Wednesday, December 31, 2008

Kwaheri 2008

Kwaheri 2008.

Mwaka huu ulikuwa wamafanikio makubwa kwa blog hii. Banzi wa Moro ameweza kuvuka lengo alilojiwekea kwa asilimia 140! Kumbe inawezekana.

Sina budi nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa afya na busara ya kuweza kukusanya habari mbalimbali na kuweza kuzining'iniza kwenye blog hii.

Nawashukuru viongozi wangu wa kazi walioniwezesha kupata safari za kikazi ndani na nje ya nchi kwazo nimepata fursa ya kuona mengi na kuyaweka ndani ya blog hii.

Kasoro kubwa iliyojitokeza kwa mwaka uliopita ni kwa wasomaji wangu kushindwa kutoa maoni yao kwa habari ambazo zililenga maeneo yenye uzoefu nao.

Ombi langu kwa wasomaji wa blog hii wajitahidi zaidi kutoa maoni yao mwaka ujao. Hii itanipa moyo wa kuweza kukusanya habari nyingi na kuzining'iniza blogini.

Mungu akipenda mwakani naweza kuwa na camera hivyo kuboresha zaidi habari katika blog hii. Mwaka huu mara chache niliweza kudowea camera na kupiga picha chache sana.

Namshukuru mdogo wangu Freddy Mloka, Dada Meab Mdimi ambao wamekuwa wakinitumia picha hasa za familia.

Wamefaulu madarasa hakuna

Matokeo ya mtihani wa darasa la saba yametangazwa lakini kwa bahati mbaya kuna baadhi ya matokeo ya wanafunzi hayajatolewa rasmi eti kwasababu shule zinazotakiwa kuchukuwa wanafunzi hao hazina madarasa! Hali hii imejitokeza zaidi katika mkoa wa Morogoro. Wanafunzi wamefaulu madarasa hakuna.

Sasa viongozi ndo wanakimbizana kutafuta suluhu madarasa yajengwe.
Juzi diwani wa kata ya Mtombozi alifika ofisini kwangu kueleza shida kama hiyo kwa Sekondari ya Mtombizi iliyopo Matombo Morogoro. Jana jioni baadhi yetu tulikutana kujaribu kuweka mikakati ya kuweza kuinasua Mtombozi Sekondari.

Tulichokiona ni kuwa uongozi katika ngazi zote za utekelezaji hauna muono, hauna mikakati. Iweje leo matokeo yanatoka ndo wanakumbuka kujenga madarasa. Hivi jamani Morogoro tuna nini? Hii si lawama kwetu tuonekane hatujali nyumbani?

Hata hivyo tumekubaliana kusaidia kutatua tatizo hilo kwa mikakati tutakayoiweka. Mojawapo ni kuwa na mtandao wa wadau. Na tayari hatua zimeshaanza kuchukuliwa. Hata hivyo tumekubaliana kuwa uongozi uelezwe wazi udhaifu wao. "Wotugwisa"

Amri inapotolewa kupumzisha MV Magogoni

Ijumaa ya tarehe 19/12/2008 saa 2.30 usiku nilipitia Kivukoni ili niweze kurudi Nyumbani kwangu Kisemvule kwa kuogopa adha ya usafiri kupitia njia ya Mbagala huku nikitegemea kuwa kwa sasa usafiri wa boti umeimarika zaidi baada ya boti MV Magogoni kuzinduliwa mwanzoni mwa mwezi Desemba mwaka huu.

Cha kushangaza mara boti hilo MV Magogoni lilipotia nanga likitokea Kigamboni Captain aliamrishwa na bosi wake akiwa nyumbani kuwa asimamishe boti hilo na boti za zamani zitumike.

Hali hii iliwakera sana abiria kiasi cha kumzonga Captain.
Sidhani kuwa ilikuwa na mantiki kusimamisha boti hilo kwa wakati huo tena kwa amri kutoka nje ya sehemu ya kazi! Tulikuwa na matatizo ya boti usafiri taabu. Boti jipya limeletwa usafiri ni taabu. Hivi Watanzania tuna nini?

Lami yaanza kumwaga Kilwa Road

Wakati tunasherehekea kuingia kwa mwaka mpya, wakazi wa Mbagala na vitongoji vyake wameanza kuonja raha ya usafiri baada ya kupungua kwa foleni za magari katika barabara hiyo hasa kutoka Mtoni Mtongani hadi Sabasaba.
yapata wiki ya pili sasa kipande cha barabara hiyo kinachoanzia Mbagala Rangi 3 hadi karibu na Kizuiani kimeshawekwa lami kwa upande mmoja. Uwekaji wa lami unakaribia kabisa eneo la sabasaba (St. Anthony Sec.School).

Yale madaraja mawili ya mtoni Kizinga wamekamilika kwa asilimia 94. Ni matumaini yangu kuwa ifikapo mwezi Aprili 2009. Wakazi wa Mbagala watakuwa wanateleza kwenye Highway. Tatizo la usafiri Mbagala litakuwa historia.

Tuesday, December 30, 2008

Mitandao ya simu Matombo hajaisaidia sana maisha ya wakulima

Miaka miwili tangu Kampuni ya simu ya Celtel (sasa Zain) iingie Matombo, ushindani wa mitandao ya simu umeongezeka kwa kasi ya kutisha Matombo. Tigo wakasimika mnara wao kwenye mlima wa "Funamandole" mwaka jana na kuufanya mtandao huo kuwa bora zaidi ya Celtel.

Mwaka huu Vodacom imeingia Matombo na kufunika kabisa Zain na Tigo. Lakini sidhani ushindani huu unawasaidia sana wakulima masikini wa Matombo kwani mawasiliano ya simu za mkononi bado ni ghali mno hasa mawasiliano yakifanyika kwa mitandao tofauti. Hili linabidi kufanyiwa kazi na vyombo husika ili wakulima hao wasiwe wanapoteza fedha nyingi zaidi kwa mawasiliano kuliko chakula!

Monday, December 29, 2008

Miaka 47 imepita kilimo cha Matombo ni kilekile

Miaka 47 tangu tupate uhuru lakini napenda nikiri kama mtaalamu wa kilimo kuwa wakulima wengi wa Matombo hawafuata kanuni za kilimo bora. Licha ya kutotumia mbolea lakini kanuni za msingikama vile kupanda kwa nafasi hawajui, mbegu bora kwao ni ajabu tu, wadudu na magonjwa ya mimea yanashambulia yapendavyo. Kwa hali hiyo si ajabu kuona uzalishaji wa mazao Matombo ni mdogo sana.

Nilijaribu kuongea na baadhi ya ndugu zangu ambao ni wakulima wanasema kwa wastani huvuna gunia moja hadi mbili za mahindi kwa eka! Kiasi hiki cha mavuno hakiwezi kumlisha hata mtu mmoja kwa mwaka!

Sijui kama bwanashamba yupo katika kijiji chetu, sijui kama uongozi wa kijiji, kata na wilaya unatambua umuhimu wa kilimo kwa uchumi wa mwananchi wa Matombo.

Matombo imebahatika kuwa na hali nzuri ya hewa na udongo mzuri. Inafikika kirahisi kutoka Morogoro, Dodoma, Iringa na Dar kwa hiyo uhakika wa soko upo. Matunda ya tropiki kama vile machungwa, maembe, mananasi na ndizi yanapatikana kwa wingi. Siku hizi wakulima wameanza kujishughulisha na kilimo cha mazao ya viungo kama vile hiliki, pilipili manga na mdarasini sehemu za Konde, Nyangala, Tawa, Kinole na Mkuyuni.

Mazao haya yakijengewa mikakati mizuri na Halmashauri ya Wilaya kupitia DADPs yanaweza kuboresha hali ya uchumi ya watu wa Matombo.

Mto wa Mfizigo na mawe yake

Mto wa mfizigo ni moja ya mito mikubwa katika tarafa ya Matombo. Mto huu humwaga maji yake katika mto wa Ruvu ambapo wakazi wa jiji la Dar Es Salaam pamoja na sehemu za mkoa wa Pwani hapata maji kutoka mto huu.

Pamoja na umuhimu wake wa kutoa maji, mto huu una aina mbalimbali ya mawe ya kuvutia sana. Licha ya kuufahmu mto mfizigo kwa muda mrefu kwani nimeutumia mto huo kwa shughuli mbalimbali ikiwemo kuoga, kufua, kuvua samaki, kuchota mchanga na mawe tangu nikiwa mtoto sikuweza kutambua hapo awali kuwa mto Mfizigo una mawe ambayo yakipangwa vizuri yanaweza kutoa mapambo ya kuvutia. Ni juzi tu nilipokuwa mtoni Mfizigo ndipo wazo lilinijia la kuokota kiasi cha mawe ya aina mbalimbali ambayo yalinivutia sana. Ajabu, mto Mfizigo, mawe yake yanavutia sana.

Matombo imeanza kupoteza umaarufu wa machungwa matamu

Miaka 20 iliyopita Matombo ilikuwa maarufu sana kwa uzalishaji wa machungwa matamu. Machungwa haya yalijulikana kwa jina la Machungwa ya Matombo. Yalikuwa matamu sana hata rangi yake ilikuwa ya kuvutia mlaji.

Ni kweli miaka hiyo hakukuwa na biashara nzuri ya matunda haya. Nakumbuka babu yangu alikuwa na miti michache ambayo aliweza kuikodisha kwa walimu wa shule ya msingi Matombo kwa bei ya sh 2 kwa mchungwa! Sasa hali hii haipo tena. Uzalishaji umepungua sana na mahitaji yameongezeka sana kiasi cha kuwafanya wafanyabiashara (walanguzi) kuvuna machungwa wakati hayajapata rangi yake nzuri ya njano! Bei ya chungwa moja kwa sasa haitofautiani sana na ile ya Dar Es Salaam.

Miti mingi ya machungwa imeanza kuzeeka au kushambuliwa na wadudu na magonjwa na sikuona jitihada za makusudi kuokoa hali hiyo kwa wakulima wa machungwa. Ndiyo maana nathubutu kusema kuwa Matombo imeanza kupoteza umaarufu wa machungwa matamu.

Nyumba za kisasa za Familia Matombo

Kuna mwamko wa ajabu huko Matombo kwa sasa kwa kila familia kujenga nyumba ya kisasa ya familia. Hii ni kweli kabisa. Mmiliki wa Blog hii alishuhudia familia nyingi zilizokuwa zikijishughulisha na ujenzi wa nyumba za kisasa za familia kule Kiswira, Mhangazi na Nige. Huu ni mtizamo wa kimaendeleo. Nyumba nyingi zinazojengwa sasa zina satelitte dish, nyingine zinafungwa umeme wa jua (solar power) na nyumba nyingine zina generator za umeme.

Shauri yako, msichelewe nendeni mkajenge angalao nyumba moja ya kisasa ya familia. Mkizubaa mtaachwa. Waluguru sasa hawataki mchezo.

Banda la Kumpuzika wasafiri lijengwe Msalabani

Kwa wenyeji wa Matombo au waliobahatika kufika Matombo, jina MSALABANI si geni ni jina maarufu. Hapa ndipo ilipo njia panda ya kwenda Matombo Mission, Tawa, Konde, Nyingwa, Kibungo, Lukenge, Nyangala na vitongoji vingine vya Matombo.

Vitongoji hivi vina wakazi wengi ambao kwa usafiri wa uhakika inawabidi kusafiri hadi Msalabani ambapo ndipo kwenye barabara kuu itokayo Morogoro kwenda Kisaki. Tatizo la mahali hapa ni ukosefu wa Kibanda cha kupumzika abiria.

Juzi Jumamosi wakati nasafiri kuelekea Morogoro mjini abiria wengi tulinyeshewa na mvua na kulowa chapachapa. Wanawake ilibidi wabadilishe nguo zao hapohapo baada ya kukatika kwa mvua.

