Tuesday, September 21, 2010

Bibi Sister ametuachia hazina ya Upendo


Tarehe 3/9/2010 itabakia kuwa moja ya siku ya kukumbukwa na familia kwa msiba mzito wakwa kifo cha Bibi yetu mpendwa Sr. Maria Magdalena (Binti Makeya Mzuanda).Bibi alifariki hospitalini Mikumi Morogoro na kuzikwa kwenye makaburi ya watawa - Convent ya Mgolole-Morogoro tarehe 7/9/2010 (Jumanne) Kwa Ibada takatifu iliyoongozwa na Mhashamu Baba Askofu Telesphor Mkude wa Jimbo na Morogoro na kuhudhuriwa na Mhashamu Baba Askofu Athony Banzi wa jimbo la Tanga pamoja na Mapadre, Masista ndugu, marafiki na jamaa. Kumbukumbu zinaonyesha kuwa Bibi alizaliwa mwaka 1920. Kwahiyo tunaweza kusema kuwa alifariki akiwa na umri wa miaka 90.

Aliingia katika utawa wa Shirika la Moyo Safi wa Bikira Maria mwaka 1939. Nadhiri yake ya daima katika shirika hilo aliiweka tarehe 15/8/1952. Mwaka 1967 alisherehekea jubilee ya kutimiza miaka 25, 1982 miaka 40, mwaka 1992 miaka 50 na mwaka 2002 miaka 60 ambayo ilifanyika Mgolole.

Katika uhai wake Bibi Sista amelitumikia Kanisa katika parokia zifuatazo:- Tangeni, Singiza,Mgeta,Kikeo,Mgolole,Mt.Patrice (Morogoro mjini), Ilonga na Parokia ya Ruaha ambako ndiko ulikomkuta umauti. Kitaaluma yeye alikuwa ni mwalimu kwa hiyo katika parokia hizo alizoishi alikuwa akifanya kazi ya ualimu kwa njia moja au nyingine.

Alikuwa mlezi mahiri wa miito kwa mapadri na masista, mcheshi, mchangamfu na mchapa kazi. Mwaka jana mwezi Desemba nilimkuta Parokiani Ruaha akipalilia mpunga wake nikaanza kumtania..bibi nitakuja kula ubwabwa mwezi wa sita. Akanijibu- karibu mume wangu. Baadaye nilimwimbia nyimbo yetu (Lololo kipenzi changuX2. Amenitia kishindo, umenitia kishindo moyo wahangaika!).Baada ya hapo alicheka sana na kusema Inno bwana! Hata hivyo nilishindwa kuimba wimbo huo wakati tunauaga mwili wake pale Mgolole tarehe 7 Septemba.

Familia imempoteza mtu muhimu sana, kwani licha ya utawa wake alikuwa ni nguzo ya familia (Wambiki). Aliweza kukemea yasiyo mazuri na kutoa ushauri pale alipoona familia inakwenda ndiko siko. Hakuwa mbaguzi binti Makeya. Kati ya watu ambao aliwasikiliza sana na ameishi naye hadi kifo chake ni kaka Venance Jakka (Padri)-Paroko wa Ruaha. Daima kama kuna jambo limekosewa alikuwa akisema Baba Jakka hapendi.. Mjukuu huyu alimpenda sana bibi naye bibi alimpenda mjukuu hadi umauti wake.

Ndiyo Bibi Sista ameondoka. Hakuna Bibi Sista tena ingawa masista wanaingia na kutoka.MUNGU AILAZE MAHALI PEMA PEPONI ROHO YA MAREHEMU BIBI SISTA MARIA MAGDALENA (Constansia Makeya).MUNGU AKIPENDA TUTAKUTANA TENA.

2 comments:

Belo said...

Poleni kwa msiba

Unknown said...

Jaman naomba msaada wa namba ya baba paroko hapa mjini parokia ya mtakatifu Patrice