Saturday, April 14, 2007

SHULE ZIWE VITUVO VYA MAENDELEO

Mwaka huu sote tumeshuhudia ujenzi wa shule nyingi za SEKONDARI. Shule zimejengwa kwa AGIZO na kweli AGIZO limefanyiwa kazi. Na sasa Wilaya zinashindana na mikoa nayo inashindana kwa kujenga shule nyingi watoto wetu wengi wamepata nafasi ya kujiunga na shule za sekondari. Hilo ni jambo zuri. Ingawa baadhi yetu wanahoji kama kweli kujenga shule ndiyo kuwa na ubora wa Elimu? Sasa baada ya shule kujengwa tuzipatie vitendea kazi na tufuatilie kuona elimu bora inatolewa

Wazo langu la leo ni kwamba hizi shule za Sekondari zinazojengwa katika kila Kata ziwe chachu za maendeleo katika nchi yetu. Sekta zote zijikite katika Kata ziliko shule kwa ajili ya kutoa huduma na kujenga uchumi. Kwa kuwa naamini kuwa kwenye shule hizo kuna watu wa aina mbalimbali ambao wasingependa kuona kuwa wametupwa. Kwa mfano hakuna mwalimu yeyote ambaye angependa kufundisha na kuishi sehemu ambayo maji, usafiri, umeme, mawasiliano ni shida. Asingependa kuishi sehemu ambayo upatikanaji wa chakula ni shida, asingependa kuishi sehemu ambayo hakuna huduma ya afya.

Kama sekta zote zitajikita ziliko shule za sekondari ni rahisi kupanga mipango ya maendeleo yenye upeo mpana zaidi na itakuwa ni rahisi kufuatilia na kupima maendeleo. Watu watajifunza kutoka kwa wengine na maendeleo yataonekana. Haya ni maoni yangu.

Nakumbuka nilipokuwa mdogo sehemu zote zilizokuwa na "Middle Schools" huduma muhimu zilipatikana. Waalimu walionekana wamaana sana, waliheshimika na walikuwa na uwezo mzuri kimaisha. Ilikuwa ni sifa kuitwa mtoto wa mwalimu kwa sababu alikuwa ni kioo cha maisha mahali pale. Sasa je? TUFUFUE MTAZAMO HUO. TUZIFUATE SHULE ZA SEKONDARI KWA MAENDELEO.

No comments: