Saturday, April 14, 2007

Wanawake wapewe kipaumbele katika kutoa mikopo

Takribani miezi miwili sasa nimekuwa nikifuatilia kwa jinsi wanawake wa Tanzania wanavyojishughulisha katika kujipatia riziki.

Kwa mfano Jijini Dar Es Salaam baadhi ya akina mama ndiyo wanaolisha wafanyakazi wa jiji hili. Si mara moja ama mbili mimi mwenyewe nilipata msosi pale Tazara karibu na Redio Tanzania kwa akina mama hao. Wanawake wanaoendesha biashara ya mama lishe wengi wao ni vijana kati ya umri wa miaka 20-45 hivi.

Kuna hii biashara ya kuuza chupa za plastic jijini Dar. Akina mama wamo, shughuli hii hapa jijini hufanywa na wanawake wa umri mkubwa kati ya miaka 40-50. Pengine vijana wanaona aibu kupita mitaani kuokota chupa ndiyo maana hawaonekani sana kwenye biashara hiyo.Pengine huokota usiku! Lakini utazionaje chupa usiku? Wazee hawaoni haya wanachotaka ni riziki. Na ikumbukwe kuwa hawa wanabeba mzigo mkubwa katika kaya wengine huishi hata na wajukuu na watoto wa ndugu zao kwa hiyo la msingi wao ni kupata riziki. Aibu ya nini?

Pale Mbagala Rangi 3 ifikapo jioni kuanzia saa 12 biashara mbalimbali huanza kufanyika. Wapo wauza matunda na mbogamboga, wapo wauza mihogo, wapo wauza korosho n.k. Lakini wanaofanya biashara hizo wengi ni wanawake wa rika mbalimbali.

Nilipokuwa kwenye semina mjini Morogoro hivi karibuni niliwakuta wanawake wakiuza nguo za aina mbalimbali kando ya kumbi za mikutano. Na si mara moja kuwaona wanawake wakifanya biashara hizo kwenye kumbi mbalimbali za mikutano. Wapo Morogoro Hotel, wapo SUA, wapo Islamic University n.k.

Baada ya kufuatilia na kudadisi sana na kuangalia ile mikopo ya bilioni moja iliyotolewa kwa kila mkoa kwa ajili ya ujasiliamali. Napenda kushauri kuwa mikopo hiyo kipaumbele wapewe wanawake. Wanawake ni nguzo ya familia kwa kweli. Wanawake wakijikwamua kiuchumi maendeleo yatapatikana kwani waathirika wakubwa kiuchumi kwenye jamii zetu ni wanawake. Lakini jitahada zao kujikwamua kiuchumi zinaonekana. TUANZE SASA

No comments: