Friday, February 26, 2010

Tunaita kudandia


Haya ndiyo watoto wetu wanayoweza.
Kijana huyu ni umri wa wanafunzi wa shule za msingi. Sasa tujiulize anadandia bus ili iweje? Hana sare za shule pengine tungesema kuwa anataka kuwahi kwenda shule. Hapa ni Dar hiyo ndiyo Taswira ya Taifa. Picha kutoka Gazeti la Mwananchi la Tarehe 26/2/10

Ushindi ni mazoezi


Asikudanganye mtu, ushindi ni mazoezi tu. Angalia jinsi mlinda mlango wa Twiga Queens (Timu ya Taifa ya Soka ya Wanawake)- Zena Juma anavyojifua kwenye mazoezi. Hii inampa stamina, uzoefu pamoja na mbinu. Hivyo vyote vikikamilika ushindi ni dhahiri. MUNGU IBARIKI TWIGA QUEENS

Mjibu Kipanya basi


Kama wewe mjuzi wa kujibu maswali mjibu kipanya tukate mzizi wa fitina wa rushwa.

Kuna nini UWT



UWT kuna fukuto kali. Vijembe na mambo kadha wa kadha. Wengine hatufahamu chochote. Lakini jinsi nilivyomsikia Makamu wa Mwenyekiti wa chama hicho Bi Asha Makame kwa kipitia TBC 1 jana jioni na leo hii kusoma kwenye gazeti la Mwananchi lenye kichwa cha Habari "Mwilima ajiandaa kujibu mapigo UWT." Gazeti hilo lilimnukuu Mwilima akisema "Mmhh! Napata utata kulijibu hilo, lakini nisema tu kwamba kwa mujibu wa katiba ya UWT, kikao cha Kamati ya Utendaji ndicho kinachoweza kuniondoa," alisema Mwilima.

Tuesday, February 23, 2010

Anauza mikate!


Leo asubuhi nimeinyaka picha hii kutoka kwenye blog ya ndugu yangu Mjengwa. Picha hii imepigwa Zanzibar. Mfanyabiashara huyu raha mustarehe anauza mikate kwenye tenga huku akiitangaza waziwazi bila kufunikwa. Usalama wa afya za walaji je. Hata huku Tanzania Bara tabia hii ya wafanyabiashara kutojali usalama wa afya za walaji ni tatizo sugu. Utaona samaki wa kukaanga wanauzwa barabarani bila kuhifadhiwa, korosho zimewekwa kwenye mafungu na kuguswaguswa na wanunuzi. Hii kwa kweli si tabia nzuri. Wafanyabiashara wajifunze utaratibu mzuri wa kuuza bidhaa zao hasa vyakula.

Monday, February 22, 2010

Kumbe Ulaya nako barabara mbovu kama bongo!


Unaulizwa, kama msichana huyu alikupita wakati ukimuomba lift. Ukimkuta kwenye hali hii utamsaidia?

Hee mizigo mitano kwenye pikipiki!


Mzee anaendesha, huku akipakia binti, nyumba ndogo na mama pamoja na tenga. Wakipata ajali ni kazi ya Mungu? Pikipiki hii haikutengenezwa kwa madhumuni hayo.

Hii ndiyo JWTZ


Kwa mazoezi haya na mengine ambayo hayawezi kuonyeshwa ovyo ovyo. Jeshi letu si mchezo. Mtu akija kicha kichwa ataumizwa vibaya sana oh! Safi sana JWTZ!

Anayesema hakuna chochote kwenye sekta ya KILIMO mwongo


Angalia kwenye picha wataalamu wakiwa kwenye viatu vya kazi (boots) mwangalie Mhe. Dkt Ali Mohamed Shein Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akifurahia shamba zuri la mahindi kwa ajili ya kuzalisha mbegu linalomilikiwa na JKT Mlale wilaya ya Mbinga.

Kisu kimenolewa acha kabisa mchezo


Ndiyo, baada ya kukaa muda mrefu kwa maumivu, Ulimboka Mwakingwe 'Uli' amerudi na makali mapya dimbani kwenye kikosi cha Wekundu wa Msimbazi (SSC). Kasi imeongezeka na shabaha ya goli kama kawa! Kuna nini tena mbona kazi kwisha. Ubingwa ni dhahiri mwaka huu. Pichani Uli katika kasi yake akimtoka Stephen Mwasika wa Moro United katika mchezo wa ligi kuu uwanja wa UHURU hapo jana (21/02/2009). Simba ilishinda kwa magoli 4-1. Picha kwa hisani ya gazeti la Mwananchi.

Friday, February 19, 2010

Kumbe chocolate kwa kiswahili ni kashata!


Hii nimeinyaka leo kutoka blog ya uncle Michuzi. Kuna chocolate inayotenngezwa kwa jina la Tanzania. Nasikia inapendwa sana huko majuu. Sasa uncle yeye ameiita ni kashata. Sikujua kama chocalate ndiyo kashata. Tuanze kutumia sasa mtoto akitaka chocolate dukani basi tunasema nipe kashata mbili za maziwa (milk chocolate)!

Vyakula dawa vinavyorefusha maisha



Leo katika pekuapekua yangu nimekuta kilichotayarishwa na Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika kinachoelezea vyakula dawa vinavyorefusha maisha kwa wanaoishi na virusi vya UKIMWI.

Vyakula hivyo ni Viungo (husaidia kutuliza au kutibu matatizo ya afya kama kutapika, kuharisha, mafua, kichefuchefu na kujaa gesi tumboni. Mboga na Matunda ni chanzo cha vitamini na madini muhimu mwilini husaidi kuongeza damu, uzito na vitamini A . Mimea kama ubuyu wenye vitamini C hutuliza mafua na kuongeza hamu ya kula, choya (rozela) husaidia pia kuongeza damu. Shubiri (alovera) husaidia kutibu magonjwa mbalimbali yakiwemo malaria na kisukari. Kipeperushi hicho kinapatiokana kupitia barua pepe: psk@kilimo.go.tz

Magufuli anatuambia nini kuhusu utafiti wa kuku wa asili?


Katika Taarifa ya mafanikio ya miaka minne ya serikali ya awamu ya nne. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli akielezea mafanikio yaliyopatikana kutoka utafiti wa kuku wa asili ni kwamba kuku wa asili anapopewa chakula cha ziada badala ya kujitafutia chakula wao wenyewe; utoaji wa mayai unaongezeka kutoka wastani wa mayai 10 hadi kufikia kati ya mayai 18 hadi 25 kwa mtago. Ukuaji wa vifaranga unaongezeka kutoka wastani wa gramu kati ya 3 hadi 5 hadi kufikia wastani wa gramu 8 na 10 kwa siku. Kiwango hiki cha ukuaji kinaonyesha kuwa kuku anaweza kufikia kati ya kilo 1.5 hadi kilo 2 kwa kipindi cha miezi 6 tu. Aidha kuachisha makinda/vifaranga ndani ya wiki 4 kunaongeza idadi ya mitago kutoka kwa wastani 2-3 kwa mwaka hadi wastani wa mitago 6 - kwa kolowa kwa mwaka na hivyo kuongeza idadi ya mayai kutoka wastani wa mayai 40-60 hadi 90-120 kwa kolowa kwa mwaka. Matokeo haya ni mazuri ni ni changamoto kwa wafugaji. Nyama ya kuku wa asili ni tamu sana tujitahidi kufuga.

Watoto na UKIMWI waambiwe kila kitu?


Ugonjwa wa UKIMWI ni balaa katika dunia. Bara la Afrika limepigika zaidi kwa ukimwi hakuna kaya isiyoathirika kwa UKIMWI.

Mikakati mingi imepangwa kupambana na ugonjwa huo ambao hadi sasa hauna tiba. Baya zaidi ni kwa watoto ambao ndiyo wanaojenga taifa la baadaye. Kuna swali je, WATOTO waambiwe kila kitu kuhusu UKIMWI? Ukizingatia uchumi, utamaduni na mazingira ya mwafrika? Tuelimishane.

Huyo ndiye ROONEY!


