Friday, May 28, 2010

Kumbe Makhirikhiri wako Dar!


Naipenda sana midundo ya "Makhirikhiri" au bush dance kutoka Botswana. Mwaka huu nimenunua karibu DVD nne za muziki wa aina hiyo. Aidha napenda kuangalia show ya Makhirikhiri wana wachezaji mahiri. Ni muziki wa asili kwa kweli. Uchezaji na mavazi unapata burudani tosha. Mungu akipenda natakwenda kuwaona. Nimenyaka picha hii sasa hivi kutoka kwenye blog ya bro Mjengwa. Asante sana

Mourinho-Kocha mwenye bahati


Hebu soma rekodi ya Kocha Mourinho

2003- Mabingwa wa Ligi ya Ureno,Kombe la Ureno na UEFA akiwa na Club ya Porto
2004-Mabingwa wa Ligi ya Ureno na Kombe la Washiondi akiwa na Club ya Porto
2005-Mabingwa wa Ligi Kuu ya Uingereza, Kombe la Ligi akiwa na Chelsea
2006-Mabingwa wa Ligi Kuu ya Uingereza akiwa na Chelsea
2007-Mabingwa wa Kombe la Ligi na FA akiwa na Chelsea
2009-Mabingwa wa Ligi ya Italia - Serie A akiwa na Internazionale Milan
2010-Mabingwa wa Ligi ya Italia - Serie A, Coppa Italia, na UEFA Champions League akiwa na Internazionale Milan

Read this piece

"But then if Jose Mourinho wishes to claim for himself the moon and the stars as well as the spoils of meticulous planning, it, is, as always, his own egocentric business. For the rest of us it is surely enough to acknowledge that, for the moment at least, he is the most effective coach of footballers on earth."

Mmea wa Sale kwa Wachagga



Kwa wale waliokwisha kubahatika kufika mkoani Kilimanjaro, natumaini wameshawahi kuuona mmea unaoonekana pichani. Mmea huu unaitwa Sale. Je, una thamani gani kwa Wachagga?

Wachagga wanaamini kuwa Sale ni mkombozi wa jamii. Mmea wa Sale hutumika kwaajili ya kuweka mipaka katika mashamba yao ili kuweza kujua eneo la mtu mmoja na mwingine.

Matumizi mengine ya sale ni katika masuala ya ndoa na mahusiano.Kwa Wachagga, kuna aina moja ya kuoa ambayo ni ya mkato isiyofuata taratibu ambazo zimezoeleka katika jamii nyingi. Kijana wa Kichagga anaweza kuelewana na masichana bila ya kuomba ridhaa ya wazazi. Kielelezo cha ndoa hii ni jani la mmea huo.

Aidha, mmea huo hutumika katika utatuzi wa migogoro kwa kuomba radhi na wahusika hukaa na kusameheana. Anayetumwa kusuluhisha mgogoro huchukua mmea wa sale. Haya ndiyo matumizi makuu matatu ya mmea wa sale kwa Wachagga (Habari hii imefupishwa kutoka Gazeti la Mwananchi la tarehe 28/05/2010)

Kwa mara ya kwanza Lindi wanaweza kuwa mabingwa wa Taifa Cup


Wamecheza kwa kujiamini na kuitoa timu yenye uzoefu ya mkoa wa Ilala magoli 3-0 kwa takwimu hizi na kwa ile kandanda waliyoionyesha, Lindi wanaweza kuwa mabingwa wa Taifa Cup mwaka 2010. Tumepata fundisho gani?

Thursday, May 27, 2010

Mkapa na misaada


"Tatizo hili lililopigiwa kelele, ikaja hoja nyingine kuwa la muhimu zaidi si misaada bali fursa za biashara. Ikasahauliwa kuwa fursa za biashara peke yake hazina maana iwapo hakuna uwezo wa kuzalisha bidhaa bora na za bei nafuu. Na uwezo huo unahitaji misaada zaidi kuujenga."

