Monday, January 29, 2007

TUNATAKIWA KUFIKIRI KIDOGO TU

Tunatakiwa kufikiri kidogo tu ili kuweza kupunguza au kuondoa kabisa msongamano wa magari njia ya Kilwa. Nafahamu kuwa barabara ya Kilwa iko kwenye mpango wa kupanuliwa na kuifanya ya kisasa zaidi. Tuliahidiwa kuwa shughuli hiyo ingeenza mwezi Desemba 2006, lakini hadi hivi sasa, hali ni ile ile.

Huku tukisubiri kutengenezwa kwa mpango huu. Watumiaji wa barabara hiyo tufikiri kidogo tu. Hivi mashimo yaliyoko kwenye barabara hiyo yangezibwa vizuri tu hali ingekuwaje. Mashimo ya pale kwa Aziz Ally, Uwanja wa Sabasaba na pale Kurasini Mivinjeni yanakera sana na ni moja ya sababu ya msongamano barabara ya Kilwa. Kama kituo cha Mtoni Mtongani kingepanuliwa au kufanyiwa marekebisho msongamano usingekuwepo. Iwapo Halmashauri ya Temeke ingetengeneza ile barabara inayoanzia daraja la Tazara kwenda Tandika, kusingekuwa na sababu ya magari yanayoishia Tandika na hata yanayokwenda Buguruni, kupitia kwa Aziz Ally, msongamano ungepungua sana. Utaratibu mwingine ni kuyapangia magari ya mizigo muda tofauti. Ningependekeza yaanze shughuli zake kuanzia saa 3.00 asubuhi. Hivi sasa hakuna utaratibu maalum. Utakuta lori la mchanga, mkaa, magogo, tanker la mafuta, vipanya,"magobori" (DCM), Coaster, Suzuki, Pikipiki, baiskeli na waenda kwa miguu - barabara ni hiyo hiyo moja kweli patokosa msongamano hapo? Patakosa ajali hapo? Tunatakiwa tufikiri kidogo tu.

Monday, January 22, 2007

BENKI KUU SARAFU CHAKAVU NI KERO

Jana Jumapili nilisafiri kwenda Mikocheni kwa basi la daladala. Nilipkuwa narudi nyumbani kwangu nilipanda basi la Kawe-Mtoni Mtongani. Nauli ni Tshs 250/- nilipotoa fedha hizo kondakta aking'aka, mzee hiyo hizo shilingi 50 chukua mwenyewe imechakaa hata kusomeka haisomeki. Mimi nilikuwa sikuiangalia sawasawa. Niliporudishiwa nikagundua kuwa kweli ilikuwa imesuguliwa sehemu ya wale swala na picha ya Mwl.Nyerere lakini bado ilikuwa inasomeka shilingi 50. Nikamwambia sina hela nyingine kama hutaki shauri yako. Dereva akazima gari akatoka kwenye kiti chake kuja kugombana na mimi. Nilijaribu kuwaelimisha lakini waliikataa sarafu ile hadi nilipotoa fedha nyingine. Ndani ya basi kuna abiria walioniunga mkono na kuna walionibeza kuniona kama msumbufu!
Sarafu hizi zinazoonyesha kuchakaa kwa kweli ni nyingi na zinaleta usumbufu mkubwa hasa kwenye usafiri na hata unapotaka kununua vitu ambavyo si vya gharama kubwa. Mtu akishaiona tu anasema mimi sipokei hiyo sarafu.

Lakini tukumbuke kuwa sarafu hizo ziko kwenye mzunguko na siyo senti ni shilingi. Je kukiwa na sarafu za thamani ya shilingi 50 milioni 10 ni kiasi gani cha fedha ambacho watu wanasema si fedha wakati bado ziko kwenye mzunguko? Milioni 500 ni shule ngapi za msingi zingejengwa? BENKI KUU SARAFU CHAKAVU NI KERO ZIONDOENI KWENYE MZUNGUKO.

Tuesday, January 16, 2007

BILA UTAFITI TUNAJIDANGANYA

Aina ya gari mpya zinatoka, aina mpya za simu zinatengenezwa, kalamu mpya zinatengenezwa. Sisi kazi yetu kununua tu, kuagiza tu. Mimi nataka shangingi VX....., mimi naipenda kweli simu ya Nokia. Ndivyo tulivyo watanzania. Kazi yetu kununua tu, kununua tu. Tunaagiza tu. Wenzetu wanafikiri na kusonga mbele sisi tunaagiza tu.

Hivi kweli tumetoa kipaumbele kwenye utafiti wa sekta zote za uzalishaji? Mimi nakataa. Sindano tunaagiza, mashati tunaagiza, viatu tunaagiza hata kiwanja cha mpira tumeagiza (unakataa nini si wachina wametujengea, kwani tumebuni sisi?).

Wataalamu tunao lakini hatuwatumii. Hatuwatumii kwenye sekta za uzalishaji ili kuinua uchumi wetu hatuwatumii hata kushauri tu. Sisi tunapenda vitu rahisi rahisi. Wenzetu wafanye sisi tutumie. Kwa kifupi hatufanyi utafiti. Halafu si wavumilivu, tunakwepa sana gharama. Mtaalamu wa umwaguiliaji anaweza kushauri kuwa inawezekana kuweka miundo mbinu ya umwagiliaji na kuzalisha mpunga mara tatu kwa mwaka na kutoa magunia 50 kwa hekta lakini zinahitajika kiasi cha fedha Tshs 50 bilioni. Utasikia, mama, mama, mama fedha zote hizo zitatoka wapi we mtoto acha balaa lako. Badala ya kuuliza je utahitaji fedha hizo kutekeleza jambo hilo kwa kipindi gani? Hilo hatufikirii hata kidogo. Lakini tunaimba tutaondoa umasikini tutaondoa njaa. Hivi hivi tu. Kirahisi rahisi tu. Haiwezekani bwana. Maendeleo ni gharama.

Hatufanyi utafiti.Tunaogopa utafiti kwa sababu ni gharama. Wanasiasa hawapendi utafiti kwasababu hawaoni matunda ya haraka. Matokeo yake utafiti kwenye Kilimo umeduamaa, kwenye Afya ndiyo kabisa huko viwandani ni zero. Pengine kidogo wataalamu wa ujenzi wanajitahidi. Lakini kibinafsi. Mtu anabuni jengo na likijengwa basi tunakiri nakusema aa jengo hilo amelibuni Banzi! Lakini kama Taifa kwa ujumla wake tumesahau utafiti na Maendeleo.

Hakuna atakayetuondolea Malaria kama utafiti wa kina kuhusu Malaria hapa nchini hautafanyika. Hakuna atakayetuondolea njaa na umaskini kama tutapuuza utafiti katika kilimo. Nasema hakuna. Bila kufanya utafiti tunajidanganya kufikia maendeleo ya kweli.

PAMOJA NA KUONDOA WAMACHINGA-Dar bado chafu

Jumapili iliyopita nilitembelea Kariakoo, Ilala, Tandika, Mbagala na Temeke.
Tusidanganyane, Dar bado chafu. Kila nilipopita malundo ya taka yamejaa kibaa kando ya barabara kuu, uchochoroni, nyumba za watu na wakati mwingine hospitalini!

Pale kwenye maghorofa ya nyumba za "NHC" Ilala, maji taka yanatiririka hovyo, hovyo inabidi uwe mtaalamu wa kuruka viunzi ili usiyakanyage na kama umevaa ndala ndiyo hakuna pa kukwepa utakanyaga tu.

Haya, pale karibu kabisa na Hospitali ya Manispaa ya Temeke pale nje, karatasi kibao, nyingine ziko kwenye mifereji ya maji machafu.

Kule Tandika sokoni mambo ni yale yale, uchafu, uchafu, uchafu mpaka mtaa wa Bubu wote kuchafu!

Mtoni Mtongani karibu kabisa ya kituo cha mabasi ya daladala kuna lundo la uchafu na kibaya zaidi watu wanachakurachakura wakiokoteza vinavyowafaa na watu wanaangalia tu.

Nakutana na magari ya kuzoa uchafu, he, kichekesho. Mengine hayana taa za mbele yamechakaa choka mbaya lakini yanapita barabarani. Hivi kweli kuna sheria inayoruhusu magari ya kubeba uchafu yawe machakavu pia? Askari wa usalama barabarani wanaona hilo wanafumbia macho wao kazi yao kukamua magari ya mkaa na daladala. Ukikutana na magari hayo ziba pua. Hiyo harufu! Kibaya yanasomba uchafu na kudondosha uchafu barabarani.

Dar bado chafu, hata pale Kariakoo mitaa karibu yote ni michafu, nenda Tandamti, Sikukuu, Kongo, na Aggrey ni michafu.

Mimi najiuliza, tumewaondoa wamachinga sawa. Lakini mbona Jiji bado chafu? Hivi itachukua muda gani kuona "impact" ya kuwaondoa wamachinga hasa kwenye suala la usafi?

TUNANAKILI HATA MAJINA!

Enyi Watanzania wenzangu, leo nimeamua kuandika kuhusu tabia iliyozuka kwa baadhi yetu ya kutaka kunakili kila kitu (copying). Kibaya zaidi tunanakili hata majina!

Hebu fikiria mtu anaanzisha shule ya sekondari, pamoja na gharama zote alizogharamia, baadaye anaiita St. Mary's au St. Mathew. Hivi ndani ya vichwa vyetu kuna nini? Kuna ulazima wowote wa kuita Saint, Saint.

Na sisi wazazi tukiona shule inaitwa St.... basi vichwa juu. Mimi nitampeleka mtoto wangu St. Elizabeth, mwingine St. Anne, mwingine St.Luka. Hivi kuna siri gani na shule hizi zinazoanzia na St? Wizara inayohusika ilijibu hili. Pengine hizi hazilipi kodi au zinapoingiza vifaa vya shule huwa hazitozwi ushuru maana ni za watakatifu hizi!

Natumaini wengi wenu mtakubaliana nami kwamba miaka kumi iliyopita upuuzi kama huu haukuwepo. Wengine tumesoma Njombe Sekondari, Tosamaganga Sekondari, Ilboru Sekondari, Tambaza Sekondari, Kilakala Sekondari, Loleza Sekondari, Mkwawa Sekondari, Iyunga Sekondari . Hata Mh. Rais Jakaya Mrisho Kikwete amesoma Kibaha Sekondari. Shule zilikuwa nzuri tu, wanafunzi walikuwa wanafaulu vizuri tu. Tena ilikuwa fahari kusema mimi nasoma Tosamaganga Sekondari. Lakini siku hizi shule hizi zinazoitwa za binafsi na majina nayo yabinafsi kweli utasikia shule inaitwa California nyingine Mississippi mh hapa ndo tumefika. Au shule hizi zinapata misaada kutoka ng'ambo kama tulivyozoea? Misaada, misaada, misaada hata vyoo misaada kutoka Japan na wafadhili wanaweza kusema jina la choo kiitwe.......... maana ni msaada!

Shule umeijenga mwenyewe, kwanini usiite Shule ya Sekondari Jambuya?. Maana unajua maana yake, pengine Jambuya ni jina la babu yako utakuwa umemuenzi babu yako na kwakweli pengine dunia nzima kutakuwa na shule hiyo tu yenye jina hilo. "that is unique".

Ikiwa hata majina tunanakili tunachokiweza hasa ni kipi? Hebu wenzangu mnieleze. Wanaohusika hawajaliona hili au nao ndiyo wale washabiki wa St au California?

Tufikiri upya.

Tuesday, January 9, 2007

WATOTO WANAMATUMAINI YA MWAKA MPYA

Mwaka mpya huo.

Wengine mwaka mpya ndo mwanzo wa matatizo. Watoto wanataka kwenda shule, mfukoni kumekauka. Lakini kibaya zaidi kuna wengine waliozaliwa tarehe 1/1/ wanatakiwa kufanyiwa "birthday party". Usiniulize, mimi sikufanyiwa. Ila watoto wangu inabidi kuwafanyia.