Wayne Rooney ni mpachika magoli maarufu kwa sasa wa timu ya soka ya Manchester United ya Uingereza ni mchezaji anayependa soka na kulicheza kwa kiwango cha juu kabisa. Awapo uwanjani Rooney hujituma sana katika kupachika magoli si mtu wa kumwacha pekee hata kidogo ni hatari kwa timu pinzani.

Akitolewa nje na kocha wake huwa anakuwa na ghadhabu isiyosemeka. Rooney anawea kupiga ngumi ukuta, anaweza kuvua gloves na kuzibwaga chini au kufanya lolote lile. Lakini utampenda akifunga goli. Husheherekea kwa mbwembwe zote unazozifahamu anaweza kuserereka kwa magoti bila kujali kuchubuka. Pichani Rooney (mwenye glovu nyeusi) akipongezwa na wachezaji wenzake baada ya kufunga goli.

Tuesday, February 16, 2010

Woman=problems

Tafakari

Tutaukumbuka Mradi wa Minazi


Tanzania tuna bahati kubwa sana ya kustawisha mazao ya aina mbalimbali katika ekolojia tofauti. Kwa kuwa tuna bahari kuna mazao yanayostawi ukanda wa pwani. Kwa kuwa tuna sehemu za nyanda za juu tuna mazao yanayostawi huko kama vile ngano pamoja na matunda ya nchi zenye baridi za ulaya.

Nazi ni zao linalostawi sehemu nyingi hapa nchini lakini kwa miaka ya hivi karibuni upatikanaji wake umekuwa ni wa shida sana hata kusababisha bei ya nazi pamoja na madafu kupanda kwa haraka sana. Uzalishaji wake umeshuka kwa kuwa minazi mingi hukatwa kupisha makazi ya watu hasa sehemu za Pwani. Vilevile magonjwa yamesababisha minazi mingi kusinyaa hivyo kushusha uzalishaji.

Zao la nazi miaka ya 80 hadi 90 lilikuwa likishughulikiwa sana na Mradi wa Kitaifa wa Kuendeleza Zao la Mnazi (National Coconut Development Project-NCDP). Mradi huu ulifanya kazi kubwa licha ya dosari ndogo ndogo zilizojitokeza baada ya kumalizika kwa mradi hasa kwa mbegu fupi kutokubaliwa na wakulima wengi baada ya kuona kuwa huchakaa baada ya muda mfupi.

Hali ikiendelea hivi bila kuchukua hatua madhubuti uzalishaji wa nazi utashuka mwaka hadi mwaka na madafu nayo yataadimika na be itapanda sana.

Thursday, February 11, 2010

Wakati Wamisri wakiomba dua muone huyo mchezaji wa Ivory Coast!


Hivi kweli huu ni ustaarabu au imani za kishirikina. Bila aibu mchezaji huyu wa Ivory Coast anakojoa uwanjani. Lakini mpiga picha makini aliinyaka hii na sasa imevuja kwenye mtandao. Pamoja na hayo yote Ivory Coast walibamizwa na Misri

ATHARI ZA KUPUNGUZA WAFANYAKAZI


Hebu soma hiyo taswira hapo juu. Wazungu wanarudi nyuma na kung'amua kuwa kupunguza wafanyakazi kuna athari kwa wafanyakazi wanaopunguzwa, uchumi pamoja na mambo mengine. Hili ni fundisho kwetu. Tulibeba kwa haraka sera ya kupunguza wafanyakazi bila kuangalia madhara yake sekta nyingi hivi sasa hapa nchini zina uhaba wa wataalamu. Wataalamu waliopo sasa wanastaafu hivyo kulazimika kuwaajiri kwa mkataba. Tutakujakung'amua hapo baaye kuwa hata ajira za mkataba zina madhara yake

Madega-Hivi Yanga wanaweza kutupa raha au kutuaibisha?

Madega, Young Africans haina historia nzuri kwenye mashindano ya kimataifa. Hivi hatutegemei kuwa itatupa raha uliyoisema. kwa mpira gani? Wanaweza kufurukuta tu hapa nyumbani kwa ushindi wa kupangwa! Hivyo mimi sina mpango wa kuja uwanja wa Taifa kuiona Yanga ikituaibisha.