Maneno hayo yalitamkwa na Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa, Februari 28,2002 wakati akihutubia taifa. Mkapa alikuwa akizungumzia haja ya kuwepo kwa mfumo mpya wa biashara duniani.

Kuharibika kwa magari ya Rais kuna sababu


Si jambo la kawaida gari la Rais kuharibikaharibika. Hii si dalili nzuri. Inawezekana kuwa ni bahati mbaya au inawezekena kuwa kuna uzembe umefanyika mahali fulani. Tuwe makini tunakwenda siko.

Miss Vodacom Mkuranga 2010 huyu hapa


Naishi Kisemvule, wilaya ya Mkuranga mkoa wa Pwani. Pichani ni mrembo wetu Miss Vodacom,Mkuranga- Miss Rahma Said. Hongera sana.Picha kwa hisani ya blog ya Mjengwa.

Machiavelli na werevu

"Kuna aina tatu za werevu.Wa Kwanza hutambua mambo yalivyo wao wenyewe. Wa pili hutambua mambo yalivyo kupitia kwa wengine. Wa tatu hawatambui mambo yalivyo si kwa kupitia wao wenyewe bali pia kwa wengine. Werevu wa kwanza ni mzuri zaidi, wa pili ni mzuri kiasi; lakini wa tatu ni hovyo na hauna manufaa."

Maneno hayo yalitamkwa na mwanafalsafa wa kale wa Italia, Nicolo Machiavelli. Alizaliwa Mei 3,1469 huko Florence, Italia na kufariki Juni 21,1527 huko Florence. Moja ya vitabu vyake vilivyopata umaarufu duniani ni The Prince (1513). Tafakari hii.

Saturday, May 22, 2010

Ah hupati kazi Bongo


Hapa si Marekani bwana. Tanzania tuna vitu ambavyo tunavithamini na kutufanya tuonekane Watanzania. Sasa ktuvalia hivi halafu unajiona msomi na kuingia navyo ofisini ndo nini? Tuondokee huko hapa hupati kazi. Stori imeandikwa vizuri kwenye gazeti la Mwananchi la tarehe 22/05/2010 siku ya Jumamosi. Mwandishi ni Henry Mdimu - Zee la Nyeti. Litafute na uinyake stori nzima. Picha kwa hisani ya gazeti la Mwananchi.

Mjukuu kumbaka bibi yake na kumuua -Hiki ni kiama

Si kuamini macho yangu kukuta habari kwenye gazeti la Mwananchi la leo hii 22/5/2010. Tukio hili limetokea mkoani Shinyanga kwa watani zangu. Watani kuna nini tena huko? Mauaji ya Albinos ni nyinyi na hili tena ni nyinyi vipi? Itakuwaje bwana mjukuu wa miaka 27 ambake kikongwe cha miaka 70? Kaeni muongelee hili. Mnakokwenda siko watani zangu.

Wizi wa mafuta ya Tansforma


Wizi wa mafuta ya transforma unatokea mara kwa mara hapa nchini. Wiki iliyopita umetokea sehemu ninayoishi mimi - Kisemvule, wilaya ya Mkuranga, Mkoa wa Pwani. Vijana wamekuja usiku wameweka mpira na kunyonya mafuta hayo. Matokeo yake ilipofika muda wa saa 1.00 asubuhi transforma ililipuka na hadi hivi sasa kijiji giza totoro hatuna umeme. Visima vya maji vilivyokuwa vikitumia umeme kupump maji havifanyi kazi, hakuna kuona TV. Wanafunzi katika shule za bweni wameaathirika kwa kuwa watapata shida kukamilisha home work zao.

Ndugu zangu Wazaramo waliopanga kuwa na 'shughuli' mambo yameharibika. Ndo maana nilipoona picha hii ya gari la TANESCO niliyoikuta kwenye blog ya Mjengwa ilibidi niiandikie stori hii.

Eti mafuta hayo yanatumiwa kukaangia chips matone machache yakichanganywa na mafuta ya kukaangia basi hayakauki! Nasikia pia mafuta hayo hutumiwa na wezi kwa kubomolea nyumba, yakimwaga ukutani, ukuta humomg'onyoka hivyo kuwa rahisi kuingia ndani. Aidha wengine husema hutumiwa kwenye pump za maji, wengine husema hutumiwa katika utengenezaji wa vipodozi vya akina mama waonekane 'wazungu'!

Aunt Ezekiel - Mcheza filamu wa Bongo


Huyu naye ni mcheza filamu wa Bongo. Ni msichana mrembo kwa kweli lakini ameingia kwenye sanaa hii ya maigizo. Ukiona filamu zake kwa kweli utakubali kuwa Mungu amempa kipaji hicho ili aweze kuendesha maisha yake. Aunt ni mmoja wa washiriki katika filamu inayoitwa signature ambayo itaanza kuonekana madukani hivi karibuni. Mtunzi ni yeye mwenyewe JB a.k.a Amitha Bachan. Bongo bwana we acha tu!

Mchekeshaji Majuto


Mmoja wa wachekeshaji mahiri wa Tanzania- Mzee Majuto. Mchekeshaji huyu ana kipaji cha hali ya juu cha kuweza kukuchekesha na kukuweka sawa hata kama ulikuwa huko katika hali nzuri kimawazo.

Friday, May 21, 2010

Wednesday, May 19, 2010

Kwetu Mbagala


Wilaya ya Temeke imejaliwa kutoa wasanii wenye vipaji katika soka na muziki. Kwenye anga za mziki kuna vijana wa TMK walikotoka Juma Nature na Mheshimiwa Temba. Hivi majuzi tu ameibuka msainii mwingine kwa jina Naseeb Abdul a.k.a. Diamond alisomba tuzo tatu kwa mpigo 'hat trick' kwenye tuzo za Kilimanjaro. Huyo ndiye aliyeimba kwetu Mbagala. Nakupa shavu Diamond mimi kwetu Kisemvule na mji wetu mkuu Mbagala. Kuna nini tena umekata ngebe mwanangu! Pichani Diamond akifurahia moja ya Tuzo yake.

Bango hili limepoteza maana


Wengi wetu hupenda kutumia lugha ya Kiingereza wakati tunapotangaza jambo lakini kwa bahati mbaya lugha hiyo wengi imetutupa mkono. Lakini inashangaza inapofikia wakati mfanyabiashara kuridhika kutangaza biashara yake kwa lugha ambayo haielweki. Hebu soma kilichoandikwa kwenye bango hilo pichani - 'BLANTAYA GROOCARE'.

Wakati nikisoma makala hii iliyoandikwa na mwana mraba Abdi Sultani katika mraba wake maarufu ujulikanao ' Our Kind of English' unaolimwa kila siku ya Jumapili katika gazeti la SUNDAY CITIZEN kumbe bango hilo linamaanisha BLANTYRE GROCERY. Blantyre ni mji wa biashara wa Malawi na Grocery ni mahali ambapo kinywaji (pombe) inapatikana kwa tafsiri ya Tanzania. Picha hii imepigwa huko Nachingwea - Kilimalondo Road. Tuwe makini katika lugha ya kiingereza.

Usiruhusu watoto wako kuangalia picha kama hizi


Si vibaya kwa watoto kuangalia luninga (TV). Kuna vipindi vizuri vinavyofaa kuangaliwa na watoto. Vipindi hivyo vinafundisha na kuburudisha pia, lakini baadhi ya vipindi havifai kuangaliwa na watoto wa umri fulani. Kwa mfano picha za mapenzi, picha za kutisha. Inashangaza kukuta baba, mama, watoto na majirani wameketi sebuleni wakiangalia picha za mapenzi!

Watanzania na ndoa za gharama


Hapa Tanzania kuna familia zenye uwezo zinazoweza kufanya sherehe za harusi hadi kufikia sh. 200,000,000/=! Wakati mwingine bila kuchangisha hata senti tano. Kila kitu familia inagharamia na kupanga ni kina nani waalikwe. Hapa ndipo tulipofikia. Wakati hayo yanatokea kuna shule hazina madawati, kuna familia zinashindwa kupata hata mlo wa mmoja kwa siku huko wengi tukishambuliwa na malaria kwa vile tu tumeshindwa kumdhibiti mdudu MBU! Wengi wanaofanya haya ni wale maarufu nchini kama vile wanamichezo, wasanii, viongozi wa serikali na wafanyabiashara wakubwa.

Tuzipende familia zetu kama afanyavyo Cameroon


Inasemekana kuwa Waziri Mkuu wa Sasa wa Uingereza Bw. David Cameroon (aliyeonyesha dole) anaipenda sana familia yake. Waziri Mkuu huyu mwenye umri wa miaka 43 ambaye amefunga ndoa na Bi. Samatha Sheffield wamebahatika kupata watoto watatu. Siajabu kumkuta Cameroon akiandaa chakula jikoni, siajabu kumuona Cameroon akiranda mitaani huku akibeba watoto wake (Angalia pichani) akiwa na mkewe. Ni vizuri kuzipenda familia zetu.

Friday, May 14, 2010

Saini na SAHIHI

Neno saini limetokana na 'sign' ambalo ni Kiingereza.Tumelikopa na kulitohoa ili lifanane na muundo wa Kiswahili na liwe ni neno kamili la Kiswahili. Linaweza kutumika kama kitenzi na pia kama nomino.

Saini (kitenzi) kutoa idhini ili kitendo fulani kitendeke au kipatikane. Matumizi yaliyozoeleka na kukubaliwa na wengi ni kutoa idhini au kuthibitisha kupatikana kwa kitu au jambo fulani na mara nyingine ni kwa kuandika jina lako.

Tunatumia neno hili tunapotaka kuweka saini mahali fulani. Ni sahihi kusema kuweka saini na wala siyo kutia saini. Kutia lina maana ya kufanya kitu kiwemo ndani ya kitu kwa mfano nitilie chai badala ya kusema niwekee chai. Kuweka kitu maana yake ni kukitua kama vile kuweka kitabu mezani au kuweka silaha chini.

Neno sahihi (nomino) lina maana ya kuthibitisha au kuidhinisha kwa jambo kutendeka au kupatikana. Tumezoea kusema, "Kazi aliyofanya ni sahihi. Pia, maswali yote aliyajibu kwa usahihi kwa maana ameyajibu yote sawasawa."

Aza ya mbegu ya mazao ya mizizi


Picha hii nimeinyaka kutoka blog ya kaka Mjengwa. Wadau hawa wamekusanya mbegu ya viazi vitamu. Tatizo la mbegu za mazao ya mizizi ni kubwa hapa nchini hata wakala wa mbegu - ASA ulioanzishwa hivi karibuni bado haujapata ufumbuzi wa kuzalisha mbegu bora za mazao ya mizizi-viazi vitamu ikiwa mojawapo.

Kwa kuwa mazao ya mizizi (hasa muhogo na viazi) hustahimili sana ukame hivyo kuwa mkombozi wakati wa njaa, juhudi lazima zifanyike kuhakikisha kuwa wakulima wanapata mbegu bora na za uhakika. Hapo ndipo Halmashauri zinapotakiwa kutenga fedha za kutosha kuwawezesha wakulima kupata mbegu.

Thursday, May 13, 2010

Daraja la UMOJA-kumbe tunaweza


Ujenzi wa Daraja la Umoja lililojengwa kwa ushirikiano wa nchi mbili za Tanzania na Msumbiji zimedhihirisha kuwa Afrika tunaweza kufanya mambo makubwa yanayoweza kuwasaidia watu wetu bila kusubiri wafadhili. Daraja hilo lenye urefu wa mita takribani 750 na thamani ya zaidi yaTzs 36 bln limefunguliwa rasmi jana tarehe 12/5/2010 ni mfano mzuri wa ushirikiano wa kuigwa barani Afrika. Daraja hili linawaunganisha si wa Msumbiji na Tanzania tu bali watu wote. Limerahisisha usafiri, litakuza shughuli za biashara, litapunguza vifo kwa wale waliokuwa wakisafiri kwa vyombo visivyovyakuaminika kuvuka mto Ruvuma na hatimaye kupata ajali. Kubwa zaidi litaboresha maisha ya wananchi wa nchi zote mbili.

Ndizi pacha wanasayansi tuelezeni


Leo asubuhi nimesoma kutoka kwenye blog ya michuzi kuwa huko Kilema Moshi kumeonekana tukio lisilo la kawaida kwa mgomba kutoa mikungu miwili ya ndizi kwa wakati mmoja. Wanasayansi wa kilimo mliobobea kwenye uzalishaji wa mazao tuelezeni sababu ya kutokea hivyo.

Monday, May 10, 2010

Unapopinga una hoja?

" ......wakati mwingine, mtu tunayempinga huwa ana makosa kweli, lakini hoja tunazozitoa ni za ki(bi) nafsi na hazihusiani kabisa na hoja zake. Nikisema mbili na tatu ni sita, nakosa. Lakini ni bora kunionesha kwamba pengine nafikiri tunazidisha kumbe tunajumlisha. Ni kweli mbili mara tatu ni sita; lakini mbili na tatu ni tano siyo sita.....Huu ni mfano wa upuuzi; lakini mara nyingi hoja tunazozitumia kuwashawishi watu wakatae mawazo yetu huwa hazihusiani kabisa na mambo tuinayojadili (Nyerere, J.K. 1962):TUJISAHIHISHE, Dar Es Salaam, National Printing Company Ltd, ukurasa wa 3)

Friday, May 7, 2010

Acha kumeza vidonge kula ndizi!


Ungejua uwezo wa ndizi usingekosa kula angalau moja kwa siku. Ndizi huupa nguvu mwili, husaidia kutibu maradhi ya kisukari, msukumo wa damu (blood pressure),kuvimbiwa,kiungulia,inaongeza uwezo wa ubongo kufanya kazi vizuri,kupunguza mfadhaiko,kuongeza damu, vidonda vya tumbo, hupunguza uzito. Jamani tule ndizi. Wakulima wa ndizi mnaona pesa hiyo nje nje!

Godluck sasa Rais wa Nigeria


Baada ya Kifo cha aliyekuwa Rais wa Nigeria Umaru Yar'Adua makamu wake Bw. Godluck Jonathan ameapishwa jana kuwa Rais wa Nigeria.

Tubadilike Kilimo ni Biashara


"Treat farming as big business" kichwa hiki cha habari kimepamba ukurasa wa kwanza wa gazeti la Daily News (Tanzania) la tarehe 7/5/2010. Ndiyo, nchi nyingi hazijawekeza katika Kilimo. Tunafikiri kilimo kinaweza kufanyika hata bila teknolojia na kwamba kila mmoja ni mkulima. Hata wataalamu wake wanadharaulika (Bwanashamba). Bajeti inayotengwa kwa kilimo ni kidogo sana. Miundo mbinu kwa ajili ya uzalishaji wa kilimo haipo. Ndiyo maana inasisitizwa kukifanya KILIMO kiwe cha Biashara mwisho wa siku lazima KILIPE!

Wanawake wanaweza


Je unafahamu kuwa Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia Kanda ya Afrika ni mwanamke na anaitwa Obiageli Ezekwe (Pichani kulia). Kwa sasa yupo Dar akihudhuria Mkutano wa Kiuchumi wa Dunia kuhusu Afrika ambao unahitimishwa leo.

Ukitegemea huwezi kuendelea


Huu ndiyo ujumbe aliyoutoa Rais wa Awamu ya Tatu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Benjamin William Mkapa (pichani). Mkapa alisema "inashangaza zaidi, kukuta viongozi wa Afrika wanazungumzia maendeleo ya nchi zao, lakini mnauliza ni nani atampa fedha; ni wapi tutapata na wala si kuazima, huu ni ugonjwa." Huu ni ukweli hata katika ngazi ya familia. Ikiwa wewe na familia yako maisha yenu ni kutegemea wengine hamwezi kuendelea na maisha yenu yatakuwa ya shida. Kibaya zaidi mtakuwa hamna maamuzi katika maisha yenu. Hebu mcheki Mkapa ndani ya suti ya 4 buttons babake bonge la tai kweli anapendeza.

