Wednesday, December 31, 2008

Kwaheri 2008

Kwaheri 2008.

Mwaka huu ulikuwa wamafanikio makubwa kwa blog hii. Banzi wa Moro ameweza kuvuka lengo alilojiwekea kwa asilimia 140! Kumbe inawezekana.

Sina budi nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa afya na busara ya kuweza kukusanya habari mbalimbali na kuweza kuzining'iniza kwenye blog hii.

Nawashukuru viongozi wangu wa kazi walioniwezesha kupata safari za kikazi ndani na nje ya nchi kwazo nimepata fursa ya kuona mengi na kuyaweka ndani ya blog hii.

Kasoro kubwa iliyojitokeza kwa mwaka uliopita ni kwa wasomaji wangu kushindwa kutoa maoni yao kwa habari ambazo zililenga maeneo yenye uzoefu nao.

Ombi langu kwa wasomaji wa blog hii wajitahidi zaidi kutoa maoni yao mwaka ujao. Hii itanipa moyo wa kuweza kukusanya habari nyingi na kuzining'iniza blogini.

Mungu akipenda mwakani naweza kuwa na camera hivyo kuboresha zaidi habari katika blog hii. Mwaka huu mara chache niliweza kudowea camera na kupiga picha chache sana.

Namshukuru mdogo wangu Freddy Mloka, Dada Meab Mdimi ambao wamekuwa wakinitumia picha hasa za familia.

Wamefaulu madarasa hakuna

Matokeo ya mtihani wa darasa la saba yametangazwa lakini kwa bahati mbaya kuna baadhi ya matokeo ya wanafunzi hayajatolewa rasmi eti kwasababu shule zinazotakiwa kuchukuwa wanafunzi hao hazina madarasa! Hali hii imejitokeza zaidi katika mkoa wa Morogoro. Wanafunzi wamefaulu madarasa hakuna.

Sasa viongozi ndo wanakimbizana kutafuta suluhu madarasa yajengwe.
Juzi diwani wa kata ya Mtombozi alifika ofisini kwangu kueleza shida kama hiyo kwa Sekondari ya Mtombizi iliyopo Matombo Morogoro. Jana jioni baadhi yetu tulikutana kujaribu kuweka mikakati ya kuweza kuinasua Mtombozi Sekondari.

Tulichokiona ni kuwa uongozi katika ngazi zote za utekelezaji hauna muono, hauna mikakati. Iweje leo matokeo yanatoka ndo wanakumbuka kujenga madarasa. Hivi jamani Morogoro tuna nini? Hii si lawama kwetu tuonekane hatujali nyumbani?

Hata hivyo tumekubaliana kusaidia kutatua tatizo hilo kwa mikakati tutakayoiweka. Mojawapo ni kuwa na mtandao wa wadau. Na tayari hatua zimeshaanza kuchukuliwa. Hata hivyo tumekubaliana kuwa uongozi uelezwe wazi udhaifu wao. "Wotugwisa"

Amri inapotolewa kupumzisha MV Magogoni

Ijumaa ya tarehe 19/12/2008 saa 2.30 usiku nilipitia Kivukoni ili niweze kurudi Nyumbani kwangu Kisemvule kwa kuogopa adha ya usafiri kupitia njia ya Mbagala huku nikitegemea kuwa kwa sasa usafiri wa boti umeimarika zaidi baada ya boti MV Magogoni kuzinduliwa mwanzoni mwa mwezi Desemba mwaka huu.

Cha kushangaza mara boti hilo MV Magogoni lilipotia nanga likitokea Kigamboni Captain aliamrishwa na bosi wake akiwa nyumbani kuwa asimamishe boti hilo na boti za zamani zitumike.

Hali hii iliwakera sana abiria kiasi cha kumzonga Captain.
Sidhani kuwa ilikuwa na mantiki kusimamisha boti hilo kwa wakati huo tena kwa amri kutoka nje ya sehemu ya kazi! Tulikuwa na matatizo ya boti usafiri taabu. Boti jipya limeletwa usafiri ni taabu. Hivi Watanzania tuna nini?

Lami yaanza kumwaga Kilwa Road

Wakati tunasherehekea kuingia kwa mwaka mpya, wakazi wa Mbagala na vitongoji vyake wameanza kuonja raha ya usafiri baada ya kupungua kwa foleni za magari katika barabara hiyo hasa kutoka Mtoni Mtongani hadi Sabasaba.
yapata wiki ya pili sasa kipande cha barabara hiyo kinachoanzia Mbagala Rangi 3 hadi karibu na Kizuiani kimeshawekwa lami kwa upande mmoja. Uwekaji wa lami unakaribia kabisa eneo la sabasaba (St. Anthony Sec.School).

Yale madaraja mawili ya mtoni Kizinga wamekamilika kwa asilimia 94. Ni matumaini yangu kuwa ifikapo mwezi Aprili 2009. Wakazi wa Mbagala watakuwa wanateleza kwenye Highway. Tatizo la usafiri Mbagala litakuwa historia.

Tuesday, December 30, 2008

Mitandao ya simu Matombo hajaisaidia sana maisha ya wakulima

Miaka miwili tangu Kampuni ya simu ya Celtel (sasa Zain) iingie Matombo, ushindani wa mitandao ya simu umeongezeka kwa kasi ya kutisha Matombo. Tigo wakasimika mnara wao kwenye mlima wa "Funamandole" mwaka jana na kuufanya mtandao huo kuwa bora zaidi ya Celtel.

Mwaka huu Vodacom imeingia Matombo na kufunika kabisa Zain na Tigo. Lakini sidhani ushindani huu unawasaidia sana wakulima masikini wa Matombo kwani mawasiliano ya simu za mkononi bado ni ghali mno hasa mawasiliano yakifanyika kwa mitandao tofauti. Hili linabidi kufanyiwa kazi na vyombo husika ili wakulima hao wasiwe wanapoteza fedha nyingi zaidi kwa mawasiliano kuliko chakula!

Monday, December 29, 2008

Miaka 47 imepita kilimo cha Matombo ni kilekile

Miaka 47 tangu tupate uhuru lakini napenda nikiri kama mtaalamu wa kilimo kuwa wakulima wengi wa Matombo hawafuata kanuni za kilimo bora. Licha ya kutotumia mbolea lakini kanuni za msingikama vile kupanda kwa nafasi hawajui, mbegu bora kwao ni ajabu tu, wadudu na magonjwa ya mimea yanashambulia yapendavyo. Kwa hali hiyo si ajabu kuona uzalishaji wa mazao Matombo ni mdogo sana.

Nilijaribu kuongea na baadhi ya ndugu zangu ambao ni wakulima wanasema kwa wastani huvuna gunia moja hadi mbili za mahindi kwa eka! Kiasi hiki cha mavuno hakiwezi kumlisha hata mtu mmoja kwa mwaka!

Sijui kama bwanashamba yupo katika kijiji chetu, sijui kama uongozi wa kijiji, kata na wilaya unatambua umuhimu wa kilimo kwa uchumi wa mwananchi wa Matombo.

Matombo imebahatika kuwa na hali nzuri ya hewa na udongo mzuri. Inafikika kirahisi kutoka Morogoro, Dodoma, Iringa na Dar kwa hiyo uhakika wa soko upo. Matunda ya tropiki kama vile machungwa, maembe, mananasi na ndizi yanapatikana kwa wingi. Siku hizi wakulima wameanza kujishughulisha na kilimo cha mazao ya viungo kama vile hiliki, pilipili manga na mdarasini sehemu za Konde, Nyangala, Tawa, Kinole na Mkuyuni.

Mazao haya yakijengewa mikakati mizuri na Halmashauri ya Wilaya kupitia DADPs yanaweza kuboresha hali ya uchumi ya watu wa Matombo.

Mto wa Mfizigo na mawe yake

Mto wa mfizigo ni moja ya mito mikubwa katika tarafa ya Matombo. Mto huu humwaga maji yake katika mto wa Ruvu ambapo wakazi wa jiji la Dar Es Salaam pamoja na sehemu za mkoa wa Pwani hapata maji kutoka mto huu.

Pamoja na umuhimu wake wa kutoa maji, mto huu una aina mbalimbali ya mawe ya kuvutia sana. Licha ya kuufahmu mto mfizigo kwa muda mrefu kwani nimeutumia mto huo kwa shughuli mbalimbali ikiwemo kuoga, kufua, kuvua samaki, kuchota mchanga na mawe tangu nikiwa mtoto sikuweza kutambua hapo awali kuwa mto Mfizigo una mawe ambayo yakipangwa vizuri yanaweza kutoa mapambo ya kuvutia. Ni juzi tu nilipokuwa mtoni Mfizigo ndipo wazo lilinijia la kuokota kiasi cha mawe ya aina mbalimbali ambayo yalinivutia sana. Ajabu, mto Mfizigo, mawe yake yanavutia sana.

Matombo imeanza kupoteza umaarufu wa machungwa matamu

Miaka 20 iliyopita Matombo ilikuwa maarufu sana kwa uzalishaji wa machungwa matamu. Machungwa haya yalijulikana kwa jina la Machungwa ya Matombo. Yalikuwa matamu sana hata rangi yake ilikuwa ya kuvutia mlaji.

Ni kweli miaka hiyo hakukuwa na biashara nzuri ya matunda haya. Nakumbuka babu yangu alikuwa na miti michache ambayo aliweza kuikodisha kwa walimu wa shule ya msingi Matombo kwa bei ya sh 2 kwa mchungwa! Sasa hali hii haipo tena. Uzalishaji umepungua sana na mahitaji yameongezeka sana kiasi cha kuwafanya wafanyabiashara (walanguzi) kuvuna machungwa wakati hayajapata rangi yake nzuri ya njano! Bei ya chungwa moja kwa sasa haitofautiani sana na ile ya Dar Es Salaam.

Miti mingi ya machungwa imeanza kuzeeka au kushambuliwa na wadudu na magonjwa na sikuona jitihada za makusudi kuokoa hali hiyo kwa wakulima wa machungwa. Ndiyo maana nathubutu kusema kuwa Matombo imeanza kupoteza umaarufu wa machungwa matamu.

Nyumba za kisasa za Familia Matombo

Kuna mwamko wa ajabu huko Matombo kwa sasa kwa kila familia kujenga nyumba ya kisasa ya familia. Hii ni kweli kabisa. Mmiliki wa Blog hii alishuhudia familia nyingi zilizokuwa zikijishughulisha na ujenzi wa nyumba za kisasa za familia kule Kiswira, Mhangazi na Nige. Huu ni mtizamo wa kimaendeleo. Nyumba nyingi zinazojengwa sasa zina satelitte dish, nyingine zinafungwa umeme wa jua (solar power) na nyumba nyingine zina generator za umeme.

Shauri yako, msichelewe nendeni mkajenge angalao nyumba moja ya kisasa ya familia. Mkizubaa mtaachwa. Waluguru sasa hawataki mchezo.

Banda la Kumpuzika wasafiri lijengwe Msalabani

Kwa wenyeji wa Matombo au waliobahatika kufika Matombo, jina MSALABANI si geni ni jina maarufu. Hapa ndipo ilipo njia panda ya kwenda Matombo Mission, Tawa, Konde, Nyingwa, Kibungo, Lukenge, Nyangala na vitongoji vingine vya Matombo.

Vitongoji hivi vina wakazi wengi ambao kwa usafiri wa uhakika inawabidi kusafiri hadi Msalabani ambapo ndipo kwenye barabara kuu itokayo Morogoro kwenda Kisaki. Tatizo la mahali hapa ni ukosefu wa Kibanda cha kupumzika abiria.

Juzi Jumamosi wakati nasafiri kuelekea Morogoro mjini abiria wengi tulinyeshewa na mvua na kulowa chapachapa. Wanawake ilibidi wabadilishe nguo zao hapohapo baada ya kukatika kwa mvua.

Hivi uongozi wa Matombo hawaoni umuhimu wa kujenga kibanda imara japo kilichoezekwa kwa makuti ili kuwahifadhi abiria wakati wa jua au mvua? Hili linawezekana. Tuanze sasa kabla ya masika.

Dakika 120 Matombo-Moro

Nimerudi kutoka Matombo. Mambo yalikuwa safi sana huko kijijini. Nimekula magimbi, mananasi, maembe na ubwabwa. Lakini cha kushangaza mwaka huu kuku ni wachache sana Matombo. Hata wa kununua hawapatikani. Kuku imekuwa ni dili kubwa sana Matombo. Unawaona lakini hauwzwi!

Ndiyo, barabara ya Matombo kwa sasa ni nzuri mno! Ndiyo maana tumeweza kutumia dakika 120 kufika Matombo kutoka Morogoro mjini kwa kutumia kibus cha 'Hiace.' Msalabani hadi Matombo Mission barabara imenyanyuliwa hata corolla inapita! Ni kweli walionazo walikuja nazo kushrehekea Xmass kijijini. Pale Chamarigo (Gubi) ambapo huwa panasumbua sana wakati wa mvua sasa pamewekewa Culvert. Safi sana. Hongera Tanroads, Hongera Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro Vijijini.

Tuesday, December 23, 2008

Safarini Matombo-Morogoro

Xmass na mwaka mpya unakaribia. Sisi hatuna utaratibu wa kurudi kwetu wakati wa Xmass kama ilivyo kwa wenzetu Wachagga. Hivi sasa huko migombani ni nyimbo za marehemu Jim Reeves tu na harufu ya mbege kumbe je!

Mwaka huu nimeamua kwenda kusherehekea Xmass na ndugu zangu huko kwetu Matombo, nikale Magimbi, Ndizi, mananasi, "ubwabwa na kuku." Nitasafiri kwenda Matombo Morogoro kwa Bibi na Babu zangu, Baba na Mama zangu, Shangazi na Wajomba zangu, Kaka na dada zangu na wengineo.

Nategemea nitaonana na marafiki zangu tuolisoma shule moja, kusali pamoja pale Matombo Mission, kucheza mpira pamoja -Kiswira Sports Club! Nategemea kuimba GLORIA! siku ya Xmass ndani ya Kanisa la Mtakatifu Paul.

Nitakaporudi nitakuwa na mengi ya kuning'iniza kwenye blog hii.

KWAHERINI

Wednesday, December 17, 2008

ARI-SELIAN nawapa shavu kwa usafi

Nipo Arusha kikazi pamoja na watafiti wa hapa. Kilichonileta hapa ni kuwasilisha miongozo na kujadiliana na watafiti waandamizi jinsi ya kuandaa viashiria vya shughuli za utafiti kanda ya kaskazini. Lakini kilichonivutia zaidi wakati nikiwa hapa kituoni Selian ni usafi wa mazingira hasa vyoo. Vyoo ni visafi kweli kweli sabuni zipo na watumiaji ni wastaarabu kwa kweli.

Tabia ya usafi katika kituo cha Utafiti wa Kilimo Selian imejengwa kwa muda mrefu kwa sasa ni utamaduni uliozooeleka hapo kituoni watakushangaa kama unachafua mazingira yao bila sababu. Hongera sana Selian.

Three Principles of Conservation Agriculture

  • Minimum soil disturbance or if possible no tillage seeding
  • Soil cover; if possible permanent; and
  • Useful crop rotations and association

INTERESTED?

For more infromation please read a book on "Conservation Agriculture as practised in Tanzania":Three case studies (Richard Shetto, Marietha Owenya editors). Published in 2007

Karibu nyumbani Dr.Doreen


Ndivyo ilivyokuwa wakati Dr.Doreen alipokaribishwa nyumbani kwao Kimara Temboni na mumewe Dr.Mainen Moshi.

Mama yake Paulina Mloka, kaka yake Freddy Mloka, Bibi yake Sister Maria Makeya, watoto wake, ndugu, marafiki, jamaa na wageni waalikwa walikuwepo katika tafrija nzito ya kumpongeza. Pichani Dr.Doreen akiongozwa kwa mbwembwe za kiluguru avho! na MC Inno Banzi huku akisindikizwa na dada yake Helena Mimata.

Dr. Doreen kumbukumbu na Marais


Hii ndiyo picha ya kumbukumbu ya siku ya kutunukiwa shahada ya uzamivu (PhD) Dr.Doreen Mloka Moshi.Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sayansi ya Tiba Muhimbili (MUCHS) Rais Mstaafu Mhe. Ali Hassan Mwinyi (Mzee Ruksa) ndiye aliyetunuku shahada hizo tarehe 13/12/2008. Mgeni rasmi alikuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Jakaya Mrisho Kikwete. Hongera sana Da Doreen.

Dr.Doreen Mloka Moshi-PhD "mukichwa"


Siku ya tarehe 13/12/2008 Jumamosi itakuwa siku ya kumbukumbu kubwa kwa Doreen, familia yake, ndugu na majamaa wakati alipotunukiwa shahada ya Uzamivu (PhD) katika tiba. Pichani kushoto Dr. Doreen ndani ya joho la Chuo Kikuu cha Sayansi ya Tiba Muhimbili (MUCHS) katika hisia kali. Kulia ni Professor Nuhunoli (naomba nisahihishwe jina sahihi) aliyetunukiwa shahada ya Udaktari wa Sayansi. Kutokana na maelezo niliyoyapata kutoka kwa wasomi, hii ni tuzo ya juu kabisa.

Friday, December 5, 2008

Shibuda atagombeaje urais katika mlango mmoja ?

Conges Mramba katika makala yake kwenye gazeti la Rai (Mraba wa Mramba) tarehe 4-10 Desemba amekuja na kichwa cha habari CCM: Damu ya kijani au geresha? Ndani ya makala hiyo ameandika mambo mengi ya kutafakari kuhusu CCM na mambo yanavyokwenda kwenye chama hicho tawala.

Binafsi nimefurahishwa na hili. Nanukuu- " Shibuda atagombeaje urais katika mlango mmoja unaoandaliwa kwa rais aliyepo madarakani? Tafakari.

Mfumuko wa bei ni aslimia milioni 230- Siamini!

Hivi kweli mfumuko wa bei Zimbabwe ni asilimia milioni 230! Mbona siamini, nashindwa kupata picha. Mimi ni mchumi, hiyo asilimia milioni 230 nashindwa kuipresent kwa kweli. Hivi Wazimbabwe wanaishije huko? Kuna tatizo na si dogo. Tuwasaidie ndugu zetu Wazimbabwe.

"Utaratibu tuliojiwekea" maana yake nini?

Siku hizi mambo yanapokiukwa utasikia kwa "utaratibu tuliojiwekea."
Kama kanuni, sheria na taratibu zipo kwanini tuwe na kitu mbadala- "Utaratibu tuliojiwekea" hapa ndipo tunapoanza kuharibu mambo. Na ndipo haki inapopindwa.

Hivi unafahamu kiswahili cha "White Elephant?"

Usipoteze wakati wako utauumiza kichwa bure! White elephant ni - Geresha (Gheresha).

Quote from Rio Ferdinand

Rio Ferdinand is a dependable centrehalf of the Manchester United Football Club of England.
I was moved with his words from the article published on the Daily News of last Friday 27/11/2008.

I quote - "Outside of Sport it would be Nelson Mandela for all he's achieved. He's devoted his life to his nation."

"It would be great if Nelson Mandela was the person who handed us a cup. There's no better man in the world to do that and tha's something to work towards, but there is a very long way to go yet."

Aliyasema haya alipokuwa akiuulizwa anafikiriaje kuhusu klabu bingwa ya dunia?

Dereva Taxi wa aina hii ni wachache

Si rahisi ukasahau kitu kwenye Taxi na hatimaye akakipata. Lakini wako madereva taxi wanaoheshimu kazi zao na wanaopedna kulinda soko.

Dereva Taxi aliyanipeleka Jomo Kenyatta International Airport hivi karibuni ni muungwana kwani baada ya kushusha mkoba wangu kumbe nilidondosha "highlighter" (kalamu kubwa ya rangi ya kuweka msisitizo) ndani ya gari. Alipoiona alisimamisha gari na kunipatia kalamu hiyo. Dereva wa aina yake ni wa chache. Nakushukuru na umependisha chati madereva Taxi wa Kenya ingawa si wote. Asante sana.

Ulemavu si hoja

Niko Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Jomo Kenyatta nikisubiri ndege yakunirudisha nyumbani Dar. Jirani yangu yuko mama mmoja wa kizungu (baadaye nakajakugundua kuwa ni Mswede) yuko "busy" na laptop yake na kifaa kingine (sikijui). Nashangaa nagundua kuwa ni kipofu lakini ana jamaa zake wawili alioandamana nao.

Baadaye nagundua kuwa naye anasafiri kuelekea Tanzania tena Morogoro. Nilifahamu hivyo baada ya kusikia mazungumzo yao na yule Mmasai kutoka Twatwatwa, Kilosa na mama mmoja kutoka Sudan. Mama huyu licha ya kutoona alikuwa na vifaa vya kisasa vinavyomsaidia kuendesha shughuli zake kama vile kutumia kompyuta. Na wakati akizungumza huwezi kugundua kama ni kipofu, ufahamu wake ulikuwa ni wa hali ya juu. Ama kweli Ulemavu si hoja.

Vijana wakiafrika sasa hufanya biashara nchi mbalimbali

Kuchelewa kuondoka uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyata siku ya tarehe 26 Novemba 2008 kumenifanya nijifunze mengi.

Wakati nilipokuwa napata chakula cha mchana cha kuponi pale uwanjani (kutokana na kucheleweshwa) niliwaona vijana wengi wake kwa waume. Nilibahatika kumuuliza mmoja wao anatokea wapi alinijibu anatoka Nigeria na anelekea Bangkok kwa shughuli ya biashara. Kwenye meza nilizunguukwa na vijana wanne waliokuwa wakizungumza kifaransa nao wako kwenye pilika ya safari za kibiashara. Nilishindwa kudodosa zaidi nijue ni biashara ya aina gani wanayofuata huko Bangkok. Sote tulikuwa tunasubiri chakula!

Kenya Airways huchelewa pia

Ndege KQ 482 kutoka Nairobi kuelekea Dar Es Salaam ilikuwa iondoke saa 6:45 mchana Jumatano tarehe 26/11/2008. Lakini haikuweza kuondoka hadi saa 12.30 jioni. Lo! Kumbe hata KA nayo huchelewa?

Unapokutana na mfugaji kutoka Twatwatwa ukiwa Nairobi

Adam Ole Mwarabu ni mfugaji kutoka kijiji cha Twatwa, Kilosa, Morogoro. Kijiji hiki ni maarufu kwa mapigano kati ya Wafugaji (Wamasai) na wakulima. Adam ni Mmasai. Hivi karibuni nilikutana na Adamu uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa JomoKenyatta Jijini Nairobi wakati tukisubiri ndege ya kurudi nyumbani Tanzania (Dar Es Salaam). Ilikuwa ni mara yangu ya kwanza kukutana na Adam. Huku akivalia lubega na kubeba "laptop" yake ni lazima utajiuliza kimoyomoyo hivi Mmasai anaweza kutumia Laptop?

Adam, ni Mmasai aliyendelea. Amesafiri nchi nyingi hapa duniani kuliko wengi wetu. Amehudhuria mikutano mingi ya kimataifa na wakati nilipokutana naye alikuwa anatokea Ubalozi wa Poland kuchukua Visa.

Adam ni Mratibu wa NGO inayooitwa PAKODEO (nitamuuliza kirefu chake). NGO hii hujishughulisha zaidi na masuala ya ardhi, mifugo, elimu, mazingira na jinsi ya kupambana na HIV-AIDS.

Adam hazungumzii zaidi kuhusu mapigano ya wakulima na wafugaji anasema ni ya kisiasa zaidi na viongozi hawako makini katika kutatua tatizo.

Tuesday, November 25, 2008

Utekelezaji mbovu Afrika ndo unaotufanya tusifikie malengo

Jana katika hotel ya Intercontinental hapa Nairobi, Kenya tulikuwa tunajadili masuala ya "kupelemba na kutathmini" (Monitoring and Evaluation) kwenye utafiti wa Kilimo.

Imedhihirika kuwa tuna mipango mizuri yenye malengo mazuri. Na malengo yetu makuu kwnye nchi hizi za Afrika Mashariki na ya Kati kwa bahati nzuri ni ya muda mrefu sana kama vile kuondoa umaskini, ujinga, maradhi lakini hadi hii leo tunazungumzia hayo hayo tokea tupate UHURU. Korea ya Kusini walikuwa kwenye hali kama yetu miaka 40 iliyopita sasa wameshatoka. India sasa wanajitosheleza kwa chakula! Sisi misaada, misaada misaada!

Eti sisi Waafrika ni wabaguzi zaidi kuliko wazungu?

Kuna baadhi ya watu wanasema kuwa Obama kuwa Rais Amerika ni rahisi zaidi kuliko Clinton kuwa Rais wa Kenya! Wanasema kuwa sisi Waafrika ni wabaguzi zaidi kuliko wazungu je ni kweli?

Monday, November 24, 2008

Huduma za Hotelini Kenya ni zaidi

Ukiwa Hotelini Nairobi Kenya, huduma nyingi zinapatikana ikiwamo hii ya Internet. Hapa nilipo nimeweza kuwasiliana nanyi kwa kutumia "Wireless internet connection" huna haja ya kuonana na mtu anayekupa hiyo huduma. Upo chumbani kwako unapiga simu na unapata huduma kwa maelekezo.Malipo baadaye na ni malipo nafuu.

Hee, hata kama mimi ni mtalii ningeweza kupendelea kwenda Kenya. Hivi vitu vinawezekana kwetu pia. Nafahamu huduma hizi zipo kwetu lakini hazijaenea kwa kiasi cha kutosha lakini inawezekana. Tunapoteza hela nyingi kwenye sekta ya mawasiliano tumeng'ang'ania simu za mkononi tu. Wenzetu wanahama taratibu!

Nikiwa Kenya niko Nyumbani

Nairobi, watu wake, miti yake na udongo wake ni kama Arusha tu. Isitoshe Wakenya wanaongea na kukipenda Kiswahili tofauti na jinsi Watanzania wengi wanavyohisi kuhusu Wakenya. Kwa kweli ukiwa Kenya unajisikia nyumbani. Utasikia watu wanakusalimia habari mzee. Wanasema yule "demu" ameondoka. Wanakuambia bia baridi ndiyo yenyewe. Wageni wengi wangependa kufahamu na kuzungumza Kiswahili wakiwa Kenya. Watanzania mpo?

Nairobi nayo inatatizo ya “traffic jam”

Mara baada ya kutua Jomo Kenyata International Airport na kuelekea Intercontinental Hotel, katikati ya jiji la Nairobi, tunapambana na Traffic jam kubwa. Pamoja na kuwa na barabara nyingi na zile zinazokatisha juu, lakini bado jiji la Nairobi lina tatizo la Traffic jams!

Kumbe si Dar tu. Kama hakuna utaratibu mzuri, kuwa na barabara nyingi na pana hakuwezi kumaliza tatizo la "traffic jam" katika miji yetu.

Kweli inawezekana watoto wasiwe wa kwako

Nipo hapa Intercontinental Hotel Nairobi, Kenya. Nimekutana na wasomi kutoka Kenya, Uganda, Eriteria, Burundi na Rwanda. Siku ya leo tumezungumzia sana kuhusu kilichotuleta hapa Kenya hasa kuhusu masuala ya "Kupelemba na Kutathmini "( Monitoring and Evaluation)shughuli za Utafiti, Ugani na Mafunzo katika eneo hili la Afrika ya Mashariki na ya Kati.

Mazungumzo nje ya hilo yanagusa masuala mbalimbali.Lakini kwa kuwa ni watu wazima na tupo jinsi mbili tunazungumza yanayotuhusu katika maisha yetu ya kila siku. Katika hilo lililochukua muda mwingi ni mahusiano ya ndoa. Imebainika kuwa mwanamke anaweza kubeba siri kubwa kuhusu baba halisi wa watoto. Je hili mnalionaje wana mtandao?

Taxi za njano

Ukitua uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta jijini Nairobi utakutana na magari mengi sana ya aina mbalimbali na mazuri kwa kusema ukweli. Hata hivyo magari madogo ya abiria yaliyopakwa rangi ya njano yanavutia zaidi hapo uwanjani (Lakini si magari ya Dar Young Africans). Magari hayo ni utambulisho kuwa ni zile Taxi zinazo park uwanjani hapo na ubavuni kuandikwa JKIA. Magari hayo ni masafi yanavutia na yana utaratibu mzuri kwa abiria. Ni vizuri kwa Taxi za zinazo park Dar- Mwl. Julius Nyerere International Airport zikaiga utaratibu huu na kuwa na nauli zakuridhisha kwa wateja na si kuwatega watejawaingizwe king! Kipato hakipatikani kwa ujanja ujanja! Tuwe wastaarabu na tuvute wateja kwa mambo mazuri.

Watanzania tulishapita hatua ya Waamerika

Niko hapa Nairobi Kenya, nimetoka kwenye "reception dinner" iliyoandaliwa na wenyeji wetu ASARECA kwenye warsha hii ya "Kupelemba na Kutathmini" miradi ya ASARECA.



Kwa faida ya wale ambao hawaifahamu ASARECA. Huu ni chombo cha Afrika mashariki na Kati kinachoangalia masuala ya Utafiti, Ugani na Mafunzo Katika Kilimo.



