Tuesday, February 1, 2011

Alivyozikwa Chief George Patrick Kunambi


Nianzie mchana wa tarehe 28/1/2010 Ijumaa, pale Msewe-nyumbani kwa marehemu Chief George Patrick Kunambi. Naingia maeneo ya msiba nakutana na rangi za kijani nyingi zilizovaliwa na vijana(napata picha kuwepo kwa CCM), hatimaye nakutana na umati mkubwa wa watu uliofurika sehemu ya msiba, wengine wakijipanga kwenye mistari mirefu.Wakati bado nashangaa, sauti kutoka kipaaza sauti 'ukishatoka kumuaga marehemu unaunga mstari wa kupata chakula kabla ya kuanza taratibu za mazishi.'
Hili la kumuaga nalipa kipaumbele (najisemea kimoyomoyo kumbe nimewahi!).

Naingia ndani ya nyumba kubwa,nyumba ya Chifu nakuta jeneza lililopambwa vizuri na la kupendeza likiwa na mwili wa marehemu Chief George Patrick Kunambi. Napiga ishara ya msalaba. Ni kweli 'Babu Kunambi' amefariki.

Taratibu za mazishi zinatangazwa kwa kupata salamu kutoka kwa wakilishi wa taasisi mbalimbali, na vyama vya siasa. Alikuwepo Mhe. Mbowe Mwenyekiti wa Chadema aliyemuelezea Chifu Kunambi kuwa alikuwa ni mwenye mapendo makubwa, mzalendo, na mchapa kazi. Kisha wasifu wa marehemu ulisomwa.

Chifu kunambi alizaliwa kijini Matombo tarehe 16, Agosti 1916.Chief Kunambi alipata elimu yake ya msingi katika shule ya msingi Matombo, Sekondari Tabora, Elimu ya Juu Makerere Uganda na hatimaye shahada ya Uzamili (MA) huko Marekani. Amefanya kazi katika Taasisi mbalimbali hapa nchini ikiwemo Chuo Kikuuu Dar Es Salaam akiwa kama Msajili. Aidha amefanyakazi katika Taasisi za Usafirishaji na hadi umauti unamkuta alikuwa Mwenyekiti wa Baraza la Majadiliano la Mamlaka ya Bandari kwa takribani miaka 25.Ni mmoja wa waanzilishi wa chama cha TANU kilicholeta UHURU wa Tanganyika.

Katika uhai wake Chifu Kunambi alijaliwa kufunga pingu za maisha na Bi.Bernadetha Namphombe Kunambi (Marehemu) na kubahatika watoto wanne (wanaume 2 na wanawake 2) walio hai ni wawili, Lucas Kunambi na Dr.Patricia Kunambi. Ameacha wajukuu wapatao saba.

Baada ya wasifu wake kusomwa watani wa waluguru (wasukuma, wanyamwezi, wangoni, wahehe,wadigo, wasambaa, Wapogoro...)walipata 'nguto' zao na hatimaye Jeneza la marehemu liliingizwa kwenye gari maalumu na kuelekea kanisani kwa misa takatifu huku ngoma maarufu ya waluguru ijulikanayo kwa jina la Keyamba ikisindikiza taratibu!

Ibada ya Misa Takatifu iliongozwa na Mhashamu Askofu Athony Banzi wa jimbo la Tanga akisaidiwa na Askofu Telesphor Mkude wa jimbo la Morogoro na mapadri wengine kama Mogella, Prof.Mkude,Padre Jakka kutoka Parokia ya Kidatu, Padri Kwembe kutoka St.Peters-DSM pamoja na Mapadre wenyeji wa Msewe.

Watu waliokuja kumsindikiza Chifu Kunambi katika safari yake ya mwisho ni wengi.Waluguru walio wengi walionekana siku ya mazishi ya Chifu wao. Wageni wengine waliohudhuria ni Mh.Pius Msekwa (Katibu Msaidizi wa CCM), Mzee Kingunge Ngombale Mwiru, Mhe. Betty Mkwasa, Mhe. Sophia Simba, IGP mstaafu Omari Mahita, Kamishna Mkuu wa Magereza Mstaafu Nicas Banzi,Bw. Nibuka Mnzeru (Mbunge wa zamani wa Morogoro mjini)na Dkt.Gregory P.Mluge.

Utani kwenye mazishi hayo haukukosa kwani kwa muda mrefu kuna watani wawili waliojifanya wanandoa waliojipamba vizuri huku wakiburudika kwa KONYAGI walionyesha utani wao kwa wafiwa ambao kwa mila za waluguru ni ruhusa!

Hatimaye muda wa saa 11.30 jioni jeneza la Marehemu Chifu Kunambi lilishushwa taratibu kaburini nyumbani kwake Msewe kuhitimisha mazishi yake.

3 comments:

www.mussa1974.blogsport.com said...

nashukuru sana kwa habari hii

emuthree said...

poleni sana na msiba huo

Unknown said...

Nimefurahi Sana kupata story ya marehemu chief Kunambi.