - KILIMO II.

Nampigia debe mrembo wa Moro 2009


Yehu! Kinyang'anyiro cha Miss Tanzania ni leo katika Ukumbi wa Mlimani City -Dar es Salaam. Mshindi ataibuka na gari aina ya Suzuki Vitara pamoja na fedha taslimu 9m/=. Banzi wa Moro anampigia chapuo mrembo wa Moro Bi Tory Oscar. Tuvute subira macho yetu wote luningani. TBC Live mwanawane!

Huyu ndiye Dkt Alfred Moshi wa mahindi


Wadau wa Kilimo hapa nchini hasa wa kanda ya Mashariki unapozungumzia mahindi basi akilini mwao unamzungumzia Dkt. Alfred Moshi aliyekuwa Mkurugenzi wa Utafiti Kanda ya Mashariki. Moshi kwa muda mwingi amekuwa akitafiti mbegu bora ya zao la mahindi. Pichani Dkt Moshi akitoa neno kwa niaba ya watafiti waliostaafu mwaka 2008/09 kwenye viwanja vya Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika - Kilimo II kwenye tafrija ya kuwaaga waliyoandaliwa na Idara ya Utafiti na Maendeleo tarehe 3/07/2009

MORO - Neema ya vyakula


Mkoa wa Morogoro ni mmoja ya mikoa iliyobarikiwa kuwa na mazingira mazuri kwa kuzalisha mazao mbalimbali ya chakula. Hivi karibuni Makamu wa Rais Mh. Dkt.Ali Shein alitembelea kijiji cha Lupilo, Mahenge mkoani Morogoro. Angalia karanga, viazi mviringo, vitungu saumu na maji pamoja na nyanya vilivyojaa sokoni bwelele!

Makwaia wa Kuhenga


Ni mwandishi mwandamizi hapa nchini. Kalamu yake imefichua mengi na kuyaweka bayana. Ni mjuzi wa lugha pia ni mcheshi katika maisha ya kawaida. Huyu ni Makwaia wa Kuhenga. Nimemfahamu mwandishi huyu tangu miaka ya 80 na hadi leo ninapoona makala zake huwa nazikimbilia kuzisoma kwani hufanya uchambuzi wa kina.

Thursday, October 1, 2009

Dr. Shao - kama FORM VI vile!


Dr.Frank Shao ni mmoja ya Wakurugenzi waliopata kuongoza Idara ya Utafiti na Maendeleo. Miaka zaidi ya kumi sasa tangu astaafu lakini yu na afya na nguvu tele. Muulize Dr. Shao atakwambi ni nidhamu ya maisha na kuwa na kiasi. Angalia kinywaji anachokunywa- MAJI. Hapa alikuwa mwalikwa kwenye tafrija ya kuwaaga wastaafu wa Idara ya Utafiti na Maendeleo mwaka 2008/09