Tuesday, September 11, 2007

HAMKUJUA KAMA NI MHINDI?

Mengi yamesemwa kuhusu Mshindi wa Miss Tanzania wa mwaka huu. Wengine wanalalamika eti kwanini mshindi amekuwa Mhindi? Jamani, huyu Mhindi ametokea mbali katika Kinyanga'anyiro hiki nafikiri kutoka Mtaa hadi pale wilayani Kinondoni. Wakati anashinda pale Kinondoni hakuwa Mhindi? Je, Richa Aidha alipokuwa Miss Earth 2000 kule Phillipines hakuwa mhindi? Miss Indian Ocean 2006 hakuwa mhindi ?Watanzania acheni ubabaishaji.

Mimi siyo mfuatiliaji mzuri wa mashindano haya kwani nayaona ni ya kibabaishaji. Tunaigaiga tu mamabo bila kufahamu jinsi yanavyoendeshwa. Ndo maana akipatikana mshindi Mhindi tunaanza kulalamika lakini huko tunakokwenda tunawata wahindi, waingereza, warusi, wajapani sasa cha ajabu kipi. Vigezo vilivyowekwa ni vya kimataifa. Si vya Kiluguru (kucheza ngoma), Kichagga (kukatiakatia majani ng'ombe) kizaramo (shughuli)................

Kama uwezo wa Richa wa kuongea Kiingereza ni mkubwa kuliko wengine kwanini wengine wasiongea lugha wanayoifahamu vizuri (kiswahili). Sote tunafahamu tulio wengi uwezo wetu wa kuongea kiingereza ni ule wa ehe eh! You know, the, the nyingi tu. Mtu anaambiwa chagua utaongea kwa kutumia lugha gani anasema "English" haya mama twende kazini. Hata kueleza jinsi anavyoifahamu Tanzania hoi! Sasa tunalalamika nini? We Hoyce Temu mwaka 1999 ulikuwa Miss Tanzania kwenye mashindano ya Miss world hukuiona hata namba 50! Hakuna siasa hapa tupeleke wawakilishi wenye vigezo vinavyokubalika. Tikitaka dada zetu weusi washinde tuwaandee vizuri kwani huko wanakokwenda weupe ni wengi kuliko WEUSI. Hongera Richa usijali maneno ya Waswahili ndo walivyo.

NI KWELI TAIFA STARS UWEZO MDOGO

Niko na karadio kangu kadogo hapa ofisini. Mimi huwa napenda kusikiliza kipindi cha "Power Break Fast" kinachorushwa na "Clouds Radio FM." Dakika chache zilizopita Gerald Hando alikuwa anajaribu kulinganisha uwezo wa "Taifa Stars" na " The Mambas." Kwanza alisema kitimu Taifa stars ilionyesha uwezo mdogo hata wachezaji binafsi hawakuonyesha uwezo wao ukilinganisha na wenzao wa Msumbiji.

Sikwenda uwanja wa Taifa siku ya tarehe 9/8/2007. Nilibaki nyumbani nikiangalia mechi hiyo kupitia Luninga. Mchana wa siku hiyo nilibahatika kwenda Magomeni kupitia uwanja wa Taifa. Kila nilikopita nilikutana na bendara ya Taifa, saa 6 tu mchana tayari nje ya uwanja wa Taifa umati mkubwa ulikuwa umefurika wakiwa na bendera za Taifa gari zilizopambwa. Lakini cha ajabu niliiona pia pickup moja yenye mashabiki wa Timu ya Msumbiji hawakuwa wengi lakini walipendeza na walijiamini. Wakati tukilipita gari hiyo kwa mzaha sijui mmoja wao alinyoosha vidole viwili akimaanisha kuwa tutafungwa magoli mawili. Huo ulikuwa mzaha . Hata hivyo support waliyoipata timu ya Taifa katika mchezo wa Jumamosi ilikuwa kubwa sana karibu kila Mtanzania alihamasika. Hapa ninapoishi nina jirani yangu Mchaga ambaye kwa kawaida si shabiki wa soka lakini nilishangaa kumuona amefunga bendara ya Taifa kichwani. Nikamuuliza vipi Mangi au ndo umaahidiwa "pesa" akasema we acha tu, vijana lazima washinde leo!

Lile goli la dakika za mwanzo lilitumaliza Watanzania. Timu ilicheza bila uelewano. Ivo Mapunda alikuwa akibabaika. Beki inakatika. Viungo hakuna. Washambualiaji ndo kabisa kulikuwa hakuna. Unategemea nini katika hilo. Nilikuwa nasikiliza kwa makini mawaidha ya Juma Pondamali Meshah aliyokuwa akiyatoa kupitia TVT. Mara kwa mara alikuwa akisema kuwa inaonekana Ivo hana mawasiliani na beki zake. Timu inashindwa kupita katikati kwahiyo wajaribu kupitia pembeni. Kwa sababu, kipindi cha kwanza hakukuwa na "fighter" pale mbele. Kaniki aliingizwa dakika 10 kabla mchezo kwisha unategemea nini? Saidi Maulidi alishindwa kabisa kufurukuta siku ile pia Shaabani Nditi.

Hata kabla ya mechi ya Jumamosi, wengi walitoa maoni yao kuwa timu yetu haina uwezo wa kufunga magoli. Kwa kifupi hatuna mfungaji/wafungaji wa kutegemea. Utasikia leo goli kafunga Badi Kassim, kesho Nizar Khalfan n.k. tena kagoli kamoja kati ya mechi tano au 10. Kweli kuna timu hapo? Kuna wafungaji hapo? NI KWELI TAIFA STARS UWEZO WAKE BADO MDOGO.