Tuesday, January 16, 2007

BILA UTAFITI TUNAJIDANGANYA

Aina ya gari mpya zinatoka, aina mpya za simu zinatengenezwa, kalamu mpya zinatengenezwa. Sisi kazi yetu kununua tu, kuagiza tu. Mimi nataka shangingi VX....., mimi naipenda kweli simu ya Nokia. Ndivyo tulivyo watanzania. Kazi yetu kununua tu, kununua tu. Tunaagiza tu. Wenzetu wanafikiri na kusonga mbele sisi tunaagiza tu.

Hivi kweli tumetoa kipaumbele kwenye utafiti wa sekta zote za uzalishaji? Mimi nakataa. Sindano tunaagiza, mashati tunaagiza, viatu tunaagiza hata kiwanja cha mpira tumeagiza (unakataa nini si wachina wametujengea, kwani tumebuni sisi?).

Wataalamu tunao lakini hatuwatumii. Hatuwatumii kwenye sekta za uzalishaji ili kuinua uchumi wetu hatuwatumii hata kushauri tu. Sisi tunapenda vitu rahisi rahisi. Wenzetu wafanye sisi tutumie. Kwa kifupi hatufanyi utafiti. Halafu si wavumilivu, tunakwepa sana gharama. Mtaalamu wa umwaguiliaji anaweza kushauri kuwa inawezekana kuweka miundo mbinu ya umwagiliaji na kuzalisha mpunga mara tatu kwa mwaka na kutoa magunia 50 kwa hekta lakini zinahitajika kiasi cha fedha Tshs 50 bilioni. Utasikia, mama, mama, mama fedha zote hizo zitatoka wapi we mtoto acha balaa lako. Badala ya kuuliza je utahitaji fedha hizo kutekeleza jambo hilo kwa kipindi gani? Hilo hatufikirii hata kidogo. Lakini tunaimba tutaondoa umasikini tutaondoa njaa. Hivi hivi tu. Kirahisi rahisi tu. Haiwezekani bwana. Maendeleo ni gharama.

Hatufanyi utafiti.Tunaogopa utafiti kwa sababu ni gharama. Wanasiasa hawapendi utafiti kwasababu hawaoni matunda ya haraka. Matokeo yake utafiti kwenye Kilimo umeduamaa, kwenye Afya ndiyo kabisa huko viwandani ni zero. Pengine kidogo wataalamu wa ujenzi wanajitahidi. Lakini kibinafsi. Mtu anabuni jengo na likijengwa basi tunakiri nakusema aa jengo hilo amelibuni Banzi! Lakini kama Taifa kwa ujumla wake tumesahau utafiti na Maendeleo.

Hakuna atakayetuondolea Malaria kama utafiti wa kina kuhusu Malaria hapa nchini hautafanyika. Hakuna atakayetuondolea njaa na umaskini kama tutapuuza utafiti katika kilimo. Nasema hakuna. Bila kufanya utafiti tunajidanganya kufikia maendeleo ya kweli.

1 comment:

MTANZANIA. said...

Umenikumbusha ule msemo "without research and enough data then no right to speak".Uko sahihi ndugu inabidi ufanyike utafiti wa uhakika.Tatizo ni kwamba taasisi zetu za elimu ya juu zimejikita kutoa elimu kwa ajili ya ajira na si utafiti.Tafiti nyingi katika nchi zilizoendelea huwa zinatoka kwa wadau wa taasisi za elimu ya juu.