Tuesday, July 31, 2012

Maini ya NjiaPanda ya Mbande

Kama unasafiri kuelekea Dodoma njiapanda ya kwenda Kongwa na Mpwapwa sehemu inayoitwa Njiapanda ya Mbande ni maarufu kwa biashara za nyama ya kuchoma. Hata asubuhi hapa unaweza kupata maini na figo za moto!

Speaker za S90-Nimezikuta Dodoma

Speaker za kirusi S90 (Sto divnosta) nimezikuta kwenye ukumbi mmoja mjini Dodoma na zinatwanga ile mbaya!Speaker hizi ni toleo la miaka ya themanini!

Hapa ndipo KILIMO IV

Hili ndilo jengo la Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika lilipo mjini Dodoma al maarufu kama KILIMO IV. Ukiwa ndani ya jengo hili ni kwa kazi maalum na hakuna kulala. Wizara hulitumia jengo hili kwa mikutano mbalimbali inayofanyika mjini Dodoma. Lakini hutumika kikamilifu wakati wa vikao vya Bunge hasa Bunge la kuwasilisha Bajeti.

Hali ngumu wazee

Wakati vijana wenzake wakiwa katika pilika za kuuza biashara zao za nyanya na maboga na wengine kuuza matenga,kijana huyu(pichani)alitulalamikia kwa kusema hali ni ngumu wazee. Sijui tungemsaidiaje.Atazidi kulalamika sana wakati wenzake wakiendelea endapo hatabadilika.

Wanawake nao wamo

Banzi wa Moro aliinyaka picha hii wakati mwanamke huyu akiwa katika harakati za kupanga matenga kwenye lori. Miaka 20 iliyopita, mwanamke asingweza kudandia lori na kupanga matenga.Sina shaka mwanamke huyu ni mfanyabiashara wa nyanya.

Biashara huria

Baada ya kununua bidhaa inabidi kukaa chemba kujadili bei na mchuuzi kwani unaweza kupunguziwa bei kutokana na ushawishi wako kwani biashara ni huria! Usishangae boga la sh 1000 likauuzwa kwa sh 500!

Nitakutumia nikifika Kisemvule

Huduma za M-Pesa, Tigo-Pesa na Airtel Money zimeingia kwa kasi kijijini kwetu Kisemvule-Mkuranga.Usiwe na wasiwasi ninaweza kukutumia ngawira au kupokea ngawira nikiwa Kisemvule!

Boga kwa futari

Tulipofika Wami Dakawa njiapanda ya kwenda Turiani, tulishindwa kujizuia kununua maboga. Wakati huu wa mfungo wa mwezi Mtukufu wa Ramadhani, futari ya maboga ni moja ya vikoromwezo vya chakula vinavyotumika kwa futuru.Hapa tulinunua boga moja kwa kiasi cha shilingi 1000/=. Pichani Bi Ishika Mshaguley akichagua boga analolipenda!

Na baadaye safarini DAR

Ndivyo tunavyotumia magari ya serikali. Ni kwa safari za kikazi na si vinginevyo. Toyota Landcruiser S/W nafikiri siyo gari la kifahari eti jamani. Pichani dereva wetu Lems Nyagawa akiwa maeneo ya Dumila mkoani Morogoro tukiwa njiani kuelekea Dar tarehe 22/7/2012 baada ya kikao cha Bunge.

Tunapokuwa Bungeni Dodoma

Tunapowakilisha Bajeti zetu Bungeni- Dodoma si lele mama. Kazi kubwa ni kujibu hoja za wabunge. Mwezi Julai 2012 Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika iliwasilisha Bajeti yake na hivi ndivyo wataalamu walivyojitayarisha kujibu hoja zilizoibuliwa na wabunge.
Mkurugenzi wa Utafiti na Maendeleo Dkt. F.Myaka (mwenye laptop)akiwa katika ukumbi wa Kilimo IV Dodoma
Wataalamu wa kilimo wakifuatilia kwa makini mawasilisho ya Bajeti ya Wizara kupitia luninga wakiwa ndani ya jengo la Kilimo IV Dodoma
Kuna hoja zilizoumiza vichwa lakini zilijibiwa na hatimaye bajeti ikapita.

Mtoto anaposaidiwa kukamilisha 'homework'

Hapa nampa big-UP my nanihii.... kwa kutenga muda kumsaidia binti yetu Maria kukamilisha homework yake!

Watoto hupenda kuzima mishumaa ya birthday

Siyo birthday yake lakini uncle Jordan Kirita alizima mishumaa ya aunt wake Dr. Doreen Moshi (aliyemshikilia).

Umoja unaanzia kwenye familia

Kikundi cha Africana kikiwa kwenye mkutano wa mwezi Julai huko Chang'ombe karibu kabisa na uwanja wa TCC nyumbani kwa Bw. na Bi. J.Kirita

Ukishuka ulizia Kisemvule gengeni!