Thursday, May 6, 2010

Kikwete aliulizwa swali kuhusu Demokrasia


Moja kati ya maswali mengi yaliyoulizwa katika mkutano wa kimataifa kuhusu masuala ya uchumi ulioanza jana jijini Dar Es Salaam na utakaodumu kwa muda wa siku tatu ni kuhusu Demorasia kama nyenzo inayofaa katika kuongoza nchi. Kikwete alilijibu swali hilo kwa werevu mkubwa. Soma magazeti.

Peniel Lyimo


Peniel Lyimo (kulia) mmoja wa Makatibu Wakuu Waandamizi hapa nchiniakiwa katika moja ya Panel kwenye mkutano wa Kimataifa wa Uchumi unaoendelea jijini Dar Es Salaam. Ni Mchumi Kilimo aliyebobea ambaye amefanya kazi Wizara ya Kilimo, Fedha na sasa ni Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu. Nitamkumbuka kwa usemi wake-"serikali inaongozwa kwa sheria, taratibu, kanuni na miongozo."

Tusije tukafanya makosa kuhusu adhabu ya kifo

Hebu fikiria mtu anamuua baba yako, mama yako, mtoto wako dada yako au binadamu yeyote yule. Halafu eti isiwepo naye kuhukumiwa adhabu ya kifo endapo atakutwa hana hatia. Tukumbuke kuwa mazingira ya Tanzania ni tofauti kabisa na nchi zilizoendelea. Kumpa kifungo cha maisha wakati ametoa uhai wa mwenzake ina maana bado mtu anaweza akaua kwa lengo la kutoa roho ya yule aliyemkusudia ili atoweke duniani. Hebu fikiria jinsi waliaachwa na yule aliyeuawa wanavyoathirika katika mazingira yetu. Tafakari.

Wednesday, May 5, 2010

Eti Bi Kizee!


Inasemekena kuwa kuna 'Bi Kizee' (Pichani) mmoja mwenye umri wa miaka 70 ametembea kwa miguu umbali wa kilomita 35 kupinga hotuba ya Rais Jakaya Kikwete. Hivi kweli kwa maisha ya Tanzania mzee wa miaka 70 anaweza kutembea km 35. Hebu angalia picha hii kulia kwako huyu kweli tunaweza kumwita Bi Kizee wa miaka 70? Waandishi tuwe makini. Habari hii imetolewa na Gazeti la Mwananchi la tarehe 5/5/2010

Gharama za kupanda miti aina ya minazi barabara ya Sam Nujoma ni ipi?

Gazeti la Daily News la tarehe 5/5/2010 limeandika habari moja kwenye kurasa za mbele inayohusu Dar Es Salaam inavyooteshwa miti katika jitihada za kupamba jiji tayari kwa mkutano wa Kimataifa utakauzungumzia masuala ya uchumi. Kilichonishtua ni gharama za kuotesha miti hiyo je ni Tzs 700,000/- kwa mti mmoja au US $ 700,000 . Haikuelezwa wazi wazi. Au gharama za kuotesha miti 50 ni Tzs 700,000/- au US $ 700,000. Kama kuna aliyeisoma habari hiyo basi anieleweshe.

Mei Mosi ya mwaka huu kulikoni?

Kwa kawaida tarehe Mosi Mei wafanyakazi duniani kote husherehekea sikukuu ya wafanyakazi. Hapa Tanzania mwaka huu mambo yamekuwa tofauti kabisa kutokuelewana kati ya mwajiri hasa Serikali na Vyama vya Wafanyakazi kumewagawa wafanyakazi. Ingawa maadhimisho haya yalifanyika Kitaifa jijini Dar Es Salaam lakini kulikuwa na vikundi viwili kimoja Mnazi Mmoja na kingine Uwanja UHURU. Ndiyo maana nauliza Mei Mosi kulikoni mwaka 2010 hapa Tanzania?