Friday, January 29, 2010

CAN2010 - Uzalendo?


Licha ya kuwa na vidonda kwenye paja lake lakini usiku wa Jana Andre Ayew alicheza kufa na kupona na kuisaidia timu yake ya Taifa ya Ghana (Black Stars) kuishinda Nigeria (Super Eagles) 1-0. Najiuliza uzalendo?

Ulaya wameanza kurudisha kwa umma huduma zilizobinafsishwa


Miaka ya 1980-90 wimbi la kubinafsisha huduma liliikumba karibu Ulaya yote. Kukiwa na dhana kuwa huduma ikitolewa na kampuni binfasi hutolewa kwa kiwango cha kuridhisha. Huduma kama vile za umeme, maji sasa zinaendeshwa na vyombo vya umma kama vile Halmashauri za miji au taasisi za kiserikali. Wakati Ulaya inabadilika hivyo sisi tunaendelea kubinafsisha karibu kila aina ya huduma. Tusimame na tuchunguze kwanza.

350 km kwa saa ndiyo garimoshi la china litakavyosafiri ifikapo mwaka 2011

Ah. Wakati mwendo wa gari moshi la kwetu ni km 35 kwa saa. China wataingiza garimoshi litakalosafiri kwa kasi ya kilometa 350 kwa saa. Hiyo ndiyo jeuri ya teknolojia. Huku sisi tukidharau Mchina bwana vitu vyake feki kabisa. Umeisoma hii?

Nyonya mwanangu


Mtoto wa kimasai akinyonyeshwa maziwa kutoka kwenye kibuyu. Wamasai ni kabila linaloenzi mila na tamaduni za kwao. Moja ya tamaduni hizo ni utumiaji wa maziwa. Tangu wakiwa wadogo wamasai hutumia maziwa kwa lishe kwas hali hiyo ni nadra sana kuwakuta watoto wa kimasai wenye utupiamlo. (Picha kwa hisani ya gazeti la DailyNews)

Kwa kandanda ya jana Misri wana nafasi kubwa yakuwa mabingwa ' AFCON'


Nimekuwa nikifuatilia mechi karibu zote walizocheza timu ya Misri 'Pharaos.' Kusema kweli ni wazuri. Kila idara imekamilika na wanacheza kitimu na mkakati wenye lengo. Wachezaji wanauwezo wa kumiliki mpira, kupiga chenga, kutoa pasi, mbio, stamina na mikikimiki ya mpira si haba wanaijua.

Kitendo cha kuidungua Algeria mabao 4-0 katika mchezo wa nusu fainali uliofanyika jana usiku nchini Angola katika kumtafuta bingwa wa 'AFCON' sio mchezo. Yameingia bila ubishi wowote. Pharao hawa wameshinda mechi zote tena wamezishinda timu ngumu. Timu tunazotegemea kutuwakilisha vizuri kwenye kombe la dunia ( wao hawamo). Kuna nini tena!
Kwa uwezo walionao shilingi yangu naiweka kwao. (Picha kwa hisani ya Website ya CAF)

HIVI NDIVYO GYAN ALIVYOSHANGILIA GOLI LAKE DHIDI YA NIGERIA


Wakicheza mpira wa kufundishwa na wenye mkakati wa ushindi, Ghana licha ya kuwa na wachezaji wengi majeruhi na vijana wameweza kuwaondosha wakongwe na jirani zao timu ya Super Eagels ya Nigeria kwa goli moja kwa nunge. Goli lililofungwa kwa kichwa katika dakika ya 20 na mshambuliaji hatari wa kimataifa Asomoah Gyan lilikuwa ni goli zuri.

