Thursday, September 23, 2010

Fr.Jakka kiganja shavuni


Kwa kawaida Fr. Venance Jakka (Kaka yetu) huwa na ujasiri mkubwa wakati misiba inapotokea lakini huu wa Bibi Sr.Maria Magdalena bila kujijua alijikuta mwenye majonzi mkubwa. Fr. Jakka alimpenda bibi na bibi alimpenda Fr. Jakka mjukuu wake. Wameishi wote kwa takribani miaka saba kwenye Parokia ya Ruaha. Kila wakati Fr. Jakka alikuwa karibu sana na bibi ikituokea shida na raha wako pamoja. Bibi amefia mikononi mwa Fr. Jakka.Fr. Jakka umeonyesha mapendo makubwa katika familia ni wachache sana wenye moyo kama wako.TUMSIFU YESU KRISTU.

Wednesday, September 22, 2010

Maua mishumaa kaburini


Kuonyesha dalili ya upendo na mwanga usiozimika maua na mishumaa ilipamba kaburi la Bibi Sr. Maria Magdalena (Binti Makeya).
ATUKUZWE BABA NA MWANA NA ROHO MTAKATIFU. AMINA

Wajukuu wakishusha jeneza kaburini


Jeneza la Bibi Sr. Maria Magdalena lilishushwa kaburini na wajukuu zake.

NENO KUTOKA KWA FAMILIA


Nilitoa shukrani kwa niaba ya familia.

TUMSIFU YESU KRISTU.

Baba Padre Laurent Kunambi kwenye Ibada ya mazishi


Baba Padre Laurent Kunambi (wa pili kutoka kulia) alishtushwa sana na msiba wa Bibi Sista. Alishiriki katika vikao vya familia na kutoa ushauri. Pichani akiwa katika Ibada ya mazishi kanisani Mgolole.

Askofu Telesphor Mkude akiendesha Ibada ya Mazishi


Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Morogoro, Mhashamu Baba Askofu Telesphor Mkude (wa nne kutoka kulia) aliendesha ibada ya mazishi. Mhashamu Baba Askofu Athony Banzi wa Jimbo la Tanga (wa pili kutoka kulia)pia alishiriki kwenye Ibada hiyo.

Tuesday, September 21, 2010

Bibi alizikwa na mapadre wa dunia nzima!




Nakumbuka niliisema hii katika kutoa shukrani za wanandugu kuwa,Baba yangu mdogo anaweza kusema kuwa mama yake amezikwa na mapadri wa dunia nzima. Pengine utasema si kweli. Lakini inawezekana kuwa na ukweli fulani, kwani walikuwepo mapadri wengi sana (idadi sijui) maaskofu wa majimbo wawili na uwakilishi wa papa pia ulikuwepo. Kwa hiyo ni sahihi kusema kuwa bibi alizikwa na mapadri wa dunia nzima. TUMSIFU YESU KRISTU.

Wajukuu na vitukuu vya marehemu walihudhuria mazishi


Wanandugu wakifuatilia ibada ya mazishi


Ndugu, marafiki na jamaa kutoka sehemu mbalimbali ndani na nje ya nchi walihudhuria mazishi ya Bibi Sr.Maria Magdalena. Pichani Ndugu wakifuatilia kwa makini ibada ya mazishi.

Masista nao waliaga

Kabla ya kuingia kanisani


Mwili unasubiri kuingizwa kanisani. Mmoja wa watoto wa marehemu -Mama Paulina Mloka akiwa (wa pili kutoka kushoto mwenye kilemba cheusi) katika majonzi mazito.

Mwili unapokelewa Kanisani Mgolole


Hatimaye tunafika Mgolole kabla ya kuuingiza kanisani kwa ibada takatifu. Ni majonzi, majonzi.

Tunajiandaa kwenda Mgolole


Hakuna aliyeamini! Lakini ndo ukweli wenyewe Bibi Sister amefariki na sasa tunajiandaa kwenda Mgolole kwa mazishi.