Ndugu zangu wa Kenya wamekiri kuwa hakuna cha kushangaza kuhusu Obama kuwa Rais wa Amerika. Watanzania wameshapita hatua hiyo siku nyingi. Wanaeleza wenyewe kuwa kwa Tanzania hawakuwa na sababu ya kufahamu kuwa Mkapa alikuwa anatoka wapi. Walichotaka ni kuwa na Rais atakayeweza kuisimamia nchi ya Tanzania. Watanzania tupige makofi basi kuwa tunawazidi hata Waamerika kwa hilo. Lakini kwa nini hatupigi hatu kwenye Maendeleo?

Friday, November 14, 2008

Habari na Mawasiliano ni nyenzo muhimu katika Kilimo

Mwezi Septemba mwaka 2008 nilibahatika kuhudhuria warsha ya wadau wa habari na mawasiliano katika sekta ya Kilimo kutoka nchi za SADC iliyofanyika nchini Botswana, jijini Gaborone.

Nchi 14 ukiondoa Afrika ya Kusini zilishiriki warsha hiyo iliyokuwa na dhumuni la kuona jinsi gani nchi za SADC zinavyoweza kuwasiliana na kutumia tekenoljia ya habari, katika masuala mbalimbali ya kilimo kwa kutumia vyombo mbalimbali kwa kuzingatia wadau.

Wakati umefika sasa wa kukitangaza kilimo kama vile inavyotangazwa " cocacola" lakini mawasiliano hayo ni vyema yakawaongezea maarifa wadau wetu wa kilimo. Tunataka kilimo chenye kumnufaisha mkulima.

Kuna mambo mazuri yanayofanyika katika nchi hizi ambazo yanawezwa kuigwa na nchi nyingine lakini hayafahamiki. Kuna matukio muhimu yanayotokea katika sekta ya kilimo lakini yanabakia palepale. Basi ilionekana kuwa kuna umuhimu wa kila nchi kuangalia jinsi ya kutumia taarifa, mawasiliano na teknolojia ya habari katika kuboresha sekta hii.

Wakati viongozi wetu wanapiga kelele na kuhamasisha uzalishaji katika kilimo, habari na mawasiliano ni nyenzo muhimu itakayosaidia kuboresha kilimo chetu. Pichani wanaonekana washiriki wa warasha hiyo.

Kanisa Katoliki Parokia ya Vikindu -Mt. Vincent wa Paulo



Hili ndilo Kanisa ninalosali mimi. Kanisa Katoliki la Parokia ya Vikindu. Kanisa hili tumelijenga kwa nguvu zetu sisi waumini pamoja na marafiki zetu wa ndani na nje ya nchi. Kanisa hili limejengwa na baadhi ya waislamu waliojitolea bila kujali tofauti ya dini.Ndiyo hatukumsubiri OBAMA.Tulijtegemea wenyewe.

Nilipohamia Vikindu-Kisemvule mwaka 2004, tulikuwa tunasali kwenye ukumbi mdogo tu. waumini tulikuwa wachache sana hata sadaka ilikuwa chache pia. Ibada Takatifu siku ya Jumapili ilikuwa ni moja sasa kuna misa ya pili ya watoto. Kanisa hili zuri lina vipaaza sauti, lina madawati mazuri ya kukalia, lina kwaya nzuri pia na kwa kweli linapendeza ndani na nje. Karibuni sana Vikindu.
Parokiani Vikindu kuna Zahanati nzuri tu, kuna shule ya watoto wadogo na shule ya msingi ambayo hufundisha kwa kiingereza zote zinamilikwa na Parokia ya Vikindu. Kanisa limeleta maendeleo ya kiroho na kimwili. Watawa wa Vikindu wanapaita mahali hapo "Jesus Town"

Hongera wanamichezo wa "KILIMO"

Timu ya michezo ya Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika mwaka huu 2008 imefanya maajabu kule Morogoro kwenye mashindano ya SHIMIWI. Wameweza kuwa washindi wa jumla wa tatu kati ya timu 54 zilizoshiriki.

Kilimo imeweza kuwa mshindi wa tatu katika mpira wa Miguu, mshindi wa nne mpira wa pete, bao mshindi wa pili na riadha wamepata medali. Hii imetokana na maandalizi mazuri, kujituma na nidhamu ya hali ya juu waliokuwa nayo wachezaji wakati wote wamaandalizi na mashindano. Hongera sana Mwenyekiti wa Kilimo Sports Klabu Bw. George Mbelwa.

Maximo unaikomoa Tanzania si Kaseja

Anayekomolewa ni Mtanzania na si Kaseja. Kama Kocha Maximo una ugomvi na Kaseja basi nendeni kortini. Usituharibie soka letu. Kaseja bado ni mlinda mlango na 1 hapa nchini. Mimi ni mpenzi wa Simba hata hivyo bado namuona Kaseja ni golikipa bora licha ya kuwa amehamia Yanga. Maximo mpange Kaseja timu ya Taifa uone vitu vyake achana na huyo Ivo Mapunda anayetematema mipira hovyo.

Machungwa yako sokoni

Watanzania sasa tunaanza kufaidi matokeo ya teknolojia bora za kilimo. Machungwa sasa yanapatikana sokoni wakati huu mwezi Novemba tena matamu sana, tena makubwa na tena kwa bei poa.

Iwapo sekta ya kilimo itaongezewa raslimali kwa asilimia 5 tu , kile kisichowezekana kitawezekana na kuwa na ziada. Mazao mengi yanayoonekana sokoni hivi sasa ni juhudi za mkulima huyu mdogomdogo, asiyekuwa na pembejeo bora za kilimo, anayetumia zana duni za kilimo na anayetegemea kilimo cha mvua!

Si mshabikii OBAMA

Nimefurahi kuwa OBAMA ameshinda kinyang'anyiro cha kiti cha Rais nchini Marekani.
  • Lakini sitegemei maajabu kutoka kwa OBAMA katika kuboresha maisha yangu
  • Kwa wale wanaotegemea misaada hiyo wasahau na haitakuwa rahisi kama wanavyofikiri wao
  • Wakumbuke kuwa OBAMA ni Mwamerika licha yakuwa ana rangi nyeusi!
  • Watanzania tuchape kazi
  • Watanzania tuongeze uzalendo na tuipende nchi yetu
  • Watanzania tuwe wabunifu
  • Watanzania tupunguze kulalamika bila sababu ya msingi
  • Tupunguze vitendo vya rushwa

Kwa hiyo simshabikii OBAMA

Viongozi wa nchi wavalia njuga kilimo na kuona kuwa inawezekana

Viongozi wetu wengi wameanza kuhamasisha na kufuatilia shughuli za uzalishaji wa kilimo kwa vitendo na sasa inaonekana kuwa kila kitu kinawezekana kwa ajili ya kuendeleza Kilimo.


Hivi majuzi tu Waziri Mkuu Mhe. Mizengo Pinda katika ziara yake mkoani Dodoma aliweka mkwara mkali kwa wakuu wa wilaya na mikoa kwamba wakati wa kuvaa suti kila siku umekwisha wanahitajika kuvalia njuga kilimo kwa nguvu zao zote.


Tayari Mkuu wa wilaya ya Kondoa Bw Seif Mpembenwe amemweleza Waziri Mkuu kuwa wilaya yake inaweza kujitosheleza kwa chakula. Sasa kama wilaya zote zitaahidi hivyo na kukipa kilimo kipaumbele katika shughuli zake, tatizo liko wapi?

Thursday, November 13, 2008

Wamisionari wametuachia urithi mkubwa lakini bado tumelala

Wiki ya jana nilisafiri kwenda Morogoro kushiriki katika mazishi ya Binti yetu Rose Aniani Mbiki (Mtoto wa mdogo wangu) aliyefariki pale Bigwa Morogoro. Mungu ailaze mahali pema peponi roho ya marehemu Rose.

Ibada takatifu ya mazishi ya kumuombea marehemu ilifanyika kwenye kanisa la Bigwa (Sekondari ya Masista-Bigwa). Sijawahi kuingia ndani ya Kanisa hilo lakini nilivutiwa sana kwa jinsi Kanisa hilo lilivyojengwa kwa matofali ya kuchoma kwa mpangilio mzuri tu. Milango ilivyotengenezwa inapendeza na utaalamu wa hali juu umetumika.

Makanisa mengi ya jimbo la Morogoro yamejengwa zamani na Wamisionari. Ukiangalia utaalamu uliotumika ni wa hali ya juu sana ukizingatia na hali halisi ya vifaa kwa wakati ule. Bado sielewi, hivi ni kwanini tunashindwa kuuendeleza utaalamu ule? Udongo ni uleule watu wapo kwanini tusiboreshe yale tuliyoyakuta na kusonga mbele? Ajira tunazozitafuta si kama hizi za ujenzi? Vijana wangapi wa Bigwa, Matombo na Morogoro kwa ujumla wamerithi taalama hii ya ujenzi au wanajenga kwa kulipua tu?

Wafanyabiashara ndogondogo waelimishwe

Idadi kubwa ya watu jijini Dar Es Salaam na miji mingine hapa nchini hufanya biashara ndogondogo. Lakini leo hii nitazungumzia biashara za vyakula, matunda na vitafunwa.

Utamkuta mtu anauza korosho, karanga, majibaridi, maembe, pilau, samaki wa kukaanga n.k. Lakini yeye mwenyewe mchafu, chombo alichowekea chakula kichafu, mazingira anayouzia chakula ni machafu. Hivi kweli kwa hali hii mteja anaweza kuvutiwa na biashara yako?

Mimi napenda sana kutafuna korosho, lakini wakati mwingine nasita kununua korosho ambazo zinauzwa na mtoto mdogo mchafu ambaye huchezea chezea korosho hizo wakati akizipanga kwenye mafungu. Au utakuta mwanamama anauza chakula huku ananyonyesha au kujikuna sehemu mbalimbali. Kwa hali hii ni vizuri wafanyabiashara ndogondogo wakaelimishwa. Si elimu ya mikopo tu bali jinsi gani wanavyoweza kuvutia biashara zao.

Sababu za foleni barabara ya Kilwa

Barabara ya Kilwa ninaitumia karibu kila siku. Kwa sasa barabara hiyo iko kwenye ukarabati mkubwa. Barabara inapanuliwa na madaraja mapya yanajengwa. Kutokana na hali hiyo huwa kunatokea usumbufu mkubwa wa usafiri wakati wa asubuhi na jioni. Safari ya dkika ishirini inaweza kuchukua zaidi ya saa moja. Sababu kubwa ya kuwa na foleni yakukatisha tamaa hata kusababisha watu wengi kutembea kwa miguu ni hizi hapa.

  • Madereva wasiozingatia sheria na taratibu za kuendesha magari
  • Wajenzi wa barabara kutoweka vizuizi kwa sehemu ambazo hazistahili kupita magari
  • Askari wa Usalama barabarani (Traffic Police) kutofanya kazi yao barabara kwa kuelekeza za kupita magari.
  • Viongozi wa Manispaa ya Temeke kutolishughulikia suala hili ili liweze kupatiwa ufumbuzi wa muda wakati barabara hiyo inajengwa.

Wafanyakazi wa Kilimo watakiwa kufanya Kazi kwa taaluma

Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi la Wizara hiyo Bw Peniel Lyimo, ametoa agizo kwa wafanyakazi wote wa wizara yake kufanya kazi kwa kuzingatia taaluma zao walizoajiriwa ili kuboresha utendaji wa kazi.
Akitoa mfano alisema kuwa si vizuri kwa Mkufunzi kufanya kazi za Mhasibu au Mhasibu kufanya kazi za ugavi. Alisisitiza kwa kusema kuwa kazi zote zinafanywa kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu kulingana na taaluma.

Mwenyekiti huyo alitoa agizo hilo wakati wa kikao cha Baraza kilichofanyika tarehe 8/11/2008 mjini Morogoro katika Ukumbi wa Morogoro Hotel na kuhudhuriwa na wajumbe mbalimbali wa Baraza hilo wakiwemo Wakurugenzi, Wakurugenzi wa Kanda, Wawakilishi kutoka Vyama Vya Wafanyakazi (TUGHE & RAAWU) na Wawakilishi wa Wafanyakazi.

Keep Left hiki cha Kituo cha Polisi Chang'ombe

Imenipasa kuandika kuhusu "Keepleft" kilichojengwa katika makutano ya barabara ya Sokota na na Chang'ombe karibu kabisa na Kituo cha Polisi Chang'ombe na Kanisa Katoliki Parokia ya Chang'ombe hapa jijini Dar Es Salaam.

Ukarabati wa barabara wa mahali hapo ambapo hapo awali palikuwa korofi sana sasa umekamilika na kipya kilichoongezwa ni kujengwa "Keepleft" asante sana. Lakini tangu kijengwe "Keepleft" hicho hakuona lolote la zaidi. Maua hayajapandwa.Kwa kifupi "Keepleft" hicho hakivutii kabisa sijui ni jukumu la nani. Manisapaa ya Temeke? TANROADS au nani ?Tuelewesheni basi.

Tuesday, November 4, 2008

Familia hii inapatikana SINZA kwa WAJANJA!



Ndiyo, familia kama hii inapatikana tu Sinza kwa wajanja. Wangalie walivyotulia. Bw na Bi Joseph Kamsopi Mdimi na wasimamizi wao pamoja na Binti yao EKA.

Hata Makaka na Madada walikuwapo na walitoa zawadi



Furaha ilioje kwa mdogo wetu, kaka yetu mpendwa wetu Kamsopi kupata jiko. Basi pokea zawadi yetu ya JIKO ili Flora akaangize!

Ninyweshe ni kunyweshe!


Ndivyo ilivyokuwa pale Africentre. Flora na Joe wakinyweshwana usiku wa tarehe 18 Oktoba 2008. Hakika raha tupu!

Flora alipata Kabati ya "Mbeho"




Inasemekana kuwa ukitaka kuchumbia mtoto wa Kichagga utaulizwa kuwa je huyo mchumba ana Kabati ya Mbeho? Na kweli Flora aliuliza swali hilo na Joseph alijibu ndiyo. Na kweli bwana, Mwenyekiti wa Kamati Bw Inno Banzi alimkabidhi Flora Yesusaa Msechu Kabati ya Mbeho siku ya harusi yao tarehe 18/10/2008.

Bwana na Bibi Mangengesa Mdimi walifurahi


Tarehe 18/10/2008 pale Afri-Centre jijini Dar- Bw na Bibi Mangengesa Mdimi walijawa na furaha kubwa kushuhudia sherehe ya watoto wao Joseph na Flora. Waangalie wanavyowakaribisha wageni waalikwa kwa kupunga mikono yao juuu juuu kabisa. Hongera sana

Monday, November 3, 2008

Joseph Kamsopi afanya kweli


Kijana mtanashati wa mchanganyiko wa Kimanda kutoka ziwa Nyasa na Kiluguru kutoka Morogoro mji kasoro bahari-Matombo, Kiswira - Joseph Kamsopi Mdimi amefanya kweli baada ya kufunga pingu za maisha na Bi Flora Yesusaa Msechu wa Kilimanjaro.



Harusi hii ilifungwa katika Kanisa Katoliki la Mwenye Heri Anuarite, Makuburi -External - Dar Es Salaam tarehe 18/10/2008 na kisha sherehe ya kufana ilifanyika katika Ukumbi wa Afri-Centre Msimbazi - jijini Dar Es Salaam. Hebu waone maharusi hapo kushoto juu wanapendeza ehee!

Friday, October 24, 2008

Watanzania wameanza kutojiamini

Inavyoonekana kuwa kwa sasa hali ya kujiamini kwa Watanzania inapungua kwa kasi ya kutisha. Hii inajionyesha kwa kuvuja mitihani, majengo kuanguka, mabarabara kujengwa kwa kiwango cha hali ya chini. Wagonjwa kupata tiba isiyowahusu. Kutofanya vizuri kwenye michezo ( olimpiki 2008).

Kama mwanafunzi amehudhuria elimu ya sekondari kwa miaka 4 kwa nini aibe mtihani? (Huko ni kutojiamini). Kama mwanamichezo amefanya mazoezi vizuri na kufuata miiko ya wanamichezo sioni sababu ya kutofanya vizuri.

Kama wahandisi wamepata elimu na uzoefu wa kutosha katika kazi yao kwanini washindwe kusimamia kazi zao za ujenzi.

Watanzania turudishe hali ya kujiamini hata kama tunakosea lakini tunajifunza kutokana na makosa tunakokwenda siko. Watakuja wageni kutufanyia kila kitu kwani hatujiamini na hatuaminiani.

Asilimia 62 ya wahitimu wa darasa la saba kupata sifuri kwenye hisabati ni hatari

Waziri Mkuu Mhe.Mizengo Pinda alipokuwa akitoa hoja ya kuahirisha mkutano wa kumi na mbili wa Bunge-Dodoma tarehe 29 Agosti 2008 moja ya mambo aliyozungumza kwa uchungu sana ni wanafunzi kushindwa vibaya mtihani wa hisabati. Alisema. Kwa mfano mwaka 2001, katika mtihani wa kumaliza Darasa la saba, asilimia 62 ya watahiniwa katika Wilaya ya Morogoro Vijijini walipata sifuri katika Mtihani wa Hisabati. Hii ina maana kuwa asilimia 62 walimaliza shule bila kujua Hisabati rahisi za kujumlisha, kutoa , kuzidisha na kugawanya.

Hali hii ni mbaya sana. Inaonekana kuwa wanafunzi hawaoni umuhimu wa somo la hesabu, walimu pia kadhalika na wazazi tuseme na taifa zima.

Enzi zetu mwanafunzi ukifahamu hesabu hizo sifa tu unazomwagiwa mwenyewe utapenda hesabu. Na kama hujui hesabu ulikuwa unadharauliwa. Hata Sekondari waliokuwa wanachukua sayansi waliheshimika na wale wa sanaa au "arts' kwa kweli walionekana kama wapo wapo tu. Hata mzazi aliona ni sifa kwa mwanae kuchukua sayansi.

Tatizo letu Watanzania ni jinsi tulivyobadilika kirahisi kimtazamo katika mambo mbalimbali hasa elimu. Tunapenda mambo rahisi. Sasa hivi kila mtu yuko kwenye menejimenti, siasa na biashara! Kwa hali hii si rahisi mtoto kupenda hesabu. Hesabu zinatakiwa kutulia. Kama alivyosema Waziri Mkuu. Hesabu inajenga dhana ya kujiamini, kujenga falsafa ya mambo kwa mpangilio wenye mantiki (Logical Thinking).

Wito wangu ni kufufua ari ya kupenda hesabu na ionekana kwa watoto wetu kuwa bila hesabu huko mbele ni giza.Ijionyeshe waziwazi katika maisha yetu ya kila siku jinsi hesabu zinavyofanya kazi. Labda nihitimishe kwa kusema kuwa mwanafunzi yeyote anayepuuzia hesabu atapata matatizo makubwa katika kuendelea na elimu yake popote pale.


Wenzangu wa Moro sijui kama tumeshaanza kuchukua hatua ya kujikwamua kutoka katika aibu hii. Na hasa ikizingatiwa kuwa ni Morogoro vijijini kwani huko hakuna shule za kulipia kwa hiyo ni watoto wa malofa hawajui hesabu toba!

Thursday, October 23, 2008

Machungwa bado yanapatikana Dar

Msimu wa maembe umeanza, lakini machungwa bado yanapatikana Dar tena kwa bei nafuu sana. Shilingi 100/= kwa chungwa moja. Machungwa ya sasa ni matamu sana. Nawapongeza sana wakulima wetu kwa jitahada zao kubwa za kuhakikisha kuwa karibu kila zao linapatikana mwaka mzima. Miaka ya nyuma ilikuwa ni nadra sana kula chungwa hapa Dar kwa wakati huu. Hii ni dalili nzuri kuwa kuna teknolojia imeongezeka katika kilimo. Hii ni dalili nzuri pia kuwa wakulima hawa wakiongezewa uwezo wanaweza kufanya makubwa.


Nchi yetu imebahatika kuwa agroekolojia mbalimbali ambazo zinaweza kustawisha mazao mbalimbali kwa nyakati tofauti. Vile vile zina aina tofauti za udongo licha ya kuwa na vyanzo vingi vya maji ambavyo bado havijatumika kikamilifu kwa uzalishaji wa kilimo.

Wednesday, October 15, 2008

Kushindwa kwa CCM Tarime ni funzo

Licha ya kuwa jimbo la Tarime hapo awali lilikuwa chini ya umiliki wa CHADEMA na sasa baada ya kufanyika uchaguzi mdogo CHADEMA imelirudisha tena jimbo hilo kwenye himaya yake huku ikikiacha Chama Cha Mapinduzi KULIKONI Tarime?

Msimu wa maembe umeanza

Msimu wa maembe umeanza. Dalili nzuri zinaonyesha ukipanda boti pale Kivukoni. Embe ndogondogo zilizoiva vizuri zikiwa zimepakiwa kwenye matenga zinavushwa kwenda mjini kwa kuuzwa. Embe hizi ni nzuri.

Tanzania tumebahatika sana kwa kuwa na hali ya hewa inayoweza kustawisha mazao mbalimbali na kwa misimu tofauti kwa gharama nafuu. Kilimo hiki ni kizuri lakini si endelevu. Kwa mfano hakuna mikakati ya kuweza kumuinua mkulima katika uzalishaji wa matunda, mboga, korosho na nafaka. Mabenki yetu haioni kuwa wakulima wanakopeshaka na kwa vile tu wanataka fedha zao zilirudi kwa msimu mmoja. Hii haiwezekani kwenye kilimo. Mkulima lazima apewe muda mrefu ili aweze kuzalisha kwa faida na kuweza kurejesha mikopo hiyo. Hali ni ile ile kila mwaka na mkulima ni yule yule, mfanyabiashara naye habadiliki kila mwaka kusukuma tenga la maembe machache kuyachuuza mitaani!

Bei ya nyama ni juu Dar


Kwa wakazi wengi wa jiji la Dar Es Salaam hasa wa kipato cha chini kula nyama ni anasa. Bei ya nyama ya kawaida kwa sasa ni zaidi ya Tshs 3800/= kwa kilo. Hivi kweli kuna vigezo sahihi vinavyofanya nyama ipande kwa kiasi hicho?


Inasemekana hali si mbaya sana kwenye soko la jumla. Lakini wauzaji wa rejareja ndiyo wanaopandisha bei kiholela. Kibaya zaidi vipimo vinavyotumiwa si sahihi. Walaji wanadhulumiwa sana. Sijui kama Uongozi wa Jiji unafahamu hili. Hali ni mbaya lishe ya wananchi inakosekana hasa proteini inayopatikana kwa kula nyama.

Thursday, October 9, 2008

Kubonyeza kengele ovyo ndani ya bus si ustaarabu

Kutokana na tatizo la usafiri hapa jijini Dar Es Salaam.Mjasiriamali mmoja, tena Mtanzania ameleta mabus mazuri licha ya kuwa ni mitumba ili kuweza kuboresha usafiri hapa jijini. Mabus haya ni ya kisasa na ni makubwa. Kila dirisha lina kengele inayotumiwa na abiria kumtaarifu dereva asimamishe bus iwapo anataka kuteremaka kituoni au kama kuna dharura.

Jambo la kushangaza, abiria wasio wastaarabu wanazitumia kengele hizo vibaya kwa kubonyeza kila wakati na hivyo kumfanya dereva kusimama wakati hakuna anayeshuka wala hakuna dharura yoyote. Ndiyo maana nasema kubonyeza kengele ovyo ndani ya bus si ustaarabu. Kutonana na hali hiyo sasa kengele hizo hazifanyi kazi (disconnected).

WIKI YA NYERERE SIJUI MNAONAJE

Vyombo vya habari vimeanza kuandika sana kuhusu wiki ya Nyerere 13-18 Oktoba.

Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere ndiye Rais wa Kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Nyerere ameongoza Taifa hili kwa muda mrefu sana yapata miaka 21 (Tanzania). Kipindi hicho si kidogo ni umri wa mtu mzima +3. Katika kipindi hicho mambo mengi yamepangwa na mengi ambayo yametekelezwa na ambayo hayakutekelezwa.

Wakati yanaandikwa mengi kuhusu Nyerere. Kuna baadhi ya Wataznania wanadai kuwa Nyerere alitupeleka pabaya! Hivi ni kweli? Kama kweli kumbukumbu hii ni ya kinafiki. Mimi namuheshimu sana Mwl. Nyerere na sera zake nazikubali. Watanzania wengi wamefikishwa hapa walipo kutoka na sera zilizokuwepo za elimu, afya na uzalishaji. Sijui wenzangu mnaonaje.

Wednesday, October 8, 2008

Dar ikitekeleza mipango yake itaipita Gaborone

Jiji la Gaborone ni dogo ukilinganisha na jiji la Dar Es Salaam. Wakazi wake pia ni wachache sana. Hakuna pilikapilika nyingi mchana na usiku. Maduka yake si mengi na wala si ya kutisha, lakini mipango ya kuendeleza jiji hilo ipo, inaonekana na inatekelezwa. Mji ni msafi, nyumba zimejengwa kwa mpangilio mzuri. Utaratibu wa usafiri umepangwa vizuri. Si rahisi kuona malori makubwa kwenye njia za magari ya abiria.


Dar Es Salaam tuna mambo mazuri mengi tu. Jiji kubwa, watu wengi, wajanja, wakarimu . Maduka mengi, bidhaaa mbalimbali na mazao mablimbali yanayopatikana wakati wote. Bahari tunayo, mvua inapatikana misimu miwili. Wasomi wapo, mipango mizuri ipo. Tatizo ni nini?


Hatutekelezi kikamilifu tuliyojipangia- Hilo ndilo tatizo kubwa! Blaa blaa nyingi tu. Mtu anakojoa mchana kweupe, hakuna anayejali! Malori yenye shenena za mafuta yanaachiwa bandarini saa 9.00 wakati wafanyakazi wanarudi kutoka kazini - matokeo take foleni yakujitakia kabisa! Hakuna anayejali. Hilo ndilo tatizo la Dar.Vinginevyo, naipenda Dar yangu na iwapo tutarekebisha mambo yetu, ukiondoa J'BURG, na Capetown miji mingine iliyobakia kusini mwa Afrika itaburuzwa na Dar.

MASAKI SASA INAPENDEZA

Ni muda mrefu sijawahi kutembelea maeneo ya Masaki (Oysterbay). Ukiondoa Baharini na beach zake sikuwa na sababu ya kwenda huko. Lakini Jumapili iliyopita nilipata mwaliko wa ndugu yangu anayeishi huko kuhudhuria sherehe za watoto wake waliopata komunio. Kwa kweli Masaki imebadilika sana. Nyumba nzuri zimejengwa na zinaendelea kujengwa. Barabara zimekarabatiwa, mitaro ya maji machafu inajengwa.Maduka mazuri yamefunguliwa. Wale mbuzi waliokuwa wakila michongoma sasa hawapo tena! Kweli Masaki sasa inapendeza hakuna tofauti na Majuu au South!

Traffic chunguza mabus ya Mkuranga-Kigamboni

Jumamosi iliyopita wakati narudi nyumbani kwangu nilipitia Kigamboni nikidhani kuwa nitapata usafiri mzuri nikiogopa foleni ya barabara ya Kilwa wakati wa jioni.

Waswahili husema nimeruka mkojo nimekanyaga mavi! Pale Kigamboni stendi ya mabus ya kwenda Kongowe, Mjimwema na Kibada mabus yenye maandishi ya Mkuranga -Kigamboni yalikuwepo lakini yalikuwa yanakatisha mwisho Kibada au Mjimwema. Usafiri ulikuwa ni wa shida sanaTulipoteza karibu saa moja kabla hatujakubaliana na kulipa shilingi 1,000/= kwenda Kongowe!

Mabus haya ya Kigamboni-Mkuranga kwa kweli hayasafiri kwenye njia iliyopangiwa ni ujanja tu wakupata njia, Traffic angalieni hilo wananchi wanaumizwa hali ni mbaya.

Mitihani kuvuja-Lawama kwa wazazi,wamiliki shule

Kuanzia Jumatatu juma hili, mitihani ya kumaliza kidato cha nne inaendelea nchini kote. Mtihani ni utaratibu uliowekwa kwa ajili ya kuwapima wanafunzi uelewa wa masomo waliyojifunza kwa kipindi fulani.

Jambo la kusikitisha kusikitisha ni kwamba mwanzo si mzuri mwaka huu. Mara kipyenga kilipopulizwa cha kuashiria kuanza kwa mitihani hiyo, tayari mtihani wa hesabu umeshavuja!
Shule za "English Medium" na za kulipia ndiyo hasa zilizobambwa katika mkasa huu-k.m. Happy Skillful! Ni aibu kwa kweli. Ni aibu kwasababu wazazi wamewasomesha watoto wao kwa gharama kubwa lakini hatimaye wanaiba mtihani.