Hivi uongozi wa Matombo hawaoni umuhimu wa kujenga kibanda imara japo kilichoezekwa kwa makuti ili kuwahifadhi abiria wakati wa jua au mvua? Hili linawezekana. Tuanze sasa kabla ya masika.

Dakika 120 Matombo-Moro

Nimerudi kutoka Matombo. Mambo yalikuwa safi sana huko kijijini. Nimekula magimbi, mananasi, maembe na ubwabwa. Lakini cha kushangaza mwaka huu kuku ni wachache sana Matombo. Hata wa kununua hawapatikani. Kuku imekuwa ni dili kubwa sana Matombo. Unawaona lakini hauwzwi!

Ndiyo, barabara ya Matombo kwa sasa ni nzuri mno! Ndiyo maana tumeweza kutumia dakika 120 kufika Matombo kutoka Morogoro mjini kwa kutumia kibus cha 'Hiace.' Msalabani hadi Matombo Mission barabara imenyanyuliwa hata corolla inapita! Ni kweli walionazo walikuja nazo kushrehekea Xmass kijijini. Pale Chamarigo (Gubi) ambapo huwa panasumbua sana wakati wa mvua sasa pamewekewa Culvert. Safi sana. Hongera Tanroads, Hongera Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro Vijijini.

Tuesday, December 23, 2008

Safarini Matombo-Morogoro

Xmass na mwaka mpya unakaribia. Sisi hatuna utaratibu wa kurudi kwetu wakati wa Xmass kama ilivyo kwa wenzetu Wachagga. Hivi sasa huko migombani ni nyimbo za marehemu Jim Reeves tu na harufu ya mbege kumbe je!

Mwaka huu nimeamua kwenda kusherehekea Xmass na ndugu zangu huko kwetu Matombo, nikale Magimbi, Ndizi, mananasi, "ubwabwa na kuku." Nitasafiri kwenda Matombo Morogoro kwa Bibi na Babu zangu, Baba na Mama zangu, Shangazi na Wajomba zangu, Kaka na dada zangu na wengineo.

Nategemea nitaonana na marafiki zangu tuolisoma shule moja, kusali pamoja pale Matombo Mission, kucheza mpira pamoja -Kiswira Sports Club! Nategemea kuimba GLORIA! siku ya Xmass ndani ya Kanisa la Mtakatifu Paul.

Nitakaporudi nitakuwa na mengi ya kuning'iniza kwenye blog hii.

KWAHERINI

Wednesday, December 17, 2008

ARI-SELIAN nawapa shavu kwa usafi

Nipo Arusha kikazi pamoja na watafiti wa hapa. Kilichonileta hapa ni kuwasilisha miongozo na kujadiliana na watafiti waandamizi jinsi ya kuandaa viashiria vya shughuli za utafiti kanda ya kaskazini. Lakini kilichonivutia zaidi wakati nikiwa hapa kituoni Selian ni usafi wa mazingira hasa vyoo. Vyoo ni visafi kweli kweli sabuni zipo na watumiaji ni wastaarabu kwa kweli.

Tabia ya usafi katika kituo cha Utafiti wa Kilimo Selian imejengwa kwa muda mrefu kwa sasa ni utamaduni uliozooeleka hapo kituoni watakushangaa kama unachafua mazingira yao bila sababu. Hongera sana Selian.

Three Principles of Conservation Agriculture

  • Minimum soil disturbance or if possible no tillage seeding
  • Soil cover; if possible permanent; and
  • Useful crop rotations and association

INTERESTED?

For more infromation please read a book on "Conservation Agriculture as practised in Tanzania":Three case studies (Richard Shetto, Marietha Owenya editors). Published in 2007

Karibu nyumbani Dr.Doreen


Ndivyo ilivyokuwa wakati Dr.Doreen alipokaribishwa nyumbani kwao Kimara Temboni na mumewe Dr.Mainen Moshi.

Mama yake Paulina Mloka, kaka yake Freddy Mloka, Bibi yake Sister Maria Makeya, watoto wake, ndugu, marafiki, jamaa na wageni waalikwa walikuwepo katika tafrija nzito ya kumpongeza. Pichani Dr.Doreen akiongozwa kwa mbwembwe za kiluguru avho! na MC Inno Banzi huku akisindikizwa na dada yake Helena Mimata.

Dr. Doreen kumbukumbu na Marais


Hii ndiyo picha ya kumbukumbu ya siku ya kutunukiwa shahada ya uzamivu (PhD) Dr.Doreen Mloka Moshi.Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sayansi ya Tiba Muhimbili (MUCHS) Rais Mstaafu Mhe. Ali Hassan Mwinyi (Mzee Ruksa) ndiye aliyetunuku shahada hizo tarehe 13/12/2008. Mgeni rasmi alikuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Jakaya Mrisho Kikwete. Hongera sana Da Doreen.

Dr.Doreen Mloka Moshi-PhD "mukichwa"


Siku ya tarehe 13/12/2008 Jumamosi itakuwa siku ya kumbukumbu kubwa kwa Doreen, familia yake, ndugu na majamaa wakati alipotunukiwa shahada ya Uzamivu (PhD) katika tiba. Pichani kushoto Dr. Doreen ndani ya joho la Chuo Kikuu cha Sayansi ya Tiba Muhimbili (MUCHS) katika hisia kali. Kulia ni Professor Nuhunoli (naomba nisahihishwe jina sahihi) aliyetunukiwa shahada ya Udaktari wa Sayansi. Kutokana na maelezo niliyoyapata kutoka kwa wasomi, hii ni tuzo ya juu kabisa.

Friday, December 5, 2008

Shibuda atagombeaje urais katika mlango mmoja ?

Conges Mramba katika makala yake kwenye gazeti la Rai (Mraba wa Mramba) tarehe 4-10 Desemba amekuja na kichwa cha habari CCM: Damu ya kijani au geresha? Ndani ya makala hiyo ameandika mambo mengi ya kutafakari kuhusu CCM na mambo yanavyokwenda kwenye chama hicho tawala.

Binafsi nimefurahishwa na hili. Nanukuu- " Shibuda atagombeaje urais katika mlango mmoja unaoandaliwa kwa rais aliyepo madarakani? Tafakari.

Mfumuko wa bei ni aslimia milioni 230- Siamini!

Hivi kweli mfumuko wa bei Zimbabwe ni asilimia milioni 230! Mbona siamini, nashindwa kupata picha. Mimi ni mchumi, hiyo asilimia milioni 230 nashindwa kuipresent kwa kweli. Hivi Wazimbabwe wanaishije huko? Kuna tatizo na si dogo. Tuwasaidie ndugu zetu Wazimbabwe.

"Utaratibu tuliojiwekea" maana yake nini?

Siku hizi mambo yanapokiukwa utasikia kwa "utaratibu tuliojiwekea."
Kama kanuni, sheria na taratibu zipo kwanini tuwe na kitu mbadala- "Utaratibu tuliojiwekea" hapa ndipo tunapoanza kuharibu mambo. Na ndipo haki inapopindwa.

Hivi unafahamu kiswahili cha "White Elephant?"

Usipoteze wakati wako utauumiza kichwa bure! White elephant ni - Geresha (Gheresha).

Quote from Rio Ferdinand

Rio Ferdinand is a dependable centrehalf of the Manchester United Football Club of England.
I was moved with his words from the article published on the Daily News of last Friday 27/11/2008.

I quote - "Outside of Sport it would be Nelson Mandela for all he's achieved. He's devoted his life to his nation."

"It would be great if Nelson Mandela was the person who handed us a cup. There's no better man in the world to do that and tha's something to work towards, but there is a very long way to go yet."

Aliyasema haya alipokuwa akiuulizwa anafikiriaje kuhusu klabu bingwa ya dunia?

Dereva Taxi wa aina hii ni wachache

Si rahisi ukasahau kitu kwenye Taxi na hatimaye akakipata. Lakini wako madereva taxi wanaoheshimu kazi zao na wanaopedna kulinda soko.