Tunaona mwili wa Bibi Sister



Tukiwa kwenye chumba cha maiti - Hospitali Kuu ya Mkoa-Morogoro tulifunguliwa jeneza la bibi na kuona mwili wa marehemu. Kilichofuata ni simanzi kwa ndugu na jamaa.

Bibi Sister ametuachia hazina ya Upendo


Tarehe 3/9/2010 itabakia kuwa moja ya siku ya kukumbukwa na familia kwa msiba mzito wakwa kifo cha Bibi yetu mpendwa Sr. Maria Magdalena (Binti Makeya Mzuanda).Bibi alifariki hospitalini Mikumi Morogoro na kuzikwa kwenye makaburi ya watawa - Convent ya Mgolole-Morogoro tarehe 7/9/2010 (Jumanne) Kwa Ibada takatifu iliyoongozwa na Mhashamu Baba Askofu Telesphor Mkude wa Jimbo na Morogoro na kuhudhuriwa na Mhashamu Baba Askofu Athony Banzi wa jimbo la Tanga pamoja na Mapadre, Masista ndugu, marafiki na jamaa. Kumbukumbu zinaonyesha kuwa Bibi alizaliwa mwaka 1920. Kwahiyo tunaweza kusema kuwa alifariki akiwa na umri wa miaka 90.

Aliingia katika utawa wa Shirika la Moyo Safi wa Bikira Maria mwaka 1939. Nadhiri yake ya daima katika shirika hilo aliiweka tarehe 15/8/1952. Mwaka 1967 alisherehekea jubilee ya kutimiza miaka 25, 1982 miaka 40, mwaka 1992 miaka 50 na mwaka 2002 miaka 60 ambayo ilifanyika Mgolole.

Katika uhai wake Bibi Sista amelitumikia Kanisa katika parokia zifuatazo:- Tangeni, Singiza,Mgeta,Kikeo,Mgolole,Mt.Patrice (Morogoro mjini), Ilonga na Parokia ya Ruaha ambako ndiko ulikomkuta umauti. Kitaaluma yeye alikuwa ni mwalimu kwa hiyo katika parokia hizo alizoishi alikuwa akifanya kazi ya ualimu kwa njia moja au nyingine.

Alikuwa mlezi mahiri wa miito kwa mapadri na masista, mcheshi, mchangamfu na mchapa kazi. Mwaka jana mwezi Desemba nilimkuta Parokiani Ruaha akipalilia mpunga wake nikaanza kumtania..bibi nitakuja kula ubwabwa mwezi wa sita. Akanijibu- karibu mume wangu. Baadaye nilimwimbia nyimbo yetu (Lololo kipenzi changuX2. Amenitia kishindo, umenitia kishindo moyo wahangaika!).Baada ya hapo alicheka sana na kusema Inno bwana! Hata hivyo nilishindwa kuimba wimbo huo wakati tunauaga mwili wake pale Mgolole tarehe 7 Septemba.

Familia imempoteza mtu muhimu sana, kwani licha ya utawa wake alikuwa ni nguzo ya familia (Wambiki). Aliweza kukemea yasiyo mazuri na kutoa ushauri pale alipoona familia inakwenda ndiko siko. Hakuwa mbaguzi binti Makeya. Kati ya watu ambao aliwasikiliza sana na ameishi naye hadi kifo chake ni kaka Venance Jakka (Padri)-Paroko wa Ruaha. Daima kama kuna jambo limekosewa alikuwa akisema Baba Jakka hapendi.. Mjukuu huyu alimpenda sana bibi naye bibi alimpenda mjukuu hadi umauti wake.

Ndiyo Bibi Sista ameondoka. Hakuna Bibi Sista tena ingawa masista wanaingia na kutoka.MUNGU AILAZE MAHALI PEMA PEPONI ROHO YA MAREHEMU BIBI SISTA MARIA MAGDALENA (Constansia Makeya).MUNGU AKIPENDA TUTAKUTANA TENA.

Friday, September 3, 2010

Kutoka Chuo Kikuu Zambia


Christina ni mhadhiri kutoka chuo kikuu cha Zambia mwanadada huyu ni mtaalamu mzuri katika masuala ya habari na mawasiliano katika kilimo. Pichani anaelezea jambo kwenye flip chart.

Utanitambuaje?


Tulipoambiwa tuchague mdau wa kumwakilisha katika warsha hii na kuleeleza mahitaji yake ya habari. Mwanamawasiliano huyu (Tsepang)kutoka Afrika ya Kusini alibandika label kwenye paji la uso wake!

Kazi kwelikweli!



Danny kutoka Zambia na Martha kutoka Msumbiji wakibandika mabango ya maarifa yaliyotoka kwa wanakikundi. Pichani wanahangaika kubandika picha zetu tulizojichora.Kazi kwelikweli.Picha ya kulia Danny anaelezea Rich Picture.

Nilivyojitambua


Kuna wakati kwenye moja ya kikundi tulitakiwa kujichora na kujieleza bila kujali wadhifa wako na utaalamu wako. Hivi ndivyo nilivyojitambua.Hii inasaidia kuvunja ukimya kwenye kikundi na pia kumuelewa mtu kwa kiasi fulani na kuwa wavumilivu la sivyo mnaweza kushikana mashati wakati wa kutoa mawazo kwa sababu kila mmoja anataka asikilizwe.Isitoshe wengine ni ving'ang'anizi kila kitu wanataka wafanye wao na wengine hawajionyeshi kirahisi lakini wana uwezo mkubwa.

Na mimi nimo


Kompyuta ni kifaa changu cha kazi. Ninakitumia sana karibu kila siku. Moja ya mzigo wangu nilipokuwa nakuja huku Pretoria ni kompyuta. Kwenye warsha hii ya Habari na Mawasiliano nimetumia sana kompyuta ni imenifanya kuwa ndani ya warsha ni siyo nje!

Thursday, September 2, 2010

Tumekwenda na vitendea kazi


Si Malawi tu hata wataalamu kutoka Tanzania tulikwenda na vyombo vya kisasa vya kupashana habari na kuwasiliana. Pichani Vidah yuko busy na kompyuta anaandaa points kwa ajili ya kuchangia kwenye mijadala inayoendelea.

Rich Picture!


Utafikiri mchoro huu umechorwa na watoto wa shule ya chekechea hapana! Hii ni moja ya matokeo ya warsha ya Pretoria. Mchoro unahusu mambo ya kupelemba na kutathmini. Unatoa picha inayomfanya mpelembaji kutambua mazingira yake,wadau na mahitaji yao katika habari na mawasiliano ili kufikia lengo.

Imemgusa!


Mjadala umemgusa Mratibu wa mradi wa SADC-ICART Dr.Cresensio Tizikara. Mradi huu ndiyo unaogharamia warsha inayoendelea hapa Pretoria-Afrika ya Kusini

Mwanahabari wa Kisasa


Moja ya kifaa muhimu kwa mwanahabri wa kisasa ni kompyuta.Aidha haitoshi tu kuwa na kopmyuta lazima kujengewa uwezo wa jinsi ya kutumia kifaa hicho upashanaji habari na mawasiliano.
Pichani ni Jerome Nkhoma kutoka Malawi akisisitiza jambo katika warsha inayoendelea hivi sasa mjini Pretoria. Jerome ni Afisa Ugani Kilimo lakini amebobea katika nyanja ya habari na mawasiliano. Ni rafiki yangu, tumeshiriki mara nyingi katika kazi za kitaalamu zinazoandaliwa na SADC katika masuala ya habari. Timu yao kutoka Malawi ni ya watu watatu pia.

Mijadala inaendelea


Ingawa yuko kwenye mfungo wa Ramadhani. Vidah Mahava (kulia mwenye shati rangi ya pink)kutoka Tanzania anashiriki kikamilifu kwenye mijadala inayoendelea.

Maarifa na ubunifu wa hali ya juu unatumika katika mijadala hii ya Habari na Mawasiliano katika Kilimo.

Siko peke yangu


Siko peke yangu katika warsha hii. Nipo na wataalamu wawili wa Habari na Mawasiliano kutoka Idara ya Utafiti na Maendeleo, Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika nao ni Dr.Janet Kaaya na Vidah Mahava.

Inabidi kutulia na kutafakari pia


Bado tunaendelea na Warsha ya Habari na Mawasiliano katika Kilimo hapa jijini Pretoria Afrika ya Kusini. Leo ni siku ya nne kuna mambo mengi sana niliyojifunza lakini pia nimechangia mengi katika warsha hii na bado naendelea kuchangia mpaka kieleweke. Kikubwa si kuwasiliana tu bali mawasiliano yanasaidia nini katika uzalishaji wa kilimo hatimaye kuboresha maisha ya wananchi katika eneo hili la kusini mwa Afrika? Inabidi kutulia na kutafakari kwa kina.

Wednesday, September 1, 2010

Akina mama wameshiriki kwa wingi

Kwenye warsha hii kuna wataalamu 16 akinamama.Hawa ni wataalamu wa habari na mawasiliano wanatoa mchango mkubwa.Sijaona idadi kubwa ya washiriki akina mama katika mikutano ya kazi kama hii .Tanzania tumewakilishwa na wataalamu wawili, Dr.Janet Kaaya na Bi.Vidah Mahava.

Wataalamu wa Habari na Mawasiliano-SADC


Hiki ndicho kikosi cha Wataalamu wa Habari na Mawasiliano katika Kilimo kwa nchi za SADC wanaoendelea na warsha yao hapa Pretoria -Afrika ya Kusini.

Davy Simumba mtaalamu wa mawasiliano kutoka Zambia


Davy Simumba (mwenye shati ya kitenge nyeusi na nyeupe) amefanya mengi kwenye mawasiliano kwa nchi yake (ZAMBIA) pamoja na SADC. Tunaye hapa Jburg. Nimeshakuwa naye kwenye makongamano mengi yanayohusu Habari na mawasiliano.

Mawazo ukutani


Kila mshiriki anatoa mawazo yake kwa kila mada. Baadaye tunakaa pamoja na kutafakari na kupata kitu kizuri ndivyo tunavyojenga mkakati wa Habari na Mawasiliano kwa nchi wanachama wa SADC. Leo ni siku ya tatu.

Wakati mwingine huchoka


Kazi kweli kweli. Moja ya dalili za kuchoka ni kupiga miayo. Mambo ya kizidi baadhi ya washiriki huchoka.

Kuna wakati nilishika kalamu na kuongoza mjadala


Ndiyo hapa kila mtu anashiriki kikamilifu.Jana nilipata fursa ya kuwakilisha yaliyotokea kwenye mazungumzo yanayoitwa World Cafe na leo niliongoza majadiliano katika kikundi nilichopangiwa mpaka kieleweke.

Wakati mwingine inabidi tupate mazoezi



Kuna maarifa mengi yanayotolewa kwenye warsha hii na wakati mwingine washiriki wanapoteza mwelekeo. Ili warudi kwenye njia mazoezi ya viungo ni muhimu. Tunaye Jimmy kutoka Afrika ya kusini ambaye hachoki kutupa mazoezi hali inapokuwa tete! Lakini naye ni bingwa wa mawasiliano na habari.

Lazima atakupa kazi


Katika picha ni Krishan Bheenick mratibu wa Warsha inayoendelea hapa Pretoria kuhusu Habari na Mawasiliano katika Kilimo kwa nchi wanachama wa SADC.Unapokuwa naye ni lazima utakuwa na la kufanya si kukaa tu na kusikiliza. Kweli tupo kwenye Warsha!