Lakini kwa upande mwingine wazazi nao wanahusika kwa kiasi kikubwakatika kashfa hii. Wanafunzi watapata wapi fedha za kununua mtihani? Pengine tuseme wamiliki wa shule, hasa hizi za kulipia maana wanataka sifa, wanataka kujitangaza kuwa wee-HappySkillful - Mathematics A- 20! Kati ya hao wasichana ni 12! Acha mchezo. Kwanini wazazi wasishawishike kuwapeleka watoto huko na kwa kufanya hivyo - definetily mwenye shule ataongeza karo. Mikakati iwekwe kukomesha mtindo huu vinginevyo watoto wa wanyonge hawataona Kidato cha Tano na huko Chuo Kikuu itakuwa ni ndoto. Hivi kweli tunalipeleka wapi Taifa hili. Ama kweli sitakosea kwa kuliita kuwa ni Taifa la "Vodacom"

Thursday, September 25, 2008

Nchi za SADC na Upashanaji Habari katika Kilimo

Wataalamu 22 kutoka nchi 14 zilizo katika umoja wa SADC wanaendelea na warsha ya kujadili jinsi ya kutumia nyenzo ya Habari na Mawasiliano katika kuboresha uzalishaji katika Sekta ya Kilimo. Wataalamu hao wanaangalia ni wadau gani wanaohitaji habari za kilimo, wanazitumiaje habari hizo, zinapatikanaje, mikakati gani itumike kuhakikisha kuwa mfumo unakuwepo wa kutumia habari na mawasiliano ili utumike katika kuwasaidia watunga sera na watoa maamuzi katika utekelezaji wa mipango ya maendeleo katika sekta ya kilimo, ni uwezo gani uliopo kwenye masuala ya habari na mawasiliano kwa wadau wa kilimo. Nyenzo na utaalamu upo? Hayo ndiyo mambo yaliyotuleta hapa Gaborone, Botswana kwa muda wa siku tatu. Tanzania inawakilishwa na wataalamu wawili huku jinsia ikizingatiwa. Wataalamu wanatoa hoja zao za nguvu mambo yanachambuliwa na kuwekwa sawa. Hatimaye viongozi wetu tutawaeleza. Cha ajabu katika kundi hili Afrika ya Kusini hawamo licha ya kuwa wanachama wa SADC. Naambiwa aah wao wameshapiGa hatua kubwa kwenye nyanja hii. Nchi zinazoshiriki katika warsha hii ni Tanzania, Zambia, Malawi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Kongo (DRC),Zimbabwe, Lesotho, Swaziland,Mauritius,Seychelles,Madagascar,Mozambique,Angola,Namibia na wenyeji wetu Botswana.

Wednesday, September 24, 2008

Mashamba katika mchoro wa "Pie Chart" Afrika ya Kusini

Ukiwa angani wakati unatua jijini Johanesburg, Afrika ya Kusini, ukichungulia dirishani utaona maumbo ya kupendeza sana ya mashamba. Hakuna sababu ya kumuuliza mtu, unaona mashamba katika maumbo mbalimbali. Kumbe inawezekana kabisa kuwa na mashamba katika maumbo ya mduara na kutengeneza maumbo ya "Pai" kutegemea na mazao unayozalisha. Kama mkulima analima ngano kwa wingi basi sehemu kubwa ya mchoro inakuwa ni ngano hivyo hivyo kwa mazao yanayolimwa kwa sehemu ndogo na wakati tofauti kiasi cha kutoa picha nzuri ukiwa angani. Hata rangi zinajionyesha waziwazi. Kumbe hata wakulima wanazitumia hesabu za "pai" vizuri. Hapo ndipo walipofikia wasouth kwenye kilimo. Kwa hali hii mwanafunzi ataogopaje hesabu kwani anaona jinsi inavyotumika.

Kweli Botswana ni nchi ya nyama

Unapoingia kwenye ndege ya Air Botswana haipiti hata dakika 10 kabla hujarushiwa kipaketi cha nyama ya kukausha safi kilichofungwa vizuri utafune kwa raha zako huku wakikuuliza ni kinywaji gani unataka ushushie. Botswana hapo wanaanza kutangaza nyama. Jana jioni kwenye chakula cha jioni pale Grand Palm Hotel kulikuwa na nyama zilizotayarishwa kwa njia tofauti na ni nyingi tu. Mchana huu tumepata chakula chetu huku nyama zikiwa nyingi tu tena zimeandaliwa vizuri hata mifupa imekatwa vizuri! Ilibidi nimuulize Mtswana mmoja . "Nyie mnakula nyama sana hampati ugonjwa wa "gaoti"? Yeye alisema tatizo hilo limeanza kujitokeza sasa hasa kwa wanaokunywa pombe! Tanzania tunashindwa hata kuwatayarisha vizuri dagaa kamba "prawns" na kufanya bite kwenye AIR Tanzania?

ATCL mnatuangusha

Niko jijini Gaborone, Botswana tangu jana kuhudhuria warsha kuhusu Menejimenti ya Habari na Mawasiliano katika Utafiti wa Kilimo na Maendeleo. Safari yangu kufika hapa haikuwa nzuri hata kidogo. Kwanza tulichelewa kuondoka Dar kwa masaa 8. Kwasababu hiyo tuliikosa ndege ya kuunganisha toka Johanesburg kwenda Gaborone. Hata hivyo tulifanikiwa kuunganishwa kwenye ndege ya AIR Botswana. Wakati wote tulipokuwa Dar tukisubiri kuundoka tulikuwa tunatangaziwa kuwa tutaondoka saa 5.30, mara saa 7.30 kitu ambacho hakikutokea hadi tulipoondoka saa 8.30. Abiria wapatao watatu ilibidi wavunje safari zao kwani walijua kuwa wasengeweza kuwahi shughuli zao au kupata ndege ya kuunganisha huko waendeko.

Wazungu wawili (mtu na mkewe) tuliosafiri ndege moja ambao walikuwa ni watalii kutoka Afrika ya Kusini hawakusita kusema kuwa walipokuwa Tanzania mambo yalikuwa mazuri sana walisifu vivutio vyetu vya utalii (Bara na visiwani) ni vizuri sana na kusema Watanzania ni wakarimu sana na ni wa amani. Tatizo ni kwenye usafiri wa ndege kwani wakati wakiwa nchini kulikuwa na uchelelewaji wa ndege kuondoka kila waliposafiri na hasa ATCL. Ndugu zangu ATCL kweli mnatuangusha. Tatizo ninaloliona mimi ni menejimenti kuto kutoa uamuzi sahihi kwa wakati unaofaa. Halafu pale Airport kuna wafanyakazi wengi tu wanazagaa zagaa sijui na wa Swissport kazi yao ni nini?

Sunday, September 21, 2008

Samaki uhai wa akina mama wa Mkuranga

Kila siku asubuhi asilimia 40 ya wasafiri kutoka Mkuranga kwenda jijini Dar ni wanawake. Wengi wa wanawake hawa hubeba ndoo za plastiki. Hii inaashiria nini? Ndoo hizo hutumika kubeba samaki wanaowanunua kutoka soka la samaki Kigamboni. Wanawake hawa ni mahili sana. Hujua kukimbilia mabasi, huamka mapema asubuhi na hutunza fedha zao sehemu ambayo itakuwa vigumu kwa vibaka kuiba! Jem biashara ya samaki inalipa? Anajibu mama mmoja. Inalipa baba ikiwa unamtaji mzuri. Pia inategemea soko kule Kigamboni. Kweli akina mama hawa wameweza kufanya mengi kupitia biashara ya samaki kama vile kusomesha watoto. Aidha huwasaidia akina baba kuboresha bajeti ya nyumbani!

Wednesday, September 17, 2008

HIVI TUNAELEWA NYIMBO ZINAZOIMBWA KWA LUGHA YA KIINGEREZA?

Adamu Lusekelo ni Mwandishi Mwandamizi hapa nchini. Mimi binafsi ninamfahamu. Jinsi anavyoandika ndivyo alivyo. Soma Mraba wake wa LIGHTTOUCH kila Jumapili kwenye gazeti la "Sunday News" utapata ujumbe kama utamwelewa unachokiandika. Anaandika kwa lugha nyepesi na ya kuvutia yenye mzaha lakini..... Hiyo ndiyo maana ya LIGHTTOUCH - pengine niseme ni "kuuma na kupuliza." Jumapili hii alikuja na kichwa cha habari " The Nasty generation gap!" (MPASUKO KWA VIZAZI ---tafsiri yangu). Alipoandika kuwa vijana walikuwa wanafurahia nyimbo iliyokuwa ikiimbwa ya " Do me ! Do me !" huku wakiirudia rudia. Nabaki nikijiuliza, je vijana hawa wanajua maana ya nyimbo zinazoimbwa kwa kiingereza? Maana wasanii huwa hawaimbi kwa lugha Nyepesi. Wastafsiri "Do me" kwa tafsiri nyepesi. Kwa kawaida wasanii hutumia lugha za mafumbo. Msikilize Juma Nature, Ali Kiba, Nyoshi El Sadat, Muhidin Gurumo. Utafahamu nini ninachozungumza. Nyimbo hiyo kwa tafsiri sahihi ni MATUSI! Niwaambieni.

Madereva Taxi wa uwanja wa ndege Dar acheni hizo

Kila Jumapili sikosi kumsoma Tony Zakaria kwenye Sunday News katika mraba wake unaojulikna kwa jina la "FIRINGLINE." Tarehe 14 September Tony alilamika jinsi tunavyoshindwa kutumia fura tuliyonayo ya utalii kuongeza pato la Taifa. Lakini alinifurahisha zaidi kwenye para moja alipoandika kuwa Madereva taxi waliopo uwanja wa Taifa wao wanaongalia jinsi gani ya kumtoza mteja fedha nyingi kutoka Uwanja wa ndege hadi anakokwenda. Kweli, ni kitu cha kawaida kabisa kuambiwa kutoka uwanja wa ndege hadi Mbagala/Kawe/Mwenge ni shilingi 40,000. Hivi kweli kwa bei hizi hata hao watalii wanaweza kulipa kweli. Tunapotoka tukiamini kuwa kila mtalii ni tajiri na yuko tayari kulipia kiasi chochote kwa huduma yoyote. Madereva taxi acheni hizo. Tuboreshe huduma zetu tutapata haki zetu.

Sera nzuri utekelezaji hafifu

Watanzania, na wasio watanzania, wasomi na wasio wasomi niolibahatika kuzungumza nao wanasema, Watanzania ni wazuri katika kuandaa sera lakini utekelezaji wa kile kilichoandaliwa una walakini mkubwa. Sekta zote zina sera nzuri iwe utalii, kilimo, viwanda, afya .... lakini kwanini hatuendelei? Je, sera zilizopo zinafuatwa? Nani wa kutekeleza sera hizo? Tatizo hilo tutalitatuaje. Tufikiri sote. Natumie maoni yako.

Saturday, September 6, 2008

Sabodo kaandika, Makwaiya "kalonga" simu za viganjani tunaibiwa

Mmoja wa matajiri wakubwa hapa Tanzania - Mzee Sabodo imembidi kulipia ukurasa mzima kwenye gazeti la "Daily News" wiki ya jana ili kulalamika jinsi watanzania tunavyoibiwa kijanja na makampuni ya simu za viganjani kwa gharama kubwa za huduma hiyo. Hakulalamika hivi hivi alikuja na mahesabu kuwa kwa sasa inasemekana kuna wateja milioni 15 wa simu za viganjani. Hebu fikiria iwapo kila mteja atutumia sh-50 tu kwa siku ni shilingi ngapi makampuni hayo yanavuna burebure tu. Kwa wiki, mwezi na mwaka je? Alihitimisha kwa kusema hii pengine ni skandali kubwa zaidi kuliko EPA au RICHMOND.

Jana Ijumaa, katika Gazeti hilo hilo la "DailY News" Mwandishi wa Habari Mwandamizi wa siku nyingi hapa nchini. Bw. Makwaia Kuhenga katika "Mraba" wake amejadili kwa kina aliyoandika Sabodo.

Hili si geni, blog hii iliwahi kumsikia Mbunge Ndesamburo akibainisha hili kwenye moja ya vikao vya Bunge kule Dodoma. Lakini Watanzania bado! Kweli simu za mkononi zina manufaa yake. Lakini tuangalie gharama yake. Kuna baadhi ya watu gharama ya simu kwa siku ni kubwa kuliko fedha anayoacha nyumbani kwa matumizi!

Wednesday, September 3, 2008

LUGALUGA WAANZA KUJITAYARISHA KWA KILIMO

Ushirika wa Kilimo na Maosko ujulikanao kwa jina la Lugaluga lenye makao yake makuu katika Manispaa ya Morogoro hivi sasa imeanza kutayarisha mashamba yao tayari kwa msimu wa kilimo 2008/9. Kwa mujibu wa Katibu wa Ushirika huop Bw. John Waziri. Ushirika huo una eneo la shamba lipatalo ekari 16,000 katika kijiji cha Kimambira wilayani Mvomero.

Ushirika huo wenye wanachama wapatao mia moja umepanga kulima ekari 2000 za mpunga kwa mwaka 2008/9.Tayari mipango ya kuwakopesha matrekta wanachama wa Lugaluga uko kwenye hatua za mwisho. Kupatikana kwa matrekta hayo yasiyopungua matano kutawawezesha washirika hao kutayarisha mashamba yao mapema tofauti ilivyokuwa mwaka jana ambapo matrekta yalichelewa kuanza kazi shambani.

Akiongea na blog hii Bw. John Waziri amesema kuwa wanapata ushirikiano mzuri kutoka kwa viongozi wa ngazi zote mkoani Morogoro wakiwemo Mkuu wa Mkoa Meja Jenerali Saidi Kalembo na Mkuu wa Wilaya ya Mvomero Bi Hawa Ngulume cha kutia moyo ni kwamba wameshatembelea eneo la shamba hilo kubwa.

Blog hii ilipata nafasi ya kufika kimambila na kuona shamba hilo na kushuhudia jinsi wananchama walivyokuwa na ari ya kujikita kwenye uzalishaji wa kilimo.

Mashamba ya Kimambila yakiboreshewa miundo mbinu (hasa barabara za kufika shambani,maji na umeme. Na iwapo wakulima watapata zana za kilimo kama vile matrekta na kupata fursa ya kupata pembejeo za kilimo (mbolea, mbegu na viuatilifu) kwa wakati wakati unaofaa.Kuandaa mtandao wa kilimo cha umwagiliaji. Yanaweza kuzalisha chakula cha kutosha na kuchangia katika adhima ya kuufanya mkoa wa Morogoro kuwa ghala ya chakula ya Taifa.

MKULLO KACHEKA KWENYE ATM

Siyo siri mtu wangu, kama zali vile, nilikuwa nimechacha ile mbaya. Hata mwanangu Mary alikuwa analitambua hilo kwani zawadi ilikuwa hakuna tena. Maana si unajua, kama alivyosema bosi wetu wa TUCTA kuwa mshahara ni "mbolea" ya wafanyakazi. Mbolea hiyo ilichelewa kutufikia si ya "kupandia" wala "kukuzia"! Ikawa malumbano kati ya "TUCTA" na Ma Ghasia na Mzee Mkullo wa "Treasury"? Si ndo ikwa ahadi, ahadi na huku "TUCTA" ikisisitiza kuwa kama hiyo mbolea haitatolewa wafanyakazi wataingia barabarani? Basi kama zali mwanangu leo asubuhi kuweka vitu kwenye ATM mbolea waaa!