Dereva Taxi aliyanipeleka Jomo Kenyatta International Airport hivi karibuni ni muungwana kwani baada ya kushusha mkoba wangu kumbe nilidondosha "highlighter" (kalamu kubwa ya rangi ya kuweka msisitizo) ndani ya gari. Alipoiona alisimamisha gari na kunipatia kalamu hiyo. Dereva wa aina yake ni wa chache. Nakushukuru na umependisha chati madereva Taxi wa Kenya ingawa si wote. Asante sana.

Ulemavu si hoja

Niko Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Jomo Kenyatta nikisubiri ndege yakunirudisha nyumbani Dar. Jirani yangu yuko mama mmoja wa kizungu (baadaye nakajakugundua kuwa ni Mswede) yuko "busy" na laptop yake na kifaa kingine (sikijui). Nashangaa nagundua kuwa ni kipofu lakini ana jamaa zake wawili alioandamana nao.

Baadaye nagundua kuwa naye anasafiri kuelekea Tanzania tena Morogoro. Nilifahamu hivyo baada ya kusikia mazungumzo yao na yule Mmasai kutoka Twatwatwa, Kilosa na mama mmoja kutoka Sudan. Mama huyu licha ya kutoona alikuwa na vifaa vya kisasa vinavyomsaidia kuendesha shughuli zake kama vile kutumia kompyuta. Na wakati akizungumza huwezi kugundua kama ni kipofu, ufahamu wake ulikuwa ni wa hali ya juu. Ama kweli Ulemavu si hoja.

Vijana wakiafrika sasa hufanya biashara nchi mbalimbali

Kuchelewa kuondoka uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyata siku ya tarehe 26 Novemba 2008 kumenifanya nijifunze mengi.

Wakati nilipokuwa napata chakula cha mchana cha kuponi pale uwanjani (kutokana na kucheleweshwa) niliwaona vijana wengi wake kwa waume. Nilibahatika kumuuliza mmoja wao anatokea wapi alinijibu anatoka Nigeria na anelekea Bangkok kwa shughuli ya biashara. Kwenye meza nilizunguukwa na vijana wanne waliokuwa wakizungumza kifaransa nao wako kwenye pilika ya safari za kibiashara. Nilishindwa kudodosa zaidi nijue ni biashara ya aina gani wanayofuata huko Bangkok. Sote tulikuwa tunasubiri chakula!

Kenya Airways huchelewa pia

Ndege KQ 482 kutoka Nairobi kuelekea Dar Es Salaam ilikuwa iondoke saa 6:45 mchana Jumatano tarehe 26/11/2008. Lakini haikuweza kuondoka hadi saa 12.30 jioni. Lo! Kumbe hata KA nayo huchelewa?

Unapokutana na mfugaji kutoka Twatwatwa ukiwa Nairobi

Adam Ole Mwarabu ni mfugaji kutoka kijiji cha Twatwa, Kilosa, Morogoro. Kijiji hiki ni maarufu kwa mapigano kati ya Wafugaji (Wamasai) na wakulima. Adam ni Mmasai. Hivi karibuni nilikutana na Adamu uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa JomoKenyatta Jijini Nairobi wakati tukisubiri ndege ya kurudi nyumbani Tanzania (Dar Es Salaam). Ilikuwa ni mara yangu ya kwanza kukutana na Adam. Huku akivalia lubega na kubeba "laptop" yake ni lazima utajiuliza kimoyomoyo hivi Mmasai anaweza kutumia Laptop?

Adam, ni Mmasai aliyendelea. Amesafiri nchi nyingi hapa duniani kuliko wengi wetu. Amehudhuria mikutano mingi ya kimataifa na wakati nilipokutana naye alikuwa anatokea Ubalozi wa Poland kuchukua Visa.

Adam ni Mratibu wa NGO inayooitwa PAKODEO (nitamuuliza kirefu chake). NGO hii hujishughulisha zaidi na masuala ya ardhi, mifugo, elimu, mazingira na jinsi ya kupambana na HIV-AIDS.

Adam hazungumzii zaidi kuhusu mapigano ya wakulima na wafugaji anasema ni ya kisiasa zaidi na viongozi hawako makini katika kutatua tatizo.