Bye Bye Richmond


Ndivyo linavyoandika gazeti la Mwananchi la tarehe 11 Februari 2020. Bunge limefunga rasmi mjadala wa mkataba tata wa Kampuni ya Richmond Development (LLC) na Tanesco na kuaacha Serikali iendelee kutekeleza maazimio yake huku wabunge wawili Christopher Ole Sendeka na Dk. Wilibrod Slaa wakipambana hadi mwisho. Hivi ni kweli. Bye Bye Richmond tungoje mengine. Hii ndiyo Bongoland!

MBARAKA MWINSHEHE MWARUKA



Leo kwenye blog ya Maggid nimepata kusoma habari fupi ya marehemu Mbaraka Mwishehe Mwaruka gwiji la muziki miaka ya sitini aliyebobea mjini Morogoro.

Mbaraka kwa kweli asili yake ni Mzaramo lakini wengi hudhani kuwa ni Mluguru. Huyu aliweza kutunga na kuimba nyimbo nyingi za Kiluguru zikiwemo:- Kukala hamwe ng'avhinogile nibita kuja Mwembosongo, pinga yumwe kanikema kanilongela nibete........ (Kukaa mahali pamoja panachosha kwahiyo katika pitapita zake kule Mwembesongo binti mmoja akamwambia nisubiri.....); Mnzese gwe mnzese kolima (Anamwimba ndege mmoja anayeitwa Mnzese mjanja sana kwa kuimba lakini hana anachokifanya shambani....); Jamani Morogoro, Morogoro, oh oo, maji yatiririka vilimani oh oh na hiyo aliyoining'iniza MJENGWA kwenye blog yake . Wajomba wamechacha wamekuja juu harusini.........

Kwa kweli Marehemu Mbaraka Mwinshehe alitunga nyimbo zenye kugusa jamii. Hakuimba mapenzi pekee. Lala salama Mbaraka falsafa yako bado inadumu kizazi hadi kizazi. (Picha kwa hisani ya Blog ya MJENGWA).

Sioni sababu ya Prof.Maghembe kujiuzulu watoto wetu hawasomi

Binafsi, matokeo ya mtihani wa kidato cha IV mwaka 2009 kwa idadi kubwa ya watahiniwa kushindwa hayakunishangaza sana. Nilitegemea hivyo kwani watoto wetu hawapendi kujifunza. Tatizo si vitabu, si walimu si kiingereza. Mbona hata hicho kiswahili ndo wameshindwa vibaya. Lugha wanayoitumia kila siku. Kwenye shule hizo hizo za kata kuna waliopata division I na II.

Idadi kubwa ya wanafunzi katika shule zetu za sekondari ni sababu ya msingi kwa wanafunzi kufanya vibaya. Njia za kuwachuja wanafunzi hawa kabla ya kufanya mtihani wa kidato cha nne zimeondolewa. Kulikuwa na mtihani wa kidato cha pili, sasa hauko unategemea nini? Si wanakwenda waliokuwemo na wasiokuwemo ili mradi kafika kidato cha IV.

Huwezi kulinganisha na mfumo wa elimu kwa shule za seminari za kikristu. Kule wanafunzi huchujwa kwelikweli kiasi kwamba yule anayebahatika kufika kidato cha nne hawezi kukosa Division 4 chunguza kwa makini utagundua hilo.

Kitu cha kufanya sasa ni kwamba wazazi, walimu na wizara husika tujipange kuhakikisha kuwa watoto wetu wanasoma. vinginevyo takwimu hizi zitazidi kuwa mbaya mwaka hadi mwaka. Kwahiyo wale wanaopiga kelele kuwa Prof.Maghembe ajiuzulu naona hawamtetendei haki.

Hivi tunasafisha nyumba zetu tunapotembelewa na wageni?