Watoto wanamatumaini mapya. Kila mwaka mpya kwao ni mwanga mpya. Lakini wanatutegemea sana sisi wazazi wao kuwatayarishia njia. Watoto wetu wana matumaini ya kuishi maisha bora kuliko sisi. Hii inawezekana iwapo tutabadilika katika nyanja zote. Kikubwa turudishe maadili mema. Tuwalee watoto wetu kwa kufuata misingi ya dini na elimu dunia. Dini zote zinafundisha Upendo, Imani, Amani na Kusaidiana na Kusameheana.
Watoto hawa (pichani) kutoka kushoto Maggie Julius na Maria Mwaka Banzi wanafurahia mwaka mpya 2007.

HERI YA MWAKA MPYA

NIMERUDI KUTOKA MATOMBO!

HERI YA MWAKA MPYA!

Ndiyo, nimerudi kutoka Matombo. Matombo ya mwaka 2006, siyo ya 1970s.
Matombo ya sasa mambo kwa fedha tu. Huna sababu ya kubeba sukari kutoka Moro au Dar, huna sababu ya kununua khanga au kitenge kutoka Dar au Moro huna sababu ya kubeba bia wala soda. Mambo yote Matombo tu.

Matombo kumekucha, Matombo kumebadilika. Matombo mtandao wa Celtel unatamba huku nayo TTCL baba wa mawasiliano akionyesha kali yake.

Matombo sasa mambo kwa Solar kama si solar basi "generator" lakini siyo za Richmond! Watu wanaona TV, humdanganyi mtu. Ndiyo, hata World Cup mbona wenzio waliona "live." Unashangaa nini sasa?

Matombo bado ukarimu uko pale pale. Natoa zawadi ya thamani ya shilingi elfu mbili. Napata jogoo mkubwaa. Kila siku kuku tu. We acha tu. Kila siku ndizi, maembe, ubwabwa, mashelisheli, mafenesi, mananasi ni tafrija tupu!

Matombo imebadilika. Vijana wanaongelea kulima kitaalamu. Nakutana na Michael Mloka Tunywe, ananitembeza kwenye bustani yake aliyopanda migomba, minazi, minanasi, midimu natembea hadi nachoka baadaye ananiomba ushauri afanye nini?Lakini soko hakuna nanasi hadi shilingi mia moja unapata. Namshauri. Kweli inatia moyo.

Mfizigo nayo je bado ipo? Ah bado. Kijiji kimepiga marufuku uchimbaji wa madini kiholela bila kuzingatia hifadhi ya mazingira. Big up wazee wangu. Nilienda kupiga "solono" nikateleza, vidonda nimerudi navyo na kuvitibu pale St. Vincent Dispensary, Vikindu kwa masista-wakaniambia pole sana.

Matombo kumekucha, vijana wanajenga nyumba bora kwa kutumia matofali ya kuchoma na kuezeka kwa mabati. Kijiji cha Lumala kinatia fora, sasa mambo yanaelekea Utunu, Mng'ombe hadi Nyangala! Kiswira, Nige, Gubi, Mhangazi bati pweya!

Kanisani je. Kwaya ya Mtamba inaendelea kutia fora. Ndiyo waliopangiwa kuimba usiku wa Christmass. Walikuja kwa mbwembwe kwa kukodi Costa wakiimba kwa mbwembwe huku wakipambwa na T-SHIRT zenye nembo ya kanisa la Mt.Paul Matombo. Kanisa nililobatizwa, kupata Komunio hata Kipaimara. Hapa ndipo nilipotumikia kanisani katika ibada za misa takatifu.

Kiswira, hapa ndipo kwetu hapa ndipo nilipopata elimu yangu ya msingi. Makao Makuu ya klabu ya Mpira ya Kiswira. Klabu ambayo tuliijenga sisi wenyewe kwa kubeba matofali moja moja hata kama ni mdogo kiasi gani na kusaidiwa na Brother Rudolph aliyekuwa kiongozi wa kiwanda cha Mayungi kilichozalisha mafundi seremala wengi kutoka Matombo. Nguvu ya Kiwanda hicho ni kutoka kwenye maporomoko ya Mayungi. Nasikia maporomoko hayo yanaweza kuzalisha umeme wakutosha na kulisha tarafa nzima ya Matombo!

Watu wanakalia taarifa, tunategemea Richmond hadi Matombo ?Hatutofika!