Friday, August 29, 2008

Amevishwa pete ya uchumba!

Hayawi hayawi, yamekuwa. Hivi karibuni, Bw. Joseph Kamsopi Mdimi amefanya jambo kubwa katika maisha yake baada ya kumvika pete ya uchumba Bi.Flora Msechu katika hafla ya kukata na shoka iliyofanyika Mwanzo Park - Mwandege Mkoa wa Pwani. Hafla hiyo ilihudhuriwa na madada wawili, kaka na shemeji. Kamsopi anatarajia kufunga pingu za maisha tarehe 18/10/2008 jijini na Dar na sherehe za kupokea maharusi zitafanyika Afri Centre karibu kabisa na Lamada Hotel - Msimbazi

Wednesday, August 27, 2008

Tumekula machungwa mwaka mzima wabunge tusubiri maembe

Wakulima wa nchi hii wanafanya makubwa ya kulisha watu waishio hapa nchini kwa vyakula mbalimbali na katika mazingira magumu. Licha ya gharama za juu za uzalishaji. Lakini bado hawsiti kuzalisha.

Mwaka huu nimeshuhudia machungwa yakiliwa jijini Dar kwa mwaka mzima sasa.Tembelea masoko ya Buguruni, Tandika na Mbagala machungwa matamu makubwa yapo kwa bei ya shilingi 100 kwa chungwa.

Machungwa haya yanazalishwa kwa kutegemea mvua, yanazalishwa bila mbolea, yanazalishwa bila kutumia viuatilifu. Machungwa bora kabisa. Yanaweza kupata soko zuri ndani na nje ya nchi. Wakulima wetu wanajitahidi sana. Rais wetu Mh.Jakaya Kikwete analifahamu hilo ndiyo maana kama kiongozi wa nchi aliamua kuwa fedha za EPA zinazorudishwa zipelekwe kwenye sekta ya kilimo ili ziwasadie wakulima. Hapa hakuna sababu ya wabunge kupanga. Kazi ya kupanga ni ya serikali wabunge kazi yao kupitisha tu. Asante sana Spika wa Bunge Mh. Samwel Sitta kwa kulifafanua hilo, vinginevyo nalo lingetusumbua. Wabunge tusubiri maembe.

MV ARINA Reggae tu!

Moja ya boti zinazovusha abiria na magari pale Kigamboni Kivukoni ni MV ARINA. Ukipanda boti hiyo hukosi kuburudishwa na muziki kupitia kwa vipaaza sauti vya kizamani-mono (vya kutangazia mikutano). Lakini cha kushangaza, kama alivyobaini msafiri mmoja wa boti hiyo kwamba "humu hakuna taarifa ya habari wala nini - Ni Reggae tu." Hakufahamu kuwa blog hii ilikuwa karibu naye na pia huwa inatumia MV ARINA mara kwa mara na kusikia muziki wa reggae tu. Kweli MV ARINA ni reggae tu.

WANAENDESHA NA KUYAACHA KIGAMBONI

Wakati Ujenzi wa Barabara ya Kilwa ukiendelea. Wenye magari kutoka Mbagala na vitongoji vyake huamua kupitia Kigamboni ili kukwepa foleni ya magari kwenye barabara hiyo wakati wa asubuhi. Hali inakuwa mbaya wanapotaka kuvuka kwa kutumia pantoni. Kunakuwa na msururu mrefu wa magari. Kutokana na hali hiyo wengi wao huamua kuyaacha magari yao Kigamboni na kupanda pantoni. Hii imekuwa biashara nzuri kwa walinzi waliopo maeneo ya kivukoni gari dogo hulindwa kwa kiasi kisichopungua shilingi 500. Blog hii ilishuhudia hali hii leo asubuhi.

Si YANGA

Ukiwa ndiyo mara yako ya kwanza kuingia jijini Dar Es Salaam. Na mara yako ya kwanza kutembelea maeneo ya Buguruni, karibu kabisa na Makao Makuu ya chama cha CUF kuna jengo dogo hivi lililopakwa rangi za njano na kijani na kuandikwa kwa herufi kubwa YANGA nafikiri utajiuliza je hayo ndiyo makao Makuu ya Klabu ya Dar Es Salaam Young Africans al maarufu -YANGA? Usidanganyike, hicho ni kitawi kidogo tu cha Yanga cha Buguruni. Makao Makuu ya Yanga yako Jangwani, ndo maana wanaitwa watoto wa Jangwani!

Lakini nyie Yanga wa Buguruni, kwanini msiandike Yanga Tawi la Buguruni? Mnawapotosha wananchi.

Monday, August 25, 2008

Wakulima wajipange fedha za EPA zinakuja


Mhe. Rais Jakaya Mrisho Kikwete ametamka kwenye hotuba yake ya hivi karibuNI wakati akilihutubia BUNGE kuwa, fedha zinazorudishwa na mafisadi wa EPA zitatumika katika kuendeleza sekta ya kilimo. Ndiyo ametamka. Je, wakulima na wafugaji wamejipanga sawa kuzipokea fedha za EPA?

Wakulima wajipangaje fedha za EPA zinakuja

Mhe. Rais Jakaya Mrisho Kikwete ametamka kwenye hotuba yake ya hivi karibu wakati akilihutubia BUNGE kuwa fedha zinazorudishwa na mafisadi wa EPA zitumike katika kuendeleza sekta ya kilimo. Ndiyo ametamka. Je, wakulima na wafugaji wamejipanga sawa kuzipokea fedha za EPA?

Usafiri Mtoni Mtongani-Mbagala ni kero tupu

Barabara ya Kilwa iko kwenye ujenzi mkubwa. Awamu ya pili imeanza na kazi inakwenda kwa kasi kwa kweli. Sambamba na ujenzi huu, usafiri kwenye barabara hiyo umekuwa wa shida sasa. Madaraja yanayojengwa (mto Kizinga) pamoja na uzikwaji wa makalavati yanafanya kuwe na michepuko ya barabara hapa na pale kiasi cha kupunguza mwendo wa magari na kusababisha msururu mrefu wa magari. Ubadilishaji wa nguzo za umeme nao huenda sanjari na ujenzi wa barabara. Miti hukatwa na mitaro kuchimbwa. Hapo ndipo shughuli inapokuwa kubwa. Unaweza kutumia masaa mawili hadi matatu kufika mahali ulipokusudia. Tatizo ni kubwa wakati wa jioni na asubuhi.

Hatukujiandaa Olimpiki

Hii ni aibu kubwa. Timu yetu ya Olimpiki inarejea mikono mitupu. Tulikuwa wasindikizaji. Umaarufu wetu umepotea kabisa. Umasikini wetu umejionyesha hata kwenye michezo. Hata siku ya ufunguzi wanamichezo wetu walijitambulisha pasi na kujiamini hata sare zao zilikuwa za ubabaishaji zilikosa mvuto. Kweli Olimpiki ya mwaka huu hatukujiandaa.

Friday, August 22, 2008

Habari ya bilioni 9 za wakulima kuwekwa kushoto uk 18 si sahihi

Leo nimepata fursa ya kulisoma gazeti la serikali la "Daily News" katika ukurasa wa 18 upande wa kushoto nakuta kichwa cha habari "Nanyumbu farmers Bask in rich harvest" kwa kuwa mimi ni mtu wa kilimo nashtushwa na habari hiyo. Nachimba zaidi napata habari kuwa wakulima wa karanga wa wilaya ya Nanyumbu wamepata zaidi ya shilingi bilioni 9 kwa kilimo cha karanga msimu huu wa 2007/08. Jamani bilioni 9 kwa kulima karanga kwa wilaya moja tena ya Tanzania hiyo siyo habari muhimu kweli? Kwa kweli mhariri hukuitendea haki habari hii. Mimi nilitazamia kuiona kwenye ukurasa wa kwanza tena upande wa kulia. Lakini hapa imewekwa ukurasa wa 18 kushoto!

Taasisi ya Utafiti Kilimo chanzo cha bilioni 9 Nanyumbu

Teknolojia ya mbegu bora za karanga kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo -Naliendele, Mtwara zimewawezesha wakulima wa karanga kuvuna tani 12,241 za karanga na hivyo kujipatia jumla ya shilingi bilioni 19.18 msimu wa 2007/08. Akitoa taarifa hiyo, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Nanyumbu Bw. Farid Mhina amesema kuwa zaidi ya asilimia 90 ya wakulima wa karanga wilayani humo wanatumia mbegu bora.

Karanga ni moja ya zao la biashara linalokuja kwa kasi katika wilaya ya Nanyumbu, huku Korosho ikishika nafasi ya kwanza kwa kuwa chanzo cha kipato cha wananchi wa Nanyumbu. Hii ni kwa mujibu wa gazeti la Daily News la tarehe 22/08/2008.

Anamwakilisha Papa nchini Tanzania

Cardinali Joseph Chernoty Balozi wa Vatican nchini Tanzania akimkabidhi cheti cha Komunio Bi. Catherine I.J.Banzi kanisani Vikindu.

Waluguru hawaachi kumnema mwali!

Palikuwa hapatoshi Vikindu-Kisemvule. Catherine Banzi akinemwa na shangazi zake.

Huenda hawa wakatuletea ushindi


Kutoka kushoto Sisty Innocent Banzi, Peter Linus Banzi a.k.a Mkude

Ngoma inapochezwa na msinga!


Thursday, August 21, 2008

Ngoma na msinga!

Wapi hapo?

Huree nimefikisha Post 100!

Namshukuru Mungu kwa kunijalia afya njema, akili timamu na fursa ya kutosha ya kuweza kuingiza post 100 hadi sasa. Hili lilikuwa ni lengo langu la mwaka 2008. Miaka iliyotangulia zikuweza kufikisha hata post 25 kwa mwaka. Lakini mwaka huu nimeweza, nimevunja rekodi yangu mwenyewe.
Lakini kuna sababu nyingi zilizonifanya niweze kuingiza post nyingi mwaka huu. Mwaka huu nilipata fursa ya kusafiri sehemu mbalimbali nchini kikazi. Nimehudhuria mikutano, semina na warsha nyingi ambazo zimeniwezesha kukusanya niliyoyaona yanafaa kuwepo kwenye blog hii. Safari yangu Mbeya kwenye maonyesho ya Nane Nane nimejifunza mengi na nimeandika mengi kwenye blog hii kuhusu Nane Nane Mbeya.

Safari za kwenye Kanda kwa ajili ya kutoa elimu kwa wadau kuhusu Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo (ASDP) nayo imeniwezesha kukusanya habari kutoka Tabora, Arusha, Mbeya, Morogoro na Pwani.
Usafiri wa daladala nao umeniwezesha kupitia na kuona mengi ya jiji hili la Dar Es Salaam. Niliyoyasikia na kuyaona nimeyaning'iniza kwenye blog hii ingawa si yote.

Maisha yangu kijijini Vikindu-Kisemvule, ushiriki wangu katika shughuli za Parokia ya Kanisa Katoliki Vikindu pia ni hazina kubwa kwangu katika kufurisha blog hii. Naamini kuwa nitaweza kuingiza mengi kwenye blog hii kabla ya mwisho wa mwaka 2008 na iwapo nitapata camera habari zitaambatana na picha. Wateja wa Banzi wa Moro naomba maoni yenu

Takwimu za wasichana wanaokatisha masomo kwa ujauzito zinatisha

Habari inayosema kuwa asilimia 40 ya wasichana katika shule za sekondari mkoani Shinyanga hukatisha masomo yao kwa kupata ujazito. Asilimia hii ni kubwa. Je, ni asilimia ngapi ambao hushindwa kimasomo na sababu nyingine? Kwa mwendo huu kweli wanawake wasomi watapatikana kutoka mkoa wa Shinyanga? Sidhani. Kwa kweli hali ni mbaya. Asilimia 40 ni picha mbaya sana hasa inapokuwa inasababishwa na sababu moja!

Takwimu za wasichana wanaokatisha masomo kwa ujauzito zinatisha

Habari inayosema kuwa asilimia 40 ya wasichana

Ripoti kubwa majina yamo?

Nimeona kupitia luningani Mhe.Rais Jakaya Mrisho Kikwete akikabidhiwa ripoti ya uchunguzi wa skandali ya EPA. Kitabu kikubwa kwa kweli na inataka umakini wa kutosha kuisoma ripoti hiyo ili kuweza kutoa maamuzi sahihi. Swali moja najiuliza, kweli ripoti kubwa kama ile inaweza kukosa majina ya mafisadi wa EPA?

Mchakato wa kupata mikopo ya kilimo ina vikwazo vingi

Wakulima James Kyandarora, Bi Salma Mlwilo na Bw.Godwin Manase kwa pamoja wanakiri kuwa kilimo kimeweza kuboresha maisha yao kwa kuweza kujenga nyumba bora, kununua zana za kilimo, kununua baiskeli na kusomesha watoto (baadhi hadi chuo kikuu). Hawa ni wakulima wa mpunga kutoka Mbarali kupitia SACCOS ijulikanayo kwa jina la "RWANDA MAJENJE SACCOS." Wakulima hawa walishiriki kwenye maonyesho ya Nane Nane ya mwaka huu kwenye uwanja wa John Mwakangale jijini Mbeya.

Wakulima hawa hujishughulisha zaidi na kilimo cha mpunga ambacho uzalishaji huweza kufikia kilo 2500 kwa hekta moja. Tatizo kubwa la uzalishaji wa mpunga ni upatikanaji wa maji kwa wakati pia mchakato wa kupata mikopo ya kilimo ina vikwazo vingi walilalamika wakulima hao.

K.F.HANSEN KUTOKA DENMARK HADI MBARALI

Maonyesho ya wakulima maarufu kwa jina la Nane Nane yaliyofanyika kwenye uwanja wa John Mwakangale jijini Mbeya mwaka huu (2008)uliwashirikisha wadau wengi. Mmoja wa wadau aliyepata bahati ya kuzungumza na blog hii ni mzungu K.F.Hansen wa asasi isiyo ya serikali ijulikanayo kwa jina la SOK iliyoko Mbarali. Asasi hii hujishughulisha zaidi na uuzaji wa pembejeo za kilimo hasa madawa na mbegu kwa ajili ya uzalishaji wa mbogamboga na matunda. SOK ilianza shughuli zake mwaka 2000.

Kwa mujibu wa Bw. Hansen, wakulima wa Tanzania wanakabiliwa na matatizo makubwa ya ukosefu wa pembejeo na elimu ya kilimo bora, aidha bei za mazao ya kilimo hailipi. Gharama za uzalishaji ni kubwa kuliko za kuuzia. Hansen anatambua kuwa wakulima wengi ni wadogowadogo. Zana za kilimo pia hazipatikani kwa urahisi lakini anakiri kuwa sasa kuna mabadiliko makubwa katika sekta ya kilimo kuhusu upatikanaji wa pembejeo na zana za kilimo. Hansen amekuwepo nchini Tanzania tangu mwaka 1985 anazungumza kiswahili kwa ufasaha na kwa kweli anafahamu matatizo ya wakulima.

Saturday, August 16, 2008

Kuiona Black Stars Tshs 35,000 hivi tunamkomoa nani?

TFF imetangaza viingilio vya mechi ya Black Stars ya Ghana na Taifa Stars huku kiwango cha juu kikiwa shilingi 35,000. Mchezo huo utakaochezwa kwenye uwanja mkuu wa Taifa Agosti 20. Hivi hapa tunajifunza nini? TFF haijawahamasisha wananchi kuhudhuria mchezo huo wa kirafiki. La msingi kwao ni kutangaza viingilio. Huku wakiweka wazi kuwa gharama ya kuileta Black Stars ni shilingi 175,000,000.

Kwa uelewa wangu Black Stars wanakuja kucheza na Taifa Stars ili kuweza kuipima timu yetu ya Taifa na ikiwezekana kujifunza kutoka kwa Waghana hao kwani tunaaamini kuwa kiwango chao cha soka ni kikubwa ukilinganisha na cha kwetu, pia wana wachezaji wengi wenye uzoefu wa kimataifa. Sasa tunapoweka viingilio vya kukomoa, tunamkomoa nani?

Manispaa ya Morogoro yaboresha miundombinu

Manispaa ya mji wa Morogoro inaendelea kuboresha barabara zake kuu zinazounganisha mji huo. Barabara ambazo zinakaribia kukamilika kwa kiwango cha lami ni ile ya Uhuru inayopita benki ya "National Microfinance (NMB) na ile inayotoka njia panda ya Hospitali Kuu wa Mkoa hadi Morogoro Hotel na kupandisha hadi "uzunguni" maji yatiririka! Huenda haya yakawa ni moja ya matayarisho ya kuufanya mji huu kuwa JIJI. Barabara hizi na nyingine zikikamilika zitapinguza vumbi kwenye mji huo na kuboresha usafiri pia kuufanya upendeze. Morogoro ni moja kati ya miji maarufu na inayopendwa na watanzania na wageni kwa vile ina huduma muhimu na hali ya hewa ni nzuri.Tusubiri tuone.

Thursday, August 14, 2008

PROKON kuzalisha mafuta kutoka mbono

Kampuni ya PROKON kutoka Mpanda inatarajia kuanza kuzalisha mafuta kutoka mmea wa mbono ifikapo mwaka 2010.

Hayo yalielezwa na wawakilishi wa Kampuni hiyo kwenye maonyesho ya nane nane 2008 yaliyofanyika kwenye Uwanja wa John Mwakangale jijini Mbeya.

Wakiwa na sampuli ya mafuta hayo, ambayo ni mbadala wa mafuta ya petroli kwa kuendesha mitambo na magari, wawakilishi hao walieleza kuwa kwa sasa kiwanda kimeshaaanza kujengwa mjini Mpanda. Kilo moja ya mbegu za mbono kwa sasa zinauzwa kwa bei ya shilingi 1,200/= huko Mpanda, lakini mara nyingi bei huwa ni makubaliano kati ya mkulima na mfanyabiashara.

Kalalu aina mpya ya mbegu ya Mpunga

Watafiti wa Kilimo wa Taasisi ya Utafiti Uyole wameweza kutoa aina mpya ya mbegu ya mpunga ijulikanayo kwa jina la Kalalu. Mbegu hiyo ilitolewa rasmi mwaka 2005.

Jina la mbegu hiyo limetokana na Mkuu wa wilaya ya Kyela aliyewahi kufanya kazi kwenye wilaya hiyo ambaye alikuwa mstari wa mbele katika kuhimiza na kusimamia kilimo Mh. Mama Kalalu.

Sifa ya mbegu hiyo ni uvumilivu wa ugonjwa wa "Yellow Mottle Virus", hutoa mavuno tani 5 hadi 6 kwa hekta.

Mpunga ni zao maarufu kwa chakula na biashara wilayani Kyela.

Ngano aina ya Sifa "bomba" kwa mkate

Mbegu ya ngano ijulikanayo kwa jina la Sifa iliyotolewa na watafiti wa Kilimo wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Uyole mkoani Mbeya ni moja ya aina nzuri ya ngano inayofaa kwa kuoka mkate.

Mbegu hiyo yenye sifa ya kukomaa kwa muda wa siku 105 (miezi 3). Ni tegemeo kubwa kwa wakulima wa wilaya za Njombe(Iringa), Sumbawanga Vijijini na Nkasi (Rukwa).

Aina hiyo ya ngano ilionyeshwa kwenye maonyesho ya wakulima yaliyofanyika mwaka huu jijini Mbeya kwenye uwanja wa John Mwakangale. Mtafiti Mkuu Elanga ilidai kuwa pamoja na kuwa na aina mbalimbali za mbegu bora za ngano zilizozalishwa na Taasisi hiyo bado hazijasambazwa kwa wakulima wengi.

Mafuta ya Alizeti yang'aayo

Kwa wale waliotembelea banda la Kilimo la Halmashauri ya Sumbawanga kwenye uwanja wa John Mwakangale Mbeya na kukutana na wakulima wa Laela, nadhani watakubaliana nami kuwa moja ya vivutio vikubwa kwenye banda hilo lilikuwa ni mafuta ya alizeti.

Mafuta hayo yalizutia wadau wengi. Baadhi ya wadau walipenda kufahamu, kwanini mafuta mengine ya alizeti yanayotayarishwa kienyeji huwa na harufu mbaya na hayana mvuto (kwa rangi). Mkulima wa Laela alijibu kuwa hii inatokana na jinsi yanavyotayarishwa. "Yakitayarishwa vibaya ni kweli huwa yanakuwa na harufu mbaya." Alikiri mkulima huyo. Mafuta hayo ya alizeti yaliuzwa kwa bei ya shilingi (T) 2500/= kwa lita moja.

Kilimo cha alizeti ni maarufu mkoani Rukwa, kama wakulima watapata mitaji ya kutosha inawezekana kuwaondolea umasikini kwa kuwaongezea kipato chao.

Acheni vifuto,pensili, calculators na rula

Mkufunzi Mwandamizi wa Teknolojia ya Mawasiliano na Habari (ICT) wa VETA - Morogoro amewataka wahasibu na maafisa ugavi wa Idara ya Utafiti na Mafunzo kutoka Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika kuachana na matumizi ya vifuto, kalamu za risasi, rula, na calculators kwani shughuli hizo sasa zinafanywa na kompyuta.

Aliyasema hayo wakati akitoa mafunzo ya ICT ya muda wa juma moja mjini Morogoro. Mkufunzi huyo alisema kuwa programu ya Microsoft Excel inaweza kuwatatulia matatizo ya wahasibu na maafisa ugavi katika kutayarisha taarifa mbalimbali zinazohusu fani yao kwa ufanisi zaidi iwapo wafanyakazi hao wataielewa vizuri na kuitumia katika kazi zao za kila siku.

Moja ya sifa za programu ya excel ni kurahisha katika kufanya mahesabu, kutengeneza majedwali na chart mbalimbali. Zaidi ya wataalamu 40 wanaendelea na mafunzo hayo yanayotarajiwa kumalizika tarehe 17 Agosti 2008. Mafunzo hayo yameandaliwa na Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika chini ya Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo (ASDP)

Wednesday, August 13, 2008

Manispaa ya Sumbawanga yazalisha tani 64,338 za mahindi

Mahindi ni zao maarufu linalolimwa kwenye Manispaa ya Sumbawanga. Katika msimu wa 2007/08 Manispaa hiyo imeweza kuzalisha tani 64,338 za mahindi.Kiasi hicho ni kikubwa ikilinganishwa na uzalishaji wa mazao mengine yanayolimwa katika Manispaa hiyo. Mazao hayo ni kama vile Maharage (tani 8,100) na viazi vitamu (tani 13,622). Wakizungumza na blog hii, wakulima walioshiriki kwenye maonyesho hayo kwenye banda la Halmashauri hiyo, walisema kuwa utaalamu wa kilimo bora na teknolojia za kisasa hupata kutoka kwa maafisa ugani na kituo cha Utafiti wa Kilimo Uyole. Sumbawanga huzalisha pia chakula cha asili kijulikanacho kwa jina la kikanda ambalo husaidia kwa wagonjwa wa vidonda vya tumbo pamoja kuwapa wagonjwa hamu ya chakula.

Ludewa imepiga hatua kwa shamba darasa

Wakati wa sherehe za nane nane mwaka huu, banda la Halmashauri ya Ludewa lilikuja na takwimu nzuri za kuonyesha jinsi wakulima walivyopokea "approach" ya shamba darasa katika kujifunza teknolojia bora za kilimo.

Taarifa inaonyesha kuwa shamba darasa lilianza kutekelezwa kwenye Halmashauri hiyo tangu mwaka wa fedha 2005/06. Mwaka huo kulikuwa na mashamba darasa 13 ambayo 8 yalikuwa ya mazao na 5 mifugo. Mwaka 2006/07 kumekuwa na mashamba darasa 35 . Kumi na tisa ya mazao na kumi na sita ya mifugo. Kwa msimu wa mwaka 2007/08 kumekuwa na mashamba darasa 40 ambayo 22 ni mazao na 18 ni mifugo. Kwa takwimu hizo inaonyesha kuwa Ludewa inaendelea vizuri na shamba darasa.

Akizungumza na blog hii, Bw. Luoga aliyewakilisha Halmashauri katika maonyesho hayo, yaliyofanyika kwenye kiwanja cha maonyesho ya kilimo cha John Mwakangale kilichopo Uyole Mbeya(Kanda ya Nyanda za Juu Kusini), mtaalamu huyo wa kilimo alisema kuwa, wanawake wanaongoza kwa kupokea haraka "approach" ya shamba darasa lakini sasa wanaume wengi hujiunga na mashamba darasa ili kuweza kujifunza teknolojia mbalimbali za kilimo na ufugaji bora.

Tuesday, August 12, 2008

Morogoro Internet kama kazi

Sasa ni saa tatu na dakika sita (6) usiku nipo ndani ya jiji la Moro. Siyo siri mwanangu mi niko kwenye mtandao. Ndiyo maana nimeweza kupost habari kama mbili tatu hivi. Kwa kweli siyo siri, Moro kumekucha. Nasikia kuna maoni yanaendelea kutolewa na wakazi wa jiji hili kama Moro inastahili kuwa Jiji? Pamoja na ukweli kuwa mimi ni Banzi wa Moro mambo bado kidogo. Manispaa inatakiwa kuboresha miundo mbinu ya mji wa huu hasa barabara. Hata ile barabara ya kwenda Mji Mpya bado ni ya udongo. DDC ileile aliyopiga Marehemu Mbaraka Mwinshehe na Cubano Marimba na yalipo makao Makuu ya Lugaluga Agricultural and Marketing Cooperative Society. Hata, lazima tuwe wa kweli. Mambo mengi mazuri yapo Moro, lakini hili la barabara lazima liboreshwe na usafi uboreshwe. Vingenevyo kwa mtandao tu Moro ni kama kazi.

Kwa huduma hizi hatuwezi kuendelea

Nipo mji kasoro bahari (Morogoro). Hali ya hewa si mbaya kwa kweli. Nimekuja kwa shughuli za kikazi. Kuna mafunzo ya teknolojia ya mawasiliano (ICT) inayoendelea hapa VETA Morogoro kwa wahasibu na maafisa ugavi wa Idara ya Utafiti na Mafunzo - Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika. Wakati wa mapumziko washiriki wanapata chai na chakula. Lakini watoaji huduma ni goigoi, wakielezwa wananuna. Hawana ahadi za uhakika. Wanaweza kukueleza kuwa chakula kitakuwa tayari baada ya dakika tano kumbe ndo kwanza ugali unasongwa! Hivi kwa huduma ya aina hii tunaweza kuendelea? Lakini wanaotua huduma hii sio VETA Morogoro, bali kuna mjasiriamali moja ambao watendaji wake wanamuangusha. Kwa mwenendo huu kweli tutaendelea?

Tujifunze kwa Wachina

Michezo ya Olimpiki inaendelea huko Uchina. Wengi hawakutarajia kuwa Wachina wangeweza kuandaa michezo hiyo kwa kiwango cha hali ya juu hasa wazungu wa Ulaya ya Magharibi na Wamarekani. Lakini tumeona jinsi ufunguzi wa michezo hiyo ilivyofana huko Beijing. Angalia halaiki yao, angalia ubunifu wao kwa kweli ni "excellent" hata hao tunaowaita wazungu walibaki kupiga makofi na kushangaa. Watu wa marika yote walishirikishwa, wa jinsi zote walishirikishwa. Lugha waliotumia ilikuwa ni ya Kichina na kila kiongozi wao alipoongea wao walishangilia. Walishangilia kwa kuwa walielewa, walshangilia kwa kuwa walikuwa wazalendo. Kwa kweli Wachina wanaweza,wanajitegemea na ndiyo maana wanakuwa tishio katika dunia ya leo. Kweli Watanzania inatupasa kujifunza kutoka kwa wachina.

Sunday, August 10, 2008

Licha ya lumbesa kupigwa marufuku - Wakulima bado wananyonywa


Hivi karibuni serikali ilipiga marufuku mtindo wa kufunga magunia ya mazao kwa mtindo wa"lumbesa" kwa sababu mtindo huo ulikuwa unawaibia wakulima.

Safari yangu ya Mbeya kwenye sherehe za nane nane nilibahatika kuongea na mkulima mmoja kuhusu agizo hilo je kwa wakulima lina manufaa yoyote? Mkulima huyo ambaye ni mwanamama alinijibu kwa kusema kuwa kwa sasa hali imekuwa mbaya zaidi.
Alitoa mfano kuwa yeye ni mkulima wa viazi mviringo. Kwa mtindo wa "lumbesa" alikuwa akiuza sh.42,000/= (Bei ya mwaka jana). Lakini sasa ujazo wa kawaida anauza kwa sh. 15,000/=. Kutokana na hali hiyo wanaibiwa sana na mkulima hapati chochote.

Wednesday, August 6, 2008

Usipofika Msamvu Makuti unakosa mengi

Ukipata bahati ya kutembelea mji wa Morogoro. Usipate shida, moja ya sehemu nzuri na za kupendeza na zenye kutoa huduma za uhakika za chakula na vinywaji ni Msamvu Makuti.