Juma la jana wakati wa kuadhimisha miaka 33 ya CCM Mwenyekiti wa chama hicho Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete alikuwa na ratiba ya kutembelea wana CCM katika jiji la Dar Es Salaam. Kilichotokea kila sehemu walijitayarisha kwa kila hali. Wakazi wa Mbagala walishuhudia mitaro ya maji kutengenezwa na kusafishwa kwenye barabara ya Kilwa. Uchafu wa siku nyingi ulifanyiwa kazi kwa siku mbili tatu tu. Haya ndiyo maisha yetu. Tunasafisha nyumba zetu pale tu wageni wanapotutembelea si kwa usafi wetu. Tunataka watu watuone tu wasafi wakati ukweli ni kwamba tunaishi kwenye uchafu daima.

Wednesday, February 3, 2010

Power Tiller


Kuna watu wanaotumia 'power tiller' kama chombo cha usafiri kuliko kulimia ndivyo inavyoonekana pichani 'power tiller' ikutumika kusomba matofali

Tunashtuka tu watu wanapokufa?


Ajali nyingi zinatokea na kupoteza maisha wananchi wengi. Ajali ya gari ni kifo hc ghafla kinashtua na tena kinaacha maswali mengi bila majibu. Jana tena ajali nyingine mbaya imetokea barabara ya Dar - Arusha na kuua watu 24! Hivi tunashtuka tu watu wanapokufa? Baadaye mambo ni kama juzi. Hivi kweli tumeshindwa kudhibiti ajali za barabarani? Kama ndivyo basi kuukomesha UKIMWI ni ndoto! (Pichani - Ajali, Taswira katika Taifa - Kwa hisani ya gazeti la Mwananchi tar 21 Novemba 2009)

Rushwa ilivyokithiri


Msome muuguzi huyu anavyohalalisha kupokea rushwa

Wakitayarishwa mapema wataweza


Iwapo mikakati itawekwa na kutekelezwa ya kuwaandaa vijana wetu katika mchezo wa soka wanaweza kutuletea ushindi siku za usoni. Pichani vijana wakiwa kwenye mazoezi ya viungo (Picha kwa hisani ya gazeti la mwananchi)

Tuesday, February 2, 2010

Nazi zimeanza kuadimika Dar


Wali ulioungwa kwa nazi ni chakula kitamu sana lakini ni cha gharama. Kiungo cha nazi kimeanza kuwa adimu siku hizi jijini Dar. Si rahisi kwa sasa kwa watu wenye kipato cha chini kutumia kiungo hicho. Bei ya nazi jijini Dar ni kati ya Tzs 500-1000/- kwa nazi. Inasemekana kuwa nazi nyingi zinasafirishwa kwenda nchini Comoro. Juhudi zifanyike zakuweza kuongeza uzalishaji wa nazi kwani ni kiungo kinachopendwa na wengi na madhara yake kiafya ni kidogo.

Hata mzungu alilia kwa Ghana kushindwa kunyakua ubingwa wa Afrika



Licha ya kutandaza kandanda safi. Timu ya Taifa ya Ghana (Black Stars) ilishindwa kuwafunga mafarao na kunyakua ubingwa wa Afrika. Mashabiki wa Ghana walilia na kupagawa.

Hivi ndivyo Mafarao walivyopokelewa


Hivi ndivyo walivyopokelewa mabingwa wa soka barani Afrika timu ya Taifa ya Misri kwa jina la kimpira "Phraos." walipotua nyumbani kwao.

Walisaini Muungano wa Tanganyika na Zanzibar


Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Hayati Abeid Amani Karume walisaini hati za Muungano wa Tanganyika na Zanzibar mwaka 1964. Kuna watu walioshuhudia tukio hilo ambao mpaka sasa wako hai. Mapatano ya Muungano yaliigawa Jamhuri ya Muungano katika Mamlaka (Jurisdiction) tatu kama ifuatavyo:-
1. Mamlaka ya Zanzibar ambayo ni mambo yasiyo ya Muungano ndani ya Zanzibar. Kwa mfano masuala ya Afya, Ardhi na Mazingira;
2.Maeneo ya Tanganyika (Tanzania Bara) ambayo ni mambo yasiyo ya Muungano ndani ya Tanzania Bara. Kwa mfano; Afya, Serikali za Mitaa, Kilimo na ;
3.Maeneo ya Muungano ambayo yameainishwa na Maptano ya Muungano kuwa ndio mambo ya Muungano.