Hapa ndipo bus la Mbagala Rangi Tatu-Mwandege-Vikindu-Kisenvule linapogezia. Ni Kisemvule magengeni.

Wako kwao

Hata kama Kisemvule, Mkuranga!

Uncle God Kyando Luhungu

Tarehe 28/7/2012 kwetu Kisemvule tulitembelewa na mgeni maarufu si mwingine ni uncle God Kyando Luhungu anayeishi Kurasini jijini Dar. God, ni mtoto wa dada yangu marehemu Averina Constantine Gega (Mrs A.Luhungu) a.k.a Dada Ave aliyefariki siku chache baada ya kuzaliwa God.God sasa yuko darasa la sita. Ingawa amevalia T-shirt ya kijani (pichani) yeye ni mpenzi mkubwa wa klabu ya Simba (mnyama) kwa hapa nyumbani na ni shabiki wa Chelsea huku majuu!.Angalia jinsi anavyofuatilia matangazo ya mechi ya Yanga na Azam iliyochezwa tarehe 28/7/2012 kupitia kiredio kidogo ambapo Yanga iliibuka mshindi na kunyakua Kombe la Kagame kwa kuibamiza Azam 2-0. Uncle God pamoja na mimi mjomba wake (Mwanachama wa Simba) hatukufurahia hata kidogo ushindi huo wa Yanga!

Dafu la Kwanza

Tupo Kisemvule takribani miaka minane sasa. Tumeanza kuonja matunda ya bustani yetu. Na hili ndilo dafu la kwanza.Mnazi ni wa Kipemba'
Na huyu alimalizia kwa kulikomba ina maana lilikuwa tamu kwelikweli!

Monday, July 30, 2012

Happy Birthday dada Doreen

Jana tarehe 29/7/2012 ilikuwa ni siku ya kumbukumbu ya kuzaliwa kwa dada Doreen (Mrs Dr.Doreen Moshi)
Mumewe Prof.M.Moshi alimwandalia ndafu.
Hii ndiyo keki yake ya Birthday
Happy Birthday Doreen! Ndivyo anavyosema Prof. Moshi wakati alipokuwa akimlisha ndafu mkewe.

TFRA Mkoani Ruvuma

Wakaguzi wa Wakala wa Mbolea (TFRA) ndani ya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mhe. Saidi Mwambungu wakijitambulisha na kueleza madhumuni ya safari yao ya kikazi mkoani Ruvuma.

Wakulima wanapodanganywa kuhusu mbolea

Hivi ndivyo wakulima wanavyodanganywa. Mbolea imewekwa kwenye mifuko yenye maandishi ya lugha isiyo ya kawaida. Kwa vyovyote vile hiki si kiswahili wala kiingereza pengine unaweza kusema ni Kichina. Ni aina gani ya mbolea, hufahamu. Matumizi yake je? Hatufahamu. Hivi ndivyo wakulima wetu wanavyodanganywa. Na haya ni mojawapo wakala wa mbolea (TFRA) imegundua katika ukaguzi wake wa maduka yanayouza mbolea mkoani Ruvuma mapema mwezi Juni.

Utafiti wa mbolea aina mbalimbali kwa zao la mahindi

Watafiti hapa nchini wanaendelea na utafiti wa matumizi wa aina mbalimbali za mbolea kwa zao la mahindi
Jaribio la Mbolea ya TSP pamoja na UREA
Jaribio la mbolea ya DAP na UREA
Utafiti wa mbolea ya Minjingu Hyper pamoja na UREA
Jaribio la mbolea ya Minjingu mazao na Urea
Urea pekee kwenye mahindi
Kulima mahindi bila kuweka mbolea Je? Katika majaribio haya mtafiti atashauri ni aina gani ya mbolea itumike katika udongo wa aina fulani kwa ajili ya zao la mahindi kutokana na matokeo aliyoyapata. Kwa kawaida utafiti huu ufanywa kwa zaidi ya msimu mmoja.

Mbolea kwenye rambo ! Haiwezekani

Ndivyo alivyokuta CEO wa Tanzania Fertilizer Regulatory Agency Dkt. Suzana Ikerra wakati wa ukaguzi wa maduka yanayouza mbolea mkoani Ruvuma. Kuna sehemu alikuta mbolea imefungwa kwenye vifuko vidogo vyepesi na vyeusi vya rambo. Wauzaji wakidai wanauza mbolea ya 'Sulphate of Ammonia' (SA)! Hii haiwezekani hata kidogo mbolea kuuzwa kwenye mifuko ya rambo. Kuna athari nyingi kwa kufanya hivyo baya zaidi hata wakulima hawana uhakika na bidhaa wanayouziwa matokeo yake mbolea hiyo ikitumiwa mashambani inaweza kutoa matokeo yasiyotarajiwa kama vile kuunguza mimea.

Monday, July 16, 2012

Mitindo hiyo!

Kama unataka kufahamu mitindo iliyopo kwenye chart basi hudhuria shughuli mbalimbali utapata uipendayo.