Msamvu Makuti ipo ndani ya kituo kikuu cha mabasi cha mji wa Morogoro. Inafikika kirahisi ukielekea Dodoma, Dar Es Salaam au Iringa. Msamvu Makuti imeweza kujijengea jina hasa kwa nyama choma, supu na mchesho!

Watoa huduma wa Msamvu Makuti ni vijana wachangamfu wake kwa waume na huwapokea wateja mara tu wanapokaribia milango ya banda hilo la Makuti lilioezekwa kiutamaduni.

Ifikapo usiku starehe ya muziki inapatokana na usafiri wa kurudi sehemu uliyofikia au nyumbani kwako ni "bwelele." Msamvu Makuti inatoa faraja kwa wasafiri wakati wote kwa huduma ya chakula na vinywaji. Ukiwa Msamvu Makuti unaweza kujinunulia matunda ya aina mbalimbali yanayopatikana mkoani Morogoro hasa ndizi ,machungwa, maembe na mananasi.

Uwapo Msamvu Makuti milima ya Uluguru inakukonyeza huku maji yakitiririka!

Gwami Internet Cafe Morogoro

Mji wa Morogoro unapanda chati kwa kasi ya ajabu. Hii pengine inatokana na taasisi nyingi kuwepo kwenye mji huu. Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA), Chuo Kikuu Mzumbe, Chuo Kikuu cha Kiislamu, Chuo cha Ardhi, VETA Morogoro, Hospitali ya Mkoa, Chuo cha Mifugo, Stesheni ya Gari Moshi (Reli) Shule za Sekondari nyingi tu, kumbi za mikutano , mahoteli na nyumba za wageni na nyingine ambazo sijazitaja. Mji huu ni wa biashara hasa yanayotokana na mazao ya kilimo na madini.

Kuwepo kwa taasisi hizi kunasababisha kuongezeka kwa idadi ya wakazi na wageni wa mji huu kila siku. Kwa kuwa wageni na wakazi wanaongezeka basi mahitaji huongezeka.

Moja ya huduma muhimu katika enzi hizi za sayansi na teknolojia ni ile ya mtandao au "Internet". Internet inasaidia sana katika kurahisisha mawasiliano. Kwa mji kama huu wenye Maprofesa, wataalamu wazamivu na wazamili pamoja na wanafunzi wa ngazi zote huduma hii ni muhimu.

Ukiwa Moro usihangaike sana ulizia ilipo ofisi ya CCM wilaya ya Morogoro karibu kabisa na mahali pa starehe panapoitwa Chipukizi utakuta Internet Cafe moja bomba sana inaitwa Gwami Internet Cafe.

Internet Cafe hii ni moja ya internet ya kisasa hapa nchini naweza kusema bila ya kuuma meno. Computer zake ni safi na mtandao una speed kubwa. Usafi ndani ya cafe ni wa hali ya juu, vijana wachangamfu na wenye utaalamu wa mtandao wanatoa huduma safi. Hata maji ya kunywa yapo ndani ya cafe yanayopatikana kupitia mashine maalum. Dakika 30 ya kutumia mtandao ni shilingi 400/= tu.

Tuesday, August 5, 2008

"B One" Mtandao bora wa nyumba za wageni Morogoro

Ukiwa ni mara yako ya kwanza kutembelea mji wa Morogoro usipate shida ulizia "B one" kwa ajili ya huduma za malazi.

Wiki iliyopita nilikuwa Morogoro. Huwa nauona mtandao wa B one wa nyumba za wageni lakini niseme ukweli nilikuwa naogopa kuulizia nikidhani kuwa ni za gharama kubwa yaani si ya kiwango changu. Kumbe nilikuwa sina taarifa sahihi za kutosha. Nilipojaribu kuulizia nafasi ya malazi nilibahatika kupta kwenye moja ya nyumba hizo. Lazima ni kiri kwa mambo yafuatayo niliyoyaona kwenye nyumba hiyo.
  • Usafi wa hali ya juu
  • Kauli nzuri ya wahudumu
  • Unapata kifungua kinywaji kamili (+juice ya matunda ya Morogoro!)
  • Ulinzi wa uhakika
  • Utulivu masaa 24
  • Kila chumba kina TV
  • Gharama ya kuridhisha

Kilichobaki "B One" ni kujitangaza kwa njia zote ikiwezekana kukamata soko la nyumba za wageni Morogoro. Kula 5 mjasiriamali wa "B one."

Kwa mtandao kama huu, Moro sasa chati yake inapanda kwa kasi ya kutisha. Tembelea Moro na usikose kuulizia "B one" halafu toa maoni yako kupitia www.innobanzi.blogspot.com

Msamvu - Morogoro "Keep left" Kikubwa Tanzania

Nimebahatika kutembelea mikoa mingi hapa Tanzania lakini sijapata kuona "keepleft" kubwa na inayotunzwa vizuri kama ile ya Msamvu, Morogoro. "Keep left" hiki kiko kwenye makutano ya barabara ya morogoro, Iringa na Dodoma kwa kweli ni kikubwa. Kinachofurahisha zaidi ni jinsi Manispaaa ya Morogoro inavyokitunza. Kina maua mazuri ya aina mbalimbali na uhudumiwa vizuri kwa kumwagiliwa maji na kuondoa magugu yasiyohitajiwa. Sasa naweza kusema kuwa " Keepleft" cha Msamvu ni nambari wani hapa Tanzania. Aliyeona kikubwa zaidi ya hicho akitaje basi!

Monday, August 4, 2008

Zongo Mwenyekiti Lugaluga Agricultural and Marketing Cooperative Society

Mkutano Mkuu wa Ushirika wa Kilimo na Masoko - Lugaluga (Lugaluga Agricultural and Marketing Cooperative Society) uliofanyika tarehe 2 Agosti 2008 kwa kauli moja umepitisha jina la Bw. Ally Rashid Zongo kuwa Mwenyekiti mpya wa chama hicho baada ya aliyekuwa Mwenyekiti wa ushirka huo Bw. Chaula kuhamia Mbeya kikazi.

Kabla ya hapo Bw. Zongo alikwa akishika nafasi ya Makamu wa Mwenyekiti katika Ushirika huo. Kwa maana hiyo, Bw. Zongo ndiye Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Ushirika huo.

Chama cha Ushirika wa Kilimo na Masoko Lugaluga kilichopo Morogoro kilisajiliwa rasmi Septemba 2005 na kupewa namba 344. Hadi sasa ushirika una wanachama 88 wanaotimiza masharti na kanuni za chama.

Ushirika wa Lugaluga una mpango kabambe wa kumiliki ekari 20,000 zitakazotumiwa na wanachama wake katika uzalishaji wa kilimo na ufugaji.

Dira ya Lugaluga ni kuinua na kustawisha hali ya uchumi na maisha ya wanachama na jamii kupitia vyama vya ushirika.

Lugaluga ni chama chenye kuona mbalimbali katika uzalishaji wa kilimo na ushirika.
Pamoja na raslimali kubwa ya ardhi iliyoko mbele yao, Lugaluga inakosa mtaji wa kujiendesha.

Kwa kuwa mkoa wa Morogoro umetajwa kuwa ni kapu la uzalishaji wa mazao ya kilimo hapa nchini kuna haja ya viongozi wa ngazi zote kutoa machango wao katika kuhakikisha kuwa Lugaluga inakuwa mfano bora wa ushirika mkoani Morogoro na kwa Taifa. Jambo la msingi ni kusimamia na kuona kuwa wanachama wake wanapata mikopo itakayowawezesha katika uzalishaji kwa kununua pembejeo za kilimo, kutayarisha mashamba na kupata teknolojia za kisasa za kilimo.

Vyombo husika vitayarishe mipango na kuitekeleza katika kuboresha miundo mbinu ya shambani na hasa barabara. Hili ni tatizo kubwa lilojitokeza wakati wa kutayarisha mashamba kwa msimu wa mwaka 2007/08.

Saturday, August 2, 2008

Nauli Mpya Utafiti wa kina haujafanywa

Jana tarehe 1 Agosti nauli za vyombo vya usafiri zimepanda nchini kote hasa kwa usafiri wa magari. Kupanda huku kwa nauli kumewafanya watanzania wengi kufikiri jinsi ya kufanya ili kuweza kukabiliana na kupanda huku kwa nauli.

Tatizo hili limejitokeza kwa kina zaidi jijini Dar Es Salaam hadi kufikia wanafunzi wa shule za msingi na sekondari kuandamana kwenda ofisi za Mkuu wa Mkoa wa Dar Es Salaam ili kuonana na Mh. Kandoro wamueleze kukerwa kwao na uwezo walio nao wanafunzi.

Wafanyakazi wengi hasa wa kipato cha chini kuongezeka kwa nauli ni kero kwao. Wafanyabiashara wadodowadogo "wamachinga, mamantilie" nao ni pigo itabidi waongeze bei ya sahani ya wali au wapige panga kwa bei hiyohiyo ili waweze kupata faida. Bidhaa feki nazo zitaoongezeka madukani.
Nasema utafiti haujafanyika kwa nauli mpya za sasa.

Asha Rose Migiro anavyoonekana kwa watu

Dkt. Asha Rose Migiro ni jina maarufu si hapa Tanzania bali hata kwa mataifa mengine.
Dkt. Migiro Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN) ni moja ya matunda bora kutoka Tanzania yanayowaka katika anga za Kimataifa.

Ninavyomfahamu mimi, Dkt. Asha Rose Migiro aliwahi kuwa mhadhiri pale Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam na ameshawahi kuwa Waziri wa Maendeleo ya Jamii na Wanawake na Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje na Uhusiano wa Kimataifa.

Hivi sasa yupo Tanzania kwa likizo fupi. Kwa muda wa wiki moja sasa amekuwa akifanya mambo mengi hapa nchini. Ameshahudhuria kikao cha Bunge na kulihutubia na kuhojiwa na vyombo vya habari hapa nchini.

Wakati wote huo nilichojifunza kutoka kwake, mwanamama huyu ni makini sana. Anajua nini cha kuongea na wakati gani na kwa akina nani. Ana kipaji kikubwa cha kutumia lugha. Anaweza kujieleza barabara kwa kiswahili fasaha na kiingereza makini.

Huyu ni mtu ambaye ameshatembelea nchi nyingi na kukutana na watu wengi maarufu na wa kawaida hapa duniani lakini haachi kujitambulisha Utanzania wake. Kwa kweli nimempenda jinsi anavyojiweka katika hali ya kawaida kabisa.

Nimesikia kuwa mpaka sasa anaishi kwenye nyumba za wahadhiri kule Chuo Kikuu Dar Es Salaam na hata alipokuwa waziri. Huyo ndiye Dkt. Asha Rose Migiro kioo cha Tanzania na mfano bora kwa wanawake.

Kamokerere-Kijiji cha Chacha Wangwe

Sijawahi kufika Musoma,Tarime husan kijiji cha Kamokerere. Sijawahi kumuona uso kwa uso marehemu Chacha Wangwe aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Tarime. Lakini kwa takriban wiki moja sasa, kijiji cha Kamokerere kimekuwa maarufu kupitia vyombo vya habari kufuatia kifo cha Chacha Wangwe.

Kwanini Kamokerere? Chacha Wangwe alikuwa mmoja wa wabunge maarufu kwa hoja zake nzito akiwa bungeni. Aliwawakilisha ipasavyo wapiga kura wake wa jimbo la Tarime ingawa alikuwa si wa chama tawala, yeye alikuwa ni wa CHADEMA.

Marehemu Chacha Wangwe alipata ajali akiwa safarini kutoka Dodoma kuelekea Dar Es Salaam. Kwa kuwa kifo chake hakikutarajiwa, wengi walidhani kuwa kifo hicho kilikuwa ni cha kupangwa yaani aliuawa ndiyo maana wapiga kura wake hasa kutoka kijiji cha Chamokerere walipandwa jazba kutaka kufahamu sababu ya kifo hicho.

Lakini kwa mujibu wa habari kupitia televesheni na magazeti ya leo asubuhi baada ya uchunguzi wa kitaalamu kufanyika mbele ya mashahidi ya pande husika imebainika kuwa marehemu Chacha Wangwe alikufa kwa ajali ya gari na kupasuka fuvu na ubongo kumwagika. Apumzike kwa amani Chacha Wangwe.

Friday, August 1, 2008

Foleni ya Mbagala inasababishwa na ubinafsi wa madereva

Licha ya kuamka mapema ili kuweza kuwahi ofisini, leo nimejikuta nikikwama Mbagala Sabasaba takribani kwa saa moja kutokana na foleni ya magari iliyosababishwa na baadhi ya madereva kutofuata utaratibu wa kuendesha gari.

Magari mengi yalikuwa yanakatiza njia wanazojua wenyewe na kusababisha magari kufungana karibu kabisa na kiwanda cha nguo- KTM.

Hali hiyo iliendelea hadi walipojitokeza askari wa usalama barabarani na kuchukua hatua kali kwa wale madereva waliokatiza njia ikiwemo kuwanyang'anya funguo za gari. Kuna askari mmoja wa kike alinifurahisha sana pale aliposimama mbele ya gari lililotaka kuingia barabara kuu kwa makosa. Bila kusema chochote alimgandisha kwa muda mrefu na hata gari letu kufanikiwa kupita. Ndiyo maana nasema foleni ya Mbagala (Barabara ya Kilwa) inasababishwa na ubinafsi wa madereva.

Viazi, mihogo hadi barabarani


Wakulima wetu wanajituma sana katika uzalishaji licha ya mazingira magumu waliyonayo lakini wameza kulisha taifa hili na kuweza kuimarisha uchumi wa nchi hii kupitia kilimo na ufugaji.


Juzi nilitembelea soko la Mbagala. Nilishangaa kuona mazao mbalimbali ya kilimo yamefurika soko hadi kuzagaa kwenye barabara.Muhogo na viazi bwerere kabisa. Ndani ya soko nyanya,bamia, mchele, maharage, vitunguu, karoti,mchicha, kabichi, mbaazi, njegere, ndimu, karanga, matango, pilipili hoho, pilipili mbuzi, tangawizi, nyanya chungu na vingine vingi vyote hivyo vimezalishwa na wakulima wadogowadogo. Licha ya kutegemea kilimo cha mvua kwa silimia kubwa lakini vyakula vipo. Kwa kweli wakulima wetu wanafanya kazi kubwa sana lakini bado mtazamo wa nchi kwenye kilimo naweza kusema ni hasi! Maneno mengi lakini wakulima tuseme ukweli hawajaendelezwa katika kilimo na hii inatokana na bajeti finyu inayotolewa kwa sekta ya kilimo