Nigeria walijaribu kila njia kuweza kusawazisha matokeo na hatimaye kupata ushindi lakini pilika hizo zilitibuliwa na ngome imara ya Black Stars. Pengine wa kumlaumu zaidi ni Obafeni Martins wa Nigeria aliyekosa mabao mengi huku akitegemea zaidi guu lake la kushoto. Pichani Gyan akishangilia bao lake.(Picha kwa hisani ya Website ya CAF)

Thursday, January 28, 2010

KISE KIDS yaiparua Mpera 3-0


Magoli matatu yaliyofungwa katika kipindi cha pili yameiwezesha timu ya KISE KIDS inayoundwa na vijana wadogo wa kijiji cha Kisemvule kilichoko wilaya ya Mkuranga mkoa wa Pwani kuiliza timu ya Mpera. Mchezo huo ni moja ya mapambano ya ligi inayoendelea kijijini Kisemvule kwa sasa yenye lengo ya kumpata bingwa atakayezawadiwa zawadi kemkem na kutoa burudani kwa wakazi wa Kisemvule kijiji kinachokua kwa kasi katika kata ya Vikindu.

Akiongea na blog hii mwalimu wa soka wa timu hiyo Bw Abdallah Pembe amesema kuwa siri kubwa ya ushindi wa timu yake ni mazoezi pamoja na nidhamu. Mwenyekiti wa kijiji cha Kisemvule Bw. Shaaban Makuka ameahidi kuiwezesha timu hiyo ya vijana ili iweze kutoa wachezaji watakaounda timu ya kijiji cha KISEMVULE ambayo kwa siku za hivi karibuni imekuwa haisikiki sana.

Jumamosi iliyopita KISE KIDS a.k.a 'Watoto Wetu' iliwatoa kamasi baba zao -timu ya VETERANS kwa kuwafunga mabao 4-2 katika uwanja wa Kisemvule Magengeni.

Timu ya KISE KIDS imeanzishwa mapema mwaka huu na tayari imeshaanza kutoa upinzani mkali kijijini hapo na kuwa gumzo kwa wazee na vijana.

Hatuna mpango endelevu wa kudhibiti ombomba jijini


Hii ndiyo hali halisi. Ombaomba wanazidi kuongezeka jijini. Na si kweli kuwa wote wanaoomba ni walemavu hata kidogo. Wengi wamejenga tabia ya kuomba. Omba omba wamezagaa sehemu mbalimbali jijini hasa wilaya ya Ilala. Wanapatikana kwa winngi pale 'fire' na kisutu. Kibaya zaidi watoto wadogo hutumika katika shughuli hiyo ya kuomba huku wazazi (hasa kinamama) wakiweka makazi yao kandokando ya barabara. Hivi tumeshindwa kuandaa mpango endelevu wa kuwadhibiti ombaomba? (Picha kwa hisani ya gazeti la Mwananchi 28/1/2010)

Morogoro mkungu shilingi elfu 3 Dar ndizi 5 miatano


Licha ya kusafirisha mikungu yake ya ndizi hadi sokoni Morogoro. Mkulima huyu anauza mkungu mmoja kati ya shilingi 2,500 hadi 3,000/- Kwa bei hii lini ataweza kujenga nyumba bora ya kisasa na kuona kuwa kweli kilimo kinalipa? Bei ya bati moja ni shilingi 16,000/- (gauge 30) atahitaji kwa wastani mikungu saba aweze kununua bati hivyo kwa nyumba ndogo inayohitaji mabati 30 itabidi auze mikungu 180. Kutoka shamba la ukubwa upi na kwa muda gani? Kwa bei hii kweli kilimo kinalipa?

Mfanyabiashara jijini Dar huuza ndizi tano kwa shilingo 500 kwahiyo akiwa na ndizi 1000 tayari amekuwa ameshaingiza shilingi 100,000/- Tafakari.

Mizengo Pinda a.k.a Mtoto wa mkulima


Waziri Mkuu wa Serikali ya Muungano wa Tanzania Mhe. Mizengo Pinda tangu ashike madaraka hayo amekuwa mstari wa mbele kuinua uzalishaji wa kilimo. Ameshatembelea wakulima wengi shambani na taasisi nyingi zinazojishughulisha na kilimo. Nafikiri anaendelea kujifunza mengi kuhusu kinachosibu uzalishaji wa kilimo hapa nchini. Pinda sema kinachotakiwa kufanyika na kilimo kipewe kipaumbele katika kutengewa raslimali power tillers pekee haitoshi. (Picha kwa hisani ya gazeti la Mwananchi tarehe 28/1/2010)

Tuesday, January 26, 2010

Ukishindwa umejitakia mwenyewe


Mazingira mazuri kama haya si rahisi kushindwa mtihani. Vitabu vipo vya kutosha. Viti ni vizuri, meza kubwa na safi na watoto wenyewe ni wasafi. Kuinua kiwango cha elimu ni lazima serikali kuboresha shule zetu za msingi na sekondari zile tunazoita za kata ili wanaosoma shule binafsi watamani kusoma shule za kata. Hii inawezekana.

Uchaguzi una mambo eti Abood anasonga ugali!


Leo asubuhi nimeinyaka picha moja ya kejeli kwa waathirika wa mafuriko wilayani Kilosa. Picha hiyo yenye maelezo kuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, kutoka Mkoa wa Morogoro, Aziz Abood, akimsaidia kusonga ugali mmoja wa waathirika wa mafuriko... Hivi kweli kusonga ugali kunasaidia wahanga wa mafuriko au dhihaka tu. Hii ni mikikimikiki kuelekea uchaguzi 2010 tuwe macho na watu hawa. Morogoro fungueni macho mnawajua wa kuwachagua!

Huyu Mtikilla vipi?


Kila tunapokaribia uchguzi mkuu, Mchungaji Mtikilla haachi vituko na kashfa ambazo mara nyingi humfikisha mahakamani na kutumia muda mwingi mahubusu. Mimi simwelewi vizuri Mtikilla ana nini au ana lengo lipi?

Misri na Algeria wako mbali kisoka


Mimi ni mmoja wa mashabiki wa soka la kiarabu iwe Misri, Algeria, Tunisia na Morocco. Hawa jamaa wanajua mpira, wanacheza kwa malengo,uzalendo na wametulia. Wanajua sana kuusoma mchezo wa wapinzani wao.

Jana niliangalia kwa makini mchezo wa robo fainali kati ya Misri na Cameroon. Wamisri walishambuliwa sana, walianza kufungwa wao na kuelemewa na mipira mingi ya kona lakini walitulia na hatimaye kuweza kuifungisha virago Cameroon mabao 3-1.

Misri wanaye mwalimu wa siku nyingi mzalendo Hassan Shihata. Anawajua wachezaji wake anaongea kwa lugha moja isitoshe anaangaliwa vizuri! Watanzania tujifunze kutoka kwa waafrika hawa. Tusishabikie rangi ya ngozi wote tunacheza CAN na tupo barani Afrika! (Pichani-Zidan wa Misri akimtoka Alexander Song wa Cameroon - kwa hisani ya gazeti la mwananchi 26/1/2010)

Tatizo huzaa tatizo


Jumapili iliyopita niliweza kuhudhuria ibada takatifu katika Kanisa Katoliki Parokia ya Vikindu. Katika mahubiri yake Paroko Tom alitoa hadithi fupi kama ifuatavyo.

Siku mmoja mwanaume fulani aliyekuwa akiendesha gari lake alimkuta binti mrembo aliyemuomba msaada wa usafiri au 'lift' kama tulivyozoea. Bila kusita alimpa msaada huo binti huyo. Lakini mara alipoingia ndani bwana huyu alianza kujawa na wasiwasi, baada ya muda alipoangalia kiti alichokaa yule binti akaona kuwa amezirai! Bwana yule alijitahidi kumpeleka binti huyo hospitali iliyo karibu. Baada ya muda mrefu akapata habari kutoka kwa wauguzi inayompa hongera kwa kuwa baba!

Bwana yule alihamaki. Itakuwaje, yeye hamjui binti huyo. Alipoulizwa yule binti akasema haswa bwana yule ndiye baba wa mtoto. Haikuishia hapo polisi waliitwa na hatimaye bwana yule aliwekwa mahabusu kwa kosa la kufanya vurugu wakati alipokuwa akikataa kuwa si baba wa mtoto.

Shauri lilifikishwa mahakamani na ikaamuriwa kuwa bwana yule apimwe. Majibu yalipotoka iligundulika hana uwezo hata wa kuweza kuwa na mtoto. Bwana alifurahi kwani alishinda. Lakini akajiuliza sasa itakuwaje? Mbona nina watoto wawili niliyezaa na mke wangu wa ndoa. Alijiuliza? Alichanganyikiwa. Tatizo limezaa tatizo. Ni kweli kama binadamu hatuwezi kukwepa matatizo. Ubinadamu ni pamoja na kukabiliana na matatizo katika maisha yetu.(Picha kwa hisani ya gazeti la Mwananchi 26/1/2010)

Friday, January 15, 2010

Mafisadi endelezeni nchi basi

Tatizo si ufisadi, tatizo ni jinsi mafisadi wanavyotumia fedha hizo walizozipata kwa namna ambayo haisaidii nchi hii. "Hebu fikiria Banzi fisadi pamoja na kuchota fedha nyingi za nchi hii anaziweka kwenye benki ya nchi za nje, sasa hii inasaidia nini hata mwenyewe sidhani kama zinamsaidia sana.' Anahoji msomi kutoka moja ya vyuo vikuu hapa nchini ambaye amewahi kusoma darasa moja na Banzi wa Moro. Kuna mantiki hapo eh! Mwenzangu unayesoma blog hii unasemaje?

Tufanye kazi kama wanajeshi

Leo asubuhi wakati blog hii ikisafiri kuelekea Morogoro mjini ikitokea Kilosa. Ilikutana na msafara mkubwa wa magari ya Jeshi la Wananchi Tanzania. Nadhani yalikuwa yakielekea Kilosa kulikotokea maafa. Naambiwa kuwa wanaenda kujenga daraja lililoendolewa kwenye mto Mkondoa.

Jeshi limepokea agizo na tayari wameanza kutekeleza wana vifaa, wana watu na nina imani kuwa wataitekeleza kazi hiyo kwa muda mfupi sana. Blog hii inajiuliza hivi kwanini tusiwe kama wanajeshi katika kufanya kazi zetu?

Tuache kujenga nyumba za biskuti!

Nyumba nyingi zilizoanguka baada ya kukumbwa na mafuriko mjini Kilosa ni zile zilizojengwa mabondeni kwa matofali mabichi au zile zisizojengwa kwa msingi imara. Nyumba hizi wenyewe wanaziita biskuti. Kwani biskuti ikiwekwa maji tu huyeyuka. Ndivyo ilivyotokea Kilosa. Wengi wameachwa bila makazi. Hili ni fundisho kwa wote kuwa tunapojenga nyumba tujitahidi kujenga msingi imara ikiwezekana tujenge kwa mawe au matofali ya saruji.

Mafuriko yaliyoikumba Kilosa Kusini yanatisha

Ukitokea Mikumi na kuingia Kilosa mjini hutaamini macho yako, sehemu kubwa imetota maji, tope. Unapoingia mjini na kupita barabara ya kwenda Ilonga kwenye shule ya msingi Mazinyungu na hospitali ya wilaya ya Kilosa unaona makundi ya watu, vitanda viko nje, madirisha , milango, mabati huku makundi ya watoto wadogo wanacheza na mahema yamejengwa kuhifadhi waathirika na mafuriko. Ni simanzi kubwa sana. Mafuriko yamewafikisha hapo walipo kwa kipindi kifupi bila kutarajia.

Mji wa Kilosa umefurika watu wa aina mbalimbali ili kuweza kurekebisha mambo. Nyumba za wageni hazitoshi na hata huduma za chakula nazo hazikidhi haja. Haya ndiyo matokeo ya maafa. Kweli maafa ya Kilosa yanasikitisha. Yameathiri watoto, wakubwa wazee, wake kwa wakulima yamerudisha nyuma maendeleo yao.

Wengi hawakifahamu Chuo cha Taifa cha Sukari (NSTI)

Kwa kuwa kinajulikana kwa jina la Chuo cha Taifa cha Sukari wengi hufikiri kuwa chuo hicho hutoa mafunzo ya kutengeneza sukari tu. Hii si kweli. Blog hii ilipotembelea chuoni hapo hivi karibuni ilijionea mengi na kujifunza mengi.

Chuo cha Taifa cha Sukari (NSTI) kiko Ruaha karibu kabisa na kiwanda cha Sukari cha Kilombero (KI). Licha ya kutoa mafunzo ya aina mbalimbali na kuwa na miundo mbinu na mazingira ya kuvutia chuo hakifahamiki na wengi.

Baadhi ya mafunzo ya muda mfupi na muda mrefu yanayotolewa chuoni hapo ni pamoja na ufundi wa umeme wa majumbani na viwandani, utengenezaji wa kompyuta, ukarabati wa magari na utengenezaji wa vipuri vya aina mbalimbali pamoja na udereva. Mafunzo ya utengenezaji wa sukari unalenga mahitaji ya nyumbani au familia pamoja na viwandani. Chuo pia hutoa mafunzo ya kujifunza.

Tofauti na vyuo vingine chuo hicho hupokea hata wanafunzi waliomaliza darasa la saba kwani wanaamini na wanayo mifano ya wanafunzi waliopitia chuo hicho wakiwa na elimu ya darasa la saba na kufanya vizuri kuliko wale wa kidato cha nne au cha sita. Tukitafute na tuwapeleke vijana wetu NSTI-Kidatu.

Ifakara sasa inafikika kirahisi

Miaka ya themanini na kurudi nyuma ukiambiwa kusafiri kwenda Ifakara hasa wakati wa masika hiyo ni adhabu kubwa sana. Barabara ilikuwa mbaya kweli kweli. Kutoka Mikumi hadi Ifakara barabara ilikuwa ya udongo yenye makona mengi na madaraja ya hapa na pale. Gari nazo zilikuwa chache na zilikuwa katika hali mbaya. Kwa kweli wenye magari yao hawakuwa tayari kupeleka Ifakara.
Hali imebadilika kabisa hivi sasa. Juzi nilisafiri kwenda Ifakara na kuona sehemu kubwa ya barabara hiyo imejengwa kwa kiwango cha lami hivyo kurahisisha usafiri kutoka Mikumi hadi Ifakara. Si ajabu kuona gari ndogo (taxi) zikisafairisha abiria kutoka Mikumi hadi Ruaha kwa shilingi 2,000/= tu. Hii ni hatua kubwa ya maendeleo. Nina matumaini kuwa hadi kufikia mwaka 2012 sehemu iliyobaki itakuwa imekamilika kwa kiwango cha lami.

Ikumbukwe kuwa inakopita barabara hiyo ni maarufu kwa uzalishaji wa mazao mbalimbali ya kilimo. Kwa kuimarisha barabara hiyo kutaongeza chachu ya uzalishaji wa mazao kama mpunga,miwa, ndizi na mahindi.

Tuesday, January 12, 2010

Soko Kuu la Morogoro bado chafu

Kila inaponyesha mvua, Soko Kuu la Morogoro ni uvundo. Linanuka.
Nipo hapa Morogoro kikazi. Leo mchana nilipata fursa ya kutembelea soko hilo ni matope, matope ,matope. Nilimuuliza ndugu yangu Fau Mizambwa. Eee bwana vipi hapa mbona hakuna mabadiliko? Kila mwaka hali ni ileile wakati mazao yanayouzwa hapa hasa matunda na mboga mboga ni vya kiwango cha hali ya juu. Lakini usafi ni duni sana. Ujue walaji wengi wa matunda wanaponunua embe au ndizi hawana muda wa kuosha kwa hali hii, homa ya matumbo na kipindupindu haviwezi kuepukika.

IVORY COAST MAJINA YATAWAPONZA

Ndiyo, IVORY COAST walikuja Tanzania na kucheza mechi za kirafiki mbili za kupasha moto kabla ya mshindano ya soka ya CAN maarufu hapa Afrika kwa kupambana na Taifa Stars na AMAVUBI timu ya Taifa ya RWANDA mechi zote mbili walishinda. Lakini hawakuonyesha soka la uhakika huku wengi wakisema kuwa wameficha makucha yao. Lakini jana wametoka suluhu na timu ya Burkina Fasso isiyo na wachezaji wenye majina. Kwa hiyo Ivory Coast wajihadhari, huko Angola hawaogopi majina oh Drogoba au Kone. Pigeni soka la uhakika tuwaone basi. Au huko nako mnategea? Mpaka lini?

Watanzania tuache uvivu tuchape kazi

Ni kweli mvua zinazonyesha hivi sasa kuna baadhi ya maeneo hapa nchini zimeleta maafa makubwa. Lakini ni kweli pia kuna baadhi ya sehemu mvua zinazonyesha ni neema. Hivi karibuni nilisafiri kwa bus Dar hadi Korogwe na leo nimesafiri kutoka Dar hadi Morogoro huko njiani nimeona jinsi mimea ya mazao iliyowahi kupandwa ilivyostawi vizuri. Kwa vyovyote vile wakulima walio wahi kutayarisha mashamba mapema na kupanda mapema watavuna. Lakini sehemu kubwa haijalimwa. Kwa hiyo utashangaa kwanini hali iko hivyo. Je, hatuna mipango mizuri ya kilimo? Au ni uvivu tu. Mimi naamini kuwa iwapo ardhi hii tunayoichezea wataruhusiwa wageni kuwekeza tutaona maajabu na sisi kubakia vibarua. Watanzania tuache maneno mengi tufanye kazi kwanza. Pengine badala ya kilimo kwanza tuseme "KAZI KWANZA."

HUDUMA HII YA ABOOD BUS INAKERA

Tarehe 9 Januari nilisafiri kutoka Dar kwenda Morogoro kwa shughuli za familia. Nilifika kituo cha Ubungo saa 3.30 asubuhi. Baada ya kukata ticket ya mabus ya Abood niliarifiwa kuwa safari itaanza saa nne kamili. Jambo la kushangaza ni kwamba niliweza kusafiri saa 7.00 mchana. Kwa nini nasema huduma ilikuwa ni mbovu ni kwasababu inasemekana gari letu lilipata hitilafu njiani. Kwahiyo wale waliokata ticket nyuma yetu mabus yao yalipokuja waliandoka na kutuacha. Kwa kuwa sisi hatukuchagua bus ilikuwa rahisi tu kwa utawala kuamua kuwa bus litakalofika kwanza ndiyo waliotangulia kukata ticket wapate huduma hiyo. Ni baada ya wasafiri kulalamika ndipo utawala wa mabus hayo ulipoamua kutupa bus lililofuata baada ya mabus matatu kutuacha.

Friday, January 8, 2010

Ninamhusudu sana Mkongwe huyu wa siasa


Robert Mugabe, Rais wa Zimbabwe ndiye ninaye muhusudu sana barani Afrika kwa msimamo wake usioyumba. Hebu angalia ndevu zake zimekaa kijasiri sana! Halafu kama hicho Kiingereza ujue kimepanda sana ndo maana waingereza na waamerika huwa wanamwangalia tu hawamtishi kwa chochote. Akiambiwa asihudhurie mkutano, ndo kwanza anakuwa wa kwanza kuingia mkutanoni au wa mwisho kwa mshangao wa wengi na huku akiwaacha wabaya wake macho ga!

Nani atawika Angola?

Hebu waangalie nyota hawa wa Afrika katika kabumbu (Essien, Etoo na Drogba) wote watakuwa Angola katika mashindano ya kutafuta Bingwa wa Afrika 2010. Kati ya hawa nani atawika? Au ninani atakayejichomoza kung'ara katika mashindano haya. Jibu tutalipata baada ya mashindano.

Daladala za Mwenge -Posta raha tupu


Kama kuna daladala zenye ustaarabu jijini Dar basi ni zile ziendazo Mwenge-Posta. Kwanza ni 'pamba' ile mbaya. Abiria wastaarabu, kondakta wasafi. Mwendo ni wa usalama. Ndani ya bus kuna vitenga vya kutupa uchafu. Hebu angalia hata wakati wakupanda basi wanapanda kwa ustaarabu kama vile wamepangwa huku konda akigani Mwenge-Posta! Mpaka raha. Big Up daladala za Mwenge-Posta. Sumatra hebu wapeleke wamiliki wa mabus wa njia nyingine wakajifunze kwa wenzao wa Mwenge-Posta.

Dar magari mazuri barabara mashimo


Ukiendesha gari jijini Dar Es Salaam ni lazima uwe makini. Si ajabu kukuta bonge la shimo katikati ya barabara. City Fathers mpo? Pichani nani ameweka kibendera chekundu cha hatari. Hii ndiyo Dar.

Maisha PLUS kuna chakujifunza?


Maisha PLUS imeanza tena katika msimu wake wa pili. Vijana wamejitokeza kwa wingi na tayari 18 wamefanikiwa kuingia kijijini. Swali - Je, Maisha PLUS kuna cha kujifunza?

Tuesday, January 5, 2010

Teknolojia mbadala ya matumizi ya mkaa


Miti inakwisha kwa matumizi mbalimbali uchomaji wa mkaa ikiwa ni shughuli mojawapo inayomaliza misitu. Watu wengi hapa nchini hutumia mkaa kama nishati ya kupikia. Hata hivyo kutokana na miti kupungua bei ya mkaa hupanda kwa kasi sana. Naambiwa gunia la mkaa jijini Dar Salaam kwa sasa ni shilingi 25,000/- Bei hii kwa vyovyote vile ni ya juu kwa watu wenye kipato cha chini.

Kwa kuwa tatizo linaeleweka, watu wamekuwa wakibuni teknolojia mbalimbali kwa kupata mbadala wa mkaa. Mojawapo ni mchanganyiko wa takataka za karatasi vumbi la mbao mabaki ya miwa, majani kwa kuyamba kwenye vitonge vidogo vidogo kama mkaa. Uganda, Kenya na hata Tanzania wameshanza kutumia teknolojia hii mbadala ya mkaa na kuonekana kupendwa zana na watumiaji wake hasa kutokana na bei ndogo ukilinganisha na mkaa wa asili.

Usipotunza mbegu si mkulima


Si rahisi mkulima kula chakula chote alichovuna bila kutunza mbegu ya kupanda kwa msimu ujao. Kwa kawaida mbegu huchaguliwa iliyo nzuri kwa mategemeo ya kutoa mavuno mazuri. Kwa kuona hilo watafiti wa kituo cha Utafiti Naliendele kila mwaka huandaa maonyesho ya mbegu. Wakulima wa sehemu fulani hualikwa na kila mmoja huleta aina ya mbegu ya mazao anayozalisha. Maonyesho haya ni muhimu na huvutia wakulima wengi kwani kwa kupitia maonyesho haya wakulima wanaweza kubadilishana mbegu, kuuziana mbegu pamoja na kujifunza usatawishaji wa mazao hayo. Huu ni utaratibu mzuri. Hata nchini Msumbiji utaratibu kama huu hufanyika. Wakulima nao wanacho cha kuonyesha kwa hiyo watafiti na wakulima hubadilishana uzoefu. Pichani wakulima wa Msumbiji katika maonyesho ya mbegu. Angalia mbegu za kunde, bamia, mtama,karanga, mahindi, ufuta zote zimeltwa

Konokono wanaliwa


Afrika hihii, konokono wanaliwa tena inasemekana kuwa ni chakula kizuri chenye protein. Konokono huokotwa msituni na kutumiwa kama mboga. Shughuli hii hufanywa na wanawake. Hebu angalia pichani mwanamke akionyesha bonge la konokono. Kweli konokono ni mali.

Ng'ombe nyumbani


Ufugaji wa ng'ombe nyumbani (zizini) ni jia bora ya kufuga sehemu zenye uhaba wa ardhi kama vile mkoa wa Kilimanjaro. Ng'ombe hupata huduma za malisho wakiwa ndani ya banda wakati wote. Lakini ufugaji huu huwahusisha zaidi wanawake na watoto kutumia muda mwingi kutafuta chakula cha wanyama, kusafisha banda pamoja na kuwalisha. Ufugaji huu kwa kweli huchosha licha ya kuwa faida zake ni nyingi.

Bongo-Dar Es Salaam mbinu za wizi usipime

Wizi wa vyombo vya magari vinaenea kwa kasi jijini Dar Es Salaam. Wenye magari wanaibiwa, vioo, wind screens, mud guards na chochote kinachoweza kutolewa. Ukikitafuta utakipata Gerezani tena kile kile ulichoibiwa na utauziwa kwa bei mbaya. Lakini ole wako kama utajaribu kuchukua hatua hukipati. Hii ndiyo hali hali ya wizi wa vyombo vya magari jijini Dar.

Dar epuka kutoa lift kwa mtu usiyemfahamu ni hatari hata kama ataonyesha kukufahamu na kukutaja kwa jina kama uko peke yako ongeza mwendo. Mtu huyo anaweza kukuibia chochote kilichomo ndani ya gari (comupter,simu ya mkononi na vinginevyo) kundi hili la wezi liko pale njia panda ya Kilwa na Nelson Mandela kama unakwenda Uwanja wa UHURU.

Dar, usione mtu mzee tena mstaarabu amevalia kanzu na kofia (bargashia) ukafikiri ni muumini mzuri, mwanafunzi kavalia uniform yenye beji ya shuli pamoja na bag lake. Kaa chonjo anaweza kukutoa upepo mara moja ukiwa ndani ya daladala.

Dar usione umekaa kwenye kiti cha daladala na binti mrembo ukafikiri wote ni wasafiri. Kaa chonjo unaweza kushtukia huna pochi na simu haiko vilevile na binti alikoshukia ni kitendawili.Hii ndiyo Bongo Dar Es Salaam. Wakati tunaanza mwaka mpya tuwe makini.

Monday, January 4, 2010

KOROGWE 2010

Baada ya kusherehekea mwaka mpya 2010 nikiwa. Tarehe 2/1/2010 nilisafiri kwenda Korogwe. Kule tulienda kushuhudia jinsi mkwe wetu anavyoagwa (Send off Party). Korogwe ni mji unaokuwa kwa haraka sana na mpango miji wake umetulia kwa kweli. Mitaa imepimwa vizuri na barabara zinajulikana. Kwa kupita barabara ya kwenda Arusha huwezi kutambua kuwa Korogwe ni nzuri na imejengeka. Hivi ilikuwaje Dar ikashindwa kupangika hadi kumetokea msongamano wa ajabu ambao sasa tunashindwa kuurekebisha?