Friday, October 24, 2008

Asilimia 62 ya wahitimu wa darasa la saba kupata sifuri kwenye hisabati ni hatari

Waziri Mkuu Mhe.Mizengo Pinda alipokuwa akitoa hoja ya kuahirisha mkutano wa kumi na mbili wa Bunge-Dodoma tarehe 29 Agosti 2008 moja ya mambo aliyozungumza kwa uchungu sana ni wanafunzi kushindwa vibaya mtihani wa hisabati. Alisema. Kwa mfano mwaka 2001, katika mtihani wa kumaliza Darasa la saba, asilimia 62 ya watahiniwa katika Wilaya ya Morogoro Vijijini walipata sifuri katika Mtihani wa Hisabati. Hii ina maana kuwa asilimia 62 walimaliza shule bila kujua Hisabati rahisi za kujumlisha, kutoa , kuzidisha na kugawanya.

Hali hii ni mbaya sana. Inaonekana kuwa wanafunzi hawaoni umuhimu wa somo la hesabu, walimu pia kadhalika na wazazi tuseme na taifa zima.

Enzi zetu mwanafunzi ukifahamu hesabu hizo sifa tu unazomwagiwa mwenyewe utapenda hesabu. Na kama hujui hesabu ulikuwa unadharauliwa. Hata Sekondari waliokuwa wanachukua sayansi waliheshimika na wale wa sanaa au "arts' kwa kweli walionekana kama wapo wapo tu. Hata mzazi aliona ni sifa kwa mwanae kuchukua sayansi.

Tatizo letu Watanzania ni jinsi tulivyobadilika kirahisi kimtazamo katika mambo mbalimbali hasa elimu. Tunapenda mambo rahisi. Sasa hivi kila mtu yuko kwenye menejimenti, siasa na biashara! Kwa hali hii si rahisi mtoto kupenda hesabu. Hesabu zinatakiwa kutulia. Kama alivyosema Waziri Mkuu. Hesabu inajenga dhana ya kujiamini, kujenga falsafa ya mambo kwa mpangilio wenye mantiki (Logical Thinking).

Wito wangu ni kufufua ari ya kupenda hesabu na ionekana kwa watoto wetu kuwa bila hesabu huko mbele ni giza.Ijionyeshe waziwazi katika maisha yetu ya kila siku jinsi hesabu zinavyofanya kazi. Labda nihitimishe kwa kusema kuwa mwanafunzi yeyote anayepuuzia hesabu atapata matatizo makubwa katika kuendelea na elimu yake popote pale.


Wenzangu wa Moro sijui kama tumeshaanza kuchukua hatua ya kujikwamua kutoka katika aibu hii. Na hasa ikizingatiwa kuwa ni Morogoro vijijini kwani huko hakuna shule za kulipia kwa hiyo ni watoto wa malofa hawajui hesabu toba!

No comments: